Posts

Showing posts from May, 2009

Jiwe la Mmbuji

Image
Hili ni Jiwe la Mmbuji. Liko mahali paitwapo Ngwambo, katika nchi ya Umatengo, wilayani Mbinga, mashariki ya Ziwa Nyasa. Jiwe hili kubwa linasemekana lina maajabu. Wamatengo tangu zamani wanasimulia mambo ya ajabu yanayotokea hapa. Wamatengo wanaamini kuna viumbe viitwavyo ibuuta . Ni kama binadamu, ila wadogo sana, na wa ajabu, na katika mataifa mengine wanajulikana pia, kwa majina mbali mbali. Wamatengo wanasema kuwa ibuuta wanakuwepo kwenye jiwe hili usiku wakifanya mambo yao. Nyumbani kwangu sio mbali na hapo, na jiwe hili tulikuwa tunalisikia tangu tukiwa wadogo. Tukipanda mlimani kijijini kwetu, tulikuwa tunaliona. Mwaka jana nilipita karibu na eneo hili, nikapiga picha ya jiwe hili kama inavyoonekana hapa. Hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kulikaribia jiwe hili namna hii. Nilishangaa kuona watu wamelima mashamba karibu yake, na wanaishi sio mbali na hapo. Habari nilizozisikia tangu utoto wangu kuhusu jiwe hili zilinifanya niamini kuwa hakuna mtu anaweza kusogea hapo, achil

Maprofesa Hatuvunji Msitu, ni Mwalimu wa Shule ya Msingi

Makala hii imechapishwa katika Kwanza Jamii , Mei 19, 2009 ********************************************************************************* Maprofesa Hatuvunji Msitu, ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Na Profesa Joseph L. Mbele TUNAONGELEA sana mfumo wa elimu. Kitu kimoja ninachoona hatukizungumzii ipasavyo ni wadhifa wa mwalimu wa shule ya msingi. Jamii haimwoni mwalimu wa shule ya msingi kama mtu wa pekee sana. Lakini, akitokeza mwalimu wa chuo kikuu, kama mimi, jamii inafungua macho na kutega masikio. Jamii inamwona mwalimu wa chuo kikuu, profesa, kuwa mtu wa pekee sana, kumzidi mwalimu wa shule ya msingi. Kwa miaka kadhaa sasa, nimejjijengea mtazamo tofauti kuhusu suala hilo. Hii ndio mada ya makala yangu hii. Hoja yangu ni kuwa, mwalimu wa shule ya msingi anastahili heshima ya pekee. Tunaposema shule ya msingi, tuzingatie neno msingi. Neno msingi tunalitumia sana tunapoongelea ujenzi wa nyumba. Basi, tuchukulie mfumo wa elimu kama nyumba. Tunapowazia kujenga nyumba, tunazingati

Podikasti ya Kwanza Jamii

Image
Waweza kujipatia picha ya hali ya maisha ya sehemu fulani za vijijini Tanzania katika podikasti ya Kwanza Jamii , kama ilivyorekodiwa na ndugu Maggid Mjengwa. Isikilize hapa

Watoto na Matatizo ya Mtindio wa Ubongo

Makala hii ya Dada Yasinta aliiandika katika blogu yake ya Ruhuwiko nami niliipenda na naiweka hapa kwa ruhusa yake. ***************************************************************************** Friday, May 15, 2009 WATOTO NA MATATIZO YA MTINDIO WA UBONGO Ngoja tuendelee na mada hii lakini samahanini imekuwa kinyume. Wapo watoto wengi wanaozaliwa wakiwa na matatizo mbali mbali, lakini mojawapo nitatizo la mtindio ya ubongo ambalo leo nimeona nilizungumzia kwa undani zaidi. Matatizo ya mtindio wa ubongo yanatokana au kusababishwa na kizalia (Genetic), dawa alizotumia mama wakati wa ujauzito, matumizi ya madawa ya kulevya, pombe, hali ya hewa, au hata ajali. Mojawapo ya sababu hizo nilizozitaja zinaweza kusababisha kuzaliwa kwa mtoto mwenye mtindio wa ubongo au mtu kupata mtindio wa ubongo. Nikianza na tatizo la pombe, ni kwamba pombe ina athari kubwa na mbaya kwa akina mama wajawazito. Lipo tatizo linalofahamika kitaalamu kama Fetal Alcoholic Syndrome (FAS) ambalo huwapata watoto am

Sophie's club: Collection yangu sasa inapatikana dukani

Sophie's club: Collection yangu sasa inapatikana dukani

Kipanya na Usomaji Vitabu

Image
Mimi kama mwalimu na mwandishi ninaliongelea sana suala la usomaji wa vitabu. Katika blogu hii, maandishi yangu mengi yanahusu suala hilo. Hapa kuna katuni ya Kipanya, ambayo nimeiona kwa Profesa Matondo . Inatoa mchango wake kwa mtazamo unaofanana na wangu. Nitatoa mfano mmoja. Tarehe 21 Juni, 2008, niliendesha warsha Arusha, na katika mazungumzo yangu nililalamikia tabia ya waTanzania kutopenda kusoma vitabu. Nilitoa mfano kama huu wa Kipanya, kwamba waTanzania wanaposafiri katika basi, hutawaona wakisoma vitabu. Hapo mwanawarsha mmoja, mama Mwingereza, alitoa hoja kuwa utamaduni wa waTanzania wa kuongea na wenzao ndani ya basi unaonyesha wanavyojali mahusiano ya mtu na mtu, tofauti na wazungu, ambao kwao ni kila mtu na lwake. Alimaanisha kuwa jamii ya wazungu imekosa mshikamano; badala ya kuongea na binadamu mwenzao, wanashikilia kitabu. Hoja hii ilinifungua macho. Kipanya ana tovuti yake hapa

Mchango wa Wabeba Boksi

Leo, siku kuu ya wafanyakazi duniani, napenda kuwakumbuka wabeba boksi. Hao ni waTanzania wanaoishi ughaibuni, wakifanya kazi za mikono, kama vile kubeba na kupanga mizigo ya bidhaa madukani, kusafisha maofisi, kusafisha vyombo mahotelini, kuwatunza wazee, na kadhalika. Watanzania wanaposema kubeba boksi, wanamaanisha kazi za aina hiyo. Na jina hilo linatokana na huu kweli kuwa wengi wa wahusika wanabeba na kupanga maboksi. Wabeba boksi wanataniwa sana katika jamii ya kiTanzania. Wabeba boksi wengi nao wanajitania. Watanzania wengi wanaziona kazi za boksi kuwa ni kazi duni. Napenda kubadili mtazamo huo kwa kuelezea umuhimu wa boksi. Natumia hilo neno boksi kwa sababu linatumika pia kumaanisha kazi ya kubeba boksi. Jambo moja la msingi ni kuwa wabeba boksi wanatumia nguvu zao kujipatia kipato. Wao ni tofauti na wezi au mafisadi, ambao wanakula jasho la wenzao. Kwa msingi huu, mbeba boksi anastahili heshima. Kila kazi halali ina umuhimu wake katika jamii, iwe ni kilimo, uvuvi, usafish