Showing posts with label Kusoma. Show all posts
Showing posts with label Kusoma. Show all posts

Tuesday, December 20, 2016

Zawadi ya Krismasi

Siku tatu zilizopita, jirani yangu m-Marekani, mama mwenye umri zaidi yangu, aliniomba nimsainie nakala za kitabu cha Africans and Americans Embracing Cultural Differences. Alikuwa amevinunua kwa ajili ya kuwapelekea rafiki zake, wa-Marekani wenzake, kama zawadi ya Krismasi.

Jambo hili lilitosha kunifanya niandike ujumbe katika blogu yangu, kwani linadhihirisha jadi ninayoiona hapa Marekani, kama nilivyowahi kudokeza katika blogu hii. Lakini nimehamasika kuandika baada ya kusoma makala ambayo ameichapisha Christian Bwaya katika blogu yake. Ameelezea umuhimu wa zawadi kwa watoto na mambo ya kuzingatia katika kutoa zawadi kwa watoto.

Kati ya mifano ya zawadi alizotaja ni vitabu. Ni jambo muhimu, nami kama mwalimu ninaliafiki moja kwa moja. Nimejionea jinsi watoto wanavyopenda vitabu, sio tu hapa Marekani, bali pia Tanzania. Nimeandika mara kwa mara umuhimu wa kuwasomea watoto vitabu na kuwajenga watoto katika utamaduni wa kusoma vitabu. Huwa ninafarijika ninaposoma taarifa za uhamasishaji wa suala hilo.

Tutakuwa tumepiga hatua kubwa iwapo tutajijengea utamaduni wa kuwanunulia watoto vitabu kama zawadi, kwani wanavipenda vitabu. Tutakuwa tumepiga hatua iwapo vijana wetu na watu wa kila rika watakuwa na utamaduni wa kuthamini zawadi ya vitabu.

Tuesday, November 22, 2016

Ninaendelea Kusoma "Hamlet"

Miaka miwili iliyopita, niliandika katika blogu hii kuwa nina tabia ya kusoma vitabu kiholela. Wakati wowote nina vitabu kadhaa ninavyovisoma, bila mpangilio maalum, na pengine bila nia ya kufikia mwisho wa kitabu chochote.

Kusoma kwa namna hii hakuna ubaya wowote, bali kuna manufaa. Nilipokuwa mwanafunzi wa sekondari, katika seminari ya Likonde, mwalimu wetu, Padri Lambert OSB alituhimiza tuwe na mazoea ya kusoma sana vitabu, na pia mazoea ya kuvipitia vitabu kijuu juu, ambayo kwa ki-Ingereza huitwa "browsing."

Nikiachilia mbali vitabu ninavyofundisha, wakati huu nimezama zaidi katika kusoma Hamlet, kama nilivyoandika katika blogu hii. Ninasoma Hamlet pole pole, ili kuyanasa vizuri akilini yaliyomo, hasa maudhui kuhusu maisha, maadili, na tabia za binadamu. Kusoma pole pole kunaniwezesha kukifurahia ki-Ingereza cha Shakespeare, ingawa si rahisi kama ki-Ingereza tunachotumia leo.

Tofauti kati ya ki-Ingereza cha leo na kile cha Shakespeare ninaifananisha na tofauti kati ya ki-Swahili cha leo na kile cha mashairi ya zamani kama yale ya Muyaka au Utenzi wa Rasi lGhuli. Kwa msingi huo, kusoma utungo kama Hamlet ni chemsha bongo inayoboresha akili, sawa na mazoezi ya viungo yanavyoboresha afya ya mwili.

Mwandishi maarufu Ernest Hemingway alielezea vizuri thamani ya vitabu aliposema, "There is no friend as a loyal as a book," yaani hakuna rafiki wa kweli kama kitabu. Ujumbe uko wazi, nami sina la kuongeza. Kitabu bora ukishakinunua, ni rafiki wa kudumu.


  

Thursday, September 8, 2016

Wasomaji Wangu Wa Nebraska Waendao Tanzania

Nina jadi ya kuwaongelea wasomaji wangu katika blogu hii, kama njia ya kuwaenzi. Ni jambo jema kwa mwandishi kufanya hivyo. Leo ninapenda kuwakumbuka wasomaji wangu wa sinodi ya Nebraska ya Kanisa la Kiluteri la Marekani, ambao tangu zamani wamekuwa na programu ya kupeleka watu Tanzania kuendeleza uhusiano baina yao na wa-Luteri wa Tanzania.

Hao wasafiri, sawa na wenzao wa sinodi zingine za Marekani, wamekuwa wakitumia kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences katika kujiandaa kwa safari, ili kuzielewa tofauti za tamaduni za Marekani na Afrika. Ni elimu muhimu katika ulimwengu wa utandawazi wa leo, ambayo nje ya ufundishaji wa darasani, ninashughulika nayo.


Wakati huu ninapoandika, waumini wa Nebraska wanajiandaa kwa safari ya Tanzania, ambayo itafanyika mwezi Februari mwaka 2017. Wameitangaza safari hii mtandaoni, na mratibu mojawapo wa safari, Martin Malley, ameniandikia ujumbe leo akisema, "We still recommend your book." Katika ukurasa wa 16 wa chapisho la maelezo na maandalizi ya safari, kitabu hicho kimetajwa.

Ninapowakumbuka wasomaji wangu wa Nebraska, ninakumbuka nilivyokutana katika uwanja wa ndege wa Amsterdam na kikundi cha watu wa Nebraska waliokuwa wanakwenda Tanzania, tukasafiri pamoja. Mimi sikuwajua, ila wao walinitambua, kama nilivyoelezea katika blogu yangu ya ki-Ingereza.


