Monday, April 11, 2011

Ugumu wa Kusoma Vitabu vya Dini Isiyo Yako

Hapo juzi, niliandika kuwa nasoma vitabu vya dini mbali mbali. Lakini jambo moja ambalo sikuongelea ni kuwa inaweza kuwa vigumu kufikia uamuzi wa kusoma vitabu hivyo. Napenda kuongelea uzoefu wangu.

Nilizaliwa katika familia na jamii ya wa-Katoliki. Dini pekee iliyokuweko katika eneo langu, kwa maili nyingi kuzungukia eneo hilo, ilikuwa ni u-Kristo, madhehebu ya Katoliki. Watu pekee ambao hawakuwa wa-Katoliki ni wale wachache ambao walikuwa hawajabatizwa.

Sikumbuki kama niliwahi kusoma kitabu cha dini nyingine yoyote au dhehebu jingine lolote zaidi ya u-Katoliki. Hata niliposoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1973, nikaanza kufundisha hapo mwaka 1976, katika idara ya "Literature," sikumbuki kama nilisoma kitabu cha dini nyingine.

Lakini nilipokuwa nasomea shahada ya juu katika Chuo Kikuu Cha Wisconsin-Madison, 1980-86, nilipata fursa ya kufahamiana vizuri na mwanafunzi mwenzangu mu-Islam kutoka Sudan. Huyu alikuwa mmoja wa marafiki zangu.

Alipoona nina hamu ya kufahamu kuhusu u-Islam, alifanya mpango akanitafutia nakala ya Quran ambayo ni tafsiri ya Abdullah Yusuf Ali. Aliniambia kuwa hiyo ndio tafsiri inayotambuliwa na kuheshimiwa zaidi.

Hiyo ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuishika Quran. Kabla ya hapo, Quran ni kitabu nilichokuwa nakisikia tu, na hata kukiogopa. Tuna umbumbumbu sana nchini mwetu, hata kufikia kuwa na hofu za namna hiyo. Sikutegemea ningethubuku kuishika Quran. Lakini baada ya kupewa namna hii, tena na mu-Islam niliyemfahamu kuwa amebobea katika dini yake, hofu ilitoweka.

Nilianza kuisoma. Kitu kilichonishangaza tangu kurasa za mwanzo, ni jinsi masimulizi yake yanavyofanana na yale ya "Agano la Kale" katika Biblia. Nilishtuka. Suali lililokuwa linazunguka kichwani mwangu ni je, kwa nini watu tunaamini kuwa vitabu hivi ni tofauti sana, kama mchana na giza? Hilo limebakia suali ambalo natafuta jibu lake, na labda hatimaye nitapata jibu lake.

Baada ya kuja huku Marekani, mwaka 1991, kufundisha masomo ya fasihi, nimejikuta nikifundisha maandishi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Mengi yamekuwa ni maandishi ya wa-Islam kutoka nchi kama Misri, Senegal, Mali, Somalia, Pakistan, na India.

Mara kwa mara, katika hadithi zao, mambo ya u-Islam yanajitokeza. Kwa hivi, ili niweze kuyaelezea vizuri katika ufundishaji wangu, imenibidi nijifunze zaidi kuhusu u-Islam. Mfano ni riwaya ya Twilight in Delhi, kama nilivyoelezea hapa.

Katika kufundisha somo hilo hilo la fasihi, nimejikuta nikifundisha fasihi ya nchi kama India, ambako dini kuu ni u-Hindu. Katika maandishi hayo, na hata baadhi ya maandishi kutoka sehemu kama visiwa vya Caribbean, dini hii inajitokeza mara kwa mara. Kwa hivyo, imenibidi kusoma kuhusu dini hii ili niweze kuelezea yale yaliyomo katika fasihi.

Kwa kifupi, nafurahi jinsi mambo yalivyotokea katika maisha yangu, hadi kunifikisha hapa nilipo, katika hali ambayo nina motisha na pia fursa ya kusoma maandishi ya dini mbali mbali.

Lakini, bila mazingira hayo, huenda ningekuwa bado nimejifungia katika dini yangu tu. Huenda ningekuwa bado naogopa kuvigusa vitabu vya dini nyingine. Huenda ningekuwa naogopa kukiuka au labda "kuchafua" imani ya dini yangu.

Naamini hofu za namna hii wanazo wengine pia. Lakini, nashukuru kuwa sioni tatizo lolote katika hayo ninayofanya, wala imani yangu katika dini yangu haijawahi kutetereka. Badala yake, naona nimejifunza kuziheshimu dini za wengine.

