Posts

Showing posts from May, 2011

Safari ya Bajaji: Lushoto Hadi Irente

Image
Agosti 6, mwaka jana, nilisafiri kutoka Lushoto kwenda Irente. Nilishawahi kusafiri hadi Irente miaka michache kabla, nikitumia teksi. Lakini mwaka jana niligundua kuwa ningeweza kusafiri kwa bajaji. Bajaji yenyewe ndio hii inayoonekana katika picha, na dreva wake. Bajai hii ilikuwa maarufu mjini Lushoto. Niliziona bajaji kwa mara ya kwanza nilipokuwa India, mwezi Aprili mwaka 1991. Wakati huo hapakuwa na bajaji Tanzania. Lakini kidogo kidogo, miaka iliyofuatia, bajaji zilianza kuonekana, na leo zimejaa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam. Sasa zinaonekana hata kwenye miji midogo kama Lushoto. Ndio mambo ya ulimwengu katika utandawazi wa leo. Safari ilikuwa murua. Bajaji ilikula milima na kukwepa mifereji na mashimo kama mchezo. Tulipofika Irente, nilianza kuwatafuta vijana wawili mapacha ambao niliwafahamu miaka iliyotangulia, wakati nafanya utafiti kuhusu masimulizi juu ya Osale Otango na Paulo Hamisi. Osale Otango na Paulo Hamisi ni maarufu katika historia ya miaka ya hamsini n

Kanisa laingilia kati mauaji ya North Mara

Kanisa laingilia kati mauaji ya North Mara By George Marato 30th May 2011 CHANZO: NIPASHE Wiki chache baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalum Tarime na Rorya, kutuhumiwa kuwaua kwa risasi raia watano na kujeruhi wengine kadhaa wakidaiwa kutaka kuvamia mgodi wa North Mara, Kanisa la Anglikana Doyosisi ya Tarime limeitaka serikali kuacha kuingiza siasa katika kutafutia ufumbuzi wa mgogoro huo. Kanisa hilo limesema mgogoro huo wa muda mrefu kati ya wawekezaji na wananchi wanaozunguka mgodi huo unaomilikiwa na kampuni ya African Barrick Gold, umechangiwa na serikali kushindwa kuchukua hatua za haraka za kuwapatia haki ya msingi wananchi wa eneo hilo. Akizungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE nyumbani kwake juzi mjini Tarime, Askofu wa Anglikana Dayosisi ya Tarime, Dk Mwita Akiri, alisema lazima serikali ibebe lawama kuhusu mgogoro huo na roho za watu zinazopotea kila wakati kwa kushindwa kuchukua hatua za kuwatengea eneo mbadala la uchimbaji wananchi hao. “Ndio tunakubali sera

Someni kwa Furaha

Image
Wiki kadhaa zilizopita, nikiwa Madison, katika mkutano wa Peace Corps , niliingia katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison . Nilifurahi kuingia katika maktaba hii, ambayo niliizoea wakati nasoma katika chuo hicho, 1980-86. Niliangalia vitabu vya ki-Swahili, ambavyo ni vingi katika maktaba hii, nikavutiwa na vitabu vya Someni Kwa Furaha , tulivyosoma tulipokuwa shule ya msingi. Nilijikumbusha kuhusu Bulicheka na mke wake Lizabeta, Wagagagigikoko na mfalme wao, Makari Hodari, Kalumekenge, na Pauli mwenye mikono michafu. Tulibahatika, enzi za utoto wetu, kuwa na vitabu vya kusisimua, vilivyotupa motisha ya kusoma. Vitabu hivi viliandikwa kuzingatia umri wetu. Walimu walikuwa makini, katika kufundisha, kwa mbinu mbali mbali, kama vile nyimbo. Tuliimba alfabeti hadi orodha. Nawasifu na kuwashukuru waalimu wale.

Nataka Tanzania Isitawalike Kamwe

Nataka Tanzania isitawalike kamwe. Kama hupendi kusikia hayo, shauri lako. Mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa, ila nataka Tanzania isitawalike. Nataka Tanzania iwe na viongozi, sio watawala. Wanaotaka kutawala wasipate nafasi hiyo. Uongozi unahitaji busara na ushawishi, kukubalika na jamii husika. Kama ni kutawaliwa, tulitawaliwa na wakoloni. Masultani walikuwa wanatawala. Walikuwa wakandamizaji, sawa na wakoloni. Wazee wetu walipambana hadi Uhuru ukapatikana. Nataka nchi yetu iimarishe misingi ya Uhuru na demokrasia. Kutawala ni suala la mabavu, kwani hakuna jamii inayokubali kutawaliwa, labda iwe ni jamii ya wajinga, au waoga, au ambao wamelishwa sana kasumba ili wasitambue haki zao. Lakini jamii inayojitambua, inayotambua maana ya uhuru, haki, na demokrasia, jamii inayothamini na kutetea hayo, haiwezi kutawalika, labda kwa mabavu na vitisho. Itakuwa ni jambo la kuhuzunisha iwapo Tanzania itatawalika. Nataka tuwe macho, tuwe makini, nchi yetu isitawalike, kamwe.

Maktaba ya Mkoa, Kilimanjaro

Image
Tarehe 3 Agosti, mwaka jana, nilikuwa mjini Moshi nikiwa na hamu ya kuufahamu zaidi mji huo. Lengo langu moja lilikuwa kuiona maktaba ya mkoa, kwani nilikuwa sijawahi kufika hapo. Haikuwa vigumu kufika mahali hapo. Niliingia ndani nikaona kuwa ni maktaba yenye hali nzuri kwa ujumla, kwa upande wa vitabu na majarida, nikifananisha na maktaba kadhaa nilizoziona sehemu zingine za nchi. Kwa kawaida, ninapoingia katika maktaba za Tanzania, nimezoea kuwaona zaidi wanafunzi. Katika maktaba ya Moshi, niliwaona watu wazima kadhaa wakisoma. Sijui kama hii ndio kawaida katika maktaba hii, lakini niliguswa na jambo hilo. Kila maktaba duniani, hata kama ni bora namna gani, inahitaji vitabu na majarida mapya muda wote, pamoja na tekinolojia na vifaa vya kisasa vya kupatia maandishi na taarifa. Na ndiyo changamoto kwa maktaba za Tanzania. Nimeona niweke hii taarifa fupi na picha kwenye blogu yangu, ili wengine wapate angalau fununu kuhusu hii maktaba ya Moshi.

"Mama m-Katoliki" (shairi kutoka India)

Uandishi wa ki-Ingereza wa India unafahamika zaidi katika tanzu ya riwaya na hadithi fupi, ingawa waandishi wa mashairi pia wapo, kama vile Kamala Das, Nissim Ezekiel na Jayanta Mahapatra. Leo wanafunzi wangu wa somo la fasihi ya Asia Kusini walifanya mtihani wa mwisho, na suali moja nililowapa lilihusu shairi la "Catholic Mother," lililotungwa na Eunice de Souza . Suali nililowapa ni hili: "Discuss the poem, "Catholic Mother," by Eunice de Souza. Say what you want about it. In addition, compare the woman in this poem with Anil, a key character in Michael Ondaatje's Anil's Ghost ." Sijui kwa nini, baada ya mtihani kumalizika, nimepata wazo la kulitafsiri shairi hili na kuliweka hapa kwenye blogu yangu. Ingawa lugha aliyotumia mtunzi inaonekana ni ya kawaida tu, ameingiza tamathali za usemi kiurahisi, lakini kwa uhodari na kufikirisha. Amepenyeza na kuchochea uchambuzi wa masuala muhimu ya jamii, kama vile dini, udini na jinsia. Vile vile, ni

Nimekutana na Mpiga Debe Wangu

Image
Leo nimekutana na mzee Don Fultz na Mama Eunice Fultz katika mji wa Eagan, Minnesota. Nilienda kule na mfanyakazi mwenzangu wa chuo cha St. Olaf ambaye tunashughulikia programu za kupeleka wanafunzi nchi za nje. Katika picha hizi, Mzee Fultz na Mama Fultz wameketi katikati. Mzee Fultz ni mchungaji wa kanisa la ki-Luteri, sinodi ya St. Paul . Anaishi hapa Minnesota na Iringa, akiendesha programu za ushirikiano. Mchungaji Fultz ni mtu wa pekee kwangu. Ni mfuatiliaji makini wa shughuli zangu za kuwaelimisha wa-Marekani na wa-Afrika kuhusu tofauti za tamaduni zao. Ni mpiga debe mkubwa wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Tangu wakati kitabu hicho kilipokuwa ni kijimswada tu kisichokamilika, Mchungaji Fultz alikibeba na kukipigia debe hapa Marekani. Hakuwa peke yake katika kufanya hivyo. Nilivyoona hivyo nilishtuka, nikaamua kukifanyia kazi kimswada hiki na kukiboresha. Kazi hiyo niliifanya kila siku kwa miezi minne, hadi nikakichapisha kitabu mwezi F

Kitabu Kuhusu Mwanamuziki Salif Keita

Image
Mchana huu nilikuwa kwenye chuo jirani cha Carleton kuhudhuria uzinduzi wa kitabu kuhusu Salif Keita , kilichoandikwa na Profesa Cherif Keita. Profesa Keita ambaye anafundisha Carleton anatoka kijiji kimoja na Salif Keita, na walikua wakicheza pamoja utotoni. Ni marafiki hadi leo, na Profesa Keita alishamleta Salif Keita kwenye mji wetu huu wa Northfield kutumbuiza. Profesa Keita ni mtafiti aliyezama sana katika masuala ya utamaduni, fasihi na falsafa ya jadi ya watu wa Mali. Ndiye hasa mtu anayeweza kutueleza kwa undani kuhusu maisha, sanaa na falsafa ya mwanamuziki Salif Keita. Salif Keita ni miongoni mwa wanamuziki wa ki-Afrika ambao ni maarufu kabisa. Salif Keita ni albino, na maisha yake tangu alipozaliwa yamekuwa na misukosuko ya kusikitisha. Profesa Keita katika maelezo yake leo alidokezea hayo. Salif pia ni mwanaharakati katika kutetea haki na maslahi ya albino. Ameanzisha na anaendesha taasisi inayoshughulikia suala hilo. Kiasi fulani cha mauzo ya kitabu hiki kitasaid

Kikombe cha Mwenyekiti Maggid

Image
Kama sote tunavyojua, wa-Tanzania tuko kwenye awamu ya vikombe. Waganga wamejitokeza nchini mwetu, wakiwa na vikombe vya kuponyesha magonjwa mbali mbali. Wateja wengi wanatoa ushuhuda kuhusu uponyaji wao. Nami napenda kutoa ushuhuda kuhusu kikombe cha Mwenyekiti Maggid Mjengwa. Nianze kwa kusema kuwa Mwenyekiti Maggid ni mwalimu, mwandishi na mwanablogu . Hajawa mganga wa kienyeji. Isipokuwa, kikombe ameninywesha. Tega sikio nikuhadithie. Mwaka 2009 mwanzoni, Mwenyekiti Maggid alianzisha gazeti la Kwanza Jamii , akaniomba niwe mchangiaji. Nilikubali. Sikutambua kuwa nilijipalia mkaa, maana nilijikuta nahangaika kuandika hizo makala na kuzituma kwa muda uliotakiwa. Ilikuwa ni kazi ya kuumiza kichwa. Kwanza kabisa, wakati mwingine nilikuwa sijui niandike kuhusu nini. Huku siku na saa za kuwasilisha makala zinaendelea kusogea, nami bila kujua mada ya kuandikia, nilibaki nimekodoa macho na jasho linanitoka. Mara kwa mara Mwenyekiti Maggid alikuwa ananiletea ujumbe usiku kwenye saa sita

Mitaani Namanga, 2007

Image
Ingawa mdogo, mji wa Namanga ni maarufu, kwa vile uko mpakani. Hapa naonekana nikiwa Namanga, upande wa Tanzania. Naelekea kwenye geti la mpaka, hatua chache mbele yangu. Kule mbali unaona Mlima Longido. Barabara inapita kulia kwake, inaingia Longido, nyuma ya mlima, na kuelekea Arusha. Hii ni moja ya hoteli ambapo napenda kufikia, kwa Bwana Minja, kupata chakula na kinywaji. Nimeshalala hapo. Nilipendezwa na mpangilio wa nyumba hizi na ile milima. Hizi nyumba ziko mwanzoni mwa mji wa Namanga, kabla hujafika kwenye geti la mpaka baina ya Kenya na Tanzania. Nilikuwa Namanga na kikundi cha wanafunzi kutoka Chuo cha Colorado na mwalimu wao, ambao walifika Tanzania katika kozi niliyoiunda, kuhusu mwandishi Hemingway . Hao ni wanafunzi waanzilishi wa kozi hii. Napangia kuibadili kidogo na kuiweka katika program ya Chuo cha St. Olaf . Hapa nipo upande wa Kenya. Kama mdau unavyoona, mapokezi hayakuwa haba. Ndio mambo ya ujirani mwema hayo. Namanga, kama ilivyo miji

Siku ya Waalimu

Image
Leo, huku Marekani, ni siku ya kuwaenzi waalimu . Wiki hii nzima ni wiki ya kuwakumbuka, lakini leo ni kama kilele. Na mimi, mwalimu wa chuo kikuu, nimeshaandika kuwa namwenzi kwa namna ya pekee mwalimu wa shule ya msingi . Kwa vile ualimu ni sehemu ya nafsi yangu, huwa natafakari suala la ualimu na dhima yake katika maisha yangu na maisha ya wanafunzi . Leo na wiki hii najisikia furaha kujumuika na wale wote wanaothamini mchango wetu. (Picha ya kwanza hapo juu niliipata kwenye blogu ya Haki Ngowi , ambaye aliripoti kuwa ilipigwa na Brandy Nelson. Picha ya pili sikumbuki niliipata kutoka blogu gani. Ningependa kutoa shukrani).

Watu Wema Wasio na Dini

Katika mizunguko yangu hapa duniani, nimepata kukutana na watu wasio na dini, lakini ni watu wema sana, waungwana. Sio wachokozi au watu wa majungu. Ni waaminifu, wala hawatakudhulumu. Nimefanikiwa kufahamiana na kuishi na watu wa aina hiyo. Wengine wamekuwa wanafunzi wangu huku ughaibuni. Ukiwauliza kuhusu dini, wanakuambia hawaamini kama kuna Mungu, na hawana dini. Hao watu ni changamoto kubwa kwetu sisi tunaosema tuna dini, hasa pale inapokuwa kwamba hatuwafikii kwa wema na utu. Ni kitendawili. Inakuwaje watu hao wawe hivyo walivyo, wakati hawana dini? Kazi kwenu wadau.