Posts

Showing posts from April, 2011

Neno Kuhusu Ualimu

Image
Picha hii ilipigwa Dar es Salaam, Septemba 2004,kwenye viwanja vya makumbusho ya Taifa, wakati wa tamasha la vitabu. Naonekana nikiwa na walimu kutoka Kunduchi Girls Islamic High School. Walikuja na hao watoto kwenye meza ambapo nilikuwa nimeweka vitabu vyangu. Tulizungumza na kushauriana mambo ya manufaa kuhusu elimu na kadhalika, nao walinialika kutembelea shule yao. Haya ndio mambo tunayohitaji katika nchi yetu. Na hao watoto katika picha wanasikia tunachoongea sisi watu wazima. Tuwaleavyo ndivyo wakuavyo. Ninapowakumbuka na kuwaangalia watoto, kama hao waliomo katika picha, hisia zangu za kiualimu zinaibuka. Kwa upande mmoja, nafurahi na kushukuru kuwa nimejaliwa uwezo na fursa ya kuwaelimisha watoto hao. Ninawapenda. Soma, kwa mfano, makala yangu hii hapa . Papo hapo, ninapowawazia watoto wa Taifa letu, najiwa na wasi wasi kwa jinsi baadhi ya watu wanavyoeneza mitazamo na mawazo kama udini, ubaguzi na uhasama baina ya makundi mbali mbali ya jamii. Hizo ni sumu, nami nahofia ath

Maktaba ya Lushoto

Image
Kila ninapokuwa Tanzania, najitahidi kutembelea taasisi za elimu kama vile shule na maktaba. Mwaka jana, wakati nipo mjini Lushoto , nilipata dukuduku ya kujua kama kuna maktaba hapo, na iko wapi. Nimeshaona maktaba za hata miji midogo kama Mbinga na Mbulu. Niliulizia mitaani, na watoto wa shule ya msingi wakanionyesha maktaba ilipo. Hiyo ilikuwa ni tarehe 5 Agosti. Niliingia ndani nikaona vitabu vya aina aina, vya taaluma mbali mbali, kuanzia fasihi, hadi masuala ya jamii na maendeleo. Niliona hata vitabu viwili vitatu vya Karl Marx, Kwame Nkrumah, na Issa Shivji. Ingawa maktaba hii haina vitabu maelfu na maelfu, nilipata hisia kuwa mtu anayeishi katika mji huu akiamua anaweza kujielimisha kiasi cha kueleweka kwa kusoma vitabu vilivyomo katika maktaba hii. Niliongea na mama mhudumu wa maktaba. Alinieleza mazingira magumu ya maktaba hii, nami nilijionea mwenyewe. Niliona jinsi yanavyohitajika makabati bora, kwa mfano. Nilimwambia kuwa nami kama mwalimu naguswa na moyo wa kujitolea

Rais Obama Awasomea Watoto Hadithi

Image
Leo, katika kuvinjari kwenye mtandao wa Facebook, nimeona video ya Rais Obama na familia yake. Wako bustanini wakiwasomea watoto hadithi. Nimeguswa sana na video hii. Niliwahi kuandika makala kuhusu kuwasomea watoto vitabu . Katika makala hii nilielezea jinsi wenzetu huku Marekani wanavyojali suala hili, kuanzia watu wa kawaida hadi viongozi wa juu kabisa. Hata dakika ile Marekani iliposhambuliwa, tarehe 11 Septemba, 2001, Rais Bush alikuwa darasani na watoto wakisoma kitabu. Makala yangu ile niliipanua na kuiboresha na imechapishwa katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii . Katika makala hiyo, na kila mara ninapoongelea masuala ya aina hii ya kutokuwa na utamaduni huo kama wenzetu. Lakini haingekuwa vigumu kuuanzisha na kuujenga utamaduni huo. Ni faraja kuona kuwa wako wengine wenye mawazo hayo hayo, na hapo napenda kumtaja Dada Sophie Kagambo Becker, ambaye ameelezea hayo katika blogu yake .

Msamvu, Morogoro

Image
Blogu yangu hii ni sehemu ya mambo mengi binafsi, zikiwemo kumbukumbu. Leo najikumbusha kuhusu Msamvu, kitongoji cha mji wa Morogoro. Ni kumbukumbu ya ziara yangu ya mwaka jana, ambayo nilishaielezea kidogo katika blogu hii . Morogoro ina vitongoji vingi, ambavyo sivijui kabisa au sivijui vizuri. Ila nimepata fursa ya kuifahamu Msamvu, maarufu kwa sababu ni kituo kikubwa cha mabasi. Msamvu ni sehemu ya biashara. Kuna migahawa na vijiduka. Kwa wafanyabiashara ndogo ndogo, wasafiri ni wateja muhimu. Wageni kutoka ughaibuni wanapofika kwetu wanashangaa kuwa basi linaposimama, ghafla linavamiwa na wachuuzi wa kila aina ya bidhaa, ambazo hupitishwa madirishani, kuanzia matunda na biskuti hadi kadi za simu. Kule mbele, kwenye miti, kuna hoteli na baa nzuri. Nimewahi kutua hapo mara mbili tatu, wakati nikingojea usafiri wa kwenda Dar es Salaam. Ni sehemu nzuri ya kupumzikia.

