Blogu hii inatoa fursa ya mawazo ya aina mbali mbali kusikika, sio mawazo yangu tu, bali ya wengine pia. Leo nimeona niweke makala ya Twahir Hussein, ambayo ilichapishwa katika twahirhussein.blog.
Hii sio mara ya kwanza kwa blogu hii kuchapisha maoni ya wa-Islam. Mfano ni huu hapa.
Utafiti na mijadala huru ni njia muafaka ya kuelimishana na kutafuta ukweli. Blogu hii inaheshimu mijadala, kama nilivyosema hapa. Basi tumsikilize Twahir Hussein, msomi mu-Islam na mhadhiri katika chuo kikuu.
----------------------------------------------------------
Wanaharakati waislamu mmekosea
Na Twahir Hussein
Majuma kadhaa yaliyopita uliwasilishwa muongozo wa waislam kuelekea uchaguzi mkuu 2010. Muongozo huo, pamoja na mambo mengine kwa kiasi kikubwa umejikita katika kuwakumbusha waislam yale ambayo wamekuwa wakiyakabili tangu baada ya uhuru mpaka miaka ya hivi karibuni katika nyanja mbalimbali za kimaisha kama vile siasa, elimu, uchumi na kadhalika.
Aidha, kwa undani zaidi, muongozo huo umesadifu kinaga ubaga katika kuwasilisha hisia,fikra na utashi binafsi wa waandishi.
Kilichotustaajabisha waumini wengi wa dini ya kiislam ni ule ukiritimba wa mitazamo ya kisekula iliyowatawala waandishi wa muongozo huo katika jambo la dini. Waandishi wameshindwa kabisa kuzitambua tunu na fanaka za maangalizo na mafunzo ya vitabu vitakatifu vya dini yao katika medani za kijamii.
Binafsi, nimeusoma muongozo huo kwa zaidi ya masaa 360. Kwa wazi kabisa muongozo huo umejenga taswira ya uchochezi miongoni mwa waislamu na jamii ya watanzania kwa ujumla.
Nikaona si jambo jema kunyamazia sampuli hii ya ufisadi wa maandishi. Mimi ni muumini wa dhati wa dini ya kiislamu. Kwa dhati kabisa sijapata kuona wala kusikia kwamba uislamu unafundisha uchochezi utakaoleta aina Fulani ya machafuko au kutokuwa na maelewano miongoni mwa wanajamii katika jamii yoyote ile iwayo.
Na sababu kuu ya uchochezi huu ni kukosekana kwa nuru ya demokrasia katika nyoyo za waandishi wa muongozo huo. Kwamba muongozo umekuwa ni mkusanyiko fikra za kikundi cha watu wachache ambao wanabainika kuwa na ajenda binafsi za siri. Jambo ambalo si la busara hata kidogo mbele ya uislamu na jamii kwa ujumla. Dini ya kiislamu imezuia na inaendelea kuonya viakali kabisa mtu au watu fulani kuchukua dhima ya kufikiri kwa niaba ya wengine. Kwamba, waandishi wa muongozo huo wameonyesha dhamira ya wazi ya kuwadharau waislamu kwa kuwaona ni wavivu wa kufikiri na kutoa mawazo.
Kimsingi, muongozo huo kabla ya kuandikwa ulipaswa kukusanya mawazo ya waislamu kitaifa. Kwamba, waandishi wa muongozo walipaswa kutumia njia za utafiti katika kukusanya maoni kuanzia ngazi ya kata,wilaya hadi mkoa.
Njia za maswali katika vikaratasi, usaili, na vikundi-mjadala(focus group discussion) zilipaswa kutumika katika kukusanya mawazo ya waislamu kuhusu dira yao katika kuelekea uchaguzi mkuu 2010.
Mawazo hayo ndiyo yangeweza kuunda kitu ambacho kinaitwa muongozo. Zoezi hili lingekuwa gumu sana lakini ndio msingi wa haki na uwakilishi huru. Hii ni kwasababu kila muislamu ana maono,fikra,utashi na upembuzi wake binafsi katika kuyaangalia na kuyaendea mambo mbalimbali katika duru za kijamii.
