Posts

Showing posts from December, 2011

Mahojiano na Profesa Mbele, "Kombolela Show"

Nimeona niwaletee wadau mahojiano niliyofanyiwa katika "Kombolela Show," Oktoba 2, 2010. Mwendesha mahojiano alikuwa Metty Nyang'oro. Kwa jinsi mtandaoni kunavyofurika taarifa, nimeona si vibaya kuyaleta tena mahojiano haya, ili wadau wayasikie na kuyatafakari na kuchangia, endapo watajisikia kufanya hivyo, kwani elimu haina mwisho, wala haina mwenyewe.

Hadithi za wa-Matengo Zatamba Ughaibuni

Image
Hivi karibuni, nilipata ujumbe kutoka kwa Profesa Paschal Kyoore wa Chuo cha Gustavus Adolphus kuwa anatunga kozi mpya, "The African Trickster," akaomba ushauri wangu, kwani mada hiyo ya "trickster" nimeifanyia utafiti na kuandika makala kwa miaka mingi. Hatimaye, Profesa Kyoore ameniletea ujumbe kuwa ameshaagiza nakala za kitabu cha Matengo Folktales kwa ajili ya darasa hilo. Kisha angependa siku moja niende kuongea na wanafunzi wake, nami nimekubali. Ninafurahi sana ninapoona watu wa ughaibuni wakipata fursa ya kujifunza mambo ya kwetu, na hadithi za jadi ni hazina mojawapo kubwa, kama nilivyoelezea hapa . Ni fursa kwetu na kwa walimwengu kutambua mchango wa wahenga wetu kwa utamaduni wa dunia, kwani katika hadithi zao, wahenga waliongelea na kutafakari kila aina ya suala linalomkabili binadamu, sawa na watu walivyofanya watu wa mataifa mengine. Hadithi za wa-Matengo zinatumika katika vyuo mbali mbali hapa Marekani, kama nilivyoelezea hapa . Yapata miaka

Maongezi na Wanafunzi Waendao Tanzania

Image
Profesa Barbara Zust , wa Chuo cha Gustavus Adolphus , amenialika kwenda kuongea na wanafunzi anaowaandaa kwa safari ya Tanzania. Anafundisha masomo ya uuguzi, na mwezi Januari anawapeleka wanafunzi Tanzania kujifunza masuala ya afya na matibabu katika utamaduni tofauti na ule wa Marekani. Profesa Zust ameshawapeleka wanafunzi Tanzania mara kadhaa. Katika kuwaandaa, hutumia kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na pia hunialika nikaongee nao. Anajisikia vizuri sana ninapokutana na wanafunzi wake kujibu masuali yao na kuwapa maelezo mbali mbali, nami huwa nafurahi kukutana na wanafunzi hao wanaosomea taaluma ambayo sikusomea, ila ni wazi kuwa wanafaidika na mawazo yangu kuhusu jinsi tofauti za tamaduni zinavyohusika katika taaluma yao. Hapa kushoto ni picha tuliyopiga na wanafunzi waliokuwa wanaenda Tanzania mwaka 2009. Tulikuwa kwenye chumba cha mkutano cha kanisa la Shepherd of the Valley, mjini Apple Valley. Habari za mkutano wetu niliziandika hapa .

Mdau Mwingine, Mwanafunzi, Kaja

Image
Mara kwa mara naandika habari za wasomaji wa maandishi yangu wanaonitembelea, au ninaokutana nao sehemu mbali mbali. Jana, baada ya kumaliza kufanya mtihani wa mwisho wa somo langu la fasihi ya Afrika Kusini, kaja ofisini mwanafunzi Logan. Alikuja na nakala ya kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , ili nikisaini. Nilisaini, tukaendelea na michapo. Logan alisoma somo langu jingine mwaka jana. Chuo Cha St. Olaf kinaamini kuwa ni muhimu wanafunzi waufahamu ulimwengu nje ya Marekani. Kilinileta hapa, mwaka 1991, kuanzisha masomo katika idara ya ki-Ingereza juu ya uandishi wa ki-Ingereza kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Wanafunzi wanavutiwa na fursa hii ya kupanua upeo wao, kuzifahamu jamii na tamaduni mbali mbali.