Ziara Yangu Shanghai

Image
Mwaka 2003 nilipata bahati ya kutembelea China. Hii ni kati ya ziara ambazo nazikumbuka sana. Nilialikwa kwenda kutoa mihadhara East China Normal University , mjini Shanghai. Mihadhara ilikuwa kama ifuatavyo: 25 Novemba, "My Folklore Research Experience," 25 Novemba "American Folklore Studies Today," 26 Novemba, "My Folklore Research Experience" 1 Desemba, "African Folklore Research." Picha zinazoonekana hapa ni za wanafunzi wa shahada ya juu. Mwalimu wao, ambaye amevaa jaketi jekundu, alinialika niongee na hao wanafunzi darasani kwao kuhusu "My Folklore Research Experience" na vile vile "Women in African Folklore" hiyo tarehe 26Novemba. Nilifurahi kupata fursa hii ya kubadilishana mawazo na watafiti wa China. Walikuwa na masuali mengi. Huyu bwana aliyesimama pembeni alikuwa katika ngazi ya juu kuliko hao wanafunzi wengine. Wao walikuwa wanasomea shahada ya uzamili, wakati yeye alikuwa katika shahada ya udaktari.

Mawaidha ya Mwakilishi Keith Ellison

Image
Leo hapa Chuoni St. Olaf tulitembelewa na mgeni maarufu, Keith Ellison , ambaye ni mwakilishi kutoka Minnesota katika Congress, ambalo ni bunge la Marekani. Keith Ellison ni mu-Islam wa kwanza kuwa mjumbe katika Congress. Aliongelea changamoto zinazoikabili Marekani na dunia katika mkabala wa kuwepo kwa tofauti za dini. Kwa kutumia mifano ya Marekani, alisisitiza kuwa watu wa dini mbali mbali tuna uchaguzi wa kufanya. Tunaweza kuchagua kuheshimiana, kuelewana na kujenga dunia ya amani, upendo na mshikamano, au tunaweza kuchagua kuwa na uhasama, ubaguzi, chuki, mfarakano, na migogoro. Alisema kuwa wahubiri wa dini wana wadhifa mzito. Wanapopanda kwenye mimbari au sehemu nyingine ya kuhubiria, wana ushawishi mkubwa mioyoni mwa waumini. Wana wajibu wa kujua hilo, kwani wanao uwezo wa kujenga umoja na maelewano katika jamii au wanaweza kujenga uhasama na chuki katika jamii. Alisisitiza wajibu wetu wa kuwaheshimu watu wa dini mbali mbali, na watu wasio na dini. Wote wanastahili heshim

Twahir Hussein: Wanaharakati Waislam Mmekosea

Blogu hii inatoa fursa ya mawazo ya aina mbali mbali kusikika, sio mawazo yangu tu, bali ya wengine pia. Leo nimeona niweke makala ya Twahir Hussein, ambayo ilichapishwa katika twahirhussein.blog . Hii sio mara ya kwanza kwa blogu hii kuchapisha maoni ya wa-Islam. Mfano ni huu hapa . Utafiti na mijadala huru ni njia muafaka ya kuelimishana na kutafuta ukweli. Blogu hii inaheshimu mijadala, kama nilivyosema hapa . Basi tumsikilize Twahir Hussein, msomi mu-Islam na mhadhiri katika chuo kikuu. ---------------------------------------------------------- Wanaharakati waislamu mmekosea Na Twahir Hussein Majuma kadhaa yaliyopita uliwasilishwa muongozo wa waislam kuelekea uchaguzi mkuu 2010. Muongozo huo, pamoja na mambo mengine kwa kiasi kikubwa umejikita katika kuwakumbusha waislam yale ambayo wamekuwa wakiyakabili tangu baada ya uhuru mpaka miaka ya hivi karibuni katika nyanja mbalimbali za kimaisha kama vile siasa, elimu, uchumi na kadhalika. Aidha, kwa undani zaidi, muongozo huo u

