Tuesday, September 20, 2016

"The Dilemma of a Ghost:" Tamthilia ya Ama Ata Aidoo

The Dilemma of a Ghost ni tamthilia ya kwanza ya Ama Ata Aidoo wa Ghana. Aliitunga alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Ghana, Legon, ikaonyeshwa mara ya kwanza mwaka 1964, na kuchapishwa mwaka 1965. Ama Ata Aidoo aliendelea kuandika na bado anaandika, na kazi zake ni pamoja na tamthilia nyingine iitwayo Anowa, ambayo ilichapishwa mwaka 1970, hadithi fupi, na riwaya kadhaa.

The Dilemma of a Ghost inaongelea juu ya kijana wa Ghana aitwaye Ato aliyekwenda masomoni Marekani na huko akakutana na Eulalie, binti Mwamerika Mweusi. Huyu ni kati ya wale wa-Marekani Weusi wanaoiwazia Afrika kwa hamu kama mtu aliyeko ugenini anavyowazia nyumbani kwake.

Ato na Eulalie wanaoana na kurejea Ghana, ambako wanakumbana na mambo magumu. Kwanza ndugu zake Ato wanashtuka kusikia kuwa Ato ameoa bila kuwashirikisha. Halafu binti mwenyewe hana kabila wanalolitambua, na hata jina lake wanashindwa kulitamka, na kibaya zaidi, kwa mtazamo wao, ni kuwa binti huyo ni kizalia cha watumwa. Wanaukoo wanaona Ato amewasaliti.

Halafu, Eulalie naye anashindwa kuelewa na kufuata mila na desturi za hao ndugu. Wao wanamwona kama kizuka, kwa tabia zake, ikiwemo kukataa kunywesha dawa za kienyeji za kumwezesha kupata mimba. Mama mkwe wake, Esi Kom, anapofanya ukarimu wa kumletea konokono, ambao ni chakula cha heshima, Eulalie anashtuka, na haamini macho yake, na hatimaye anawatupilia mbali hao konokono. Jambo jingine linalowashangaza ndugu hao ni jinsi Eulalie anavyovuta sigara. Basi, inakuwa shida juu ya shida, na hatimaye binti anajikuta katika upweke na msongo wa mawazo.

Lakini, hatimaye, mama yake Ato anaridhia kumpokea huyu mkwe wake na anachukua hatua za kuwashawishi ndugu wote wampokee, kwa hoja kwamba mgeni hastahili kulaumiwa, bali mwenye lawama ni mwenyeji, yaani Ato. Ato anajikuta akiwa mpweke, aliyesongwa na mawazo, karibu kuchanganyikiwa. Ndivyo tamthilia inavyokwisha.

The Dilemma of a Ghost imejengeka katika mfumo wa hadithi za jadi ambazo huitwa "dilemma tales" ambao ni muundo unaowaacha wasikilizaji wakiwa na masuali yasiyojibika kirahisi. Katika tamthilia hii, suali moja muhimu ni nani wa kulaumiwa kwa matatizo yanayoibuka. Tamthilia hii inatumia pia aina nyingine za fasihi simulizi, kama vile nyimbo na methali. Vile vile kuna imani za jadi, kama vile juu ya mizimu na matambiko.

Ama Ata Aidoo ni mmoja wa waandishi wa ki-Afrika ambao ni hodari wa kutumia miundo na dhamira za masimulizi ya jadi. Hilo suala la kijana kujifanyia mwenyewe uamuzi wa kuoa au kuolewa bila kuwahusisha wazazi ni dhamira maarufu katika fasihi simulizi za Afrika, na matokeo ya kiburi hiki huwa si mema. Katika tamthilia ya Anowa, Ama Ata Aidoo ameiweka pia dhamira hiyo. Msichana Anowa anaamua kuolewa na kijana aliyemkuta bila wazazi kuhusika.

Tangu mwanzo, nilivutiwa na mtindo huu katika uandishi wa Ama Ata Aidoo, ambaye miaka ile alikuwa anajulikana kwa jina la Christina Ama Ata Aidoo. Ninakumbuka vizuri, kwa mfano, hadithi yake moja ya mwanzo kabisa iitwayo "In the Cutting of a Drink" ambayo niliisoma kwa mara ya kwanza miaka ya sitini na kitu, nilipokuwa mwanafunzi katika shule ya sekondari.

Nilivutiwa sana na hadithi hiyo kwa mtiririko wake sawa na wa mtambaji hadithi. Miaka ya baadaye, nilipojifunza somo la fasihi simulizi, nilianza kuelewa vizuri jinsi waandishi kama Ama Ata Aidoo wanavyotumia jadi hiyo.

Jambo muhimu sana jingine kuhusu Ama Ata Aidoo ni kuwa ni mwandishi mwenye kuchambua masuala ya jamii. Alivyokuwa anatunga The Dilemma of a Ghost, masuala kama ya mshikamano na mahusiano ya watu weusi ulimwenguni yaani "Pan-Africanism," yalikuwa yakivuma na kuwashughulisha viongozi maarufu kama George Padmore, W.B. Dubois, Kwame Nkrumah, Ahmed Sekou Toure, Jomo Kenyatta, na Julius Nyerere. Miaka iliyofuatia, Ama Ata Aidoo amekuwa akienda na wakati kama mwanaharakati katika masuala ya ukoloni mambo leo, haki za wanawake, na hata ujamaa. Sawa na ilivyokuwa kwa Mwalimu Julius Nyerere, Ama Ata Aidoo ni muumini wa fikra za kijamaa.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...