Waislamu wa Tanzania bado hawalazimiki kujifungamanisha na mrengo wa siasa za aina fulani ili kukidhi mahitaji yao kama ambavyo waandishi wa muongozo wanainisha. Badala yake watabakia kuwa watu wa kundi maslahi.
Waandishi wa muongozo wanatiririsha maelezo kwamba CCM imelikumbatia kanisa katoliki ili kuwahujumu waislamu kupitia serikali. Hapa waandishi wanajaribu kuifitinisha serikali na waislamu, na kuwafitinisha waislamu na wakatoliki. Jambo hili ndugu zangu waislamu mlioandika muongozo si zuri. Huu ni uchochezi. Mnawaongoza waislam katika vita kali sana ambayo hamtoweza kuizima.
Na hatari zaidi waandishi wa muongozo wamelemazwa kabisa akili na maneno ya kilaghai ya kitabu cha padri aliyefukuzwa na kanisa katoliki,bwana Sivalon. Ukweli ni kwamba maelezo ya sivalon yalikuwa na utashi binafsi,hayakutafitiwa na yamepitwa na wakati. Ilikuwa ni presha tu. Ukweli wa hili unathibitishwa na kifungu kifuatacho cha muongozo huo kilichopewa anuani ya “mapinduzi ya kanisa” ambacho kinanukuu melezo ya Sivalon kama ifuatavyo:
“Padri sivalon anafafanua kuwa viongozi wa kanisa katoliki walikuwa katika nafasi nzuri ya kuelekeza ujamaa na viongozi wa serikali waliwatambua hivyo. Kwa kutumia mapinduzi haya ya kimya kimya kanisa limefanikiwa kuitumia mno serikali kwa maslahi yake, kiasi cha kufunga mikataba mikubwa na ya kudhulumu raia wa jamii ya wengine wasiokuwa wakristo. Mfano hai wa hili ni ule makataba wa mwaka 1992 ujlikanao kama memorandum of understanding between Christian council of Tanzania and Tanzania Episcopal conference and the united republic of Tanzania (MoU)”
Kifungu hiki kimenukuliwa kwa dhamira na dhana ileile ya uchochezi ya waandishi wa muongozo. Msingi wa kifungu hiki si wa kweli. Kwanini? Kwasababu: mkataba wa MoU uliwanufaisha na unaendelea kuwanufaisha watanzania wa dini zote.
Ukweli ambao waandishi wa muongozo wa waislamu walipaswa kuuainisha kuhusu mkataba wa MoU ni kwamba kwa wakati ule tayari makanisa kupitia wazungu ambao ni wafadhili wao waliweza kujenga hospitali kubwa kama vile KCMC, Bugando na nyinginezo.
Hospitali hizi dhahiri zimekuwa zikihudumia jamii kubwa ya watazania. Ili kukidhi gharama za uendeshaji zilihitaji msaada wa serikali. Na kiutaratbu serikali haiwezi kutoa msaada kama raia mwema anavyotoa msaada kwa kwa ombaomba barabarani. Lazima pawe na mkataba. Hii ndio kusema baada ya mkataba wa MoU haspitali hizi zikaidhinishwa kuwa za rufaa.
Waislamu ni miongoni mwa watu wanaopata huduma na ajira katika hospitali za KCMC,BUGANDO na hospitali nyinginezo za misheni. Hili hakuna muislamu atakayethubutu kulipinga.labda asiyemuogopa Allah.
Lakini waandishi wa muongozo huo wameficha kabisa kuainisha hili! Ni ajenda gani hii kama si uchochezi? Ajenda hii inajenga mustakabali gani wa waislamu na Taifa?
Rejea pia kifungu hiki “waislamu wengi hunyimwa huduma stahiki na kuzuiliwa fursa muhimu kwa sababu tu ya uislamu wao. Ubaguzi huu umepelekea taasisi nyingi za umma, kwa mfano wizara ya elimu, baraza la mitihani, bodi ya shirika la taifa la utangazaji(TBC) na TRA kuwa na twaswira ya parokia. Katika maofisi ya serikali waislamu hunyimwa uhuru wa ibada na hasa swala, ikiwemo ijumaa na kuvaa mavazi ya stara”
Kifungu hiki pia ni cha kichochezi. Waandishi wameficha kuweka wazi orodha ya majina ya watumishi yanayounda taswira hiyo ya kiparokia. Pili, mheshimiwa rais Jakaya Kikwete aliepuka uteuzi wa aina hiyo. Kwa mfano, wizara ya elimu inaundwa na waziri(muislamu), manaibu waziri wawili(mkristo na muislam), Katibu mkuu(muislam) na naibu katibu mkuu(mkristo). Parokia inajengwaje hapo? Halikadhalika, baraza la mitihani, bodi ya shirika la taifa la utangazaji(TBC) na TRA muundo ni wa aina hiyo.
