
Nilielezea katika blogu yangu ya ki-Ingereza nilivyosimulia hadithi katika tamasha la Afrifest, hapa na hapa. Nilisimulia hadithi mbili kutoka katika kitabu cha Matengo Folktales. Mama aliyeniletea mwaliko wa tarehe 14 amenikumbusha kwamba mtoto wake na wengine walioshuhudia hadithi zangu katika Afrifest walivutiwa na wanataka nikasimulie tena.

Hadithi za jadi ni hazina yenye mambo mengi, kama vile falsafa, mafundisho kuhusu saikolojia na tabia za wanadamu, kuhusu mema na mabaya. Ziko zinazosikitisha, zinazofurahisha na kuburudisha, na zinazochemsha bongo, kama zile ziitwazo kwa ki-Ingereza "dilemma tales." Zote ni muhimu katika maisha ya wanadamu, kama nilivyojaribu kuelezea katika kitabu cha Matengo Folktales.