Posts

Showing posts from May, 2015

Ualimu ni Wito

Image
Ualimu unahitaji moyo. Anayedhani ni mchezo, aiangalie na kuitafakari katuni hii. Bahati mbaya jina la mchoraji sijalipata, ningemshukuru.

Toleo Jipya la "Green Hills of Africa" Linaandaliwa

Image
Nilimpigia simu Mzee Patrick Hemingway tarehe 22 mwezi huu, tukaongea kwa saa moja na robo. Tuliongelea mambo mengi, kama nilivyogusia katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Mzee Patrick Hemingway ni mtoto pekee aliyebaki wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway. Mwandishi huyu ni wa pekee, sio tu kwa kuwa alishinda tuzo ya Nobel, bali pia kwa kuwa mtindo wake wa kuandika ulichangia kubadilisha uandishi wa ki-Ingereza wa karne iliyopita. Katika mfumo wa elimu wa Tanzania wa miaka ya sitini na kitu na sabini na kitu, wanafunzi tulikuwa tunasoma angalau kitabu kimoja cha Ernest Hemingway, For Whom the Bell Tolls, sambamba na vitabu vingine maarufu vya waandishi mbali mbali. Katika mazungumzo yetu, Mzee Patrick Hemingway aliniarifu kuwa toleo jipya la kitabu cha Green Hills of Africa litachapishwa miezi ya karibuni. Nilifurahi kusikia habari hii. Green Hills of Africa ni masimulizi ya Ernest Hemingway juu ya safari aliyofanya nchini Tanganyika, mwaka 1933-34. Nilisisimka Mzee Hemingway

Mwaliko Chuo Kikuu cha Winona

Image
Nimepata mwaliko kutoka Chuo Kikuu cha Winona, Minnesota, kwenda kutoa mhadhara tarehe 23 Juni. Huu utakuwa ni mchango wangu katika semina ya mafunzo kwa wanafunzi kutoka sehemu mbali mbali itakayofanyika Juni 17-27. Kama ilivyo kawaida yangu, nimeona niweke kumbukumbu hapa. Mafunzo haya yatalenga kuwaandaa wanafunzi hao kwa masomo ya juu, waweze kuifahamu hali halisi ya maisha ya chuoni na taratibu za taaluma, waweze kujijengea hali ya kujitambua na uwezo wa uongozi. Mratibu wa mafunzo, Alexander Hines, ambaye anafahamu kiasi shughuli zangu,  aliniambia tuangalie ni kipi kati ya vitabu vyangu viwili kitafaa zaidi kwa semina hii: Africans and Americans: Embracing Cultural Differences au Matengo Folktales . Nilishauri kwamba hicho cha pili kingeendana vizuri zaidi na dhamira kuu ya semina. Tumekubaliana. Tumekubaliana nikaelezee ni nini tunaweza kujifunza kutokana na tamaduni za jadi za Afrika katika masuala haya ya kujitambua, falsafa ya maisha, na uongozi katika dunia ya leo

Angalizo kwa Wenye Vyama: Tanzania ni Yetu Wote

Image
Mimi ni m-Tanzania ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Natoa angalizo kwa wa-Tanzania wenye vyama, hasa CCM, wazingatie kuwa Tanzania ni yetu wote. Naitaja CCM namna hii kwa sababu ni chama tawala, chenye wajibu wa kuongoza njia na kuwa mfano kwa wengine. Wa-Tanzania wenye vyama wakumbuke kuwa wao ni wachache kwa kufananisha na idadi ya wa-Tanzania kwa ujumla. Wafanye siasa zao, ila wasisahau jambo hilo. Nasema hivyo kwa sababu wana tabia ya kujiona kuwa wao ndio Tanzania, na Tanzania ni wao. Kinachonikera zaidi ni fujo. Wa-Tanzania wenye vyama wana tabia ya kuleta fujo na kuhujumu amani, hasa kinapokaribia kipindi cha uchaguzi. Ni aibu sana kwamba, kutokana na fujo za wa-Tanzania wenye vyama, tumefikia mahali sasa ambapo watu wanasali na kufanya ibada kuombea amani. Hii ni fedheha ambayo tumeletewa na wa-Tanzania wenye vyama. Ni sahihi kumwomba Mungu atupate mvua ya kutosha kwa mazao yetu. Ni sahihi kumwomba atuepushe na majanga kama vile matetemeko ya ardhi. Ni

