Hatimaye Itabidi Nielezee Nilivyotoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam

Mwaka 1991 niliondoka Chuo Kikuu Dar es Salaam, nikaja kufundisha Chuo cha St. Olaf hapa Marekani. Kulikuwa na mlolongo wa masuala yaliyonifanya nikaondoka, baada ya kuwa mwalimu pale kuanzia mwaka 1976. Sijaelezea masuala hayo, ingawa yamo katika maandishi kwenye makabrasha, ambayo yalikuwa mawasiliano rasmi baina ya wahusika.

Mwaka jana, nikiwa maeneo ya Mwenge, Dar es Salaam, na marafiki zangu, nilikutana na Profesa Sam Maghimbi wa Chuo cha Elimu cha Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Nilishangaa alivyokumbushia nilivyotoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na marafiki zangu wakasikia. Nilifarijika kuona kuwa kumbukumbu bado zipo kiasi hiki.

Wako wengi wanaokumbuka nilivyofundisha Chuo Kikuu Dar es Salaam, na jinsi nilivyoondoka. Lakini, kwa jinsi miaka inavyopita, wanafikia umri wa kustaafu, na wengine wamefariki. Nami natatizwa na fikra ya wa-Tanzania wengi za kudhani kila m-Tanzania anayeenda kufanya kazi nje hana sababu nyingine bali kufuata maslahi binafsi. Hata mafisadi waliozagaa nchini nao wanaimba wimbo huo huo waonekane wazalendo. Jambo hili linanikera, na ndio maana naona itabidi niandike habari zangu.

Comments

John Mwaipopo said…
mimi pia nadhani ni vema ukafanya hivyo. ni sehemu ya historia sasa, historia yako na ya chuo. nadhani hata kama kulikuwa na uonevu wa upande mmoja, mlikwisha weka kando tofauti za kibinadamu
Mbele said…
Mkuu, shukrani kwa ujumbe wako. Ni kweli, sio vizuri historia isahauliwe, iwe ni ya mtu binafsi, ya taasisi, jamii, nchi na kadhalika.

Kama nilivyogusia, wako ambao tulifanya kazi pamoja pale Chuo Kikuu Dar na walinifahamu vizuri kabisa. Nitakuwa radhi iwapo ukiwakuta huko mitaani ukawaulizia habari zangu. Huenda ikawa bora zaidi kuliko mimi kupiga ngonjera juu yangu mwenyewe.

Baadhi yao ni Profesa Hamza Njozi (makamu wa mkuu wa Chuo Kikuu cha ki-Islam Morogoro), Dr. Balla Masele na Dr. Adam Korogoto (wa Idara ya "Literature" Chuo Kikuu Dar), Mheshimiwa Richard Mabala, Profesa Issa Shivji, Profesa Mugyabuso Mulokozi (aliyestaafu Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili CHuo Kikuu Dar), Profesa Kulikoyela Kahigi (Mbunge wa Bukombe, CHADEMA), Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Shaaban Mlacha (wa UDOM) na Profesa Joshua Madumula (wa UDOM). Hao ni baadhi tu ya watu walionifahamu vizuri sana.

Ukiwakuta, jisikie huru kuwaulizia. Wakikuambia kuwa nilikuwa mbabaishaji na mkorofi, itabidi uzingatie, kwani hao ni watu makini. Nitakachohitaji ni kuandika historia sahihi iwezekanavyo, kuzimisha majungu.
Anonymous said…
mh! inavyoonekana kuna mambo mazuri prof..tuweke wazi sasa kihistoria
Mbele said…
Mdau anonymous, shukrani kwa kupitia hapa kijiweni pangu. Masuala yenyewe ni tata, au labda niseme tete.

Popular posts from this blog

Tenzi Tatu za Kale

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Filamu ya "Papa's Shadow:" Fursa ya Kuitangaza Tanzania