Vitabu Kama Zawadi ya Idd el Fitr na Krismasi

Hebu fikiria: sikukuu ya Idd el Fitr au Krismasi imewadia na unataka kuwapa zawadi ndugu na marafiki zako, wa-Tanzania wenzako. Unaamua kwenda kwenye duka la vitabu, na unawanunulia nakala za kitabu kama Kufikirika cha Shaaban Robert, au Binadamu na Maendeleo cha Mwalimu Nyerere, au kwa wanaojua ki-Ingereza, The Tempest cha Shakespeare. Unawafungia vizuri, kisha unawapelekea. Je, watajisikiaje hao wa-Islam na wa-Kristu wa Tanzania?

Miaka ya tisini na kitu, katika jumuia ya mawasiliano ya mtandaoni iitwayo Tanzanet, ambayo wanachama wake ni wa-Tanzania na marafiki wa Tanzania, niliwahi kuandika, kiutani, kwamba siku za usoni huenda nikaamua kwamba, kwenye mialiko ya arusi nisipeleke kreti ya bia, bali kreti ya vitabu. Ingawa ulikuwa ni mchapo, nilikuwa na jambo muhimu kichwani, kwani ni kweli kuwa vitabu ni hazina, na ni bora kuliko bia.

Hapa Marekani, ni kawaida watu kutoa au kupokea zawadi ya vitabu. Msimu kama huu wa Krismasi, watu wengi wananunua vitabu ili kuwapa zawadi wenzao. Hata kwenye arusi, mtu unaweza kutoa zawadi ya kitabu.

Je, ukimpa m-Tanzania zawadi ya kitabu wakati wa Idd el Fitr au Krismasi, itakuwaje? Tafakari hilo.

Comments

www.visionowners.com said…
Nimefurahishwa sana na jambo hili la kupenda vitabu... Ninatafakari unayoyayaandika humu...Napata faraja moyoni mwangu kuona kuwa bado kuna watanzania wenye kupenda ufahamu kwa kupitia katika vitabu.

Naungana na wewe katika wazo lako. Tafadhali usilione kuwa ni utani. Toa vitabu hata kama watu hawatakuelewa. Vitabu ni hazina ya ajabu ambayo huwa haiozi ikiwa kichwa cha msomaji (na mwenye uwezo wa kuelewa)kinabaki kuwa makini.

Endeleza kazi njema ya kuielimisha jamii ya dunia nzima bila kujali mipaka, itikadi za watu, imani zao au mawazo ya wachache yenye kukatisha tamaa..
Mbele said…
Mdau hapo juu, shukrani kwa ujumbe wako ambao umenifanya niamue kuwa nitafanya jaribio hilo la kuwapelekea watu vitabu kama zawazi ya Idd el Fitr, Krismasi, "send=off," arusi, kipaimara, na kadhalika.

Umenikumbusha jambo ambalo niliwahi kuandika katika blogu hii, kwamba watoto wa Tanzania wanapenda vitabu. Kwa maana hiyo, watoto wakipewa vitabu kwenye sherehe zao, watafurahi.

Halafu, nawazia kuwa nikipeleka vitabu kwenye arusi, wahusika labda watajiuliza kulikoni, lakini labda, wakiwa makini, wataelewa kuwa ni hazina kwao na kwa watoto ambao huenda Mungu akawajalia.

Mapinduzi ya fikra yanaweza kuanza kidogo kidogo namna hii. Shukrani kwa kuniongezea motisha.
Anonymous said…
Nitafurahi sana kupata kitabu kama kufikirika. Natafuta Kichomi 9 kezilehabi) na Fadhili Msiri wa Naugua ( simkumbuki mtunzi) Hazina Binti Sultani ( nadhani Shaaban)
Mbele said…
Mdau anonymous, vitabu vya Shaaban Robert, kama vile "Kufikirika," vimechapishwa upya na kampuni ya Mkuki na Nyota, na vinapatikana kiurahisi kwenye maduka kama Tanzania Publishing House, pale Mtaa wa Samora karibu na sanamu ya Askari.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini