Barua za Shaaban Robert

Nilikinunua kitabu cha Barua za Shaaban Robert mwaka 2008 katika duka la Taasisi. Nilifurahi na pia kushtuka kugundua kuwa Yusuf Ulenge alikuwa mdogo wa Shaaban Robert. Jina la Yusuf Ulenge nililifahamu tangu kwenye mwaka 1964, nilipokuwa darasa la sita. Nilinunua kitabu kiitwacho Nguzo ya Maji na Hadithi Nyingine, kilichotungwa na Yusuf Ulenge. Miaka yote sikuwa na wazo hata kidogo kuwa huyu alikuwa mdogo wa Shaaban Robert.
Sasa, hizi barua zimenifungua macho kabisa, kwani nimejionea jinsi uhusiano wa hao ndugu wawili ulivyokuwa mkubwa na jinsi Yusuf Ulenge naye alivyokuwa mwandishi mahiri. Katika kitabu hiki kuna taarifa za maandishi mengi ya Yusuf Ulenge, vikiwemo vitabu alivyochapisha na vingine alivyopangia kuchapisha. Mzee Yusuf Ulenge alifariki tarehe 16 Desemba, 2002.
Shaaban Robert ni mfano wa mlezi bora, kwa jinsi alivyokuwa anamshauri na kumwongoza mdogo wake Yusuf katika masuala mbali mbali ya maisha, kama vile elimu. Siwezi kuelezea kwa ufasaha jinsi Shaaban Robert alivyothamini elimu na maadili mema, akawa anamwongoza Yusuf katika njia hiyo. Shaaban Robert alikuwa tayari kutoa gharama zozote zilizohitajika kumlipia Yusuf katika masomo yake, kuanzia daftari hadi usafiri. Ni mfano mzuri sana kwetu wazazi na walezi wa watoto.
Kitabu hiki kinaelimisha sana. Kinautikisa kabisa moyo wangu kwa undani na uzito wa maudhui yake. Kitabu hiki kinafaa kuwemo katika kila nyumba ya wa-Tanzania, ili kisomwe na wazazi na watoto. Hakuna kisingizio cha kutokuwa na kitabu kama hiki, na vitabu vingine vya Shaaban Robert, ambaye ndiye gwiji wa uandishi wa ki-Swahili, mwanafalsafa na mwalimu wa jamii. Hayo nimeyaelezea katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, uk. 30-41
Ingekuwa ni hapa Marekani, tukio la kuchapishwa kitabu kama hiki lingekuwa na kishindo, na watu wangepanga foleni kwenye maduka ya vitabu kukinunua. Kingezungumziwa magazetini na vyombo vingine vya habari. Wa-Tanzania tunapaswa kujiuliza iweje hatuna utamaduni wa aina hiyo. Iweje hatuna hata habari wala hamu ya kujua mwandishi kama Shaaban Robert alizaliwa wapi na aliishi wapi na mchango wake katika jamii na ulimwengu ni upi. Tuko wa-Tanzania yapata milioni arobaini. Ni nyumba ipi katika Tanzania, kuanzia nyumba za walalahoi hadi za hao tunaowaita viongozi, yenye vitabu vya mwandishi muhimu kama huyu?
Kwenye mtandao wa Facebook kuna ukumbi wa wadau na wapenzi wa Shaaban Robert, uitwao Ukumbusho wa Shaaban Robert. Walioanzisha ukumbi huu si wa-Tanzania, bali wa-Kenya. Hii ndio hali halisi, kwamba nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake. Kuthibitisha zaidi jambo hili, jionee jinsi mwanafunzi m-Marekani alivyokichangamkia kitabu hiki cha Barua za Shaaban Robert, akakiandikia uchambuzi huu hapa.
Comments
Lakini huwa najiuliza kila siku, kwa nini isianzishwe tuzo ya umahahiri ya Shaaban Robert? Ingependeza kila mwaka kungekuwa na tuzo kwa waandishi wa Kiswahili. Hii ingependeza sana ili kuzidi kuenzi kazi zake na pia kuchochea wanaandishi kufanya vema zaidi.
Hicho kitabu cha Barua za Shaaban Robert kina mengi sana. Unaona jinsi mtu huyu alivyozingatia mambo mema maishani. Kitabu hiki kingefaa sana iwapo kingekuwa kinatumika katika malezi ya watoto wetu na kuhimiza maadili katika jamii kwa ujumla.
Si vema kuona bingwa kiasi hicho akisahaulika ila wengine kama waigizaji, waimbaji na wanasiasa wanapigiwa debe bila kuchangia hata kidogo katika kuikuza lugha yetu teule.
Iwapo kuna njia ya kukipata (kitabu hicho ulichozungumzia) hapa Kenya, usikose kutujulisha. Vitabu vingine vyake vyauzwa huku ila hicho sijakiona.