Posts

Showing posts from July, 2016

Ujumbe kwa Rais Magufuli: Shirikiana na UKAWA

Image
Mheshimiwa Rais Magufuli, salaam na pole kwa majukumu ya kutumbua majipu. Mimi ni raia wako, ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Nimeona nikuandikie, ingawa ninajua kuwa jadi ya ovyo iliyojengwa na chama chako cha CCM ni ya kutotambua uwepo wa sisi raia tusio na vyama. CCM imekuwa na historia ya kutotambua kuwa sisi tusio na chama ni raia wenye haki sawa katika nchi yetu, na wenye akili na mitazamo kuhusu mustakabali wa nchi yetu. Achana na hii jadi. Itakuponza. Ninaandika ujumbe huu kukushauri ushirikiane na UKAWA. Nina sababu za kukushauri hivyo. Kwanza, kumbuka kwamba tangu ulipoingia madarakani kama rais, UKAWA walionyesha mapenzi yao kwako kwa dhati, wakadiriki kutangaza mara kwa mara kwamba ulikuwa unatekeleza ajenda yao. Mheshimiwa Rais Magufuli, hakuna hazina kubwa kwa kiongozi kama kukubalika kiasi hiki. Na katika nchi yenye wapinzani, kuweza kuwakonga nyoyo zao kama ulivyofanya ni jambo la pekee. Ni baraka uliyojaliwa. Tafadhali usiifuje. Sisemi ujiunge na

Serikali ya CCM na Mikutano ya Kisiasa

Katika siku hizi chache, tumeshuhudia ubabe wa CCM na serikali ya CCM ambao ni hujuma dhidi ya haki za binadamu. Baada ya UKAWA kutangaza azma yao ya kufanya mikutano na maandamano ya amani nchi nzima (Tanzania) tumesikia kauli za vitisho kutoka kwa CCM na serikali yake. Napenda kusema kuwa ninapinga msimamo wa CCM na serikali ya CCM kuhusu suala hilo kwa sababu ni hujuma dhidi ya haki za binadamu. Katiba ya Tanzania, ya mwaka 1977, 20 (1) imeweka wazi msimamo wake: Every person has the freedom to freely and peaceably assemble, associate and cooperate with other persons, and for that purpose, express views publicly and to form and join with associations or organizations formed for purposes of preserving or furthering his beliefs or interests or any other interests. Tamko hili la katiba ya Tanzania linaendana na tangazo la kimataifa la haki za binadamu ("The Universal Declaration of Human Rights"), vifungu namba 18, 19, 20, na 21. Nashauri kila mtu ajisomee, kwani tang

Tumejadili "Valley Song," Tamthilia ya Athol Fugard

Image
Leo katika darasa langu la African Literature, tumejadili Valley Song , tamthilia ya Athol Fugard, mwanatamthilia maarufu wa Afrika na ulimwenguni. Alizaliwa Afrika Kusini mwaka 1932. Ametunga tamthilia nyingi ambazo kwa ujumla wake ni kama rekodi ya yale ambayo Afrika Kusini imepitia kisiasa, kijamii, na kitamaduni. Kitabu chake cha Notebooks: 1960-1977 ni hazina ya kumbukumbu zake za kukua kwake kama msanii, falsafa yake ya sanaa, na tathmini yake ya wasanii mbali mbali kama vile Samuel Beckett, Bertolt Brecht, na Albert Camus. Nimefundisha tamthilia kadhaa za Fugard, na ninaguswa zaidi na zaidi na kazi zake. Miaka ya karibuni, kwa mfano, nimejikuta ninafundisha Sorrows and Rejoicings tena na tena. Baadaye niliamua kufundisha tamthilia ambayo sikuwahi kuifundisha, nikachagua Valley Song . Valley Song inahusu familia ya Buks, mkulima chotara nchini Afrika Kusini . Anaonekana tangu mwanzo akiwa ameshika mbegu za maboga. Ni mkulima anayefurahia kuona mbegu zinavyoota shamban

CCM: Ni Chama cha Mapinduzi?