Makari Hodari

Image
Kwa sisi tuliosoma shule ya msingi zamani, Makari Hodari ni jina tunalolikumbuka sana. Tulisoma habari zake zilizotungwa na Padri Alfons Loogman, mwandishi wa vitabu vya Someni Bila Shida na Someni Kwa Furaha . Kwa kweli, padri huyu aliziteka nyoyo zetu watoto, akatufanya tupende kusoma. Aliandika vitabu kadhaa vya masomo ya ki-Swahili na hata mwongozo kwa walimu kuhusu kufundisha kusoma. Nakumbuka kuwa katika shule yangu ya msingi ya Litembo , tulikuwa tunasoma hadithi ya Makari Hodari kwa kuiimba. Watoto wote darasani tulikuwa tunaimba kwa pamoja, kwa furaha. Hadi leo naweza kuimba tulivyoimba. Na mwalimu alikuwa akiimba nasi. Pamoja na utamu wa hadithi, tulivutiwa na picha. Nikiitafakari hadithi ya Makari Hodari, naona kuwa ilijengeka katika mfumo wa zile hadithi za kale za mashujaa, ambazo zinasimuliwa katika tamaduni mbali mbali. Kwa mfano, Wa-Haya wana hadithi za mashujaa kama Mugasha, Rukiza, na Kilenzi. Wa-Chagga wana hadithi ya Mrile, wa-Swahili hadithi ya Liongo Fumo. Had

Wanafunzi Wangu Wameondoka Tanzania

Image
Mapema leo, wanafunzi niliowaleta Tanzania mwaka huu wameondoka nchini, baada ya kumaliza masomo ya miezi kadhaa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam . Wanafunzi hao nami tunaonekana katika picha hapa kushoto, tuliyopiga kwenye hoteli ya Wilolesi , mjini Iringa, tarehe 10 Agosti. Kama nilivyoelezea mara kadhaa katika blogu zangu, tulizunguka sehemu mbali mbali, kama vile Kalenga , Matema Beach , Lyulilo na Bagamoyo . Baada ya mizunguko hiyo niliwafikisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam , nami nikarejea Marekani kwani muhula wa masomo ulikuwa unaanza. Ni faraja kuona wameondoka salama, kwani nilikuwa na wasi wasi kutokana na taarifa za migomo, vurugu na mabomu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam . Kwa miaka yote niliyofundisha hapa Marekani nimekuwa mshauri katika programu kadhaa zinazopeleka wanafunzi Tanzania na nchi zingine za Afrika, kama nilivoelezea hapa . Huwa tunawaambia hao wanafunzi kuwa wasishiriki maandamano au migomo katika nchi husika. Kwa upande wa Tanzania, nimekuwa mwepesi kuwaeleza j

Vitabu Kama Zawadi ya Idd el Fitr na Krismasi

Hebu fikiria: sikukuu ya Idd el Fitr au Krismasi imewadia na unataka kuwapa zawadi ndugu na marafiki zako, wa-Tanzania wenzako. Unaamua kwenda kwenye duka la vitabu, na unawanunulia nakala za kitabu kama Kufikirika cha Shaaban Robert, au Binadamu na Maendeleo cha Mwalimu Nyerere, au kwa wanaojua ki-Ingereza, The Tempest cha Shakespeare. Unawafungia vizuri, kisha unawapelekea. Je, watajisikiaje hao wa-Islam na wa-Kristu wa Tanzania? Miaka ya tisini na kitu, katika jumuia ya mawasiliano ya mtandaoni iitwayo Tanzanet, ambayo wanachama wake ni wa-Tanzania na marafiki wa Tanzania, niliwahi kuandika, kiutani, kwamba siku za usoni huenda nikaamua kwamba, kwenye mialiko ya arusi nisipeleke kreti ya bia, bali kreti ya vitabu. Ingawa ulikuwa ni mchapo, nilikuwa na jambo muhimu kichwani, kwani ni kweli kuwa vitabu ni hazina, na ni bora kuliko bia. Hapa Marekani, ni kawaida watu kutoa au kupokea zawadi ya vitabu. Msimu kama huu wa Krismasi, watu wengi wananunua vitabu ili kuwapa zawadi wenzao

Hatimaye Itabidi Nielezee Nilivyotoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam

Mwaka 1991 niliondoka Chuo Kikuu Dar es Salaam , nikaja kufundisha Chuo cha St. Olaf hapa Marekani. Kulikuwa na mlolongo wa masuala yaliyonifanya nikaondoka, baada ya kuwa mwalimu pale kuanzia mwaka 1976. Sijaelezea masuala hayo, ingawa yamo katika maandishi kwenye makabrasha, ambayo yalikuwa mawasiliano rasmi baina ya wahusika. Mwaka jana, nikiwa maeneo ya Mwenge, Dar es Salaam, na marafiki zangu, nilikutana na Profesa Sam Maghimbi wa Chuo cha Elimu cha Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam . Nilishangaa alivyokumbushia nilivyotoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam , na marafiki zangu wakasikia. Nilifarijika kuona kuwa kumbukumbu bado zipo kiasi hiki. Wako wengi wanaokumbuka nilivyofundisha Chuo Kikuu Dar es Salaam , na jinsi nilivyoondoka. Lakini, kwa jinsi miaka inavyopita, wanafikia umri wa kustaafu, na wengine wamefariki. Nami natatizwa na fikra ya wa-Tanzania wengi za kudhani kila m-Tanzania anayeenda kufanya kazi nje hana sababu nyingine bali kufuata maslahi binafsi. Hata mafisadi walioza

Leo Nimekuwa Marley Katika Hadithi ya Charles Dickens

Image
Leo katika idara yetu ya ki-Ingereza tulifanya onesho la tamthilia kutokana na hadithi ya A Christmas Carol iliyotungwa na mwandishi maarufu Charles Dickens. Watu tuliosoma shule zamani tunakumbuka sana vitabu vya Charles Dickens, hasa Oliver Twist . Ni nani asiyekumbuka wahusika wa hadithi hii, kama vile Oliver Twist mwenyewe, The Artful Dodger, na Fagin m-Yahudi? Ilikuwa raha kusoma miaka ile, na tulikuwa tunapenda hata kukariri baadhi ya kauli za hao wahusika. Basi katika kipindi hiki cha kuelekea Krismasi, idara yetu ina jadi ya kufanya jambo la kumbukumbu na burudani. Kwa miaka kadhaa, tumekuwa tukiigiza mchezo huu unaotokana na riwaya hii ya Dickens. Katika A Christmas Carol kuna wahusika wakuu kadhaa, na Scrooge ndio kinara. Huyu ni mfanyabiashara bahili, ambaye zamani alikuwa na mshiriki wake wa kibiashara aliyeitwa Jacob Marley. Wakati hadithi inapotokea, tunaambiwa kuwa Jacob Marley alifariki miaka saba iliyopita. Tunachoona ni mzimu tu wa Marley, ambao unamtokea Scroo

Posho za Wabunge Hazitoshi

Yapata mwaka 1997 nilipokuwa katika utafiti Mwanza, mimi na washiriki wa utafiti tulikutana na mbunge katika hoteli ya Ramada. Sikumbuki alikuwa ni mbunge wa sehemu gani nchini. Katika maongezi yetu, alilalamika kwa masikitiko kuwa wa-Tanzania wanaamini kuwa mbunge ni mtu mwenye hela sana. Akatoa mfano wa maisha yake mwenyewe, kwamba nyumbani kwake, watu wamejaa kwenye makochi muda wote. Mchana wako hapo, na usiku wanalala hapo. Na yeye anawajibika kuwalisha na kuwanywesha siku zote. Wakati huu ambapo wa-Tanzania wanalumbana kuhusu kuongeza posho za wabunge, mimi nakumbuka kilio cha yule mbunge. Nasita kuwalaumu wabunge wanapodai kuongezewa posho. Naamini kuwa posho zao hazitoshi. Tatizo ni sisi wa-Tanzania, sio wabunge. Mtu akishapata ubunge, tunamtegemea atufanyie mambo mengi sana yanayohitaji hela. Mbunge akiingia baa, tunategemea ofa zake, tena za uhakika, sio soda za reja reja. Tunamtegemea achangie hela nyingi kwenye vikao vya "send-off," kipaimara, arusi, na kadhalik

Miaka 50 Baada ya Uhuru, Mtoto Albino Anaogopa Kwenda Shule

Image
Jana ilikuwa ni kumbukumbu ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika. Nilijaribu sana kuandaa makala kuhusu siku hiyo ya jana, lakini nilipata kigugumizi. Kwa upande moja, ninafahamu kuwa ndoto ya uhuru aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere, ya kuleta ukombozi wa kweli katika nyanja mbali mbali na kujenga taifa linalojitegemea, imezimishwa na sera zilizopo, ambazo zinaimarisha ukoloni mamboleo. Kama ningeandika makala jana kuhusu kumbukumbu za uhuru wa Tanganyika, pangekuwa hapatoshi. Lakini jambo jingine lililonipa kigugumizi ni kuwa mawazo yangu yalikuwa yanarudi tena na tena kwenye taarifa niliyosoma wiki kadhaa zilizopita, kuhusu mtoto albino wa Ludewa ambaye anaogopa kwenda shule asije akauawa na watu wenye imani za kishirikina. Habari hii niliiweka hapa . Siku nzima ya jana nilikuwa najiuliza, inakuwaje miaka 50 baada ya uhuru, mtoto huyu anaishi katika hofu ya kuuawa? Tumepiga hatua mbele au nyuma? Enzi za Mwalimu Nyerere, mtoto huyu angekuwa anaenda shule sawa na watoto wengine. Ndoto ya M

