Posts

Showing posts from January, 2014

Andikeni Vitabu Vyenu, Viwe Bora na Maarufu Kuliko Changu

Nawashauri akina anonymous wanaokikejeli kitabu changu wakati hata hawajakisoma waandike vitabu vya mada ile ile tuone kama wataweza. Vinginevyo hao ni wapumbavu. Halafu, hakuna chuo kikuu kinachoweza kumtuza mtu cheo cha uprofesa kwa kuandika kitabu kama changu. Sio kitabu cha kitaaluma. Nimeshasema hayo tena na  tena katika blogu hii.

Wiki Mbili Zijazo Kitabu Hiki Kinatimiza Miaka Tisa Tangu Kichapishwe

Image
Wiki mbili tu kuanzia sasa, kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kitatimiza miaka tisa tangu kichapishwe. Sitaiacha siku hiyo ipite hivi hivi. Nawazia nini cha kufanya. Labda nitaandika ripoti kadhaa juu ya mafanikio yake. Kitabu hiki sikukiandika kwa ajili ya kujipatia pesa, ingawa kimeniletea pesa, tena sio chache. Lengo langu na mafanikio yangu makubwa yamekuwa katika kuwagusa na kuwasaidia watu. Katika hilo najivunia kazi ngumu niliyofanya katika utafiti na uandishi wake. Wako wachache ambao wamekuwa wakiniletea kejeli. Hao nawaona kama watu wasio na akili timamu. Kinachoudhi ni kuwa watu hao wanaongelea kitabu ambacho hawajakisoma. Sitaweza kuleta maoni ya wote waliokisoma wakanipa maoni yao. Hao ni watu makini. Nawashukuru.

Vitabu Ulivyonunua au Kusoma Mwaka 2013

Mwaka ni muda mrefu. Hata mwezi ni muda mrefu. Tafakari uliutumiaje mwaka 2013. Uliitumia fursa ile kwa kujiendeleza? Ulijiongezea ujuzi na maarifa katika fani yoyote? Ulisoma vitabu? Kama una watoto, uliwanunulia vitabu? Kama hukufanya hivyo, wewe una matatizo, wala usijidanganye. Kama wewe ni mnywaji wa bia, unadhani ulitumia fedha kiasi gani kwa unywaji huo, kwa wiki, mwezi au kwa mwaka? Utasema hukuwa na hela ya kununulia vitabu? Kuna maktaba katika miji mingi, wilayani na mikoani. Baadhi nimezitembelea na kuandika ripoti zake katika blogu zangu, miji kama Lushoto, Mbulu, Karatu, Dar es Salaam, Mbinga, Moshi, Iringa na Songea. Je, mwaka 2013 uliingia humo? Mara ngapi, na ulisoma vitabu vipi?

MUFTI SIMBA AWATAKA WAISLAMU KUACHA KULALAMIKA

Tuesday, January 14, 2014 MUFTI AWATAKA WAISLAMU KUACHA KULALAMIKA SHEKHE Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban Simba, ametaka Waislamu kuacha kulalamika, kwamba Wakristo wamekuwa wakipewa upendeleo, badala yake watumie fursa wanazopata kuondokana na malalamiko hayo. Akizungumza katika maadhimisho ya Maulidi ya Kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW), yaliyofanyika kitaifa mkoani Kigoma jana, Mufti Simba alisema chanzo cha malalamiko hayo ni Waislamu kushindwa kujitolea katika mambo mbalimbali ya maendeleo. Akitoa mfano, alisema Waislamu wanapaswa kupeleka watoto wao kusoma elimu zote mbili na kuwaandaa kushika nafasi za kiutendaji ambazo wanalalamikia kuwa zimetolewa kwa upendeleo kwa Wakristo. Alisema hata katika kukamata maeneo ya uwekezaji, Waislamu wamebaki nyuma kutokana na kushindwa kujitolea kuchangia fedha za kutosha za kuanzisha miradi ya maendeleo kwa ajili ya kuimarisha dini na kuendesha maisha yao.  “Msilalamike, tunisheni mifuko katika misikitini yenu muwe na fedha za kuto

Zawadi Nyingine Ya Krismasi: "Robert Frost: Selected Poems"

Image
Krismasi iliyopita, tulipeana zawadi, katika familia na marafiki, kama ilivyo jadi. Kati ya zawadi alizonipa binti yangu aitwaye Zawadi ni kitabu, Robert Frost: Selected Poems . Watoto wangu wanajua tangu zamani ninavyopenda vitabu. Sina hakika kama kitabu hicho ninacho kati ya vitabu vyangu, ambavyo vinazidi elfu tatu, vingine vikiwa Tanzania na vingine hapa Marekani. Lakini ameninunulia toleo jipya, lililochapishwa na Fall River Press mwaka 2011. Robert Frost ni moja kati ya washairi maarufu Marekani na duniani. Wajuzi wa fasihi ya ki-Ingereza wanafahamu, kwa mfano, shairi moja maarufu la Robert Frost, "The Road Not Taken," ambalo hata sisi tulipokuwa wanafunzi wa "high school" Tanzania, miaka ya mwanzoni ya sabini na kitu tulilisoma na kulitafakari. Kama nakumbuka vizuri, shairi hili ndilo lilitutambulisha ushairi wa Robert Frost. Robert Frost: Selected Poems ni mkusanyiko wa mashairi mengi, na mengi yanaongelea hali ya kaskazini mashariki ya Marek

Yule Mama Kutoka Togo Kaja Mara ya Tatu Kununua Vitabu

Yule mama kutoka Togo, ambaye nimemtaja mara kadhaa katika blogu hii, kaja tena leo. Amenunua nakala sita za kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Amesema ni kwa ajili ya mabosi kazini kwake, kuwasaidia kufahamu namna ya kuhusiana na wa-Afrika.  Nakala nilizokuwa nazo zimeisha sasa. Imebaki moja tu. Watu siku hizi, hasa hapa Marekani, hununua vitabu mtandaoni. Tekinolojia imepiga hatua. Sio kama zamani, ambapo mwandishi alikuwa na shehena ya vitabu vyake nyumbani, na watu wakawa wanavipata kwake. Mimi mwenyewe huwa na nakala kiasi tu, kwa ajili ya matamasha ya vitabu ninayoshiriki, ambayo nayaelezea katika blogu hii mara kwa mara.  Lakini, hata hapa Marekani kuna watu wanaosita kununua vitu mtandaoni, wakihofia usalama wa "credit card" zao. Hao ni baadhi ya wale wanaomwendea mwandishi, au wanakwenda kwenye maduka ya vitabu kama tulivyozoea.  Kutokana na kuishiwa nakala zangu, leo hii nimeagiza nakala 20 huko mtandaoni www.lulu.com/content

Mdau, Rafiki Yangu

Image
Nina furaha kuongelea habari za huyu bwana tunayeonekana pamoja pichani. Ni mfanyakaxi mwenzangu hapa chuoni St. Olaf. Yeye ni mfanya usafi katika hilo jengo tulimo, lijulikanalo kama Buntrock Commons. Miezi mingi iliyopita, kabla hatujazoeana, aliniita wakati napita katika jengo hili, akanionyesha nakala ya kitabu changu cha Matengo Folktales , ambacho alikuwa amekinunua. Alionekana mwenye furaha kuwa na kitabu hicho. Kadiri siku zilvyopita, tukiwa tunaongea, nilipata kufahamu kuwa yeye ni kati ya wale wenye dukuduku na hamu ya kufahamu kuhusu Afrika. Siku nyingine aliniambia kwa furaha kuwa kijana wake anatarajia kwenda Afrika. Na kweli, miezi ya baadaye aliniambia kijana alishaenda Kenya na Tanzania, akapanda mlima Kilimanjaro. Katika maongezi yetu ya siku za karibuni, nilimwambia kuwa kwa vile anacho kitabu changu cha Matengo Folktales , nitafurahi kumpa kingine tofauti ambacho nilikichapisha baadaye. Basi, jana tulikutana, nikampa nakala ya Africans and Americans ambayo

Huenda Nitaenda Iringa Mwaka Huu Kufuatilia Habari za Hemingway

Nafanya mipango ya kwenda Iringa kufuatilia habari za mwandishi Hemingway. Pamoja na kuishi na kuzunguka Afrika Mashariki, miaka ya 1933-34 na 1953-54, alitumia muda mwingi Tanganyika. Kumbe, alitumia wiki kadhaa Iringa ule mwaka 1954.  Habari hii ni ya kusisimua, kwa mtafiti. Mwanae, Mzee Patrick Hemingway anayeishi Montana, amekuwa akinipa taarifa na dokezo muhimu. Safari kama hii, na kukaa Tanzania wiki tatu nne, itagharimu dola zisizopungua 4000. Lakini chuo changu kimeomyesha kiko tayari kugharamia.  Utafiti wa aina hii ni muhimu sana. Mbali na umuhimu wake kitaaluma,faida mmoja ni kuwavutia watalii. Laiti kama wa-Tanzania wagekuwa watu wanaothamini na kusoma vitabu. Tungeshirikiana vizuri.

Mama Kutoka Togo Kaja Tena Kununua Kitabu

Jana jioni, yule Mama kutoka Togo, ambaye nilimwelezea siku chache zilizopita, alifika tena hapa kwangu, akanunua nakala nyingine ya kitabu cha Africans and Americans . Alisema ni kwa ajili ya marafiki zake, Mark na Carol, wa-Marekani. Aliniomba nisaini, nami nikafanya hivyo.  Kama kawaida, huwa naandika taarifa za aina hiyo katika blogu hii, tangu zamani. Ni kumbukumbu zangu.  Nilipata taabu sana kuandika kitabu hiki, ingawa kinaonekana kidogo. Nilihangaika nacho kwa miezi mingi. Miezi sita ya mwisho ya mwaka 2004 nilikuwa katika likizo iitwayo "sabbatical." Nilitumia fursa hii kushughulikia mswada wangu. Nilikuwa natumia masaa mengi karibu kila siku katika kazi hii. Nafarijika na kufurahi kuona matunda ya jasho langu. Siku za usoni, Mungu akipenda, nitaelezea taabu nilizopata na mbinu nilizotumia katika kufanikisha uandishi wake.