Aidha kuhusu kunyimwa uhuru wa kuvaa hijabu, waadishi wa muongozo wa waislam wanazidi kutia petroli moto wa uchochezi. Hebu ndugu yangu muislamu na mtanzania mwingine yeyote mtazame waziri Hawa Ghasia;havai hijab? Waziri Mwantum Mahiza havai hijab? Waziri Batilda Buriani havai hijab; halikadhalika wanafunzi waislamu vyuoni na mashuleni hawavai hijab? Labda ni idara za serikali ipi ambazo waandishi wa muongozo wanazikusudia?
Uchochezi si jambo jema hata kidogo. Kwa nini waandishi wa muongozo wanathubutu kupandikiza mbegu hiyo kwa jamii ya waislamu? Rejeeni kwa Mola wenu. Kaeni chini mtubu dhambi hiyo. Dhambi yenu italitafuna Taifa.
Mwisho niseme tu hakuna haja ya kutumia mbinu ya uchochezi ili kuwachota waislamu na kuwamimina katika chama fulani cha upinzani. Hii si mbinu muafaka. Waacheni wanasiasa wapige kampeni na kunadi sera na ilani za vyama vyao kisha waislamu na watanzania wengine waamue.
Mimi nimesikitika sana kuona waandishi wa muongozo wa waislamu wananakili vvipengele vya ilani ya chama Fulani cha siasa kuwa vipengele vya muongozo wa waislamu. Ni kufilisika gani huku!
Mathalan, katika muongozo huo, vipengele vya taswira ya uchaguzi mkuu uliopita, dhana ya uchaguzi, uhuru wa kutoa maoni, tumefikaje hapa tulipo,maadili, elimu, afya,kilimo, fedha na uwezeshaji, maisha bora, sheria, umoja na amani, muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uwakilishi wa umma, hadaa za uchaguzi na dira ya uchaguzi, waandishi wa muongozo wamenakili bila woga sera zilizoainishwa katika ilani na katiba ya chama Fulani cha siasa! Dhamira hasa ni kuwalazimisha waislam waamini tu CCM ni mbaya na badala yake wawe chama Fulani cha upinzani. Huu si mkakati mwema wa kutamalaki maslahi ya waislamu na Taifa, na wala si mtindo huru wa kupiga kampeni.
Ningewashauri waandishi wa muongozo kwa waislam waitishe mkutano na waandishi wa habari watangaze kuufuta muongozo huo na badala yake watangaze kuandaa muongozo mwingine mpya ambao utakuwa wa kidemokrasia, huru na wenye kujenga mustakabali mwema wa waislamu na watanzania wengine .
Mwandishi wa makala haya ni muumini wa dini ya kiislam, mwalimu wa chuo kikuu na pia ni msomaji wa gazeti la Tanzania Daima. Anapatikana katika simu nambari 0713 111058
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
7 comments:
NAPENDA NIKUPONGEZE MR TWAHIR HUSSEIN KWA MAELEZO YAKO MAZURI-
KUNA VIONGOZ WA DINI WANAJARIBU KUTUMIA NYAZIFA ZAO VIBAYA PASIPO KUANGALIA MAMBO KWA UNDANI-NA KUJIKUTA WANAWAJAZA CHUKI ZISIZO ZA MSINGI WANANCHI-WANAFANYA HIVYO PASIPO KUWA WAKWELI-NA WATU WA MTINDO HUU WASIPOKEMEWA WATAHARIBU JAMII
Mi nafikiri kusema kwake mwandishi kunawanufaisha yeye na wanaokubali mtazamo wake.
Kama waislamu wanakosea, mjuwe kuandika hivi hakuwakosoi chochote kwa sababu ya manunguniko ya dhuluma ambayo yamedumu vizazi na vizazi (yakirithishwa kwa maandishi na simulizi) tangu wakati wa serikali za ki-mishenari. Hii itadumu kama utumwa unavyosimuliwa marekani mpaka kesho.