Hatimaye, Bia Zitazinduliwa Ikulu

Ni juzi tu hapo niliandika makala kuhusu jinsi wa-Tanzania wanavyowajibika katika unywaji wa ulabu. Makala hiyo ni "Kazi ya Kunywa" . Katika kuhitimisha, nilitamka kuwa, kwa mwendo tunaokwenda, huko mbele ya safari ulabu utakuwepo hadi shuleni na Bungeni. Ni kama vile niliota. Wiki hii wabunge wa Tanzania wameweka historia kwa kuzindua vinywaji vikali huko Dodoma. Soma hapa . Nchi yetu ni ya pekee. Tunauenzi ulabu kiasi hiki, ingawa unasababisha au kuchangia matatizo mengi, kuanzia ajali barabarani zinazosababisha vifo vingi na watu wengi kuumia, uharibifu wa mali, magomvi katika jamii, kuharibika akili na matatizo ya kisaikolojia. Tunakwenda kwa kasi na ari kiasi kwamba siku si nyingi kuanzia sasa, bia zitakuwa zinazinduliwa Ikulu. Na siku ya kuzindua bia itakuwa ni ya kukumbukwa ki-Taifa. Enzi za uongozi wa Mwalimu Nyerere, wabunge wangekuwa wanazindua maktaba, si ulabu. Hakuna mtu aliyethubutu kufanya mambo yanayofanyika leo. Lakini mambo ndio hayo: akiondoka paka, pa

Ugumu wa Kusoma Vitabu vya Dini Isiyo Yako

Hapo juzi, niliandika kuwa nasoma vitabu vya dini mbali mbali . Lakini jambo moja ambalo sikuongelea ni kuwa inaweza kuwa vigumu kufikia uamuzi wa kusoma vitabu hivyo. Napenda kuongelea uzoefu wangu. Nilizaliwa katika familia na jamii ya wa-Katoliki. Dini pekee iliyokuweko katika eneo langu, kwa maili nyingi kuzungukia eneo hilo, ilikuwa ni u-Kristo, madhehebu ya Katoliki. Watu pekee ambao hawakuwa wa-Katoliki ni wale wachache ambao walikuwa hawajabatizwa. Sikumbuki kama niliwahi kusoma kitabu cha dini nyingine yoyote au dhehebu jingine lolote zaidi ya u-Katoliki. Hata niliposoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1973, nikaanza kufundisha hapo mwaka 1976, katika idara ya "Literature," sikumbuki kama nilisoma kitabu cha dini nyingine. Lakini nilipokuwa nasomea shahada ya juu katika Chuo Kikuu Cha Wisconsin-Madison, 1980-86, nilipata fursa ya kufahamiana vizuri na mwanafunzi mwenzangu mu-Islam kutoka Sudan. Huyu alikuwa mmoja wa marafiki zangu. Alipoona nina hamu

Kuwalea Watoto Katika Usomaji Vitabu

Image
Huwa natafakari sana suala la kuwalea watoto katika usomaji vitabu. Mtoto huyu hapa kushoto alikuwa anaangalia vitabu vyangu katika maonesho ya elimu na ajira yaliyofanyika mwaka jana Diamond Jubilee Hall, Dar es Salaam. Hiki kitabu alichoshika kinaitwa CHANGAMOTO . Katika matamasha ya aina hiyo, hasa ya vitabu, navutiwa ninapowaona wazazi wamekuja na watoto wao. Huku Marekani ni jambo la kawaida. Katika tamasha hilo la elimu na ajira Dar es Salaam, nilimwona mama mmoja amekuja na mtoto wake. Mama huyu, anayeonekana katika picha hii, alikuja kwenye kibanda changu, ambapo nilikuwa nimeweka vitabu vyangu, akaniuliza masuali kadhaa, huku mwanawe akisikiliza. Niliongelea masuali yake, kuhusu shughuli zangu katika elimu na uandishi, na kadhalika. Ilikuwa ni fursa kwangu pia ya kumhamasisha mtoto wake. Sitasahau mfano alioonyesha mama huyu. Wahenga walisema, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Picha hii ilipigwa Minneapolis, Oktoba 4, 2008, wakati wa sherehe ya kumbukumbu ya Uhuru wa Niger

Hapa Kwetu: Akina "Anonymous" Sasa Ruksa

Tangu nilipoanzisha blogu yangu hii, sikupenda niruhusu akina anonymous kuchangia. Nilielezea duku duku zangu katika makala hii . Lakini leo nimerekebisha mambo, kufuatia ombi la mdau mmoja ambalo amelitoa kwenye blogu ya Mwenyekiti Mjengwa . Nimeguswa na lugha ya kiungwana aliyotumia huyu anonymous. Kilichobaki sasa ni kuona hali itakavyokuwa.

