Kumbukumbu na Picha Nilizopiga na Edwin Semzaba

Naleta kumbukumbu na picha za Edwin Semzaba nami, tulizopiga Chuo kikuu Dar es Salaam, mwaka 2010. Tulipiga picha hizi nje ya ofisi yake kwenye majengo ambayo miaka tulipokuwa tunasoma katika chuo hicho, 1973-76, yalikuwa idara ya "Estates."

Semzaba tulisoma darasa moja, tangu Mkwawa High School, 1971-72, ambapo tulikuwa katika kikundi cha michezo ya kuigiza. Semzaba alikuwa na kipaji sana cha kuigiza. Kuna picha tulipiga tukiwa wanafunzi wengi, ambao baadhi yao nawakumbuka, kama vile Rajabu Mwajasho, Yusuf Ngororo, Jumbe, Hashim Mvogogo, Edwin Semzaba, Edward Jambo, Mathias Chikawe, na Gondwe.

Kimasomo, Mkwawa ilikuwa maarufu. Nusu ya darasa letu tuliingia Chuo Kikuu Dar es Salaam, mwaka 1973. Semzaba na mimi tulisoma "Literature," tukifundishwa na Grant Kamenju, Mofolo Bulane, Gabriel Ruhumbika, William Kamera,  Keorapetse Kgositsile. Kulikuwa pia wahadhiri chipukizi: Ismael Mbise, Clement Ndulute, na Christon Mwakasaka.
  
Walikuja pia walimu kama Stephen Arnold wa Chuo Kikuu cha Alberta, Canada; Stephen Sorkin wa Chuo Kikuu cha Indiana, Marekani; na Phanuel Egejuru. kutoka Nigeria. Pia tulitembelewa na kufundishwa na Stanley Mitchell wa Uingereza, Alex La Guma, mwandishi maarufu wa Afrika Kusini aliyekuwa anaishi u-Ingereza, na George Lamming, mwandishi maarufu wa Barbados aliyekuwa anaishi u-Ingereza.

Tukiwa wanafunzi wa mwaka wa pili, tulisoma riwaya ya Lamming, In the Castle of my Skin katika kozi aliyotufundisha Grant Kamenju. Wakati Lamming alipokuwa anatufundisha kuhusu uandishi wa Caribbean, ninakumbuka kuwa nilifanya mahojiano naye, nikishirikiana na Semzaba, na mahojiano haya yalichapishwa katika gazeti la "Sunday News," kama sikosei.

Nakumbuka tulipiga picha ya darasa zima, tukiwa na George Lamming na mwalimu wetu Grant Kamenju. Tulikuwa sisi wanafunzi wa mwaka wa pili na wengine wa mwaka wa tatu. Baadhi ya hao wa mwaka wa tatu walikuwa wa-Tanzania, kama vile Mugyabuso Mulokozi na wa-Kenya kama vile Alice Bulogosi. Bahati mbaya sijui nakala yangu ya picha ile iko wapi.

Pamoja na "Literature," Semzaba alisomea "Theatre Arts," akifundishwa na Bob Leshoai, Ebrahim Hussein, Louis Mbughuni, Penina Mhando, Godwin Kaduma, na Amandina Lihamba. Mimi sikusomea "Theatre Arts," bali ki-Ingereza, nikifundishwa na waalimu kama Pauline Robinson, Trevor Hill, na Derek Nurse.

Katika somo la "Literature," tulikuwa tunapenda sana kunukuu misemo maarufu na ile ya kuchekesha iliyokuwemo katika riwaya kama The Ragged Trousered Philanthropists ya Robert Tressell, na tamthilia kama Purple Dust ya Sean O'Casey. Semzaba alikuwa anapenda sana jambo hilo.

Maongezi na Semzaba daima yalikuwa ya kuburudisha roho na akili, kwani alikuwa na kipaji cha kuongea, kuchekesha, na kucheka. Kicheko chake kilisababisha wengine mcheke. Hata kama mtu ulikuwa na wingu mawazoni, kama ulikutana na Semzaba, ilikuwa lazima uburudike na kufurahi. Mungu alimjalia haiba hiyo.

Tulihitimu shahada ya kwanza mwaka 1976, tukaajiriwa kufundisha pale pale Chuo Kikuu, Semzaba akiwa idara ya "Theatre Arts" na mimi idara ya "Literature." Kwa bahati mbaya, muda mfupi tu baada ya kuajiriwa, Semzaba alianza kuugua akiwa na matatizo ya miguu. Ilibidi aende nyumbani kuuguzwa kwa miezi mingi.

Familia yake walikuwa wanaishi Dar es Salaam, katika jengo mojawapo la ghorofa pembeni mwa barabara ya Morogoro, linalotazamana na kituo cha zimamoto. Nilikwenda hapo kumjulia hali, nikafahamiana vizuri na mdogo wake ambaye jina lake nimesahau.

Nimeona niandike kumbukumbu hizi chache za rafiki yangu Edwin Semzaba. Baada ya mimi kuja kufundisha Chuo cha St. Olaf huku Marekani, nilipata fursa ya kumleta Semzaba huko Pacific Lutheran University katika programu ya LCCT mwaka 1999. Alikuwa rafiki yangu tangu ujana wetu hadi mwisho wa maisha yake.

Nilipokuwa ninakwenda Tanzania na kufika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nilikuwa ninampitia Semzaba. Alikuwa ananielezea habari za uandishi wake na hali ya vitabu, uchapishaji, na kadhalika nchini Tanzania. Siku tulipopiga picha hizi, kwenye mwezi Julai au Agosti, 2010, alinielezea tuzo alizopata, na ndiyo siku aliponipa nakala ya kitabu chake, Marimba ya Majaliwa, kama nilivyoandika katika blogu hii. Ninaonekana nimeshika kitabu hicho katika picha hapa kushoto.

Comments

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini