Monday, April 25, 2011

Msamvu, Morogoro

Blogu yangu hii ni sehemu ya mambo mengi binafsi, zikiwemo kumbukumbu. Leo najikumbusha kuhusu Msamvu, kitongoji cha mji wa Morogoro. Ni kumbukumbu ya ziara yangu ya mwaka jana, ambayo nilishaielezea kidogo katika blogu hii.

Morogoro ina vitongoji vingi, ambavyo sivijui kabisa au sivijui vizuri. Ila nimepata fursa ya kuifahamu Msamvu, maarufu kwa sababu ni kituo kikubwa cha mabasi.


Msamvu ni sehemu ya biashara. Kuna migahawa na vijiduka. Kwa wafanyabiashara ndogo ndogo, wasafiri ni wateja muhimu. Wageni kutoka ughaibuni wanapofika kwetu wanashangaa kuwa basi linaposimama, ghafla linavamiwa na wachuuzi wa kila aina ya bidhaa, ambazo hupitishwa madirishani, kuanzia matunda na biskuti hadi kadi za simu.

Kule mbele, kwenye miti, kuna hoteli na baa nzuri. Nimewahi kutua hapo mara mbili tatu, wakati nikingojea usafiri wa kwenda Dar es Salaam. Ni sehemu nzuri ya kupumzikia.

4 comments:

Christian Sikapundwa said...

Profesa karibu sana Morogoro,karibu Msamvu.Kweli Morogoro inavijitongoji vingi,lakini vya mwanzoni kabisa kabla hujaingia Msamvu,kuna kitongoji cha Chamwino,baadaye unapita liwanda cha tumbaku.

Ukitoka kituo cha mabasi ukielekea Dar es salaam utavuka kidaraja pembeni mkono wa kushoto kuna maliri ya mafuta yakioshwa pale panaitwa Tungi.

Mbele yake kidogo kuna kituo cha mafuta Oil Com ambapo kwenye eneo la wazi kabla yake kwa juu kuna kijilima na miashoki pale ni nyumbani kwangu.

AST said...

Nilishangaa kwamba hata chupi na nguo za ndani zinapatikana kwenye standi za mabasi.

Nilipokaa Morogoro, nilikaa Kihonda kwa hiyo ninapafahamu vizuri Msamvu. Asante kwa kumbukumbu zako!

Albert Kissima said...

Likizo yangu ya Pasaka nilikuwa Morogoro hususani Kihonda. Nilipata bahati ya kupita stand ya Msamvu mara nyingi.

Nimefurahia sana milima ionekanayo kwa uzuri kabisa pindi uwapo Msamvu Stand, bila shaka ni ni mwendelezo wa milima ya Uluguru.

Kuna jambo lilinishangaza na kunifurahisha sana pale Msamvu. Nilipata bahati ya kuona teknologia mpya ya uuzaji mishikaki. Mimi nimezoea kuona mishikaki inaandaliwa katika sehemu maalumu. Ukishaondoka sehemu hiyo, basi ni hadi upate tena sehemu nyingine maalumu. Katika Stendi ya Msamvu, nilimuona jamaa anatembea huku anachoma/anaandaa mishikaki, yaani anatembea na jiko, jepesi tu, limeandaliwa vyema kwa kazi hiyo, kama wauza karanga vile. Hili sikuwahi kuliona popote. Sikubahatika kupiga picha teknolojia hiyo mpya.

Mbele said...

Wadau nawashukuruni sana. Kweli blogu ni kitu kizuri. Unaweka kitu kidogo, halafu wadau wanakuja na kukipanua na kukiongezea. Mmepanua upeo wangu kuhusu eneo hilo la Msamvu na mambo yake.

Mzee Sikapundwa kumbe ni mwenyeji wa maeneo hayo. Habari nzuri. Nitakapokuwa napita humo barabarani kuelekea au kutokea kwetu Ruvuma nitakuwa nakumbuka.

Itabidi nifanye mkakati wa kutua Msamvu mara kwa mara, maana ni kwa watani zangu.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...