Makari Hodari

Kwa sisi tuliosoma shule ya msingi zamani, Makari Hodari ni jina tunalolikumbuka sana. Tulisoma habari zake zilizotungwa na Padri Alfons Loogman, mwandishi wa vitabu vya Someni Bila Shida na Someni Kwa Furaha. Kwa kweli, padri huyu aliziteka nyoyo zetu watoto, akatufanya tupende kusoma. Aliandika vitabu kadhaa vya masomo ya ki-Swahili na hata mwongozo kwa walimu kuhusu kufundisha kusoma.

Nakumbuka kuwa katika shule yangu ya msingi ya Litembo, tulikuwa tunasoma hadithi ya Makari Hodari kwa kuiimba. Watoto wote darasani tulikuwa tunaimba kwa pamoja, kwa furaha. Hadi leo naweza kuimba tulivyoimba. Na mwalimu alikuwa akiimba nasi. Pamoja na utamu wa hadithi, tulivutiwa na picha.

Nikiitafakari hadithi ya Makari Hodari, naona kuwa ilijengeka katika mfumo wa zile hadithi za kale za mashujaa, ambazo zinasimuliwa katika tamaduni mbali mbali. Kwa mfano, Wa-Haya wana hadithi za mashujaa kama Mugasha, Rukiza, na Kilenzi. Wa-Chagga wana hadithi ya Mrile, wa-Swahili hadithi ya Liongo Fumo. Hadithi ya Makari Hodari imerahisisha na kufupisha masimulizi ili yawavutie watoto kwa umri wao. Lakini inataja vitendo vya ushujaa, majigambo, na nafasi ya mama katika maisha ya shujaa.

Leo ni mara ya pili kwangu kuandika kuhusu vitabu hivi vya Padri Loogman katika blogu hii. Nilipoandika mara ya kwanza, ujumbe wangu uliwafikia watu wengi, hasa baada ya kutokea katika blogu ya Michuzi. Leo nimeona niwaletee wadau hadithi ya Makari Hodari, waione pia picha yake na picha ya mama yake.

Comments

Anonymous said…
Hahhaaaaaaaaaaa Katika siku ambazo umenikumbusha mbali basi ni leo hii.Asante sana
Rachel Siwa said…
Duuhhh hahahahah umenikumbusha mbali sana,Ahsante sana, nipo na wanangu hapa naimba wao wanacheka tuu,nami nitajitahidi nivipate.
Mbele said…
Mdau anonymous, shukrani kwa ujumbe wako. Tuko pamoja. Swahili na Waswahili, nimefurahi kuwa unawaburudisha wanao kwa wimbo wa Makari Hodari.

Kuwasomea watoto vitabu ni jambo ambalo nahamasisha sana. Nimeandika kuhusu jambo hilo katika blogu hii na pia katika kitabu changu kiitwacho CHANGAMOTO: Insha za Jamii, ambacho kinapatikana Dar es Salaam, simu namba 0754 888 647 na 0717 413 073.
Anonymous said…
yaani um,enifikisha mbali sana. Shukurani.Vipi hadithi ya Kishwira binti ya Sultani?
Anonymous said…
Unbakumbuka hadithi ya Nicolai Paganini? Imagine my surprise when Ilater leaned that Nicolo Paganini was an actual Italian Composer> My God I will forever tyreasure my Primary education.
Anonymous said…
Kofia yenye Mreri>
Mbele said…
Wadau naona mmenifany nijikune kichwa, kwa kumbukumbu zenu za kusisimua. Kishwira binti Sultani yaonekana nimesahau. Paganini nakumbuka kiasi. Kofia yenye Mreri ndio sikumbuki kabisa. Lakini ni changamoto, maana natamani sasa kuanza kutafuta habari hizo.

Enzi zetu, shule ilikuwa shule kweli. Walimu walikuwa makini, na walipenda tufanikiwe, hata kwa bakora. Vinginevyo, bila hizo bakora, siamini kama ningefika hapa nilipo.
Anonymous said…
umenikumbusha hadithi za kwetu buhaya na sio hadithi ni vitu vilivyotokea kweli enzi na enzi ila wazee wetu zamani walikuwa hawaandiki lakini walikuwa wakariri sio kawaida sasa katika hizo hadithi kuna,kagoro,wamara hawa walikuwa wanadamu wenye karama nyingi na mpakasasahivi tunawafanyia matambiko
Anonymous said…
Eti "Makari Hodari"? Sisi Kenya tulisoma kama "Omari Hodari"
Mbele said…
Anonymous uliyeandika Januari 4, shukrani kwa mchango wako. Nimesomasoma na hata kufundisha masimulizi ya wa-Haya, kama vile ya Kilenzi (Kachwenyanja) na Mugasha. Ni masimulizi murua, yaliyojaa falsafa, maudhui, na mitazamo mbali mbali ya maisha na mahusiano ya wanadamu.

Mbele said…
Asante anonymous uliyeandika Mei 30, kwa kutufahamisha. Je, mchoro ulikuwa huo huo, au Omari alivaa kanzu na barakashia?
babumbwa said…
Prof, umenikumbusha vitabu vilivyonifanya nipende kujisomea katika maisha yangu yote! Pia naukumbuka ushauri ambao wewe binafsi uliotupatia tukiwa wanafunzi wako wa "oral literature" pale "University of Dar" 1987-90.
Mbele said…
Ndugu Anonymous uliyeandika August 4, shukrani kwa ujumbe wako. Lo, kumbe ulichukua somo langu la "Oral Literature."

Basi napenda kukueleza kuwa nimeendelea na utafiti kwa dhati miaka yote hii. Nitakaporejea Tanzania, nikishastaafu hapa Marekani, nitakuwa natoa elimu ya hali ya juu kuliko zamani. Sina sababu ya kumezea maneno hapa. Na pia nazingatia kuwa ni Mungu aliyenipa fursa hii.

Nakutakia kila la heri.
Unknown said…
Ninahitaji vitabu hivyo jmn nitavipataje? Mawasilia beno yangu ni 0758050374

Popular posts from this blog

Tenzi Tatu za Kale

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Filamu ya "Papa's Shadow:" Fursa ya Kuitangaza Tanzania