Leo Nimenunua Kitabu: "Jesus: Prophet of Islam"

Image
Leo nilikwenda Minneapolis kwenye mkutano mdogo wa watu wanne ambao tulifanyia katika jengo la maduka na biashara mbali mbali liitwalo Somali Mall. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuingia katika jingo hili. Nilipata fursa ya kuingia katika duka la vitabu liitwalo Akmal Bookstore, ambalo limejaa vitabu vya ki-Islam katika ki-Arabu na ki-Somali. Niliuliza iwapo kuna vitabu vya ki-Ingereza, nikaonyeshwa. Niliviona vingi vilivyonivutia, nikanunua kimoja, Jesus: Prophet of Islam , kilichoandikwa na Muhammad 'Ata' ur-Rahim na Ahmad Thomson. Nimefahamu kwa miaka mingi kuwa katika u-Islam, Yesu anatambulika kama mtume maarufu, ila sio mwana wa Mungu, kama tunavyomwona sisi wa-Kristu. Sioni tatizo, wala sikosi usingizi kwa sababu hiyo. Ninachozingatia ni waumini wa dini mbali mbali kuheshimiana, kila mtu na imani yake. Tukumbuke kwamba dini zinatofautiana, na kuna dini ambazo hamzimjui Yesu kabisa, iwe ni kama mtume au mwana wa Mungu. Mara yangu ya kwanza kuelewa namna wa-Isla

Msikiti Wachomwa Moto Saudia

Nimeona taarifa leo kuwa msikiti umechomwa moto huko Saudi Arabia. Ni msikiti wa dhehebu la Shia. Kwa wale wasiofahamu, wa-Islam, kama walivyo wa-Kristu, wana madhehebu mengi, kama vile Sunni, Shia, Ismailia, Ahmadiya na Tijanniya. Habari ya msikiti kuchomwa moto imenikera, kama ninavyokerwa na habari za kuchomwa moto kanisa au nyumba nyingine ya ibada ya dini yoyote. Nimesema tena na tena kuwa ninaziheshimu dini zote, ninaiheshimu misahafu ya dini zote, na ninazihehimu nyumba za ibada za dini zote. Ninaamini kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya busara ambayo tunapaswa kuifuata. Sawa na waumini wa dini zingine, nami nililelewa katika imani kwamba dini yangu ndiyo pekee dini ya kweli. Nilifundishwa kwamba nje ya dini yangu, nje ya u-Katoliki, hakuna wokovu. Ninajua kuwa wa-Islamu nao wanafundishwa hivyo hivyo, kuwa nje ya u-Islamu hakuna wokovu. Niliwahi kuwa mwanachama katika mtandao wa Radio Imaan, wa wa-Islam. Waliniambia kuwa mimi ni kafiri na kwamba nisiposilimu sitaingia ahera.

Kusonga Mbele na Kutoyumbishwa

Image
Naandika makala hii kuwapa moyo wengine, hasa vijana, wanaojituma kujiendeleza katika fani yoyote na kimaisha kwa ujumla. Kwa ujumla, mawaidha haya yanapatikana vitabuni. Katika vitabu vinavyoelezea mikakati ya mafanikio, kitu kimoja kinachosisitizwa ni kutambua kwamba unaposonga mbele, kuna watu watakaokuandama kwa mategemeo ya kukukatisha tamaa na kukurudisha nyuma. Watabeza shughuli zako na mafanikio yako. Kwa mujibu wa vitabu hivyo, hao ni watu wa kuwapuuza. Ni muhimu pia kuwapuuza wale wasio na mtazamo wa maendeleo yao wenyewe. Badala ya kupoteza muda kuwa na watu wa namna hiyo, andamana na watu waliomo katika njia ya mafanikio, au waliofanikiwa. Utajifunza kutoka kwao. Watu wenye mafanikio, wanajiamini, na hawaoni shida kuwashauri au kuwasaidia wengine nao wafanikiwe. Napenda kunukuu maneno ya Henry Rogers mtu maarufu aliyeanzisha na kuendesha Rogers & Cowan, kampuni ya mahusiano ya jamii: Not only is it essential to make someone feel important, the art of psychorela

