Posts

Showing posts from December, 2008

Warsha: Utamaduni, Utandawazi na Maendeleo

Kati ya mambo ninayofanya ni kutoa ushauri kwa mashirika, taasisi, vyuo, vikundi na watu binafsi kuhusu masuala ya tofauti baina ya utamaduni wa Mwafrika na ule wa Mmarekani. Ninafanya hivyo kwa njia mbali mbali, kama vile kuandika makala na vitabu, kuendesha warsha, au kukutana watu binafsi ana kwa ana. Ninaposema utamaduni, namaanisha vitu kama hisia, tabia, maadili, namna tunavyofikiri na tunavyoongea. Vipengele hivi vyote vinatutofautisha watu wa tamaduni mbali mbali, na ni muhimu kuvielewa ili kuepusha migongano. Katika dunia ya leo, ya utandawazi, masuala ya tofauti za tamaduni yanahitaji kupewa kipaumbele, kwani yanaweza kuwa pingamizi kubwa, chanzo cha migogoro, au chachu ya hii migogoro. Nitaendesha warsha kuhusu masualaa hayo tarehe 4 Julai, 2009, kwenye kituo cha Meeting Point Tanga. Watu kutoka mashirika, makampuni, taasisi, na jumuia mbali mbali watapata fursa ya kuyatafakari masuala kadha wa kadha yanayojitokeza wakati huu ambapo watu wa tamaduni mbali mbali wanalazimi

Kijitabu Changu Kipya

Image
Miaka miwili iliyopita niliombwa kushiriki katika maonyesho ya utamaduni wa Mwafrika, soma hapa , yaliyofanyika kwa mara ya kwanza mjini Minneapolis katika jimbo la Minnesota, Marekani. Maonyesho hayo yalipangwa kujumlisha mambo mengi: historia ya Mwafrika duniani na harakati alizopitia, mafanikio na mchango wake, na hali yake ya sasa na baadaye. Wasanii, wabunifu wa mavazi, wanamuziki, na wengine walialikwa kutoa mchango wao. Mimi nilialikwa kuandaa vielelezo vya mambo muhimu katika historia ya Mwafrika, kuanzia chimbuko la binadamu Afrika hadi kusambaa kwa Waafrika sehemu mbali mbali za dunia, kama vile Marekani, Ulaya, na Asia. Nilifanya utafiti nikaandika habari hizo kwa mtindo wa insha fupi kumi. Kila insha niliiweka kwenye bango kubwa na kila bango liliambatana na picha kadhaa. Siku ya tamasha, niliyabandika mabango hayo kwenye kuta za ukumbi niliopangiwa. Watu walifika humo na kusoma kwa wakati wao, wakiangalia pia zile picha. Mama mmoja aliyehudhuria na kuanga

CCM: Ni chama cha Mapinduzi?

Sielewi kwa nini watu wanaamini kuwa CCM ni chama cha mapinduzi. Sijawahi kuelewa na bado sielewi kwa nini. Dhana ya mapinduzi ilielezwa vizuri na TANU, katika "Azimio la Arusha," "Mwongozo," na maandishi, hotuba na mahojiano mbali mbali ya Mwalimu Nyerere. Matokeo ya yote hayo ni kuwa Watanzania tulifahamu vizuri na kukubali dhana na maana ya mapinduzi katika nchi yetu. Yeyote ambaye hajasoma maandishi hayo, au kusikiliza hotuba hizo, ningemshauri afanye hivyo, ili aweze kufahamu msingi wa ujumbe wangu. CCM ilipoanza, ilijinadi kuwa ni chama cha mapinduzi. Lakini baada ya muda si mrefu, mwelekeo wake ulijionyesha kuwa si wa mapinduzi. Badala ya kuendeleza fikra na mwelekeo wa "Azimio la Arusha," "Mwongozo" na mengine yote niliyoyataja hapo juu, CCM ilitoa "Azimio la Zanzibar." Ingawa CCM haikutoa fursa iliyostahili kwa wananchi kuliangalia na kulijadili "Azimio la Zanzibar," habari zilizojitokeza ni kuwa Azimio hili liliki

Kuku kwa Mrija

Watanzania wana uwezo mkubwa wa kubuni misemo na kudumisha uhai na utamu wa lugha ya kiSwahili. "Kuku kwa mrija" ni usemi moja ambao umepata hadhi ya pekee katika kiSwahili cha mazungumzo. Naamini kuwa wengi wanaweza kueleza maana ya usemi huu na matumizi yake, lakini napenda kuelezea machache, kwa kuchambua mantiki yake. Kuku kwa mrija ni usemi unaobeba dhana ya maisha ya raha, starehe, na vyakula tele. Kwa vile kuku ni nyama inayothaminiwa sana katika utamaduni wetu, kula kuku sana ni dalili ya kuishi maisha ya raha na mafanikio. Kwa ujumla, Watanzania wanaamini kuwa maisha hayo yanapatikana nchi za nje, hasa Ulaya na Marekani. Mtanzania anayeishi huko anahesabiwa na Watanzania walioko nyumbani kuwa anakula kuku kwa mrija. Maisha yake ni ya starehe na kuku ndio chakula chake kikuu. Mimi mwenyewe nilikuja Marekani mara ya kwanza mwezi Agosti 1980, kusoma katika chuo kikuu cha Wisconsin-Madison, nikitokea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo nilikuwa nafundisha. Wakati ul

Ubora wa huduma: msingi wa mafanikio

Ni muhimu kuelewa misingi ya mafanikio katika dunia ya leo, yenye ushindani mkubwa. Ushindani huu uko ndani ya nchi na kimataifa. Wapende wasipende, wafanya biashara na watoa huduma mbali mbali wanajikuta katika mazingira ya mashindano ambayo yanaongezeka kwa kasi na yanazidi kuwa magumu. Katika hali hii, ni muhimu kwa kila mhusika kujua siri za mafanikio. Siri mmoja ni ubora wa huduma. Kuna usemi kuwa mteja ni mfalme. Nimeona sehemu mbali mbali duniani ambapo dhana hii inazingatiwa sana. Wako watu wanaofahamu vema umuhimu wa mteja. Wawe ni wafanyabiashara au watoa huduma, wanaonyesha kumjali sana mteja. Hata kama mteja ni msumbufu wafanyabiashara na watoa huduma hao wako tayari kumsikiliza, kumvumilia na kumsaidia hadi aridhike. Sio rahisi kuwaona wafanyabiashara au watoa huduma hao wakimkasirikia mteja. Hapa Marekani, kwa mfano, mteja anaponunua kitu, anapewa risiti, na kama hataridhika na kitu alichonunua, ana uhuru wa kukirudisha na kurudishiwa hela yake, au kubadilisha alichonun