7 comments:

Anonymous said...

Profesa nakuheshimu sana kwa bidii yako na kujifunza ya dini na dunia.Kwani elimu ndio msingi wa kila kitu.Mimi ni muisilamu lakini hupenda kuona watu ambao wanajitahidi kujua ukweli na uongo ktk mambo mbalimbali ktk maisha ya kila siku.Ni ngumu kujua ukweli na uongo bila ya kuhakikisha kwa kujifunza.Nadhani pia itawasaidia watu wengine kufuata nyayo zako ili kutafuta maendeleo kwa vizazi vijavyo.kwani ikiwa tutawasihi watoto wetu kwa kujifunza kutoka ktk vitabu mbalimbali ili kujifunza historia tofauti.Historia nyingi zimetoka ktk dini kama tukifuatilia.Kwani jesus (piece be upon him)ametajwa na kusifiwa zaidi ya mara 90 ktk Qura-an.Lakini wakristo wengi hawafahamu kama uisilamu tunamkubali Jesus(piece be upon him)Isipokuwa ni jina ambalo hutumiwa na waisilamu kama Nabii ISSA (piece be upon him)Profesa Good luck.

Mbele said...

Shukrani kwa mchango na mawaidha hayo. Ni kweli tutakuwa tunafanya jambo la maana sana iwapo tutajenga utamaduni wa kujielimisha muda wote.

Binafsi, najisikia kama akili na nafsi yangu inakuwa mpya kutokana na kila kitabu ninachosoma. Napata faraja maishani.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

ndio, labda ni hofu kama unavyosema na sasa imeisha, kumbuka huwa tunashauriwa kutokusoma vitabu vya dini nyingine eti tutapotea! lakini wanaotuzuia huwa wao wanavisoma sana tu, kwa hiyo wanakuwa wajuaji wa kutupangia tusome nini.

mimi hiyo hali niliipinga nikiwa bado kinda.

ila sasa tatizo la kusoma vitabu vya dini tofuti kama biblia na koron ni kugundua kuwa vyote vinaongelea kitu kilekile kwa mazingira na tamaduni tofauti zisizokihusu sana kitu kiongelewacho.

tatizo la kusoma vitabu vya wahindi kama hicho cha-Hindu, bhagavadgita, adhigranth/granthsahib nk ni kwamba utakutana na ukweli fulani unaovutia zaid ya biblia na hivyo kujikuta una kiu ya kitu kingine kikubwa usichokijua labda!

kwa hiyo unaweza kujikuta unakuwa atheist kama mimi au meditato. labda utugundua dini zina mikwara kuliko uhalisia.

Anonymous said...

prof Mbele asante sana mimi ninasomaga mtandao wako.ktk wale waliokuwa wanakutukana juzi bado hawajasoma eidha biblia au korani hivyo hawana maarifa.mimi nilikuwa mkristo wa kilutheri baadaye nikaigia uislam sasa angalia mimi nilikuwa nafikiri mitume karibu wote ni wakristo ukiondoa mohamed tu.sasabasi kumbe uislam unawatambua karibu wote.baada ya hapo kumbe kwanini sasa tunabishana??? kumbe ni upumbavu unaotusumbua lakini kusomanakupata maarifa ni bora zaidi

Mbele said...

Kauli hizo hapa juu, kuwa kuna kufanana kwa hizi dini, ni muhimu.

Kwa mujibu wa Karen Armstrong, ambaye anaheshimiwa na watu wa dini mbali mbali kwa utafiti wake kuhusu dini hizo, ametufundisha kufanana kwa mafundisho ya msingi ya dini mbali mbali. Fundisho la msingi kabisa ni kuwatendea wengine kama tunavyopenda kutendewa, au tusiwatendee wengine yale ambayo hatupendi kutendewa.

Tungezingatia hayo, magomvi, jazba, na mabaya mengine watu wa dini mbali mbali wanayofanyiana yangetoweka. Msikilize Karena Armstrong hapa.

Anonymous said...

Prof, kazi yako ni kuwafanya wasiopenda kusoma wasome ili wapanue mawazo.

Ila juwa kuwa unapigana na wale wanaozuia usomaji. Ikiwemo viongozi wa dini kadhaa.

Mbele said...

Anonymous wa April 18, ni kweli usemayo. Tukisema tuwahoji waumini wa dini mbali mbali iwapo wana mtazamo gani kuhusu vitabu vya dini isiyo yao, huenda tukasikia mengi ya ajabu.

Tumeigeuza dini kuwa kitu cha kuendeshea magomvi na uhasama.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...