Kitabu cha Honwana Kimefika Leo

Image
Leo nina furaha sana. Nimepata kitabu cha Luis Bernardo Honwana, We Killed Mangy Dog and Other Stories , ambacho nilikiagiza siku chache zilizopita. Hiki ni kitabu ambacho nimekuwa ninakikumbuka kwa namna ya pekee, tangu miaka ya mwanzoni kabisa ya sabini na kitu nilipokisoma kwa mara ya kwanza. Furaha iliyoje kuzikumbuka enzi zile za ujana wangu, nilipokuwa tayari nimetekwa moyo na akili na somo la fasihi ya ki-Ingereza. Ingawa wakati huu ninapoandika, na kwa siku chache zijazo, niko katika kusahihisha mitihani, nitaanza kukisoma kitabu hiki mara. Siwezi kujizuia. Hatimaye, nitaandika uchambuzi mfupi katika blogu hii. Kama nilivyosema kabla, kitabu hiki, kutoka Msumbiji, kitakuwa ni kianzio kwa ajili ya kufundisha riwaya ya Mia Couto, The Tuner of Silences , wakati wa kiangazi.

Kitabu cha Dr. John C. Sivalon, M.M.

Image
Leo nimejipatia kitabu cha Dr. John C. Sivalon, M.M. Kanisa Katoliki na Siasa ya Tanzania Bara 1953 Hadi 1985 . kilichochapishwa na shirika la Kanisa Katoliki la wa-Benediktini, Ndanda. Kutokana na kutopatikana madukani hapa Marekani, nimekipata kupitia maktaba ya hapa Chuoni St. Olaf, kwa utaratibu wa uazimishanaji wa vitabu baina ya maktaba. Nimejitengenezea nakala kwa matumizi yangu, kama inavyoruhusiwa kisheria. Hiki ni kitabu kinachojulikana Tanzania kwa kuwa kinatajwatajwa sana na viongozi wa wa-Islam wanaosema kwamba wa-Islam wamekuwa wakihujumiwa na bado wanahujumiwa na serikali ya Tanzania kwa manufaa ya kanisa na wa-Kristu. Kutokana na madai hayo, kwa miaka yote hii nimekuwa na hamu ya kujisomea kitabu hiki. Sikuwahi kusema lolote juu yake, kwa vile sikuwa nimekisoma. Baada ya kukipata, kama saa mbili tu zilizopita, nimekipitia chote, ila bado sijakisoma kwa makini. Hata hivi, nimeona kuwa mwandishi ameandika kitabu hiki kwa busara bila ushabiki, nikakumbuka kitab

Tuziheshimu Dini Zote

Image
Yeyote anayefuatilia blogu hii anafahamu kuwa ninahimiza tuziheshimu dini zote,  tuiheshimu misahafu yote, tuheshimu haki na uhuru wa kila binadamu kuwemo katika dini yoyote anayoona inamfaa, haki na uhuru wa kubadili dini kufuatana na dhamiri yake, na yeyote asiye na dini anastahili heshima sawa na mwenye dini. Tuzingatie tangazo la kimataifa la haki za binadamu, ambalo linataja uhuru wa kuabudu kama mmoja ya haki za binadamu. Naamini kuwa msimamo wangu, kama nilivyoueleza hapo juu, ndio njia sahihi inayotupasa kuifuata. Kufanya vingine ni kuendeleza matatizo, migogoro, na dhuluma, na hata umwagaji damu, mambo ambayo tumeyashuhudia kwa karne na karne. Ninamshukuru Mungu kwa kunipa akili na utashi niweze kutafakari mambo na kuyafanyia maamuzi kwa namna ninayoamini inaendana na mategemeo yake. Simanini kwamba Mungu anataka wanadamu tuwe tunagombana, tunadharauliana, tunakandamizana, au tunapigana. Mungu huyo huyo amenipa fursa ya kutembea katika nchi nyingi na kuonana na watu wa