Makala ninayoleta hapa niliichapisha mwaka 2008 katika blogu hii. Ninaileta tena hapa ili kuchochea tafakari, hasa kwa wakati huu ambapo mkutano mkuu wa CCM unafanyika Dodoma. ------------------------------------------------------------------------------------------------------------- CCM: Ni Chama cha Mapinduzi? Sielewi kwa nini watu wanaamini kuwa CCM ni chama cha mapinduzi. Sijawahi kuelewa na bado sielewi kwa nini. Dhana ya mapinduzi ilielezwa vizuri na TANU, katika "Azimio la Arusha," "Mwongozo," na maandishi, hotuba na mahojiano mbali mbali ya Mwalimu Nyerere. Matokeo ya yote hayo ni kuwa Watanzania tulifahamu vizuri na kukubali dhana na maana ya mapinduzi katika nchi yetu. Yeyote ambaye hajasoma maandishi hayo, au kusikiliza hotuba hizo, ningemshauri afanye hivyo, ili aweze kufahamu msingi wa ujumbe wangu. CCM ilipoanza, ilijinadi kuwa ni chama cha mapinduzi. Lakini baada ya muda si mrefu, mwelekeo wake ulijionyesha kuwa si wa mapinduzi. Badala ya ku

Ki-Ingereza cha Shakespeare

Image
Miaka mia nne imepita tangu alipofairki Walliam Shakespeare. Lakini dunia haiwezi kumsahau, kwa mchango wake uliotukuka katika utunzi wa tamthilia na mashairi. Leo, ninarejea tena kwenye mada hii ya mchango wa Shakespeare, ambayo nimekuwa nikiiongelea katika blogu hii. Napenda kujikumbusha suala la ki-Ingereza cha Shakespeare. Kumbukumbu hii imenijia leo kwa sababu maalum. Leo, katika kozi yangu ya African Literature, nimeanza kufundisha  The Dilemma of a Ghost , tamthilia ya Ama Ata Aidoo. Nimeongelea mistari nane ya mwanzo ya "Prologue," yaani utangulizi, nikataja mambo mengi, kuanzia "folklore" hadi tamthilia za Shakespeare. Mistari hiyo ni hii: I am the Bird of the Wayside-- The sudden scampering in the undergrowth, Or the trunkless head Of the shadow in the corner. I am the asthmatic old hag Eternally breaking the nuts Whose soup, alas, Nourished a bundle of whitened bones-- Miaka yetu, tulipokuwa tunasoma sekondari,  ambayo kwangu ilikuwa ni

Nimealikwa Maoneshoni Faribault, Minnesota

Jana nilipigiwa simu ambayo sikutegemea. Ilitoka kwa mjumbe wa kamati ya maandalizi ya International Festival Faribault. Hayo ni maonesho ya tamaduni za kimataifa yanayofanyika kila mwaka mjini Faribault, Minnesota. Mtu aliyenipigia simu alikuwa ananiulizia iwapo ninapangia kushiriki maonesho mwaka huu, ili wanitengee meza. Nimewahi kuhudhuria maonesho haya miaka iliyopita, na nimekuwa nikiandika taarifa zake katika blogu hii.  Nimekuwa nikishiriki kama mwandishi na mwalimu, nikiwa na meza ya vitabu vyangu na machapisho mengine. Hapo ninaongea na watu juu ya shughuli zangu za uandishi, ufundishaji, na utoaji ushauri kuhusu tofauti za tamaduni na athari zake katika ulimwengu wa utawandazi wa leo. Kila mara, nimekuwa nikifuata utaratibu wanaofuata washiriki wengine, yaani kupeleka maombi kabla kwa kujaza fomu na kuipeleka, pamoja na malipo. Kutokana na jadi hiyo, niliguswa kupigiwa simu jana. Nilipata hisia kuwa waandaaji wa maonesho wanathamini ushiriki wangu, nami nitakuwa nao b

Hemingway Auneemesha Mji wa Pamplona kwa Utalii

Image
Wiki hii mji wa Pamplona nchini Hispania unafurikwa na maelfu ya watalii kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Ni kwa nini? Ni kwa sababu ya jadi ya tangu karne kadhaa zilizopita ya kusherehekea tamasha liitwalo San Fermin. Sherehe hizi hufanyika kila mwaka wakati huu wa Julai. Kati ya mambo yanayofanyika ni michezo ya kukimbizana na mafahali ("running of the bulls") na michezo ya kupambana na mafahali ("bull-fighting"), kama nilivyogusia katika blogu hii. Ingawa jadi hii iko katika miji mingi nchini Hispania, dunia inafahamu zaidi Pamplona. Hii inatokana na mwandishi maarufu Ernest Hemingway. Baada ya kushuhudia tamasha hili mjini Pamplona kuanzia mwaka 1923, hasa hiyo "running of the bulls" na "bull-fighting," alivutiwa sana, akaielezea kwa ustadi katika riwaya yake ya kwanza The Sun Also Rises. Ingawa ilikuwa ni riwaya yake ya kwanza, The Sun Also Rises ilimjengea Hemingway umaarufu kama mwandishi. Ulimwengu ulivutiwa na bado unavutiwa na

Kumbukumbu na Picha Nilizopiga na Edwin Semzaba

Image
Naleta kumbukumbu na picha za Edwin Semzaba nami, tulizopiga Chuo kikuu Dar es Salaam, mwaka 2010. Tulipiga picha hizi nje ya ofisi yake kwenye majengo ambayo miaka tulipokuwa tunasoma katika chuo hicho, 1973-76, yalikuwa idara ya "Estates." Semzaba tulisoma darasa moja, tangu Mkwawa High School, 1971-72, ambapo tulikuwa katika kikundi cha michezo ya kuigiza. Semzaba alikuwa na kipaji sana cha kuigiza. Kuna picha tulipiga tukiwa wanafunzi wengi, ambao baadhi yao nawakumbuka, kama vile Rajabu Mwajasho, Yusuf Ngororo, Jumbe, Hashim Mvogogo, Edwin Semzaba, Edward Jambo, Mathias Chikawe, na Gondwe. Kimasomo, Mkwawa ilikuwa maarufu. Nusu ya darasa letu tuliingia Chuo Kikuu Dar es Salaam , mwaka 1973. Semzaba na mimi tulisoma "Literature," tukifundishwa na Grant Kamenju, Mofolo Bulane, Gabriel Ruhumbika, William Kamera,  Keorapetse Kgositsile. Kulikuwa pia wahadhiri chipukizi: Ismael Mbise, Clement Ndulute, na Christon Mwakasaka.    Walikuja pia walimu kama Step

Ninasoma " The Sun Also Rises"

Image
Kwa  sasa, katika usomaji wangu wa maandishi ya Ernest Hemingway, ninatumia muda mwingi zaidi katika kusoma The Sun Also Rises . Hii ni baada ya kusoma A Moveable Feast, ambayo niliiongelea katika blogu hii. Ingawa sikuwahi kusoma The Sun Also Rises , nilikuwa nimesoma habari zake. Nilikuwa ninafahmu umaarufu wa riwaya hii na niliwahi kuiongelea katika blogu hii. Nilifahamu, kwa mfano, kwamba riwaya hii inawaongelea wa-Marekani waliokuwa wanaishi Paris na walijulikana kama "the lost generation," yaani kizazi kilichopotea. Katika A Moveable Feast , nilisoma kuwa Gertrude Stein aliwaita hivyo wa-Marekani hao. Nilikuwa ninafahamu pia kuwa The Sun Also Rises ndio riwaya iliyoupa umaarufu mji wa Pamplona wa Hispania, kwa jinsi Hemingway alivyoielezea jadi ya mji huo ya sikukuu ya San Fermin, ambapo kunafanyika mchezo wa kukimbizana na mafahali ("running of the bulls") na mchezo wa kupambana na mafahali ("bull fighting.") Katika "running of th