Freeman Mbowe: Kiongozi wa Mfano

Kwa miezi kadhaa nimekuwa nikiwazia kuandika ujumbe kuelezea kuwa ninamkubali Freeman Mbowe kuwa ndiye kiongozi wa kitaifa wa kupigiwa mfano. Nina sababu zangu, ambazo nitazieleza hapa.
Kabla sijafanya hivyo, nataka nifafanue kuwa mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Baadhi ya watu wamekuwa wakinibambikiza uanachama wa CHADEMA. Ukweli ni kwamba sijawahi kukanyaga katika ofisi yoyote ya CHADEMA, wala sijawahi kuiona hata kadi ya CHADEMA, isipokuwa katika picha mitandaoni. Sijawahi kuhudhuria mkutano wa CHADEMA. 
Watu hao wanaonibambikiza chama sijui akili yao ikoje. Mimi ni mtu huru ninayetambua na kutumia haki yangu ya kutoa maoni na kujieleza kuhusu masuala yoyote, yakiwemo ya siasa. Nikisema jambo kuikosoa CCM, kwa mfano, sifanyi hivyo kwa sababu ya kuwa katika chama tofauti. Akili yangu haihitaji chama ili iweze kufikiri.
Baada ya ufafanuzi huo, napenda kurejea kwenye mada. Kwa nini ninamwenzi Freeman Mbowe kama kiongozi wa kupigiwa mfano? Si suala la mihemko au ushabiki. Ni suala la hoja.
Leo, katika taaluma ya saikolojia, tunaambiwa kuwa kuna aina nyingi za akili. Suala hilo kitaaluma linaongelewa chini ya kichwa cha "multiple intelligence" au "multiple intelligences."
Kufuatana na ufuatiliaji wangu wa mada hiyo, nimejifunza kwamba uongozi unahitaji aina ya akili iitwayo "emotional intelligence." Labda kwa ki-Swahili niseme akili hisia. Kwa maneno mengine, mtu mwenye akili hiyo ndiye anaumudu uongozi. Anakuwa kiongozi wa kweli.
Mtu huyo anakuwa mwenye kujitambua. Anatambua hisia zake na hisia za wengine. Kutokana na hilo, anazimudu hisia zake na hisia za wengine, kwa maana kwamba anajitawala vizuri, na anajali hisia za wenzake. Hana mihemko. Anakuwa msikivu. Watu wakitofautiana, yeye anakuwa msuluhishi. Anajenga umoja na maelewano. Anavutia watu. Watu wa kila aina wanamkubali kama kiongozi.
Mtu huyu anajiamini. Wale anaowaongoza wanakuwa huru kung'ara katika maeneo ya ujuzi wao. Yeye hawi mtu wa kutaka sifa, aonekane yeye ndio zaidi. Wenzake waking'ara kumzidi, kwake ni sawa. Vipaji vya kila moja anaviona ni mtaji wa manufaa kwa wote. Anachofanya si kuzuia vipaji hivyo visijitokeze, bali anaviratibisha kwa manufaa ya wote. Hii kwa ki-Ingereza huitwa "leveraging."
Nikirejea kwa Freeman Mbowe, ninaona anakidhi vigezo hivyo. Kuna watu wanambeza Mbowe, eti hana elimu ya kutosha. Wengine wanasema huyu ni DJ. Watu hao ni wajinga, kwa namna mbili. Kwanza hawaelewi kuwa elimu si ya shuleni na vyuoni tu. Inapatikana pia nje ya shule na vyuo. Pili hawaelewi hiyo dhana "emotional intelligence" kama kigezo na msingi wa uongozi.
Wangejua, wasingeshangaa kwa nini huyu Mbowe wanayemsema hana elimu ya kutosha, lakini ndiye kiongozi wa maprofesa, wanasheria maarufu, na kadhalika. Ni kwa sababu yeye hatingishiki na kung'ara kwa hao wenye kisomo zaidi yake. Hatingishiki na umaarufu wa wenzake, akina Tundu Lissu, Msigwa, Lema, au Halima Mdee. Wote wako naye, naye yuko nao. Hiyo ndio tabia ya mtu anayejiamini.
Kutokan na akili yake hiyo na busara zitokanazo, Mbowe amefanikiwa kuijenga CHADEMA mwaka hadi mwaka, hadi leo imekuwa ni chama kikuu cha upinzani, chenye kuongoza majimbo na miji mikubwa. Ingekuwa kuna fursa na uhuru sawa kwa kila chama kufanya shughuli zake kama inavyoelekezwa na katiba na sheria, nina hakika CHADEMA ingekuwa mbali zaidi.
Jambo jingine la muhimu sana linalonivutia kwa Freeman Mbowe ni uzalendo wake. Hata pamoja na magumu yote ambayo chama chake kinawekewa na utawala, daima anaongelea mustakabali wa Taifa. Hata mimi ambaye si mwana CHADEMA ninaguswa na hilo, kwamba anatuwazia wa-Tanzania, na nchi yetu sote, si wana CHADEMA pekee. Huyu ndiye Mbowe ninayemwona mimi.
Nimesema kuwa mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Ila napenda kusema kuwa kutokana na kwamba mimi ni mwanataaluma na mwalimu, kama ingekuwa ni lazima kuwa na chama, ningekuwa CHADEMA. Ninaona jinsi CHADEMA inavyopigania uhuru na haki zilizomo katika katiba, ikiwemo uhuru na haki ya kutoa mawazo na kujieleza, na uhuru wa mikutano. 
Uhuru wa fikra ni msingi wa kustawi yale ninayofanya kama mwanataaluma na mwalimu. Elimu haistawi bila uhuru wa kutoa mawazo na kujieleza. Elimu inaihusu jamii nzima. Mikutano ni sehemu ya hiyo elimu ya jamii. Kwa hivyo, ni wazi kwangu kuwa kama ingekuwa lazima kuwemo katika chama, ningekuwa CHADEMA. Ningekuwa huko si kwa sababu CHADEMA inakidhi mategemeo yangu yote kuhusu masuala yote ya kitaifa, bali kwa sababu hii moja ambayo nimeelezea. Kama mwanataaluma ninayehitaji uhuru wa kufikiri na kutoa mawazo, na ninayetaka elimu ishamiri katika nchi yetu, ningejisikia huru kuwa na kiongozi Freeman Mbowe.

