Saturday, September 3, 2016

Shakespeare Ametawala Mawazo Yangu Leo

Leo Shakespeare ametawala mawazo yangu, nami ninapenda kuelezea ilivyotokea. Ni maelezo yanayoweza kubainisha namna akili yangu inavyofanya kazi ninapohangaika kuandika makala ya kitaaluma.

Kwa miezi kadhaa, nimekuwa nikiwazia kuandika makala juu ya utangulizi wa The Dilemma of a Ghost, tamthilia ya Ama Ata Aidoo wa Ghana. Utangulizi huu umeitwa "Prelude" katika tamthilia hiyo, ambayo Ama Ata Aidoo aliitunga alipokuwa mwanafunzi wa chuo kikuu Ghana, Legon, ambapo alihitimu mwaka 1963. Tamthilia yake iliigizwa kwa mara ya kwanza mwaka 1964 na kuchapishwa mwaka 1965.

Nimefundisha tamthilia hii mara kadhaa, na kwa miezi kadhaa nimepata hamu ya kuchambua utangulizi wake, yaani "Prelude." Nimeona kwamba hakuna mhakiki yeyote ambaye ameichambua sehemu hii ya tamthilia hii kwa kiwango kinachoniridhisha. Hii "Prelude" si rahisi kuifafanua. Ninahisi hii ndio sababu ya wachambuzi kuiacha kando.

Katika kuitafakari hii "Prelude," nimeona kuwa ujuzi wangu wa taaluma ya "Folklore" utakuwa nyenzo muhimu. Vile vile, nimeona kuwa italazimu kugusia jadi ya tamthilia ya nchi za Magharibi kuanzia Ugriki ya zamani.

Ni katika kuwazia jadi hii ndio nikajikuta ninamkumbuka Shakespeare. Katika "Prelude" yake, Ama Ata Aidoo ametumia dondoo za lugha ambazo zinatupeleka kwa Shakespeare. Sishangai, nikizingatia kuwa Ama Ata Aidoo alisomea ki-Ingereza na fasihi katika mfumo wa elimu wa ukoloni wa ki-Ingereza. Kwa maana hiyo, Ama Ata Aidoo alilelewa katika mfumo ambao walilelewa waandishi wa enzi zake, na waliofuatia, kama vile Efua Sutherland, Wole Soyinka, na James Ngugi, ambaye baadaye alibadili jina na kujiita Ngugi wa Thion'go.

Baada ya kujiridhisha kwamba kuna athari za Shakespeare katika "Prelude" ya The Dilemma of a Ghost, ndipo nikawa nawazia kutafuta ushahidi katika tamthilia za Shakespeare. Kwa miezi yote hii, nilikuwa na uhakika kwamba baadhi ya athari zimetoka katika tamthilia kadhaa na pia mashairi ya Shakespeare, na baadhi ya athari nilihisi zilitokana na au tamthilia ya The Merchant of Venice au Hamlet.

Kwa hivi, leo nimeteremsha kabatini buku langu kubwa liitwalo The Yale Shakespeare, ambalo lina tamthilia zote za Shakespeare na mashairi yake yote. Kila tamthilia imetanguliwa na insha iliyoandikwa na mchambuzi mahiri na imeambatana na maelezo ya dhana, misemo na maneno ambayo watumiaji wa leo wa ki-Ingereza inaweza kuwawia vigumu kuelewa.

Kwa miezi kadhaa, kabla ya kuanza kufukuafukua maandishi ya Shakespeare leo, nimekuwa nikitafakari vipengele vya "Folklore" ambavyo ninavyoviona katika "Prelude." Pia nimekuwa nikitafiti zaidi vipengele hivyo, kwa kufuatilia maandishi ya wataalam kama William Bascom. Sina shaka kwamba tafakari hiyo na utafiti vitaniwezesha kuifafanua "Prelude" na matumizi ya "Folklore" katika tamthilia nzima ya The Dilemma of a Ghost.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...