Nasoma Vitabu vya Dini Mbali Mbali

Kati ya mambo ya manufaa kabisa maishani ni kujielimisha. Nami husoma vitabu kila siku kama njia mojawapo ya kujielimisha. Pamoja na vitabu vya taaluma mbali mbali, hadithi, mashairi, na kadhalika, hupenda kusoma vitabu vya dini. Nina vitabu vya dini mbali mbali, hasa u-Hindu, u-Islam, na u-Kristu. Nina vitabu kama vile Bhagavad-Gita , Upanishads, Quran , na Biblia. Nina vitabu kuhusu watu muhimu wa dini hizo, kama vile Yesu Kristu, Muhammad na Swami Vivekananda. Vyote hivyo ninavipitia, angalau mara moja moja. Mimi ni m-Katoliki; habari ndio hiyo. Kwa msingi wa dini yangu, nawajibika kuwajali na kuwapenda wanadamu wote. Yesu alifafanua amri kuu kuliko zote kuwa ni kumpenda Mungu kwa uwezo wetu wote, akili yetu yote, na nafsi yetu yote; kumpenda jirani yetu vile vile, na kuwapenda maadui zetu vile vile. Huu ndio mtihani aliotuachia Yesu. Sasa kwa vile ukweli ndio huo, ninajiuliza ni njia ipi ya kufuata ili niweze kufaulu mtihani huo. Nimeamua kuwa ni wajibu kujielimisha : kuwafa

Mijadala ya Dini ni Muhimu

Watu wengi katika jamii yetu wanasema kuwa tusiendekeze mijadala ya dini. Wanasema kuwa ni tishio kwa amani na maelewano. Ninapenda kutafakari suala hilo. Binafsi, naamini kuwa watu wenye akili timamu wanaweza kujadili mada yoyote bila matatizo. Watu wa aina hiyo wanajua kuwa katika mjadala wanachopaswa kufanya ni kutoa hoja, kusikiliza hoja, na kupinga hoja kwa hoja. Watu wenye akili timamu wanafahamu kuwa, katika mjadala, kila mtu ana uhuru wa kuelezea fikra zake na mtazamo wake, na ana haki ya kusikilizwa. Na kila mtu ana wajibu wa kusikiliza hoja na mtazamo wa wengine. Suala la mijadala, kwa watu wenye akili timamu, ni suala lililojengeka katika haki, uhuru, na wajibu, kama nilivyoelezea hapo juu. Wajibu huo ni pamoja na wajibu wa kuheshimiana katika hiyo mijadala. Kwa maana hiyo, mada yoyote inaweza kujadiliwa na watu wenye akili timamu, iwe ni siasa, uchumi, au dini. Kuna pia wajibu wa kujielimisha. Mbali ya kwenda shule, au kusoma vitabu, mijadala ni njia mojawapo muhimu

Mwalimu Nyerere Aongelea Uongozi, 1995

Image
Suala la uongozi lilikuwa moja ya vipaumbele vya Mwalimu Nyerere maisha yake yote. Tunasikia, kwa mfano, jinsi alivyolichukulia suala hili alipokuwa kiongozi wa wanafunzi katika shule ya Tabora. Wakati wa kupigania Uhuru na baada ya Uhuru aliliongelea suala hili tena na tena, kama vile katika "Azimio la Arusha" na "Mwongozo." Mwalimu aliliongelea suala hili tena, kwa masikitiko, katika kitabu chake cha "Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania," akiihofia hatima ya Tanzania kutokana na uongozi mbovu wa CCM. Niligusia suala hilo katika makala hii hapa . Hata baada ya kuandika kitabu hiki, Mwalimu aliendelea kuongelea suala la uongozi. Hebu msikilize katika hotuba yake hii ya mwaka 1995.

Kitabu Kumhusu Hemingway

Image
Leo nilipita tena katika duka la vitabu la Half Price Books la mjini Apple Valley. Kama kawaida, kutokana na ushabiki wangu wa maandishi ya Ernest Hemingway , nilianza kwa kwenda moja kwa moja kwenye sehemu vinapouzwa vitabu vyake: vile alivyoandika yeye mwenyewe au vilivyoandikwa juu yake. Hadi sasa nina vitabu vingi vya Hemingway, lakini kila ninapoona kitabu kipya, au ambacho sina, napenda niwe nacho. Leo nimevikuta vitabu kadhaa vya aina hiyo, ila nilivutiwa zaidi ni Hemingway in Cuba , kilichoandikwa na Norberto Fuentes. Sikuwa nimekiona kitabu hiki kabla. Nilikiangalia, nikaona kina utangulizi ulioandikwa na Gabriel Garcia Marquez. Hapo niliishiwa nguvu, kwani Marquez ni mmoja wa waandishi maarufu kabisa duniani. Mawazo mengine yakafurika akilini mwangu. Ninajua kuwa Marquez ni rafiki mkubwa wa Fidel Castro, Castro ambaye watu wa kizazi changu tumemwenzi tangu tulipopata Uhuru. Najua pia kuwa Castro ni mshabiki wa maandishi ya Marquez. Cha zaidi ni kuwa najua kuwa Hemingway k