Posts

Showing posts from September, 2016

M-Kenya Kaniandikia Kuhusu Kitabu Changu

Image
Nimefurahi sana, tangu usiku wa kuamkia leo, kupata maoni ya msomaji wa kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Msomaji huyu ni mama m-Kenya ambaye anaishi hapa Minnesota, Marekani. Aliniandikia katika Facebook ujumbe huu: I did not tell you how precious your book is. My friend and I were reading it to our kids during a sleep over and it is amazing how your culture is similar to ours. You did well and it was very easy to understand and flow with. You are gifted Mwalimu. God bless you more. Thank you again for the great gift. Huyu mama tulikutana tarehe 30 Aprili, mwaka huu, kwenye tamasha mjini Rochester. Alikuja kwenye meza yangu, tukasalimiana na kuongea. Alivutiwa na kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , akaulizia namna ya kukipata siku nyingine, kwa kuwa hakuja na hela. Hapo hapo nilimpa nakala ya bure. Alishangaa, akashukuru sana. Nimefurahi kuwa ameniandikia maoni yake kuhusu kitabu hicho. Ninamfananis

Darasa ni Popote

Image
Tangu nilipokuwa mdogo, nilikuwa nataka kuwa mwalimu. Mungu si Athmani, ndoto yangu ilitimia. Ninafurahia kazi yangu na ninaifanya kwa dhati na kwa uadilifu. Ninaona raha kuwa na wanafunzi katika kutafakari masuala. Zaidi ya kufundisha darasani katika jengo, ninapenda kushiriki matamasha. Matamasha hayo ni kama shule, fursa ya kuongea na watu juu ya shughuli zangu, kama vile utafiti na uandishi. Uandishi ninauchukulia kama aina ya ufundishaji. Ni ufundishaji usio na mipaka, kwani maandishi yanakwenda popote, iwe ni vitabu halisi au vitabu pepe, iwe ni makala katika majarida au mtandaoni,  zote hizo ni njia za kuniwezesha kufundisha bila mipaka. Ninafurahi kuwa nimejiingiza katika uwanja wa blogu. Blogu ni kumbi zinazonipa fursa ya kueneza mawazo yangu, ingawa kwa ufupi. Mara kwa mara ninaongelea vitabu na kutoa dondoo za kiuchambuzi zinazoweza kumpa mtu fununu ya mambo muhimu yaliyomo katika vitabu hivyo. Blogu zangu zinatoa fursa kwa watu kuchangia mawazo na mitazamo. Ninaendes

David Robinson Ahutubia Chuo Kikuu cha Minnesota

Image
Leo mchana nilikwenda Chuo Kikuu cha Minnesota , Minneapolis, kumsikiliza David Robinson, m-Marekani Mweusi anayeishi Mbeya, Tanzania, ambako ni mkulima wa kahawa. Huyu ni mtoto wa mwisho wa mwanariadha maarufu sana wa Marekani, Jackie Robinson, ambaye alikuwa pia mpinzani shujaa wa ubaguzi na mtetezi wa haki za wa-Marekani Weusi. David Robinson aliamua kwenda kuishi Tanzania, kwenye kijiji cha Bara wilaya ya Mbozi. Alijitambulisha kwa wanakijiji akajieleza kuwa ni mtoto wa Afrika aliyepotezewa ughaibuni kwa karne kadhaa, katika utumwa, na sasa ameamua kurudi nyumbani. Wanakijiji walimpa shamba akaanza kulima kahawa. Aliungana na wanakijiji wengine, wakaanzisha chama cha ushirika kiitwacho Sweet Unity Farms Aliongelea shughuli za chama chao cha ushirika, wanavyoshughulikia matatizo na changamoto na kujifunza. Alielezea mahusiano yao na wateja wa nchi mbali mbali, ikiwemo Marekani. Ingawa wao wako kijijini, wanashiriki katika uchumi wa ulimwengu, na ndio hali halisi ya utandawazi. D

"The Dilemma of a Ghost:" Tamthilia ya Ama Ata Aidoo

Image
The Dilemma of a Ghost ni tamthilia ya kwanza ya Ama Ata Aidoo wa Ghana. Aliitunga alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Ghana, Legon, ikaonyeshwa mara ya kwanza mwaka 1964, na kuchapishwa mwaka 1965. Ama Ata Aidoo aliendelea kuandika na bado anaandika, na kazi zake ni pamoja na tamthilia nyingine iitwayo Anowa, ambayo ilichapishwa mwaka 1970, hadithi fupi, na riwaya kadhaa. The Dilemma of a Ghost inaongelea juu ya kijana wa Ghana aitwaye Ato aliyekwenda masomoni Marekani na huko akakutana na Eulalie, binti Mwamerika Mweusi. Huyu ni kati ya wale wa-Marekani Weusi wanaoiwazia Afrika kwa hamu kama mtu aliyeko ugenini anavyowazia nyumbani kwake. Ato na Eulalie wanaoana na kurejea Ghana, ambako wanakumbana na mambo magumu. Kwanza ndugu zake Ato wanashtuka kusikia kuwa Ato ameoa bila kuwashirikisha. Halafu binti mwenyewe hana kabila wanalolitambua, na hata jina lake wanashindwa kulitamka, na kibaya zaidi, kwa mtazamo wao, ni kuwa binti huyo ni kizalia cha watumwa. Wanaukoo wan

Jionee Ukakamavu wa UVCCM

Image
CCM ina kila sababu ya kujivunia vijana wake, yaani UVCCM. Sio tu ni vijana wanaozingatia wajibu wao wa kutetea na kutekeleza ajenda za serikali ya CCM, kama wanavyotamka katika tovuti yao, bali ni wakakamavu, ambao wako tayari kwa lolote. Hapa naleta picha kadhaa kuthibitisha jambo hilo, nikizingatia usemi wa ki-Ingereza kwamba "a picture is worth a thousand words," yaani picha ina thamani sawa na maneno elfu. Jionee mwenyewe uwajibikaji na utendaji wa hao vijana. Kwenye masuala ya itikadi, vijana hao wako mstari wa mbele pia. Angalia hilo bango walilobeba katika maandamano yao huko Visiwani. Kama hizi picha hazitoshi kukushawishi, basi angalia video hii hapa chini. Kwa kweli, CCM ina kila sababu ya kujivunia vijana wake.

Ujumbe kwa Ndugu na Marafiki

Image
Napenda kuwajulisha ndugu na marafiki kuwa leo tumemaliza wiki ya kwanza ya muhula mpya wa masomo hapa chuoni St. Olaf. Nimeanza vizuri, kama nilivyogusia katika blogu hii, kwa ari kubwa. Wanafunzi wanaonekana wenye ari ya kujifunza. Sitawaangusha. Tarehe 17 mwezi uliopita ilikuwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu. Nilitimiza miaka 65 ya maisha yangu. Ninavyoingia mwaka wa 66, ninamshukuru Mungu kwa kuniweka hai na mwenye uwezo wa kutekeleza majukumu yangu kama nilivyozoea. Uhai na afya ni baraka kutoka kwa Mungu. Nitaendelea kutumia fursa hii, ambayo ni dhamana, kwa kufanya kazi zangu za kufundisha kwa juhudi yote na uadilifu, kusoma kwa bidii, na kuandika ili kuuneemesha ulimwengu kwa elimu. Nawaombeni ndugu na marafiki mniombee ili nizingatie mwelekeo huo, nami nawaombea baraka na mafanikio.

Utangazaji wa Vitabu

Image
Mara kwa mara, katika blogu hii, ninaandika kuhusu vitabu. Ninaongelea masuala kama uandishi wa vitabu, uchapishaji, na uuzaji. Mara kwa mara ninaviongelea vitabu kwa namna ya kuvitambulisha kwa wasomaji wa blogu hii, na pia kujiwekea kumbukumbu. Ninafurahi ninapopata taarifa kutoka kwa wasomaji wa blogu hii kuwa wamefuatilia taarifa zangu na kuvisoma vitabu nilivyoviongelea. Ujumbe wa leo ninauelekeza kwa waandishi wa vitabu. Kama ilivyo desturi yangu, maelezo yangu yanatokana na uzoefu wangu kama mwandishi. Ujumbe wa leo ni mwendelezo wa yale ambayo nimewahi kuandika katika blogu hii. Katika kutafiti suala hili la utangazaji wa vitabu, nimejifunza kuwa, kwa mwandishi, kuandika na kuchapisha kitabu si mwisho wa safari. Nimejifunza kutoka kwa waandishi na wachapishaji kwamba kwa namna moja au nyingine, mwandishi analo jukumu la kukitangaza kitabu chake. Inaweza kutokea kwamba mchapishaji ana uwezo mkubwa wa kutangaza kitabu. Ana bajeti kubwa au mfumo wa kusambazia matangazo. Lak