Friday, February 19, 2016

"Tenzi Tatu za Kale:" Makala Inayosomwa Kuliko Zote

Mara kwa mara, ninaangalia takwimu zinazohusu blogu yangu hii: idadi ya watembeleaji, makala wanazozitembelea, na nchi walimo. Kuanzia wiki kadhaa zilizopita, makala inayotembelewa kuliko zote ni "Tenzi Tatu za Kale." Idadi ya watembeleaji iliongezeka ghafla pale Ndugu Michuzi alipoiweka makala hii katika blogu yake.

Ninajiuliza kwa nini makala hii inawavutia wasomaji namna hii. Je, hii ni ishara ya kupendwa kwa somo la fasihi ya ki-Swahili? Siamini kama ni hivyo, kwani ninaandika makala nyingi kuhusu fasihi, ambazo zinagusia tungo mbali mbali. Ingekuwa uwingi wa wasomaji unaonekana kwenye makala hizo pia, ningeamini kuwa kuna msisimko wa kupenda fasihi.

Ninapata hisia kwamba labda uhusiano na mahitaji ya shuleni au vyuoni. Ninahisi kuwa labda wanaosoma makala ya "Tenzi Tatu za Kale" ni wanafunzi ambao wanatakiwa kusoma Utenzi wa Al Inkishafi, au Utenzi wa Mwana Kupona, au Utenzi wa Fumo Liyongo: moja, mbili, au zote tatu.

Kama ni hivyo, si jambo la kuridhisha wala kufurahisha. Uwanja wa fasihi ya ki-Swahili ni mpana, na mwenye mapenzi na fasihi hii ninamtegemea awe anasoma tungo nyingi. Hata wanafunzi wa fasihi wanatakiwa kusoma tungo mbali mbali, si zile zilizomo katika mitaala tu.

Ningependa sana kuona mijadala ya fasihi ya ki-Swahili katika blogu hii. Ndio maana ninaweka taarifa mbali mbali kuhusu tungo za ki-Swahili. Tuienzi fasihi hii kwa kuisoma bila mipaka, kuichambua, na kuitangaza.
 

Thursday, May 26, 2011

Someni kwa Furaha

Wiki kadhaa zilizopita, nikiwa Madison, katika mkutano wa Peace Corps, niliingia katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Nilifurahi kuingia katika maktaba hii, ambayo niliizoea wakati nasoma katika chuo hicho, 1980-86.

Niliangalia vitabu vya ki-Swahili, ambavyo ni vingi katika maktaba hii, nikavutiwa na vitabu vya Someni Kwa Furaha, tulivyosoma tulipokuwa shule ya msingi.

Nilijikumbusha kuhusu Bulicheka na mke wake Lizabeta, Wagagagigikoko na mfalme wao, Makari Hodari, Kalumekenge, na Pauli mwenye mikono michafu.

Tulibahatika, enzi za utoto wetu, kuwa na vitabu vya kusisimua, vilivyotupa motisha ya kusoma. Vitabu hivi viliandikwa kuzingatia umri wetu. Walimu walikuwa makini, katika kufundisha, kwa mbinu mbali mbali, kama vile nyimbo. Tuliimba alfabeti hadi orodha. Nawasifu na kuwashukuru waalimu wale.

Saturday, April 24, 2010

Nimepita Tena Kwenye Duka la Vitabu

Leo nilikuwa Minneapolis nikihudhuria kikao cha kuandaa mkutano wa waAfrika, Wamarekani Weusi na wengine wenye asili ya Afrika ambao tutafanya Oktoba tarehe 9, 2010. Nilihudhuria pia kikao cha bodi ya Afrifest.

Nilipokuwa narudi, nilipita mjini Apple Valley, nikaingia kwenye duka la vitabu la Half Price Books. Duka hili nimelitembelea mara nyingi na nilishawahi kuandika habari zake katika blogu hii. Niliyoyaona leo ni yale ambayo nayaona daima ninapotembelea maduka ya vitabu hapa Marekani. Watu wengi walikuwemo, watoto, vijana, wazee, wake kwa waume. Wazazi wengine walikuwemo na watoto wadogo sana, na hata watoto wachanga.

Duka ni kubwa, lakini watu walikuwa wanapishana kila sehemu, wakiangalia vitabu, wakivisoma, na kuvinunua. Wengine walikuwa wanawasomea watoto wao hadithi. Watoto wadogo sana niliwasikia wakiongea na wazazi au kujibizana nao kuhusu vitabu. Ni jambo la kugusa sana moyoni unapomwona mama ameketi akijibizana na mtoto wake kuhusu kitabu ambacho mtoto anaangalia.

Ndivyo watoto wa ki-Marekani wanavyolelewa. Nimeshaandika kuhusu suala hili katika makala mbali mbali katika blogu hii na katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Muda wote niliokuwa katika duka lile nilikuwa na fikra zile zile za kila siku, nikiwazia malezi ya watoto hao na kufananisha na malezi ya watoto wetu Tanzania. Hatuna maduka ya vitabu kama Marekani, ingawa tunazo baa katika kila mji, hata miji midogo, na kila kona. Hatuna utamaduni wa kusoma vitabu na kuwapeleka watoto wetu kwenye maduka ya vitabu au maktaba.

Wakati wenzetu wanawajengea watoto wao msingi imara wa kutafuta elimu, sisi tunachezea maisha yetu na maisha ya watoto wetu. Je, katika dunia hii, inayohitaji elimu na maarifa, watoto wetu wataweza kushindana na hao watoto wa wenzetu?

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...