Comments

Ndio. Huyo ndio kiongozi. Nimependa sifa nyingi hasa hasa hii ya kuwa kiongozi unayejali wengine na vipaji vyao na kuweza kuviendeleza na kuvichukulia kama manufaaa kwako na kwa jamii.
Asante sana Prof kwa makala yako hata mimi niliwahi kuandika nilivomfahamu nimeshare na wewe pia
Tumaini Temu
Mbele said…
Shukrani, ndugu Tumaini Temu, kwa kusoma makala yangu, na pia kwa kunisogezea makala yako. Nimeisoma. Kubadilishana mawazo kwa uhuru na uwazi ni muhimu. Kama ni kutofautiana kwa hoja, na iwe hivyo, kwa uwazi na uhuru. Tena basi, kwa wasomi ni wajibu kuhoji, kujihoji, kuhojiana na kulumbana kwa hoja. Hiki ni kigezo muhimu cha kuwabaini wasomi wa kweli na wasomi hewa.
Unknown said…
Salaam mwalimu Mbele...
Umeongea mengi ya kusifu lakini kwangu mimi naona Mbowe hafai kwasababu hatoi uhuru wa wanachama wengine kugombea uenyekiti hata hawaandai wengine kushika nafasi hii kwangu mimi mbowe si kiongozi wa mfano. Ni kiongozi mbinafsi anayewaaminisha wafuasi wake kuwa hakuna mwenye uwezo wa kuwa mwenyekiti zaidi yake. Na hata waliojaribu kuomba au kuleta ushindani kwenye nafasi hiyo walikumbwa na mabalaa kwa mifano michache ni Zitto kabwe ambaye alinusurika kufa kwa sumu walipomshindwa wakampa usaliti kisha wakamtimua mwingine ni chacha wangwe aliyeuwawa kwenye ajali ya gari. Zitto alipoingia kwenye mgogoro aliwahi kusema “ CHACHA DIED BUT I WONT “ .
Mbele said…
Athumani Yatera

Nina wasi wasi na madai yako dhidi ya Mbowe. Ingekuwa yanatoka kwa wana CHADEMA, tena si wachache, bali wengi, ningeyatilia maanani. Hilo moja. Pili, nimeshasikia majungu mengi dhidi ya Mbowe. Kapakaziwa hata madawa ya kulevya. Ninayapuuza haya yote, kwa sababu kuu mbili.

