Tuesday, September 13, 2016

Utangazaji wa Vitabu

Mara kwa mara, katika blogu hii, ninaandika kuhusu vitabu. Ninaongelea masuala kama uandishi wa vitabu, uchapishaji, na uuzaji. Mara kwa mara ninaviongelea vitabu kwa namna ya kuvitambulisha kwa wasomaji wa blogu hii, na pia kujiwekea kumbukumbu. Ninafurahi ninapopata taarifa kutoka kwa wasomaji wa blogu hii kuwa wamefuatilia taarifa zangu na kuvisoma vitabu nilivyoviongelea.

Ujumbe wa leo ninauelekeza kwa waandishi wa vitabu. Kama ilivyo desturi yangu, maelezo yangu yanatokana na uzoefu wangu kama mwandishi. Ujumbe wa leo ni mwendelezo wa yale ambayo nimewahi kuandika katika blogu hii.

Katika kutafiti suala hili la utangazaji wa vitabu, nimejifunza kuwa, kwa mwandishi, kuandika na kuchapisha kitabu si mwisho wa safari. Nimejifunza kutoka kwa waandishi na wachapishaji kwamba kwa namna moja au nyingine, mwandishi analo jukumu la kukitangaza kitabu chake.

Inaweza kutokea kwamba mchapishaji ana uwezo mkubwa wa kutangaza kitabu. Ana bajeti kubwa au mfumo wa kusambazia matangazo. Lakini, wachapishaji wengi hawana uwezo huo, au uwezo wao ni hafifu, na hivyo kumlazimu mwandishi abebe jukumu la kutangaza kitabu chake.

Hata kama mchapishaji ana uwezo mkubwa, mwandishi anayo pia nafasi ya kuchangia katika kukitangaza kitabu. Kwa hapa Marekani, jadi iliyojengeka ni kwa mwandishi kwenda sehemu mbali mbali kukitambulisha kitabu chake. Sehemu hizo zinaweza kuwa vyuo, maktaba, au maduka ya vitabu.

Ziara hizo, ambazo kwa ki-Ingereza huitwa "book tours," ni muhimu sana. Ratiba ya ziara hutangazwa kwenye vyombo vya habari mapema. Sehemu ambapo mwandishi ametegemewa kuja kuzungumzia kitabu, kama vile maktaba au duka la vitabu, panakuwa na matangazo pia. Wateja wanaofika hapo wanayaona matangazo hayo.

Kwa kuwa usomaji wa vitabu umejengeka katika utamaduni wa Marekani, ziara ya mwandishi huwavutia watu. Wakati mwandishi anapokuja, zinakuwepo nakala za kutosha za kitabu chake, ili watu wanaohudhuria waweze kununua nakala na kusainiwa na mwandishi.

Watu hapa Marekani wanapenda kusainiwa vitabu, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii. Mimi mwenyewe nimealikwa sehemu mbali mbali hapa Marekani kwenda kuongelea vitabu vyangu, hasa Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Njia nyingine muhimu kwa mwandishi kutangaza vitabu vyake ni kushiriki maonesho ya vitabu. Hapa Marekani kuna maonesho ya vitabu mara kwa mara, kwenye maeneo mbali mbali ya nchi. Mengine huwa ni ya sehemu fulani ya nchi, na mengine huwa ni ya kitaifa. Nimeshiriki maonesho haya mara kwa mara, na nimekuwa nikiandika taarifa katika blogu hii na pia blogu ya ki-Ingereza.

Mwandishi anaweza kulipia matangazo katika vyombo vya habari. Lakini kutokana na uzoefu wangu, ninasita kupendekeza utangazaji wa aina hii. Ni bora mwandishi atumie njia zisizo na gharama. Kwa mfano, mwandishi anaweza kupeleka nakala za kitabu chake kwa wahakiki, ili wasome na kuandika uchambuzi katika magazeti.

Vile vile, tuzingatie kuwa tunaishi katika dunia ya mitandao, ambayo imeleta fursa nyingi. Kwa mwandishi mwenye blogu au tovuti, ni rahisi kutangaza kitabu chake. Mimi mwenyewe ninafanya hivyo katika blogu zangu na katika tovuti ya Africonexion. Vile vile tekinolojia za uchapishaji zinatuwezesha kuchapisha moja kwa moja mtandaoni, na vitabu vikapatikana huko, kama ilivyo kwa vitabu vyangu.

Hata hivyo kuna aina ya utangazaji ambayo huenda ni muhimu kuliko zote. Hii ni aina ya utangazaji unaofanywa na wasomaji. Kama ilivyo katika biashara yoyote, wateja ni watangazaji wakuu. Mteja akiridhika au kufurahi, anakuwa mpiga debe mkuu wa bidhaa au huduma.

Sisi wote tunafanya utangazaji wa bidhaa na huduma. Tukiona filamu nzuri, tunawaambia wenzetu. Tukinunua simu bora, tunawaambia wenzetu. Tukiwa katika mji mgeni, tukataka kujua nyumba bora ya kufikia wageni, au hoteli nzuri, wenyeji au madreva wa teksi watatuelekeza. Tunafanya kibarua cha kutangaza bidhaa za watu bila malipo.

Na vitabu ni hivi hivi. Msomaji akishasoma kitabu akakipenda, hakosi kuwaambia wengine. Hivi ndivyo kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kilivyoenea kwa kasi hapa Marekani. Baadhi ya wasomaji wangu ambao wamekuwa wapiga debe wangu nimekuwa nikiandika habari zao katika blogu hii.

Utangazaji huu unaofanywa na wateja walioridhika au kufurahi unaaminika sana. Sisi sote tukiambiwa na marafiki au ndugu zetu kuhusu ubora wa bidhaa fulani au huduma fulani tunaamini bila kusita. Tunaweza kuwa na wasi wasi na matangazo yanayowekwa na watu tusiowajua katika vyombo vya habari. Huenda tunahisi kwamba wafanya biashara hawaangalii maslahi yetu bali yao wenyewe, na wako tayari hata kutuuzia bidhaa mbovu. Lakini tunajua kuwa marafiki au ndugu zetu wanazingatia maslahi yetu. Hii ndio sababu utangazaji unaofanywa na wateja una umuhimu sana.

Pamoja na yote niliyosema hapa juu, uamuzi wa kukitangaza kitabu unaweza kuwa na utata. Kwa upande moja, kitabu kikishachapishwa, kuna umuhimu wa kukijulisha kwa jamii. Kwa upande mwingine, kuna busara ya wahenga kuwa chema chajiuza; kibaya chajitembeza. Je, mwandishi afanyeje? Kwa mtazamo wangu, ni juu ya kila mwandishi kutafakari suala hili na kufanya uamuzi.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...