Sunday, July 3, 2016

Ninasoma " The Sun Also Rises"

Kwa  sasa, katika usomaji wangu wa maandishi ya Ernest Hemingway, ninatumia muda mwingi zaidi katika kusoma The Sun Also Rises. Hii ni baada ya kusoma A Moveable Feast, ambayo niliiongelea katika blogu hii.

Ingawa sikuwahi kusoma The Sun Also Rises, nilikuwa nimesoma habari zake. Nilikuwa ninafahmu umaarufu wa riwaya hii na niliwahi kuiongelea katika blogu hii. Nilifahamu, kwa mfano, kwamba riwaya hii inawaongelea wa-Marekani waliokuwa wanaishi Paris na walijulikana kama "the lost generation," yaani kizazi kilichopotea. Katika A Moveable Feast, nilisoma kuwa Gertrude Stein aliwaita hivyo wa-Marekani hao.

Nilikuwa ninafahamu pia kuwa The Sun Also Rises ndio riwaya iliyoupa umaarufu mji wa Pamplona wa Hispania, kwa jinsi Hemingway alivyoielezea jadi ya mji huo ya sikukuu ya San Fermin, ambapo kunafanyika mchezo wa kukimbizana na mafahali ("running of the bulls") na mchezo wa kupambana na mafahali ("bull fighting.") Katika "running of the bulls," mafahali huachiwa katika mtaa mwembamba mjini kuwafukuza watu waliojazana humo, ambao hutimka mbio, huku mafahali wakiwafukuza na kuwashambulia. Watu wengi huumizwa na baadhi kubaki mahututi na mara moja moja hata kufa. Ni mchezo unaopendwa sana.

Katika mchezo wa kupambana na mafahali, wanaume waitwao "matador" hutokea uwanjani kwa utaratibu maalum, na kukabiliana na fahali kwa mbinu mbali mbali kama inavyoeleza hapa. Taratibu na sheria za mchezo huu zimekuwa zikibadilika na kutofautiana katika vipindi mbali mbali vya historia na sehemu mbali mbali za dunia. Hutokea fahali anafanikiwa kumjeruhi "matador," pengine vibaya sana. Hemingway aliipenda sana michezo hii ya hatari, kwani alithamini na kusifia ushujaa.

Sasa ni fursa yangu kujisomea mwenyewe The Sun Also Rises, riwaya ambayo imeufanya mji wa Pamplona kuwa maarufu wenye kuvutia idadi kubwa ya watalii. Tayari nimeona jinsi Hemingway anavyoelezea mji wa Paris na maisha ya watu miaka ile ya elfu moja mia tisa na ishirini na kitu. Maelezo yake yananikumbusha A Moveable Feast. Nimekuta pia sehemu katika The Sun Also Rises ambapo mhusika mkuu anamwambia mwenzake kuhusu Afrika. 

Kutokana na jinsi ninavyofuatilia uhusiano wa Hemingway na Afrika, nimefurahi kukutana na taarifa hii katika The Sun Also Rises. Wakati alipoandika riwaya hii, Hemingway alikuwa bado hajasafiria Afrika, bali alikuwa anafahamu habari zake kutokana na kusoma vitabu kama Batouala cha Rene Maran na maandishi ya rais wa Marekani mstaafu Teddy Roosevelt ambaye, mwaka 1909, alikuwa amefanya safari ya miezi mingi ya uwindaji nchini Kenya.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...