Tuesday, December 4, 2018

Nashukuru Niliandika Kitabu Hiki

Nashukuru niliandika kitabu kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nasema hivi kutokana na jinsi kinavyothaminiwa na watu wanaokitumia. Taarifa hizi ninazipata kutoka kwao.

Wiki hii kwa mfano, nimepata mawasiliano kutoka kwa waalimu wawili. Profesa Artika Tyner, kiongozi mojawapo wa Chuo Kikuu cha St. Thomas ameniandikia kuwa anahitaji nakala za kitabu hii, nami nimempelekea. Niliwahi kumwongelea katika blogu hii, baada ya kukutana naye kwa mara ya kwanza. Tangu tukutane, amekuwa mpiga debe wangu wa dhati. Namshukuru.

Nimepata pia ujumbe kutoka kwa Profesa Barbara Zust wa Chuo cha Gustavus Adolphus kunialika kwenda kuongea na wanafunzi anaowapeleka Tanzania katika programu ambayo imedumu miaka mingi. Kama ilivyo kawaida yake, ananiomba nikaongee na wanafunzi kuhusu masuala yaliyomo katika Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Kama kawaida, watakuwa wameskisoma na wanasubiri fursa ya kuniuliza masuali. Miaka yote nimefurahi kukutana na wanafunzi hao.

Ninafarijika na kushukuru kwamba nilijiingiza katika shughuli hii ya kuwasaidia watu kutafakari na kuelewa tofauti za tamaduni na athari za tofauti hizo, ili kujizatiti kabla na wakati wa kukutana na watu w utamaduni wa kigeni. Nashukuru niliandika kitabu hiki, ambacho  kimenirahishia kazi hiyo, na papo hapo ni chachu ya tafakari na mazungumzo ya kuelimisha. Nashukuru kuona kuwa wadau kama hao niliowataja, wenye wadhifa mkubwa katika jamii, wanaona umuhimu wa mchango wangu, nami sitawaangusha.

6 comments:

Mbele said...

Kitabu hiki kinapatikana katika duka la vitabu la Kimahama Literature Center mjini Arusha, na duka la vitabu liitwalo A Novel Idea sehemu iitwayo Slipway eneo la Msasani, Dar es Salaam.

Anonymous said...

Na Nairobi, kinapatikana wapi? Ikiwa huna mahala unaonaje kunipa jukumu la kusambaza Nairobi.
Tunaweza kuzungumza zaidi kwa email kmgeituff@gmail.com



Mbele said...

Ndugu Khalfan

Asante sana kwa ujumbe wako. Ni ajabu, kwa sababu nami kwa miezi mingi nimekuwa nikiwazia kutafuta namna ya kukifikisha kitabu changu Kenya. Kujitokeza kwako ni kama muujiza. Alhamdulillah. Nitakuandikia kwenye hii anwani uliyoleta. Nakutakia kila la heri.

Anonymous said...


Nimefarijika kwa maneno yako. Mimi naishi Nairobi na nayafahamu vyema maduka ya vitabu maarufu ktk jiji hili. Nasubiri andiko lako kwa hatuwa zaidi.

Anonymous said...

Prof, nikiwa nasubiri kwa hamu email yako nimejaribu kukitafuta kitabu Novel Idea lakini naambiwa kimekwisha. Iwapo unayo mawasiliano na duka la Arusha naomba namba zao ili niwasiliane nao.

Ahsante.

Khalfan.

Mbele said...

Ndugu Khalfan

Samahani sana kwa kuchelewa kwangu kujibu ujumbe wako. Nilifika hapa Dar es Salaam tarehe 27 Januari na baada ya kuona ujumbe wako, nilienda kwenye duka la A Novel Idea kufuatilia suala la vitabu. Vilikuwepo vitabu viwili: "Matengo Folktales" na "Africans and Americans: Embracing Cultural Differences." Niliarifiwa kwamba nakala za "Matengo Folktales" zilikuwa zimenunuliwa zote. Nakala chache za "Africans and Americans: Embracing Cultural Differences" bado zilikuwepo, na niliziona. Nitakuandikia ujumbe kwenye anwani uliyonipa. Nakutakia kila la heri.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...