Umuhimu wa Kusoma Vitabu

Image
Kusoma vitabu kuna manufaa mengi kwa mtu binafsi na kwa jamii. Tunaweza kuitafakari kauli hii kwa namna nyingi. Binafsi, daima ninakumbuka usemi wa Ernest Hemingway, "There is no friend more loyal than a book," yaani hakuna rafiki wa kweli kuzidi kitabu. Ni kauli fupi na rahisi kukumbukwa, lakini ninaiona kuwa yenye ukweli kabisa. Kitabu ni rafiki ambaye yuko kwa ajili yako muda wowote unapomhitaji. Kitabu kinaweza kuwa mshauri wako, kiongozi wako, nguzo ya kuitegemea. Akili ya binadamu inahitaji matunzo, sawa na bustani. Bustani inahitaji kurutubishwa na kupaliliwa. Ikiachwa ivamiwe na magugu, inageuka kichaka. Kusoma vitabu ni kurutubisha akili na kuipalilia. Kama mtu anaweza, ni muhimu kusoma vitabu vya aina mbali mbali: vya siasa, saikolojia, fasihi, sayansi, maisha ya watu maarufu, falsafa, historia, uchumi, na kadhalika. Ni makosa kudhani kuwa kusoma vitabu kunawahusu wanafunzi na waalimu pekee. Kila mtu anapaswa kusoma vitabu. Tutafakari manufaa yake kwa afya ya a

Mashairi Mawili ya Edmund Spencer

Image
Edmund Spencer ni mmoja kati ya washairi maarufu kabisa katika ki-Ingereza. Alizaliwa London mwaka 1552, akafariki 1599. Ni sahihi kusema kwamba shairi maarufu kabisa la Edmund Spencer ni utenzi uitwao "The Faerie Queene." Lakini Edmund Spencer ni maarufu pia kwa utunzi wa mashairi ya muundo wa "sonnet." Mwanatamthilia Shakespeare, ambaye alizaliwa mwaka 1564 na kufariki mwaka 1616, naye alikuwa mtunzi maarufu wa "sonnet." Hapa naleta "sonnet" mbili za Edmund Spencer ambazo zinabainisha sanaa ya mshairi huyu. Ki-Ingereza cha mashairi haya ni cha zama zile, lakini ukikisoma kwa utulivu na umakini, utakielewa. Katika "Ye Tradefull Merchants," mshairi anawasuta wafanya biashara wanaosafiri mbali kutafuta utajiri. Anawaambia kuwa mpenzi wake ana utajiri wa uzuri kuliko hata vito wanavyovihangaikia hao wafanya biashara. Utajiri wa mpenzi huyo si tu wa kimaumbile, bali pia akili. Katika "Trust Not the Treason," mshairi anatahad

Nimeanza Kufundisha Leo

Jana tumeanza muhula mpya wa masomo hapa chuoni St. Olaf, nami nimeanza kufundisha leo. Masomo yangu kwa muhula huu ni matatu: First Year Writing, African Literature, na Muslim Women Writers. Tumeanza vizuri. Nimepata fursa ya kuwaeleza wanafunzi mambo ya msingi kuhusu falsafa yangu ya ufundishaji, na kuhusu masomo. Nimesisitiza wajibu wa kufikiri na kuchambua masuala, wajibu wa kujenga hoja. Nimesisitiza msimamo wangu wa kulinda na kutetea uhuru wa fikra na kujieleza. Nimewahahakishia wanafunzi kuwa wawe tayari kukabiliana na fikra na hoja mbali mbali. Siku ya kwanza ya muhula ni kama kitendawili. Hatujui safari itakuwaje, siku hadi siku, lakini tunategemea matokeo mema. Ingawa uzoefu wangu wa kufundisha unaendelea kuongezeka muda wote, haiwezekani kupanga na kuwa na uhakika nini kitatokea. Jambo pekee lisilobadilika ni kwamba kila muhula ni tofauti na mwingine.

Wasomaji Wangu Wa Nebraska Waendao Tanzania

Image
Nina jadi ya kuwaongelea wasomaji wangu katika blogu hii, kama njia ya kuwaenzi. Ni jambo jema kwa mwandishi kufanya hivyo. Leo ninapenda kuwakumbuka wasomaji wangu wa sinodi ya Nebraska ya Kanisa la Kiluteri la Marekani, ambao tangu zamani wamekuwa na programu ya kupeleka watu Tanzania kuendeleza uhusiano baina yao na wa-Luteri wa Tanzania. Hao wasafiri, sawa na wenzao wa sinodi zingine za Marekani, wamekuwa wakitumia kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences katika kujiandaa kwa safari, ili kuzielewa tofauti za tamaduni za Marekani na Afrika. Ni elimu muhimu katika ulimwengu wa utandawazi wa leo, ambayo nje ya ufundishaji wa darasani, ninashughulika nayo. Wakati huu ninapoandika, waumini wa Nebraska wanajiandaa kwa safari ya Tanzania, ambayo itafanyika mwezi Februari mwaka 2017. Wameitangaza safari hii mtandaoni, na mratibu mojawapo wa safari, Martin Malley, ameniandikia ujumbe leo akisema, "We still recommend your book." Katika ukurasa