Vitabu Nilivyonunua Karibuni

Image
Napenda kujiwekea hapa kumbukumbu za vitabu nilivyonunua katika siku chache zilizopita. Ni faraja kuweza kupita tena katika maduka ya vitabu, baada ya miezi ya kuwa katika hali ngumu kiafya. Yapata wiki moja iliyopita,  katika duka la vitabu la hapa Chuoni St. Olaf, ambamo daima kunakuwa na vitabu vingi ambavyo sijawahi kuviona, niliguswa kukiona kitabu cha Terry Eagleton,  How to Read Literature , ambacho nilikuwa sijawahi hata kukisikia. Terry Eagleton ni mwananadharia wa fasihi ambaye ni maarufu kabisa. Nilinunua vitabu vyake kadhaa na kuvisoma miaka ya 1980-86 nilipokuwa masomoni Chuo Kikuu Cha Wisconsin Madison. Nimeanza kusoma na kuvutiwa na How to Read Literature . Juzi tarehe 14, wakati narudi kutoka Columbia Heights, nilipitia Apple Valley, nikaingia katika duka la vitabu la Half Price Books ambalo nimelitaja mara nyingi katika blogu hii. Nilinunua vitabu vitatu. Kimoja ni Without a Name and Under the Tongue. Hizi ni riwaya mbili ambazo zimechapishwa katika hiki k

Hadithi za Luis Bernardo Honwana wa Msumbiji

Image
Leo nimeagiza mtandaoni kitabu cha hadithi za Luis Bernardo Honwana wa Msumbiji kiitwacho We Killed Mangy Dog and Other Stories . Kwa wiki kadhaa, nimemwazia sana mwandishi huyu, ambaye kitabu chake hiki nilikipenda sana nilipokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1973. Nilivutiwa na jinsi alivyoielezea maisha nchini Msumbiji, ambayo ilikuwa daima mawazoni mwetu kutokana na vita vya ukombozi vilivyoongozwa na FRELIMO. Nimeamua kununua kitabu hiki wakati huu kwa sababu katika wiki hizi nimeandaa orodha ya vitabu vya kufundishia kozi yangu ya "Post-colonial Literature" muhula wa kiangazi, mwezi Julai na Agosti. Kwa mara ya kwanza tangu nianze kufundisha hapa Chuoni St. Olaf, nimeamua kuingiza kazi ya fasihi kutoka Msumbiji. Sitafundisha We Killed Mangy Dog and Other Stories, ingawa ningeweza kufanya hivyo kwa furaha kabisa. Badala yake, nitafundisha riwaya ya mwandishi mwingine maarufu Mia Couto iitwayo The Tuner of Silences, ambayo sijaisoma.

Vitabu vya Shaaban Robert

Image
Jina la Shaaban Robert ni maarufu miongoni mwa wa-Tanzania na wengine wa nchi zingine wanaokijua ki-Swahili. Lakini, tujiulize ni wa-Tanzania wepi ambao wamesoma angalau vitabu vichache vya Shaaban Robert. Ni wangapi wamesoma au wanasoma mashairi yake, tenzi zake, insha zake, barua zake, na riwaya zake? Ni wangapi wamesoma vitabu vyake vingine, kama vile Wasifu wa Siti Binti Saad , Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini , na tafsiri yake ya mashairi ya Omar Khayyam? Kama hatuna majibu ya kuridhisha, tuache kujigamba, kujidanganya na kudanganyana kuwa tunamwenzi mwandishi wetu huyu maarufu. Ingawa kulikuwa na kipindi cha uhaba, leo vitabu vya Shaaban Robert vinapatikana kirahisi Tanzania, baada ya kampuni ya uchapishaji ya Mkuki na Nyota kuanza kuvichapisha upya. Mwaka hadi mwaka, ninapokwenda Tanzania, nimekuwa nikijinunulia vitabu hivyo, kama hivi vinavyoonekana pichani, sambamba na vitabu vya waandishi wengine maarufu katika lugha ya ki-Swahili. Imekuwa ni faraja kwangu ku

