Posts

Showing posts from February, 2018

Freeman Mbowe: Kiongozi wa Mfano

Image
Kwa miezi kadhaa nimekuwa nikiwazia kuandika ujumbe kuelezea kuwa ninamkubali Freeman Mbowe kuwa ndiye kiongozi wa kitaifa wa kupigiwa mfano. Nina sababu zangu, ambazo nitazieleza hapa. Kabla sijafanya hivyo, nataka nifafanue kuwa mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Baadhi ya watu wamekuwa wakinibambikiza uanachama wa CHADEMA. Ukweli ni kwamba sijawahi kukanyaga katika ofisi yoyote ya CHADEMA, wala sijawahi kuiona hata kadi ya CHADEMA, isipokuwa katika picha mitandaoni. Sijawahi kuhudhuria mkutano wa CHADEMA.  Watu hao wanaonibambikiza chama sijui akili yao ikoje. Mimi ni mtu huru ninayetambua na kutumia haki yangu ya kutoa maoni na kujieleza kuhusu masuala yoyote, yakiwemo ya siasa. Nikisema jambo kuikosoa CCM, kwa mfano, sifanyi hivyo kwa sababu ya kuwa katika chama tofauti. Akili yangu haihitaji chama ili iweze kufikiri. Baada ya ufafanuzi huo, napenda kurejea kwenye mada. Kwa nini ninamwenzi Freeman Mbowe kama kiongozi wa kupigiwa mfano? Si suala la mihemko au u

Maana ya Uzalendo

Image
Kwa kuzingatia jinsi dhana ya uzalendo inavyovurugwa na watu mbali mbali, nimeona nilete tamko la Ilhan Omar, Msomali Mmarekani ambaye ameweka historia hapa Marekani kwa kuchaguliwa kuwa mwakilishi katika bunge la jimbo la Minnesota. Anafafanua kwa lugha rahisi maana ya uzalendo. Anachosema ni kuwa uzalendo si kutetea uongozi au kiongozi wa nchi, bali ni kutetea na kuzingatia maslahi ya nchi, katiba yake, na watu wake. Anasema ni kosa kufikiri kwamba mkuu wa nchi asikosolewe. Anasema kwamba katika nchi ya kidemokrasia, na katiba inayotambua uhuru wa watu kutoa mawazo na kujieleza, watu wana haki ya kumkosoa mkuu wa nchi, kumshinikiza afanye mambo ya manufaa, na kumwajibisha, bila wasi wasi au woga wa kueleweka kwamba si wazalendo.

Ripoti ya Mhadhara wa Red Wing

Image
Nashukuru nimeweza kwenda leo Red Wing na kutoa mhadhara juu ya "African Storytelling," kama ilivyotangazwa. Barabara zilikuwa na theluji, kwa hivyo ilibidi niendeshe gari kwa uangalifu. Lakini nilifika salama, saa tatu na dakika hamsini. Mhadhara ulipangiwa kuanza saa nne, na ndivyo ilivyokuwa. Nilipokelewa vizuri na wahudumu wa maktaba ya Red Wing, hasa Lindsey Rindo ambaye ndiye aliyefanya mawasiliano nami tangu mwanzo, mwaka jana, kuniulizia kama ningeweza kwenda kutoa mhadhara, akafuatilia na kufanya mipango yote hadi kufanikisha shughuli ya leo. Walikuwepo watu wa kila rika, kuanzia watoto wadogo hadi wazee. Nilianza kwa kuelezea umuhimu wa Afrika kama chimbuko la binadamu, tekinolojia, lugha, na usimuliaji wa hadithi. Nilielezea jinsi falsafa na maadili yalivyohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi katika aina za fasihi simulizi kama vile methali. Nilitoa mifano ya methali. Kisha nilisimulia hadithi ya "Spider and the Calabash of Knowledge,&qu

Mrejesho Kuhusu Kitabu

Image
Ni furaha na faraja kwangu kama mwandishi kupata mrejesho kutoka kwa wasomaji. Leo asubuhi, nilipoamka, niliona ujumbe kutoka kwa mwalimu wa chuo cha St. Lawrence. Ameandika: Mimi ni ndugu Kitito. Tulikuwa wageni wako katika kongamano la African network. Mimi na Robin tunashukuru mno kwa kitabu chako "Africans and Americans." Tunakitumia darasani mwetu. Wanafunzi wamefaidika mno... Huyu mwalimu Robin anayetajwa nilishaandika habari zake katika blogu hii. Baada ya mimi kusoma ujumbe wake, mwalimu Kitito amenipigia simu, akanielezea zaidi kuhusu kitabu kinavyotumiwa. Nami nilimwelezea nilivyokiandika, baada ya miaka mingi ya kukabiliana na maisha ya Marekani. Nilimweleza kwa nini nilitumia mtindo ambao si kawaida kwa wanataaluma. Nimefarijika kupata mrejesho kutoka kwa waalimu hao ambao wanatumia kitabu changu, nami nimeona niweke kumbukumbu hii hapa, kama ilivyo kawaida yangu.

Nasubiri Mhadhara wa Red Wing

Image
Tarehe 17 mwezi huu, nitakwenda Red Wing kutoa mhadhara, kama nilivyoripoti katika blogu hii. Mada itakuwa "African Storytelling" yaani jadi ya hadithi za Afrika. Maandalizi yamefanyika kikamilifu, kama inavyoonekana katika tangazo la mhadhara. Hii si shughuli ya kwenda kusimulia hadithi tu. Ni kuelimisha kuhusu misingi, maana, na dhima ya hadithi za jadi katika utamaduni wa Afrika. Jadi ya kusimulia hadithi ni sanaa yenye kugusa vionjo na hisia za binadamu, pia ni nia ya kuhifadhi elimu na kuelimisha. Hadithi zinayotafakari maisha, tabia na mahusiano ya binadamu, na masuala ya maadili. Hadithi zimefungamana na aina zingine za sanaa ya maneno kama vile methali na nyimbo. pia zimefungamana na mila, desturĂ­, na imani. Ni kioo cha jamii, lakini pia ni kichocheo cha mwenendo wa jamii. Upana huo wa mtazamo kuhusu hadithi nimeubainisha katika kitabu changu, Matengo Folktales ambacho kina hadithi kumi, pamoja na uchambuzi wangu wa kila hadithi. Pia kina insha juu ya padithi kw

Mteja Anapokupigia Debe

Image
Tarehe 3 Februari, nilipata ujumbe wa barua pepe kutoka kwa dada au mama ambaye amejitambulisha kwa jina la Cynthia, ila simjui. Ameandika kuulizia kitabu changu namna hii: Hello, I am planning a trip to Tanzania and someone recommended your book about cultural differences between Africans and Americans. How can I purchase your book? Thank you very much. Kwa wasiojua ki-Ingereza, tafsiri yake ni hii: Habari Ninapanga safari ya kwenda Tanzania na mtu fulani alikipendekeza kitabu chako juu ya tofauti za tamaduni za wa-Afrika na wa-Marekani. Nitakinunuaje kitabu chako? Shukrani sana. Kwa mwandishi, habari ya aina hii ni habari njema. Kwamba mtu fulani ambaye alitumia hela zake kununulia kitabu chako alikisoma akaridhika au kufurahi kiasi cha kukipendekeza kwa mwingine, si jambo jepesi. Mtu anapopendekeza kitu kwa mwingine namna hii, anajiweka katika hali ya kueleweka vibaya, iwapo kile anachopendekeza hakitamridhisha huyu mwingine. Tunapendekeza vitu kwa marafiki zetu tukiwa na