Wednesday, July 27, 2016

Tumejadili "Valley Song," Tamthilia ya Athol Fugard

Leo katika darasa langu la African Literature, tumejadili Valley Song, tamthilia ya Athol Fugard, mwanatamthilia maarufu wa Afrika na ulimwenguni. Alizaliwa Afrika Kusini mwaka 1932. Ametunga tamthilia nyingi ambazo kwa ujumla wake ni kama rekodi ya yale ambayo Afrika Kusini imepitia kisiasa, kijamii, na kitamaduni. Kitabu chake cha Notebooks: 1960-1977 ni hazina ya kumbukumbu zake za kukua kwake kama msanii, falsafa yake ya sanaa, na tathmini yake ya wasanii mbali mbali kama vile Samuel Beckett, Bertolt Brecht, na Albert Camus.

Nimefundisha tamthilia kadhaa za Fugard, na ninaguswa zaidi na zaidi na kazi zake. Miaka ya karibuni, kwa mfano, nimejikuta ninafundisha Sorrows and Rejoicings tena na tena. Baadaye niliamua kufundisha tamthilia ambayo sikuwahi kuifundisha, nikachagua Valley Song.

Valley Song inahusu familia ya Buks, mkulima chotara nchini Afrika Kusini . Anaonekana tangu mwanzo akiwa ameshika mbegu za maboga. Ni mkulima anayefurahia kuona mbegu zinavyoota shambani, kustawi na kuzaa mazao. Lakini, anakabiliana na matatizo kadhaa. Kwa mfano, binti yake alitorokea mjini, ambako alifariki katika mazingira ya kutatanisha, akiwa ameacha mtoto mchanga aitwaye Veronika.

Ana wasi wasi kwamba atapoteza shamba na nyumba yake kutokana na kishawishi cha wazungu wenye fedha wanaofika fika kuangalia shamba na nyumba hiyo.  Juu ya yote, Veronika, ambaye sasa ni msichana mkubwa, anasema tena na tena kuwa anataka kwenda mjini akawe mwimbaji maarufu. Hapendi kuendelea kuishi shamba ambapo anaona hakuna fursa kama mjini.

Ndoto hii ya Veronika inamsumbua Buks, kwani anawazia jinsi binti yake alivyotorekea mjini na kufariki huko.  Hata hivyo, baada ya kumsikiliza sana Veronika, anamwacha aende. Dhamira ya jinsi mbegu za maboga zinavyoota na kustawi na kuzaa maboga makubwa makubwa inahusishwa na ndoto ya Veronika ya kukuza kipaji chake cha uimbaji na kisha kuwa na mafanikio makubwa.

Valley Song inaishia kwa matumaini ya namna hiyo, ambalo ni jambo jema lenye kugusa mioyo yetu. Tamthilia hii, ingawa fupi, ni uthibitisho mwingine wa kipaji cha Fugard kama msanii mwenye ufahamu wa kina wa uhalisia wa maisha, majaribu yake na uwezo wa binadamu wa kupambana nayo.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...