Makala hii imechapishwa katika KWANZA JAMII, Oktoba 13-19, 2009 Profesa Joseph L. Mbele Imetimia miaka kumi tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alipofariki London, Oktoba 14, 1999. Ni jambo jema kutumia muda huu kumkumbuka kwa namna ya pekee, kwa mchango wake kwa Tanganyika (na baadaye Tanzania), Afrika na dunia kwa ujumla. Ni vizuri pia kutumia muda huu kutafakari mwenendo wa nchi yetu, tukilinganisha na makusudio aliyokuwa nayo Mwalimu wakati wa uhai wake. Mchango wa Mwalimu katika harakati za kupigania Uhuru wa Tanganyika unatambulika. Akishirikiana na viongozi wengine wa sehemu mbali mbali za nchi, wa dini na rangi mbali mbali, na wananchi kwa ujumla, Mwalimu Nyerere aliongoza Tanganyika kufikia Uhuru, Desemba 9, 1961. Hapo alitoa hotuba ambayo maneno yake ni vigumu kusahaulika, kwa jinsi yalivyoelezea kwa ufasaha hisia na matumaini ya Taifa letu changa. Mwalimu alisema, “Sisi tunataka kuwasha mwenge, na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, ili umulike hata nje ya mipaka yetu,