Kwanza, kuna suala la haki ya kila binadamu anayetuhumiwa kwa kosa kuhesabiwa kwamba hana kosa hadi ithibitishwe mahakamani. Ungeniletea ni yepi ambayo yamethibitishwa namna hiyo, ningeafiki kauli yako. Jambo jingine muhimu ambalo unapaswa uzingatie ni kuwa kuna mtu aitwaye msajili wa vyama vya siasa. Moja ya majukumu yake ni kujiridhisha kwamba vyama vinaendeshwa kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi, na kwa mujibu wa katiba ambazo ziliviwezesha vyama hivi kupata usajili. Hayo madai yako kuhusu Mbowe anavyoendesha chama chake siyatilii maanani. Unamaanisha msajili wa vyama vya siasa ni mzembe ambaye hayaoni au anayamezea? Hilo moja. Pili, kama una ushahidi wa hayo usemayo, kwa nini hupeleki kwa msajili? Tunarudi pale pale. Majungu ni mengi dhidi ya Mbowe, na baadhi ni hayo uliyoleta hapa.
Mwalimu Mbele, binafsi nimefuatilia kwa kina sana makala yako na hata majibu yako kwa Bwa.Athmani Yatera kwenye hoja zake. Katika hoja ya kuwa Mbowe amewaaminisha watanzania hasa wafuasi na wanachama wa CHADEMA kuwa hakuna anayeweza kuingoza CHADEMA zaidi ya yeye. Hoja ulizoitoa katika kumjibu mtoa hoja uliyemkusudia ni hoja nyepesi sana na kamwe sikutaraji majibu mepesi kwenye hoja nzito namna ile. Ifahamike kuwa ofisi ya msajili wa vyama vingi ipo kikatiba na inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria. Ndani ya katiba ambayo ndio sheria mama kwenye sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010 hakuna kipengele kinachotamka wazi kuhusu okomo wa uongozi wa vyama vya siasa. Hoja ya kuwa kama Mbowe angekuwa amevunja sheria kwa kukaa kwenye uongozi wa chama kwa muda mrefu na hivyo kushughulikiwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini sio kweli kwa kuwa ofisi haina meno kisheria ya kushughulikia mambo hayo. Kwa mantiki hivyo basi, Mbowe ametumia mwanya huo kufinyanga finyanga katiba ya CHADEMA inayoweka wazi ukomo wa uongozi ndani ya chama.
Inawezekana kabisa sifa ulizomwaga kwa Mh. Mbowe zikawa zinastahili kweli kufika kwake. Kuna tofauti kubwa sana kati ya muonekano wa Mbowe kwenye majukwaa ya kisiasa na makusudio aliyonayo kwa taifa hill lenye kila aina ya rasilimali. Kwenye majukwaa ya kisasa anaonekana na "Public vision" ila ukweli ni kwamba kisiasa Mbowe ana "Personal interest". Hii ni kutokana na misingi na malengo ya uanzishwaji wa chama chake. CHADEMA imebeba dhana ya utaifa kinadharia tu lakini kiuhalisia kuna fukuto kubwa la Ukabila na ukanda ndani yake. Mifano ipo mingi ya kinadharia na kivitendo. Tukiwa tunazungumzia siasa tuziache mbali hisia na mihemko yetu ya kichama badala yake tuangalie maslah mapana ya taifa. Dhamira ya chama chochote cha siasa ni kushika dola na kuunda serikali. Mbowe na chama chake sio wa kuwaamini hata kidogo
Mbele said…
Nurdin R. Mwetta, kuna mambo ambayo juu yake tunaweza kuwa na mitazamo tofauti. Hii si ajabu katika kutafakari masuala ya jamii. Ingekuwa tunajadili suala kama la hisabati, tungejua kuwa kuna jawabu moja. Mambo yanayohusu mitazamo sitayagusia. Ila siwezi kukubali kauli yako kwamba CHADEMA kina ukabila na ukanda. Hili si suala la mtazamo. Lazima tufikie kwenye ukweli.

Hata kipofu anaona ukweli kwamba CHADEMA imejijenga pande mbali mbali za nchi. Hebu niambie: Iringa na Mbeya ni ukanda moja na Arusha? Ni ukanda moja na Dar es Salaam? Mwaka huu nilikuwa Tanzania kwa wiki sita. Nilisafiri kuona nchi kuanzia Namanga (mpaka wa kaskazini wa nchi) hadi Mbambabay (kusini kabisa, kando ya Ziwa Nyasa). Nimeona bendera za CHADEMA kuanzia kaskazini hadi kusini. CHADEMA haikuwepo kule Nyasa miaka michache iliyopita. Leo utaikuta kule. Ukanda upi unaoongelea? Ukabila upi?

Jielimishe kabla ya kuja kuandika hapa. Katika Tanzania, hairuhusiwi kusajiliwa chama cha siasa ambacho ni cha kikabila au ukanda. Kama una uhakika na hicho usemacho kuhusu CHADEMA, peleka ushahidi wako kunakohusika.

Makala yangu ni juu ya Mbowe kama kiongozi wa mfano. Niliandika makala hii mwezi Februari, na hadi leo sijaona mtu kujitokeza akatutajia kiongozi anayemwona kuwa ni wa mfano. Ninasubiri makala ya aina hiyo, iwe imejenga hoja kama nilivyojaribu kujenga. Kadiri miezi inavyopita nami nisione makala ya aina hiyo, ninapata uhalali wa kusema kwamba niliyosema juu ya Mbowe ni ukweli kabisa. Kama unabisha, lete hiyo makala.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini