Posts

Showing posts from July, 2015

Tamasha la Afrifest ni Kesho, Agosti 1

Image
Kesho ndio siku ya tamasha la Afrifest, mjini Brooklyn Park, Minnesota. Ni fursa ya watu kukutana, kujifinza kuhusu mambo mbali mbali ya historia, siasa na tamaduni za wa-Afrika na wanadiaspora wenye asili ya Afrika. Ni fursa ya kuuenzi mchango wa watu weusi katika dunia. Afrifest inafuata nyayo za viongozi maarufu waliofanya juhudi katika kujenga mshikamano miongoni mwa watu wenye asili ya Afrika, mshikamno ulioendana na ajenda za kujitambua na kupigania uhuru na ukombozi. Watu hao maarufu ni kama Henry Sylvester-Williams,  Marcus Garvey, George Padmore, W.E.B. DuBois,  Kwame Nkrumah, Jomo Kenyatta, Nnamdi Azikiwe, Julius Nyerere, Kenneth Kaunda na Walter Rodney. Katika sanaa, tunawakumbuka watunzi na waandishi maarufu kama Antar bin Shaddad (Saudi Arabia), Alexander  Pushkin (Urusi), Claude McKay (Jamaica na U.S.A), Peter Abrahams (Afrika Kusini na Jamaica) na Leopold Sedar Sengor (Senegal). Tunawakumbuka wanamuziki kama Bob Marley (Jamaica) na Miriam Makeba (Afrika Kusini)

Nimepata Vitabu vya Warsha: Jamii na Taaluma

Image
Leo nimepata vitabu vya warsha itakayofanyika hapa chuoni St. Olaf tarehe 17-20, mwezi Agosti, kuhusu jamii na taaluma. Warsha itawahusisha maprofesa wachache, kuongelea masuala kama nafasi ya mwanataaluma katika jamii, itikadi katika taaluma, na uhuru wa taaluma. Washiriki wa warsha tunapata vitabu vya bure, ambavyo tutavijadili katika warsha. Tutaanza na viwili. Kimoja ni Not for Profit: Why Democracy Needs the Humanities , kilichotungwa na Martha C. Nussbaum. Cha pili ni Versions of Academic Freedom , kilichoandikwa na Stanley Fish. Kwetu tuliomo katika masomo ya nadharia ya fasihi, maandishi ya Stanley Fish katika uwanja huo ni maarufu sana. Baada ya vitabu hivyo, tutajadili Compromising Scholarship: Religious and Political Bias in American Higher Education , kitabu cha George Yancey, na Professors and Their Politics , ambacho kimehaririwa na Neil Gross na Solon Simmon. Hiki cha pili ni mkusanyo wa insha za wataalam mbali mbali. Warsha itakuwa nzito, sawa na masomo ya k

Kitabu Umechapisha, Kazi ni Kukiuza

Image
Pamoja na kuandika vitabu, ninajitahidi kujielimisha kuhusu masuala yanayohusiana na uchapishaji, utangazaji, na uuzaji wa vitabu. Kwa bahati nzuri, kuna vitabu vingi na vingine vinaendelea kuchapishwa, na pia makala nyingi kuhusu masuala hayo. Napenda kuongelea suala la kukiuza kitabu. Niliwahi kuongelea suala hili katika blogu hii. Nimeliongelea pia katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii . Ni suali linalonigusa na kunifikirisha daima, nami napenda kuwashirikisha waandishi wengine katika kulitafakari. Usemi kwamba chema chajiuza, kibaya chajitembeza unaweza kuwa na mantiki nzuri kuhusiana na vitabu. Wateja wakiridhishwa au kufurahishwa na kitabu, hawakosi kuwaambia wengine. Aina hii ya utangazaji, ambayo kwa ki-Ingereza huitwa "word of mouth," ni muhimu sana. Mimi mwenyewe nimeshuhudia hivyo kutokana na kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Tangu nilipokichapisha kitabu hiki, mwaka 2005, wasomaji wamekuwa wakiwaamb

Rais Obama na Dada Yake Auma Obama

Image
Ujio wa Rais Obama nchini Kenya juzi umezua mambo mengi, ikiwemo furaha isiyo kifani miongoni mwa watu wa Kenya, Afrika Mashariki, na kwingineko. Kitendo cha Rais Obama kukutana na ndugu zake katika chakula cha jioni ni jambo la kukumbukwa. Kwa namna ya pekee, wengi tuliguswa na namna Rais Obama na dada yake Auma Obama walivyokutana. Nilivyomwona dada huyu, nilikumbuka kuwa niliwahi kumtaja katika blogu hii baada ya kununua kitabu chake, And Then Life Happens: A Memoir . Niliingia mtandaoni nikaona mahojiano aliyofanyiwa na mtangazaji wa CNN. Halafu nilikitafuta kitabu chake katika maktaba yangu nikakipitia, kwa kuwa nilikuwa sijakisoma, bali nilikuwa nimekipitia juu juu tu. Hakuna ubishi kwamba Auma Obama ni mama mwenye fikra za kusisimua na uwezo mkubwa wa kujieleza. Hilo linajitokeza wazi katika mahojiano yake. Masimulizi ya maisha yake, yaliyomo katika kitabu chake, yana mambo yanayoweza kuwahamasisha watoto wetu, hasa wasichana, wawe wanajiamini na kuwa watafuta elimu na m

Mdau Kanikumbuka

Image
Katika ujumbe wangu wa leo, naendelea na jadi yangu ya kuandika habari za wadau wangu, yaani wasomaji wa vitabu vyangu au wale wanaofaidika na ushauri ninaowapa, hasa kuhusu tamaduni na utandawazi katika dunia ya leo. Napenda kujiwekea kumbukumbu hizi. Mwanzoni mwa wiki hii, tarehe 19, nilipata ombi la urafiki katika Facebook. Nilivyoona jina la mhusika, Sandy, nilihisi kuwa si jina geni. Nilipoangali picha yake, nilikumbuka kuwa ni mama aliyewahi kunitembelea hapa Chuoni St. Olaf akiwa na rafiki yake, Desemba 2011. Niliandika habari za ujio wao katika blogu hii. Bila kuchelewa, nilikubali mwaliko wa urafiki. Jana nimepata ujumbe wa mama huyu katika Facebook. Wakati tulipoonana, huyu mama na mwenzake walinunua vitabu vyangu, na aliniambia kuwa nakala ya Africans and Americans: Embracing Cultural Differences alikuwa anamnunulia rafiki yake ambaye alikuwa anapanga safari ya kwenda Afrika. Kwa bahati mbaya tulipoteana kwa miezi mingi. Hatukuwa na mawasiliano. Baada ya kuungana

Kinachotokea Ukidondosha Pochi Yako Dubai

What happens if you drop your Wallet in Dubai ??Hats Off (y) Posted by RJ Rijin on  Thursday, January 15, 2015

Tumesoma "The Dilemma of a Ghost" na "Anowa"

Image
Leo Ijumaa tumemaliza wiki ya kwanza ya muhula wa kiangazi. Tumesoma tamthilia mbili za Ama Ata Aidoo wa Ghana: The Dilemma of a Ghost na Anowa , ambazo ni miongoni mwa tamthilia maarufu za Afrika. Hata hivi, kama ilivyo kawaida yangu, nimewatahadharisha wanafunzi kuwa dhana ya kumaliza kusoma kazi ya fasihi ni dhana potofu. Haiwezekani kumaliza, kwa maana ya kuielewa kikamilifu hadi kikomo, hata tukiisoma tena na tena Ninapenda kufundisha The Dilemma of a Ghost sio tu kwa kuwa ni kazi nzuri kisanaa, bali pia kwa namna inavyoyaanika masuala ya maisha. Mfano muhimu ni suala la mahusiano baina ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi. Msingi wa mahusiano hayo katika tamthilia hii ni ndoa baina ya kijana aitwaye Ato, kutoka Ghana, na Eulalie, mwanamke m-Marekani Mweusi. Hao wawili wanakutana na kuoana wakiwa Marekani, ambako Ato alikuja kusoma. Eulalie, kama walivyo wa-Marekani Weusi wengi, anafurahi sana kwamba atakwenda Afrika, ambako ni asili ya watu wake. Ana imani kuwa atapokelewa kam

Tamasha la Afrifest: Agosti 1

Image
Tamasha la Afrifest linakaribia. Litafanyika Agosti 1 mjini Brooklyn Park, Minnesota. Tamasha hili, ambalo hufanyika kila mwaka wakati kama huu, ni fursa kwa watu wenye asili ya Afrika kuonyesha mchango wao kihistoria katika nyanja mbali mbali. Kunakuwa na maonesho ya mchango wa watu wenye asili ya Afrika katika historia ya binadamu, kuanzia chimbuko lake Afrika hadi kuenea katika nchi za mbali, kama vile Mashariki ya Kati, Asia, Ulaya, Marekani ya Kaskazini, ya Kati, na ya Kusini. Ni fursa ya kujikumbusha historia ya himaya za kale barani Afrika, utumwa, ukoloni, mapambano dhidi ya ukoloni, juhudi za kuwaunganisha watu wenye asili ya Afrika ulimwenguni ("Pan-Africanism"). Afrifest hukumbushia itikadi na harakati zingine zaidi ya "Pan Africanism," kama vile "Negritude" na "Rastafarianism." Tangu kuanzishwa kwa Afrifest, jukumu la kutoa elimu hii limekuwa juu yangu, na niliandaa kijitabu kiitwacho Africans in the World , ambacho hupatikana

Nawashangaa CCM

Ninawashangaa wanaCCM wanaolalamikia mchakato wa chama chao wa kumpata mgombea urais. Mwaka 2010 CHADEMA walilalamika sana kwamba wamefanyiwa rafu na CCM. Hakuna yeyote katika CCM aliyewasikiliza CHADEMA, wala kuwaonea huruma. CCM wote waliibeza CHADEMA, kwamba ingojee uchaguzi ujao. Sasa leo wanalalamika kuwa wamefanyiwa rafu huko huko CCM. Sio kwamba hao wanachukia rafu. Wanalalamika kwa sababu rafu wamefanyiwa wao. Mimi kama raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa naona kuwa hawana sababu ya kulalamika, kwani wanavuna walichopanda. Labda watajifunza umuhimu wa kutetea haki wakati wote na kwa yeyote.

Kesho Naanza Tena Kufundisha

Hiki ni kipindi cha kiangazi, ambacho kwa ki-Ingereza huitwa "summer." Katika chuo chetu cha St.Olaf, walimu hatuwajibiki kufundisha kipindi hiki, ambacho hudumu karibu miezi minne. Ila kama mwalimu anapenda, anaweza kufundisha. Kozi za kipindi hiki cha kiangazi hudumu wiki yapata tano, lakini kozi inafanana kwa uzito wake sawa na kozi za muhula wa kawaida. Kwa miaka niliyofundisha hapa, mara kwa mara nimefundisha kozi wakati wa kiangazi. Uzuri wake mojawapo ni kuwa wanafunzi huwa wachache, na kwetu tunaofundisha fasihi, ni wakati mzuri wa kujaribisha vitabu vipya. Kozi ambayo nitafundisha kipindi hiki ni fasihi ya Afrika (African Literature).  Nitatumia vitabu kutoka sehemu mbali mbali za Afrika. Kitabu kimojawapo ni Minaret , ambayo ni riwaya ya Leila Aboulela wa Sudan. Nilifundisha riwaya hii muhula uliopita, na iliwavutia wanafunzi na mimi pia. Ingawa ni hadithi ya kubuniwa inatupa picha nzuri ya maisha ya watu wa Khartoum, ambao ni wa-Islam wa tabaka la juu, si wa

Ukiwa na Siri Iweke Kitabuni

Image
Wengi wetu tumesikia kwamba ukiwa na siri iweke kitabuni; mw-Afrika hataiona. Kwetu wa-Tanzania, hali ni hiyo hiyo. Mwaka hadi mwaka, tumekuwa tukisikia jinsi utamaduni wa kusoma vitabu unavyokosekana Tanzania. Si jambo la kujivunia. Nimekuwa nikiandika mara kwa mara hali ninayoiona hapa Marekani, katika matamasha ya vitabu, maduka ya vitabu, na maktaba. Wa-Marekani kama inavyoonekana katika picha nilizoweka hapa, wana tabia tofauti. Picha ya katikati niliipiga katika tamasha la vitabu Minneapolis. Ya chini niliipiga katika tamasha la vitabu Mankato.  Picha ya juu kabisa sikumbuki niliipata wapi. Zote zinaonyesha jinsi watu wanavyosaka vitabu na kuchungulia yaliyomo. Sijui kama kuna siri iliyofichwa kitabuni ambayo hawataigundua. Ninaweza kuleta mfano moja mdogo kutokana na kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , ambamo nimeweka taarifa kuhusu wa-Marekani na wa-Afrika. Tangu kichapishwe, mwaka 2005, maelfu ya wa-Marekani wamekisoma. Wanazijua

Majadiliano na Profesa Joseph Mbele

Image
MAJADILIANO HAYA YAFENYIKA KATI YA MANDELA PALLANGYO. NA PROFESA JOSEPH MBELE WA CHUO KIKUU CHA OLAF CHA MAREKANI. PROFESA JOSEPH MBELE Safari yako ya uandishi ilianza muda mrefu. Je ni kipi kinakutia moyo na kuzidi kufanya kazi hii ngumu? PROF: JOSEPH MBELE Mimi ni mwalimu na ninauona uandishi kama sehemu ya ufundishaji au aina ya ufundishaji. Ndio maana uandishi wangu unaelekea zaidi katika mambo yanayoelimisha. Kazi pekee niliyoitamani hata kabla sijaanza shule ilikuwa ni ualimu. Kwa hivyo, ninapenda kuandika kama ninavyopenda kufundisha darasani. Uliwahi kukutana na maneno mabaya kama kukatishwa tamaa au kukashifiwa wakati ulipokuwa unaanza fani? PROF: JOSEPH MBELE Sikuwahi kukutana na maneno ya aina hiyo tangu mwanzo. Uandishi wangu umekuwa zaidi wa kitaaluma, ambao unatokana na utafiti. Hakuna wakati ambapo uandishi wangu huo umeleta maneno mabaya au ya kukatisha tamaa. Lakini kwa kuwa ninaandika pia magazetini na mitandaoni kuhusu masuala ya kawaida ya maisha, wakati

Mungu (Allah) Hana Ubaguzi

Blogu yangu hii ni uwanja huru kwa fikra na mijadala, ikiwemo mijadala kuhusu dini. Leo, kwa kifupi na lugha rahisi, napenda kuibua suala la dini na ubaguzi. Laiti sisi tunaosema tuna dini tungetambua kuwa Mungu hana ubaguzi. Mungu, ambaye kulingana na tofauti za lugha, huitwa kwa majina mbali mbali, anathibitisha jinsi anavyowapenda wanadamu, wa dini zote, na wasio na dini. Mungu anateremsha baraka zake bila ubaguzi. Anawapa uzazi watu wenye dini, sawa na wasio na dini. Wa-Islam wanazaa, wa-Kristu wanazaa, wa-Hindu wanazaa, na wa dini zingine kadhalika. Wasio na dini wanazaa. Mungu anateremsha mvua kuotesha mbegu katika mashamba ya wa-Islamu, ya wa-Hindu, ya wa-Kristu, na ya wengine, hata wasio na dini. Kuku wa mu-Islam anataga mayai na kuangua vifaranga, sawa na kuku wa m-Kristu, sawa na kuku wa asiye na dini. Mungu hana ubaguzi katika kuteremsha neema zake. Sasa basi, kwa nini wanadamu wengi wanaosema wana dini ni wabaguzi? Kwa nini wanatumia kigezo cha dini kujifanya wao

Leo ni Kumbukumbu ya Kifo cha Hemingway

Image
Leo ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha mwandishi Ernest Hemingway. Alikufa tarehe 2 Julai, mwaka 1961, nyumbani mwake Ketchum, Idaho. Alikufa katika nyumba nayoonekana pichani ambayo ilipigwa na Jimmy Gildea wakati wa safari zake za kuandaa filamu ya Papa's Shadow. Maelezo ya namna Hemingway alivyokufa yanapingana kidogo. Kila mtu anakiri kuwa alikufa kwa risasi ya bunduki. Karibu kila mtu anasema kuwa Hemingway alijiua kwa kujipiga risasi, akiwa peke yake ghorofa ya juu. Lakini mke wake, Mary Welsh Hemingway, ambaye wakati wa tukio alikuwa katika nyumba hiyo kwa chini, alitoa tamko kuwa ilikuwa ni ajali: Mr. Hemingway accidentally killed himself while cleaning a gun this morning at 7:30 A.M. No time has been set for the funeral services, which will be private. Kila ninapowazia kifo cha Hemingway, nakumbuka jinsi alivyokuwa na mikosi ya ajali katika maisha yake. Ninavyowazia kuwa alijiua, nakumbuka misiba kadhaa ya watu kujiua katika ukoo wa Hemingway. Ninawazia pia kuw

Vitabu Nilivyojipatia Wiki Hii

Image
Kama ilivyo kawaida yangu, napenda kuongelea vitabu nimeongeza katika maktaba yangu. Wiki hii, ambayo bado haijaisha, nimejipatia vitabu vinne. Cha kwanza ni Jake Riley: Irreparably Damaged, kilichotungwa na  Rebecca Fjelland Davis. Nilikinunua tarehe 28 mwezi huu, katika tamasha la vitabu, Deep Valley Book Festival, mjini Mankato kutoka kwa mwandishi, ambaye tumefahamiana miaka kadhaa. Kufuatana na maelezo, hii ni hadithi ya kubuniwa. Katika tamasha hilo, nilinunua pia kitabu kiitwacho No Behind , kilichotungwa na Louise Parker Kelly. Tuliongea kidogo, na mwandishi, akaniambia kuwa ni mwalimu na kuwa kitabu chake ni hadithi ya kubuniwa, kuhusu maisha na harakati za mtoto wa shule eneo la Washington D.C. Kitabu kingine ambacho nilikipata jana ni Noontide Toll . Ni mkusanyo wa hadithi fupi za Romesh Gunesekera, mwandishi mahiri sana wa Sri Lanka. Sikumbuki kama nilikinunua kitabu hiki. Huenda wachapishaji wameniletea kwa kuwa nimewahi kuagiza vitabu vingine vya Gunesekera kwa