Neno Jingine Kuhusu Uandishi na Uchapishaji

Image
Mimi ni mwandishi wa vitabu. Ninaandika vitabu vya tahakiki ya fasihi, juu ya masuala ya jamii, fasihi simulizi, na masuala ya athari za tofauti za tamaduni, hali halisi ya uandishi wa vitabu, mbinu za kujichapishia vitabu. Naandika kuhusu utangazaji na uuzaji wa vitabu, na kuhusu hali halisi ya usomaji wa vitabu Tanzania na ughaibuni. Ninatoa ushauri kwa wengine kupitia blogu hii na katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii . Yeyote anayetaka kujifunza kutoka kwangu anaweza kufanya hivyo, bila kipingamizi. Lakini namtegemea aanze kwa kusoma nilichoandika, mawasiano ya ziada yafuate baadaye. Siwezi kuwasiliana na kila mtu na kuongelea hata yale ambayo tayari nimeshaandika. Nina kazi yangu na majukumu mengine kila siku. Nikisema niwasiliane na kila mtu hata kwa yale ambayo nimeshaandika, nitashindwa kufanya kazi zangu zinazoniwezesha kuishi, kulipia nyumba, matibabu, na mahitaji mengine. Labda niache kazi niliyoajiriwa kufanya, nijiajiri kama mshauri. Ikiwa hivyo,

Vitabu vya Moyez Vassanji

Image
Siku chache zilizopita niliandika taarifa kuhusu vitabu nilivyonunua hivi karibuni. Kati ya vitabu kilikuwepo kimoja cha Moyez Vassanji, The Gunny Sack . Wakati huo, nilikuwa navingojea vitabu vingine viwili vya Moyez Vassanji, ambavyo nilikuwa nimeshavilipia. Vimefika. Kimoja ni Uhuru Street , mkusanyo wa hadithi za kubuniwa,ambazo zinatokea katika mtaa wa Uhuru, mjini Dar es Salaam. Nasikitika kuwa kitabu hiki sijakisoma ingawa nimetamani kukisoma kwa miaka mingi. Kutokana na taarifa, nilijua kuwa kwa yeyote anayeijua Dar es Salaam, hiki ni kitabu kinachogusa hisia. Nimeanza kukisoma na ninajionea mwenyewe ukweli huo. Kitabu cha pili ambacho kimewasili ni The Book of Secrets , ambacho, kama nilivyosema, niliwahi kukifundisha katika semina ya walimu katika Chuo cha Colorado.  Mtu akisoma kitabu hiki, naamini atapata hamu ya kusoma vitabu vingine vya Moyez Vassanji. Kitabu cha tatu ambacho kimewasili ni The In-Between World of Vikram Lall . Sijaanza kukisoma, ila nimekuwa

Going Visual: Kitabu Kuhusu Mawasiliano Kwa Taswira

Image
Leo napenda kukiongelea kitabu kiitwacho Going Visual: Using Images to Enhance Productivity, Decision-Making and Profits , kilichoandikwa na Alexis Gerard na Bob Goldstein. Nilikinunua kitabu hiki miaka michache iliyopita. Kama ilivyo kawaid yangu ninaponunua kitabu, sikiweki katika maktaba yangu bila kukipitia angalau juu juu, ili nijue kinahusu nini. Hivi ndivyo nilivyofanya niliponunua Going Visual . Niliona ni kitabu kinachoelezea maendeleo katika utumiaji wa taswira katika mawasiliano, kitabu kinachoelezea matokeo ya utafiti na uzoefu na mikakati ya matumizi ya taswira katika biashara na ujasiriamali. Kitabu kinaelezea jinsi tekinolojia ya kuzalisha, kuhifadhi, kuandaa, na kusambaza taswira, kuanzia za digitali hadi video, zinavyowezesha ufanisi katika biashara na ujasiriamali katika ulimwengu wa leo. Wakati nilipokinunua kitabu hiki, nilikipitia juu juu, nikaelewa haya niliyoelezea. Lakini leo nimekitoa maktabani ili nikisome ipasavyo. Mada yake inanivutia, na ukweli kwamb

