Zawadi ya Krismasi

Siku tatu zilizopita, jirani yangu m-Marekani, mama mwenye umri zaidi yangu, aliniomba nimsainie nakala za kitabu cha Africans and Americans Embracing Cultural Differences. Alikuwa amevinunua kwa ajili ya kuwapelekea rafiki zake, wa-Marekani wenzake, kama zawadi ya Krismasi.

Jambo hili lilitosha kunifanya niandike ujumbe katika blogu yangu, kwani linadhihirisha jadi ninayoiona hapa Marekani, kama nilivyowahi kudokeza katika blogu hii. Lakini nimehamasika kuandika baada ya kusoma makala ambayo ameichapisha Christian Bwaya katika blogu yake. Ameelezea umuhimu wa zawadi kwa watoto na mambo ya kuzingatia katika kutoa zawadi kwa watoto.

Kati ya mifano ya zawadi alizotaja ni vitabu. Ni jambo muhimu, nami kama mwalimu ninaliafiki moja kwa moja. Nimejionea jinsi watoto wanavyopenda vitabu, sio tu hapa Marekani, bali pia Tanzania. Nimeandika mara kwa mara umuhimu wa kuwasomea watoto vitabu na kuwajenga watoto katika utamaduni wa kusoma vitabu. Huwa ninafarijika ninaposoma taarifa za uhamasishaji wa suala hilo.

Tutakuwa tumepiga hatua kubwa iwapo tutajijengea utamaduni wa kuwanunulia watoto vitabu kama zawadi, kwani wanavipenda vitabu. Tutakuwa tumepiga hatua iwapo vijana wetu na watu wa kila rika watakuwa na utamaduni wa kuthamini zawadi ya vitabu.

Comments

Anonymous said…
Sijapita siku nyingi sana huku, nimekaa nikakumbuka,
Nakutakia sikukuu njema prof.
Mbele said…
Shukrani ndugu Anonymous kwa kunitembelea. Kama unavyoona, bado ninajikongoja na hiki kiblogu changu. Nami nakutakia sikukuu njema.

Popular posts from this blog

Tenzi Tatu za Kale

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Filamu ya "Papa's Shadow:" Fursa ya Kuitangaza Tanzania