Hifadhi za Historia Bagamoyo

Image
Bagamoyo ni mji maarufu katika historia ya nchi yetu na dunia. Kwa mtu anayetaka kujifunza historia hiyo, napendekeza ziara Bagamoyo kuangalia hifadhi zilizopo. Mwaka huu, nilitembelea Bagamoyo, na wanafunzi kutoka Marekani, kama nilivyoelezea hapa . Mahali pamoja tulipotembelea ni Caravan Serai, hifadhi mojawapo ya historia. Hapa kushoto ninaonekana mbele ya mlango wa kuingilia Caravan Serai. Kuna sanamu ya mtumwa aliyebeba pembe ya ndovu. Hapa kushoto tunaonekana katika eneo la Caravan Serai, tukiwa na mfanyakazi wa hifadhi hiyo, ambaye alikuwa anatuonyesha na kutuelezea yaliyomo. Hapa anaonekana mtaalam wetu akitoa maelezo ya historia ya Caravan Serai. Humo ndani kuna nyaraka, picha na vitu mbali mbali, kama vile vyombo vya nyumbani, na maelezo kuhusu vitu hivyo. Hapa kushoto, katika picha ya katikati, anaonekana Tippu Tip. Hapa kushoto ni picha ya watumwa. Hapa kushoto ni picha ya "bangili," kwa mujibu wa bandiko la ma

Barua za Shaaban Robert

Image
Kitabu cha Barua za Shaaban Robert ni mkusanyiko wa barua alizoandika Shaaban Robert kwa mdogo wake Yusuf Ulenge baina ya mwaka 1931 na 1958. Yusuf Ulenge alifanya busara ya kuzihifadhi na sasa zimechapishwa kama kitabu, na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam . Mhariri Profesa Mugyabuso Mulokozi amefanya kazi kubwa na watafiti wenzake katika kuzichapisha na kuziwekea maelezo. Nilikinunua kitabu cha Barua za Shaaban Robert mwaka 2008 katika duka la Taasisi . Nilifurahi na pia kushtuka kugundua kuwa Yusuf Ulenge alikuwa mdogo wa Shaaban Robert. Jina la Yusuf Ulenge nililifahamu tangu kwenye mwaka 1964, nilipokuwa darasa la sita. Nilinunua kitabu kiitwacho Nguzo ya Maji na Hadithi Nyingine , kilichotungwa na Yusuf Ulenge. Miaka yote sikuwa na wazo hata kidogo kuwa huyu alikuwa mdogo wa Shaaban Robert. Sasa, hizi barua zimenifungua macho kabisa, kwani nimejionea jinsi uhusiano wa hao ndugu wawili ulivyokuwa mkubwa na jinsi Yusuf Ulenge naye alivyokuwa mwand

Wadau Wamekuja Ofisini Kwangu

Image
Leo, bila kutegemea, nimetembelewa na akina mama wawili ofisini kwangu. Walijitambulisha, wakasema wamekuja ili nisaini nakala za vitabu vyangu. Anayeonekana kushoto ni Mama Kay wa Lanesboro, Minnesota, na huyu wa kulia ni Mama Sandy wa maeneo ya St. Louis, Missouri. Nimesaini nakala tatu za Matengo Folktales na moja ya Africans and Americans: Embracing Cultural Differences ambazo wamezinunua leo hapa Chuoni St. Olaf . Tumeongelea vitabu hivi na masuala mengine ya aina hiyo. Kumbe, Mama Kay, tulishaonana miaka kadhaa iliyopita hapa St. Olaf , alipokuja na mumewe, ambaye ni marehemu sasa, pamoja na Mchungaji Gabriel Nduye, Mchungaji Mengele (ambaye sasa ni askofu) na mkewe, wote kutoka Njombe. Mama Kay ameshafika Tanzania. Nimewaambia kuwa nimeguswa na ujio wao. Ninaguswa na namna wadau wanavyoyafuatilia maandishi yangu, na falsafa yangu ni kumshukuru Mungu kwa yote. Kama inavyoonekana katika picha, tumefurahi kukutana.