Leo Nimepata Bendera ya Tanzania

Image
Leo nimepata bendera ya Tanzania. Niliwahi kuandika katika blogu hii kuwa mara kwa mara ninashiriki matamasha hapa Marekani ambapo watu huja na bendera za nchi zao, nami nilijisikia vibaya kwa kutokuwa na bendera kubwa ya nchi yangu. Nilifanya uamuzi muafaka, nikaagiza, na leo nimeipata. Mwaka jana, nilipoandika ujumbe wangu, nilikuwa napeleleza katika tovuti kadhaa zinazouza bendera. Lakini safari hii, kwa kubahatisha tu, nimeingia katika tovuti ya Amazon nikaona bendera ziko, tena kwa bei rahisi sana. Nimejionea hapa Marekani jinsi wa-Kenya walivyo hodari kwa suala hilo, na hapa naleta picha niliyopiga katika tamasha la Afrifest,  tarehe 2 Agosti, mwaka jana, mjini Brooklyn Park, Minnesota. Inamwonyesha m-Kenya akitamba na bendera ya nchi yake. Jiulize mwenyewe, ungejisikiaje kuwepo mahali ambapo wenzako wanatamba na bendera za nchi zao, nawe huna. Kwa nini ukae mahali hivyo, kama vile huna nchi? Hisia hizi ni kubwa unapokuwa ughaibuni. Sikutaka kuendelea kudhalilika na

Kuiheshimu Misahafu ya Dini Zote

Image
Pichani hapa kushoto ninaonekana nimeshika nakala yangu ya Bhagavad Gita , msahafu wa dini ya Hindu. Ingawa mimi ni m-Kristu (m-Katoliki), ninaamini kwa dhati kuwa ni wajibu kuiheshimu misahafu ya dini zote. Kwa mfano, ninayo Qur'an . Siku moja nilimwuliza kijana mmoja mu-Islam kuhusu heshima itakiwayo kwa Qur'an . Kuna baadhi ya mambo niliyajua, lakini kijana aliniambia jambo la ziada. Alisema kwamba pasiwekwe chchote juu ya Qur'an . Basi, daima ninakumbuka na ninazingatia hilo. Ingawa ofisi yangu imefurika vitabu, na  mezani pangu panakuwa pamefurika vitabu, na Qur'an yangu iko hapa hapa mezani muda wote, siwezi kuweka kitabu, karatasi, au kitu chochote juu yake. Nafanya hivi kwa kufuata dhamiri yangu, si kwa kuogopa labda atafika mtu ofisini akute hali nyingine. Ninaamini kuwa kama dini yoyote inajinadi kuwa ni dini ya amani, ni lazima idhihirishe jambo hilo kwa kuziheshimu dini zingine. Ni lazima iwaheshimu waumini wa dini zingine, na misahafu yao. Kufan

Vitabu Nilivyonunua Karibuni

Image
Napenda kuendelea na jadi yangu ya kuvitaja vitabu nilivyoongeza katika maktaba yangu katika siku chache zilizopita. Kitabu kimoja ni The Poetic Edda: Stories of the Norse Gods and Heroes , kilichotafsiriwa na Jackson Crowford. The Poetic Edda ni kitabu maarufu sana ambacho nimekisikia kwa miaka mingi. Ni mkusanyo wa hadithi na mashairi ya mapokeo juu ya miungu na mashujaa wa Iceland. Nimeamua kujipatia nakala wakati huu ambapo nimekuwa nafundisha utungo maarufu wa Finland uitwao Kalevala .  Kwa pembeni nimekuwa nayapitia pia mashairi ya mapokeo ya Finland yaliyokusanya na Elias Lonnrot katika kitabu kiitwacho Kanteletar . Nina hamu ya kuona kama The Poetic Edda inahusiana na hizo tungo zingine, kwa kuzingatia kuwa zote ni za Ulaya ya kaskazini. Kitabu kingine nilichonunua ni The Village by the Sea , cha Anita Desai wa India. Nilipangia kukifundisha muhula huu katika kozi yangu ya Post-colonial Literature, lakini tumeishiwa muda. Nimeshafundisha riwaya kadhaa za Anita Desai