Picha hii ilipigwa Dar es Salaam, Septemba 2004,kwenye viwanja vya makumbusho ya Taifa, wakati wa tamasha la vitabu. Naonekana nikiwa na walimu kutoka Kunduchi Girls Islamic High School. Walikuja na hao watoto kwenye meza ambapo nilikuwa nimeweka vitabu vyangu.
Tulizungumza na kushauriana mambo ya manufaa kuhusu elimu na kadhalika, nao walinialika kutembelea shule yao. Haya ndio mambo tunayohitaji katika nchi yetu. Na hao watoto katika picha wanasikia tunachoongea sisi watu wazima. Tuwaleavyo ndivyo wakuavyo.
Ninapowakumbuka na kuwaangalia watoto, kama hao waliomo katika picha, hisia zangu za kiualimu zinaibuka. Kwa upande mmoja, nafurahi na kushukuru kuwa nimejaliwa uwezo na fursa ya kuwaelimisha watoto hao. Ninawapenda. Soma, kwa mfano, makala yangu hii hapa.
Papo hapo, ninapowawazia watoto wa Taifa letu, najiwa na wasi wasi kwa jinsi baadhi ya watu wanavyoeneza mitazamo na mawazo kama udini, ubaguzi na uhasama baina ya makundi mbali mbali ya jamii. Hizo ni sumu, nami nahofia athari zake kwa watoto wetu.
Ualimu ni wito, nami nilisikia wito huu wakati nikiwa bado mdogo, sijaanza hata shule. Ni wito wa kuwa mtafuta elimu muda wote, wito wa kuwalea wanafunzi wawe wanaothamini na kutafuta elimu; wawe watu wema kwa mujibu wa maadili ya jamii yao. Elimu haina mwisho. Mimi ni mwalimu wa madarasa ya chuo kikuu, kuanzia mwaka 1976, lakini ningefurahi kama ningekuwa pia na utaalam wa kuweza kufundisha shule ya msingi. Nimeelezea hayo katika kitabu cha CHANGAMOTO.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
4 comments:
'Neno kuhusu ualimu' Hapo zamani ualimu ulikuwa wito,kwani mwalimu alikuwa anaguswa sana na mwanafunzi wake akiwa hamwelewi katika somo lake,pamoja na mapungufu ya mahitaji kwa mawlimu yule yalikithiri katika mazingira yake ya kufanya kazi.
Lakini kwa kipindi hiki ualimu umekuwa ni kimbilio la wale walioshindwa kwenda kufanya kazi kule alikoitwa ama kwa kushindwa kufanya vizuri katika mitihani ya mwisho au kukosa eneo la kufanyia kazi.
Lakini pia hata wale walimu ambao wamekuwa walimu wa wito wamekatishwa tamaa na mazingira ya kutolea elimu kwa kuwa haki ya mtoto imeharibu mazingira ya kutolea elimu.
Isitoshe watu hawana utamaduni wa kusoma vitabu ndiyo maana wazazi hawana mwamko wa kuwasomea watoto vitabu kama wanavyo fanya wenzetu kule marekani.
Profesa napenda kazi yako na inamanufaa kwa nchi kwa kuelimisha mambo mbalimbali ya kujisomea.Kusoma vitabu mbalimbali ndio kujua mambo mbalimbali ktk dunia.
Lakini kuna kitu kimoja ambacho ni muhimu sana na nauhakika utaweza kuwahusia wasomaji hasa ktk mtandao na ukaomba watu watoe maoni yao.
Ni kuhusu utumiaji wa lugha ya Taifa.Watu wamekuwa wanaitumia lugha ya kiswahili vibaya yaani sio tu kwa kuongea hata ktk kuandika.Nimegundua ktk mitandao mbalimbali jisi watu wanavyoelezea jambo fulani na kuandika kimakosa.
Utakuta anaelezea jambo na badala ya kuweka "L" anatumia "R".Sijui kwa wewe profesa na umesoma vizuri lugha unaionaje.Naweza kufahamu kama sisi wananchi tumetoka mikoa tofauti na kila mkoa kunakuwa na "accent"tofauti,na hii inaeleweka na haina matatizo.Lakini profesa ktk maandishi lazima tuweke lugha fasaha hata kama tunamatatizo ktk matamshi tukiongea.
Mimi nipo uingereza hivi sasa, na huku kuna mikoa tofauti na "accent"zipo tofauti lakini sijawahi kuona ktk maandishi wakatofautiana.
Utakuta ameandika "rikizo"=likizo,"luhusa"=ruhusa na mengi tu ambayo sisi wenyewe tunatakiwa tuwe wajuzi wa kutumia lugha yetu na sio tena waje watu kutufundisha kutoka nje. Sijui pro.. kwa haya maelezo yangu unayaonaje ikiwa kuna wageni wengi wanapenda kujifunza kiswahili sasa je tuwafundishaje ili waijue kwa ufasaha zaidi.
Pro..naomba utoe mada ili watu wachangie hata kupitia kwa mjengwa na Global kama utaweza.Nadhani ni moja ya kuwafundisha na kukumbushana matumizi ya lugha yetu nzuri na ya kujivunia.
Asante Mzee Sikapundwa, kwa mchango wako. Ni kweli; tunapowapeleka watu walioshindwa masomo wakafundishe, tunajichimbia kaburi.
Mimi nilikuwa na bahati kuwa nilipata huo wito wa kuwa mwalimu tangu utotoni, na nilipokuwa shuleni nilikuwa nashika namba za juu kabisa kimasomo, na bado ndoto yangu ilikuwa ni kuwa mwalimu tu. Sikuwahi kuwazia wala kuchagua mkondo mwingine wowote. Na mpaka leo, ualimu ndio maisha yangu, wala sitaki kingine chochote.
Namshukuru Mungu kwa kunijalia hayo, kwani wengine wameingia kazi hii kwa shingo upande au kwa vile hawakuwa na jinsi. Nawasikitikia.
Nakushukuru pia mdau uliyegusia suala la lugha. Ni suala zito. Ni kweli kuwa tuna tatizo kubwa katika jamii yetu, la watu kutotumia vizuri kiSwahili. Inanikera sana. Hata wabunge na hao wengine tunaowaita viongozi wanakosa nidhamu katika suala hilo, kwa kuchanganya kiSwahili na maneno ya kiIngereza wanapokuwa kwenye mazingira rasmi kama Bunge au mkutano wa hadhara.
Watangazaji wengi katika televisheni nimeona wanakosa hii nidhamu pia, na huwa napata kichefuchefu.
Kutotumia lugha yetu ipasavyo ni kujidhalilisha. Inaleta picha kuwa hatujiheshimu, kwani nafsi ya jamii imejengeka katika lugha yake. Kutoheshimu lugha ni kutojiheshimu.
Kutokana na kutambua hayo, mimi binafsi nimekuwa nikifanya juhudi ya kujifunza kiSwahili sanifu na kukiandika. Hadi sasa nimeandika makala na hicho kitabu kiitwacho CHANGAMOTO.
Huyu msomaji ambae analalamika kuhusu matumizi ya lugha anaonekana kabisa kuwa ni mtumiaji wa lugha na si muelewa wa lugha. Kwanza anasema eti yeye yuko UK ambako kuna accent tofauti na hajaona watu wakifanya makosa yanayofanana na L and R. Kwanza nimuulize hajaona wapi hayo makosa? Hajaona kwenye magazeti ya UK au kwenye blogs. Kitu ambacho ameshindwa kuelewa ni kuwa Waingereza English ndio lugha yao ya kwanza.Wabongo waliowengi Kiswahili sio lugha yao ya kwanza wengi wana lugha za makabila yao kama lugha zao za kwanza. Sasa lugha za kwanza zinaathiri matumizi ya kugha yako ya pili. Watu wengi ambao wana lugha mbili ambazo moja wanaielewa sana na moja sio sana wanaonesha athari za lugha moja kaika maandishi na hata katika matamshi. Hebu kwa haraka angalia maneno haya kutoka katika blog ya Mjapani "University Cantine Food - Japanese Style" (http://inanban.blogspot.com).Vipi umeona kosa gani hapo. Neno canteen limekosewa. Hii ni athari ya lugha yao ya kwanza kijapani. Sasa usiwalaumu Wakurya au wasukuma kwa makosa katika uandishi wa Kiswahili. Kiswahili sio lugha yao.
Post a Comment