Tamko la ACT-Wazalendo Kuhusu Hali ya Nchi

Tamko Rasmi la Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo kuhusu HALI YA NCHI Dar Es Salaam, Jumanne, 06 Septemba 2016 Utangulizi Jana Jumatatu, 5 Septemba 2016, Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo ilikutana katika kikao chake cha kawaida. Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ilipokea, kujadili na kuidhinisha Taarifa kuhusu HALI YA NCHI. Taarifa hii sasa inatolewa rasmi kwa umma. Taarifa ipo katika maeneo makubwa manne: Hali ya kisiasa, hali ya kiuchumi, umoja wa kitaifa na hitimisho. Hali ya Kisiasa Kamati Kuu imezingatia kuwa Kikatiba, nchi yetu inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Katiba na Sheria mbalimbali zimeanisha utaratibu wa kazi na shughuli za vyama vya siasa. Ili kuhakikisha kwamba kazi na shughuli za vyama vya siasa zinakuwa endelevu, vyama vyenye kukidhi vigezo hupewa ruzuku kupitia Bajeti ya Serikali inayopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania. Hata hivyo, katika awamu hii ya tano, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeamua kuzuia shughuli za si

Naomba Kitabu Changu Kipigwe Marufuku

Image
Naiomba serikali ikipige marufuku kitabu changu, CHANGAMOTO: Insha za Jamii . Kitabu hiki kina mawazo ambayo ni kinyume na yale yanayotakiwa na serikali. Kama vile hii haitoshi, kitabu hiki ni cha uchochezi. Tusikubali kurudia makosa kama yale ya kale ambapo Socrates alikuwa anawachochea watu, hasa vijana, wahoji mambo yanayokubalika katika jamii. Imenibidi nitoe ombi hili la kupigwa marufuku kitabu changu kwa sababu za msingi. Kwanza kama mtu mwingine yeyote mtiifu kwa serikali, ninatambua wajibu wangu wa kuripoti jambo lolote linalokwenda kinyume na maelekezo au matakwa ya serikali. Pili, mimi sina mamlaka kisheria ya kukipiga marufuku kitabu chochote. Kwa hivi, ninaiangukia serikali. Mawazo yaliyomo katika kitabu hiki yasipodhibitiwa, yakiachwa yaenee, yatajenga ukaidi miongoni mwa raia na tabia ya kutowaheshimu viongozi. Ninaelewa kuwa ni juu ya serikali kufikiri na kufanya maamuzi. Wajibu wa raia ni kutii. Raia wakiachwa huru kufikiri na kujiamulia mambo, kuna hatari kwamb

Shakespeare Ametawala Mawazo Yangu Leo

Image
Leo Shakespeare ametawala mawazo yangu, nami ninapenda kuelezea ilivyotokea. Ni maelezo yanayoweza kubainisha namna akili yangu inavyofanya kazi ninapohangaika kuandika makala ya kitaaluma. Kwa miezi kadhaa, nimekuwa nikiwazia kuandika makala juu ya utangulizi wa  The Dilemma of a Ghost , tamthilia ya Ama Ata Aidoo wa Ghana. Utangulizi huu umeitwa "Prelude" katika tamthilia hiyo, ambayo Ama Ata Aidoo aliitunga alipokuwa mwanafunzi wa chuo kikuu Ghana, Legon, ambapo alihitimu mwaka 1963. Tamthilia yake iliigizwa kwa mara ya kwanza mwaka 1964 na kuchapishwa mwaka 1965. Nimefundisha tamthilia hii mara kadhaa, na kwa miezi kadhaa nimepata hamu ya kuchambua utangulizi wake, yaani "Prelude." Nimeona kwamba hakuna mhakiki yeyote ambaye ameichambua sehemu hii ya tamthilia hii kwa kiwango kinachoniridhisha. Hii "Prelude" si rahisi kuifafanua. Ninahisi hii ndio sababu ya wachambuzi kuiacha kando. Katika kuitafakari hii "Prelude," nimeona kuwa ujuzi