Thursday, December 8, 2016

Tamko la CUF Kuelekea Maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika


Kesho, Alhamisi, tarehe 9 Disemba, 2016 ni siku ya maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanganyika, Watanzania tunaadhimisha miaka 55 ya kuwa huru baada ya harakati za miaka mingi ya kudai uhuru wa nchi yetu kutoka kwa wakoloni waliotutawala.

The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) kinaungana na wananchi wote katika kuadhimisha siku hii muhimu katika historia ya nchi yetu, na kutoa wito kwao kuendelea kusimamia malengo, dhamira, na nia za viongozi wetu katika kupigania Uhuru kama yalivyowahi kusema na kuainishwa kuwa ni kupambana na maadui wakubwa watatu ambao ni Umasikini, Ujinga, na Maradhi.

Sambamba na siku ya uhuru wa Tanganyika, tarehe 9 Disemba, ni siku ya maadhimisho ya kimataifa kuhusiana na waathirika wa mauaji ya halaiki na kuzuia jinai zake, (International Day of Commemoration and Dignity of the Victims of the Crime of Genocide and of the Prevention of this Crime) kama ilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa (UN) kwa tamko lake namba (A/RES69/363). Tarehe hii ya 9 Disemba pia ni siku ya kimataifa kuadhimisha juhudi za kupinga na kupambana na rushwa, (Internatinal Anti Corruption Day) kama ilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa (UN) kwa tamko lake namba (A/RES/58/4).

THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama Cha Wananchi) kinaungana na mataifa yote duniani kuadhimisha siku hizi na kuiahidi Jumuiya ya Kimataifa kuwa itaipa kila aina ya ushirikiano ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwa maadhimisho ya siku hizo. Kwa kutumia mifano michache ya maadhimisho ya siku kama hizi za kimataifa juu ya jinai dhidi ya ubinadamu na kutamalaki kwa rushwa, na kufuatilia mwenendo wa matukio yanayoendelea kutokea katika nchi yetu kwa pande zote mbili za Muungano (Tanganyika na Zanzibar), inabainika kuwa malengo halisi ya mapambano ya kudai uhuru hayajafikiwa kama ilivyodhamiriwa na viongozi na majemedari walioongoza harakati za kudai uhuru na ukombozi wa nchi yetu. Kwa hakika, mapambano ya kudai Uhuru yamefanikiwa kwa kiwango kidogo mno cha kumuondosha mkoloni mzungu, na badala yake ndugu zetu na wananchi wenzetu wamejiweka katika nafasi hiyo kwa kuendeleza yaleyale aliyokuwa akiyafanya Mkoloni kwa takribani nchi zote za kiafrika. 

Wakati huu nchi yetu ikiwa inatimiza miaka 55 ya kuwa huru, kumeshuhudiwa uvunjifu mkubwa wa Haki za binaadamu, Ukandamizaji wa demokrasia uliochupa mipaka ikiwa ni pamoja na kupuuzwa na kuminywa kwa maamuzi ya kidemokrasia ya wananchi kuchagua viongozi wanaowataka, uvamizi, ushambuliaji na utekaji wa viongozi wa kisiasa, na utawala usiozingatia matakwa ya kisheria katika kuongoza kwake.

Katika siku za hivi karibuni hali imeendelea kuwa mbaya zaidi ambapo vyombo vya Ulinzi na Usalama, vyenye wajibu na jukumu la kulinda Raia na Mali zao, vimekuwa vikikubali kupokea amri na kutumiwa na wanasiasa wa Chama tawala na vibaraka wao kushiriki jinai mbalimbali kama vile kunyanyasa na kudhalilisha wananchi wasio na hatia kwa kuwabambikizia kesi, kuvamia, kupiga na kujeruhi wananchi na au kutoa ulinzi na kufanikisha njama za matukio hayo, kama inavyofanywa na kikosi cha askari kinachojulikana kwa jina la ‘Mazombi’ kisiwani Zanzibar na kushindwa kwa vyombo hivyo kuchukuwa hatua zozote za kisheria kwa wahusika wa uratibu na utekelezaji wa jinai hizi zinazofanywa wazi wazi.

Vitendo vyote hivi vinaashiria namna Viongozi wa CCM na Serikali yake walivyoshindwa kusimamia nia, dhamira na malengo ya Viongozi wetu waliopigania Uhuru. Bila ya shaka haya yote ni dalili na mwelekeo mbaya wa kuvurugika kwa amani ndani ya nchi yetu. The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) inatowa wito kwa Serikali na viongozi wa CCM, kuheshimu na kuzingatia misingi ya HAKI, USAWA, DEMOKRASIA NA KUFATA UTAWALA WA SHERIA ili kuiepusha nchi yetu kuingia katika majanga yanayoweza kuepukika.

HAKI SAWA KWA WOTE

SALIM BIMANI

MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA MAHUSIANO NA UMMA

MAWASILIANO: 0777 414 112 / 0752 325 227

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...