Manunguniko haya huwa yanakuwa-dismissed kama vile " ni kweli wako duni kielimu na kiuchumi na wako wengi magereza lakini wenyewe hawataki shule, wanataka madrsa tuu ili waende mbinguni." Kauli hizi hazimsaidii yeyote, mlalamishi, mkimya, wala mkataaji.
Hakuna hata utafiti mmoja umefanywa kuona je minunguno ina ukweli? na majibu yake yana suluhu? majibu na manunguniko bado yako kwenye kiwango cha dhana kitaalamu. Hii haimaanishi manunguniko yanaweza yasiwe ya kweli.
Na data mbona ziko wazi tuu. Ila kila mtu huzitumia data kwa faida yake mwenyewe ya kiimani au kichama. hiyo ndo kawaida ya takwimu.
IJULIKANE "kama kweli ubaguzi wa elimu kwa misingi ya imani ulikuwepo tangu wakati wa mkoloni au baada ya uhuru, SI KOSA LA UKRISTO, bali la viongozi ambao hawakuuelewa" hivyo ukristo hautakiwi KULAUMIWA bali wakosefu. Watu hujitetea kwa hofu ya kuumizwa imani zao.
Lakini kama pia ni kweli wazee wetu walikacha shule kwa kuogopa kusoma dhana ya Darwin, pia si kosa la Uislamu bali la waislamu hao.
Kuzomeana hakutatatua tatizo lolote bali kushirikiana woote kuwakwamuwa walio nyuma kwa faida ya taifa(ukiacha wanaotaka kuonekana dini yao ndo ya kweli kwa sababu wafuasi wao wamebarikiwa elimu na uchumi: hata farao alibarikiwa ufalme, elimu, na utajiri) .
Pia kutaka watu wakae kimya kwa sababu wanchokisema kinakuumiza si uungwana.
hivi kwenye nchi yenye takriban 50% ya raia ni waislamu, kwa nini mpaka leo kuna kuomba ruhusa kwenda kusali ijumaa?
hivi kwa nini wanafunzi huruhusiwa kwenda kusali ijumaa na madarasa yanaendelea wakati huo? Hivi haki hii siyotekelezeka si ni sawa na iliyonyimwa? (unasemaje hapo Prof?)wakifeli somo hilo majibu yake ni yepi?
anayewabagua wavaa hijabu si serikali bali kadhaa wenye mamlaka wapatapo fursa ya kulifanya hilo.
na hapa kwetu hakuna sheria ya ubaguzi useme utadai haki itendeke kama katika nchi za magharibi ambapo waislamu ni <2% lakini kuna sheria inawalinda wakizomewa ugaidi au kubaguliwa.
ukilalama we ndo unaitwa mdini, hivyo meza pini.
katiba mpya inabidi iwe na vifungu vya kudhibiti ubaguzi wa kidini, kikabila, na kirangi. siyo kutangaza tuu "tunalaani ubaguzi wa aina zoote". Je ukitokea mnatatuaje?
dhamana ya kuzuia ubaguzi inaweza kuwa mikononi mwa mbaguzi. hakuna cheki andi balansi.
NAKUPONGEZA BWANA TWAHIR HUSSEIN.
NAOMBA NIULIZE NANI NI MBORA KULIKO WOTE WENYE ELIMU/NANI ANAJUA ZAIDI?WAJUA KISA CHA MUSA(A.S)NA KHIDHR(A.S)?HIVYO TUSITAFUTE LESENI YA UHALALI WA KUWASEMEA WENGINE KWA MGONGO WA ELIMU.
WAKATI JUMUIYA YA KIISLAM YA EAST AFRICA ILIPOVUNJWA,BW.TWAHIR ALISHIRIKI KUTOA MAWAZO YAKE AU HATA SASA AMETOA?KWA NINI?
BW.TWAHIR ANAWEZA TUWAELEZEA SABABU YA WAISLAM KUWA NYUMA KIMAENDELEO?
NADHANI AKITOA MAJIBU HAYO NDIPO TUTAWAHUKUMU WENGINE,KUTOA RAI SI DHAMBI
Post a Comment