Leo nimemaliza kufundisha muhula wa kwanza. Nilikuwa ninafundisha kozi tatu: "First Year Writing," "African Literature," na "Muslim Women Writers." Nilihitimisha ufundishaji wa "First Year Writin"g wiki iliyopita, ili kuwapa wanafunzi muda wa kuandika insha kuu ya mwisho. Katika kozi hii, ninafundisha uandishi bora wa ki-Ingereza, na uangalifu unaotakiwa katika vipengele vyote , kuanzia neno, hadi sentensi, hadi insha.
Katika African Literature tumemalizia muhula tukisoma riwaya ya Mia Couto, The Tuner of Silences. Mia Couto ni mwandishi wa Msumbiji, ambaye ni maarufu sana. Amepata sifa na tuzo kem kem, ikiwemo tuzo ya Neustadt. The Tuner of Silences ni riwaya inayosisimua akili kwa jinsi ilivyosheheni ubunifu wa kisanaa na kifikra.
Kuna mengi ya kutafakari katika riwaya hii, hasa yatokanayo na dini, fasihi linganishi, historia, falsafa kama vile "existentialism," na mikondo ya falsafa ya sanaa kama vile "surrealism." Vile vile, taaluma ya saikolojia, kama vile mkondo wa "psychoanalysis," inasaidia kutafakari dhamira zilizomo. Kuisoma na kuufaidi utajiri wa riwaya kama The Tuner of Silences kunahitaji upeo mpana wa mawazo ambao unatokana na kusoma kwingi, sio tu fasihi bali taaluma mbali mbali.
Katika kuiongelea The Tuner of Silences darasani, nimesisitiza jambo hilo, Nimefundisha wanafunzi umuhimu wa kuzingatia nadharia za usomaji kama zilivyoelezwa na Cleanth Brooks katika insha yake, "The Language of Paradox," na pia zilivyoelezwa na Roland Barthes katika kitabu chake kiitwacho S/Z: An Essay.
Katika kozi ya "Muslim Women Writers," tumemalizia muhula tukisoma riwaya ya Monica Ali, Brick Lane. Ni riwaya ndefu, inayoelezea maisha ya watu wa Bangladesh ambao wanaishi Uingereza. Ni jamii ya ki-Islam, na tunaiona inavyojitahidi kustahimili na kustawi katika mazingira ya ugenini.
Hii ni jamii kama jamii zingine, yenye watu wenye maadili mema na ari ya kuwa mfano kwa wengine, na pia wako ambao tabia zao zina walakini. Wanapenda kufuatilia habari za wenzao, na ni wapiga majungu. Tofauti baina ya utamaduni wao na ule wa wa-Ingereza zinajitokeza, na pia tofauti baina ya vijana na watu wazima au wazee. Vijana wanaonekana kuiga mambo ya vijana wa kizungu, yakiwemo ambayo si mazuri.
Kufundisha kazi ya fasihi kutoka Bangladesh imekuwa ni fursa ya kuelezea historia ya fasihi ya nchi hiyo, ukiwemo mchango mkubwa wa Rabindranath Tagore, mwandishi wa mashairi, tamthilia, riwaya, na insha, ambaye aliitwaa tuzo ya Nobel mwaka 1913. Kwa bahati nzuri, Tagore ametajwa katika Brick Lane, kwa jinsi alivyo hazina kwa watu wa Bangladesh. Lakini jambo la kuzingatia ni kuwa Tagore ni mwamba katika fasihi ya ulimwengu, aliyeheshimiwa na miamba wenzake kama vile W.B. Yeats wa Ireland, aliyekuwa na urafiki na mawasiliano na Tagore.
Leo, katika kuhitimisha kozi yetu ya "Muslim Women Writers," nimewaomba wanafunzi ushauri juu ya kuitumia tena riwaya hii siku za usoni, nitakapofundisha kozi hii. Wameniambia kuwa ni riwaya muhimu sana, ingawa inachukua muda sana kuisoma. Wameshauri kwamba nitakapofundisha tena kozi hii, Brick Lane iwe mwanzoni, wakati wanafunzi wakiwa bado hawajachoka na masomo. Riwaya zingine, ambazo ni fupi fupi, zije baadaye. Nimewashukuru kwa ushauri huo wa wanafunzi ambao wamepitia kozi yangu, nikizingatia kuwa adhabu ya kaburi aijuaye maiti.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment