Posts

Showing posts from September, 2010

Programu za Kupeleka Wanafunzi Tanzania

Image
Leo hapa chuoni St. Olaf tulikuwa na shughuli ya kuzitangaza programu za masomo ambamo chuo kinapeleka wanafunzi wake. Tunafanya hivyo mara moja kwa mwaka. Walimu washauri wa programu tunakuwepo na taarifa mbali mbali za programu tunazohusika nazo, na wanafunzi wanakuja kupata taarifa hizo, na pia kujiandikisha iwapo wana nia ya kujiunga na programu hizo. Vyuo vingi hapa Marekani vina programu za aina hiyo, na vyuo kadhaa vinapeleka wanafunzi Tanzania. Hii inatokana na kufahamu faida wanayopata wanafunzi kwa kwenda kuishi na kujifunza katika nchi zingine. Inapanua akili na upeo. Kuishi miongoni mwa watu wa utamaduni tofauti kunampa kijana fursa ya kukomaa kwa namna mbali mbali na kuwa tayari kwa maisha ya zama zetu za utandawazi wa leo. Programu hizi zinachangia maelewano mema duniani. Pamoja kazi yangu ya kufundisha katika idara ya ki-Ingereza hapa St. Olaf , ninashughulika katika program zinazopeleka wanafunzi nchi za ki-Afrika, ikiwemo Tanzania. Nimefanya shughuli hii kwa mia

Ujumbe Kuhusu Vitabu

Image
Leo nilienda mji wa Duluth kwa matembezi ya masaa machache nikiwa na mwalimu mwenzangu katika idara yetu. Baada ya kuzunguka na gari sehemu kadhaa za mji huo, niliegesha gari kwenye mtaa uitwao Superior Street, unaoonekana katika picha hizi mbili, tukaanza kutembea katika mtaa huu, kuangalia mazingira. Hatukwenda mbali, tukaona duka la vitabu na moja kwa moja tukaingia humo. Humo ndani kulikuwa na vitabu vingi sana na vitu vingine vidogo vidogo vya nyumbani, kama vile sahani, glasi, mishumaa, na maua ya mapambo. Nilipoingia tu, kwenye meza moja karibu na mlango niliona ujumbe uliowekwa kwenye fremu, kuhusu vitabu. Nilivutiwa sana na ujumbe ulioandikwa na Clarence Day, Jr. Nilimwuliza mama mhudumu humo dukani kama naweza kupiga picha. Alisema kwa uchangamfu kuwa ni sawa kabisa. Jioni hii, wakati naandika habari hii kwenye blogu, nimetafuta taarifa nikagundua kuwa Clarence Day, Jr. aliandika ujumbe wake mwaka 1920. Kwa jinsi nilivyoupenda, nimeona niuweke hapa na nijaribu kuuta

Nimeipata Nakala ya "Tendehogo."

Image
Nilipokuwa Tanzania mwaka huu, nilikutana na rafiki yangu, mwandishi Edwin Semzaba, kama nilivyoandika hapa . Jambo moja tuliloongelea ni kutafsiri tamthilia yake ya Tendehogo . Basi, niliporejea hapa chuoni St. Olaf ninapofundisha, nilienda maktaba na kuagiza nakala ya tamthilia hii. Kwa vile nakala haiko hapa, waliniagizia kutoka Maktaba ya Congress iliyoko Washington DC. Nimeshapata nakala hiyo, na sasa inabidi nianze mikakati ya kuitafsiri. Kazi ya kutafsiri kazi ya fasihi ni ngumu, yenye changamoto nyingi, hata kama mtu unazijua lugha husika vizuri sana. Hata kama lugha husika ni zako za kuzaliwa nazo au za tangu utotoni, kama kilivyo ki-Matengo na ki-Swahili kwa upande wangu. Ninasema hivyo kutokana na uzoefu. Nimejishughulisha na kutafsiri tungo za ki-Swahili na hadithi za ki-Matengo kwenda ki-Kiingereza. Niliwahi hata kuandika makala kuhusu kutafsiri hadithi ya ki-Matengo. Soma hapa . Miaka michache iliyopita nilianza kutafsiri Tendehogo , lakini nakumbuka nilitafsiri kur

Kiboko ya Wachawi

Image
Nilipokuwa Tanzania mwaka huu, nilipata wazo la kupiga picha za matangazo mbali mbali ya waganga wa kienyeji, ambayo ni mengi kwenye miji kama Dar es Salaam. Matangazo hayo yanahusu uponyaji wa magonjwa na matatizo mengine ya afya, mafanikio ya biashara na maisha, kuwavuta wapenzi, na kadhalika. Tangazo hili la "Kiboko ya Wachawi" nililiona Kibamba, kandokando ya barabara itokayo Dar es Salaam kwenda Morogoro, tarehe 28 Julai. Nilipita hapo na walimu wengine watatu kutoka Marekani, kutembelea shule ya sekondari ya Shulua ambayo iko maeneo hayo.

Kwa Nini Ninablogu

Jana niliandika makala, lakini nadhani nilikosea wakati wa kuichapisha, maana naona imeenda bila kichwa. Nimeona kwenye blogu za wengine hakuna kichwa, bali jina la blogu tu. Kwa hivi nimeona nilete taarifa kuwa makala ilikuwa na kichwa, "Kwa nini ninablogu." Soma hapa .

Kwa Nini Ninablogu

Image
Wiki kadhaa zilizopita, wanablogu watatu tulikutana Sinza, Dar es Salaam, tukaongea kuhuau masuala mbali mbali. Kati ya mambo mengi, tuliondoka na suali: kwa nini tunablogu? Bofya hapa . Baada ya kulitafakari suali hili kiasi, napenda kuelezea kidogo kwa nini ninablogu. Kwanza, nakumbuka kuwa nilianza kublogu baada ya kuhamasishwa na ndugu Freddy Macha na Jeff Msangi, mmiliki wa Bongo Celebrity . Hao wawili walifahamu kuhusu maandishi yangu, wakanishawishi nianzishe blogu. Nami nilifuata ushauri wao. Nilianzisha blogu mbili: ya ki-Swahili , na ya ki-Ingereza . Nilijifunza na naendelea kujifunza huku nikiblogu. Katika harakati hiyo, Dada Subi, mmiliki wa Wavuti amekuwa akinisaidia, kama anavyowasaidia wanablogu wengine. Kwangu mimi blogu ni ukumbi wa kuelezea mawazo, hisia, fikra na mambo yangu mengine, na hivi kuyahifadhi na kuwashirikisha wengine. Siblogu kwa imani kuwa nina ujuzi au busara kuliko watu wengine. Blogu ni baraza inayonikutanisha na wengine kwa mazungumzo, mijadala

Nimekutana na Mwandishi Edwin Semzaba

Image
Katika mizunguko yangu Tanzania mwaka huu, nilitembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mara kadhaa, kwa shughuli rasmi na pia shughuli binafsi. Kwa vile nilisoma na kufundisha hapo, daima ninakutana na watu wengi tuliosoma au kufundisha pamoja au niliowafundisha ambao baadhi yao ni walimu pale. Kwa mfano, soma hapa na hapa . Mmoja wa wale niliokutana nao mwaka huu ni Edwin Semzaba, mwandishi maarufu wa tamthilia na riwaya na ni mwigizaji hodari. Anaandika kwa ki-Swahili. Tamthilia zake, kama vile Ngoswe , zinafahamika Tanzania nzima na nje. Baadhi ya riwaya zake, ambazo ninazo, ni Tausi Wa Alfajiri (Heko Publishers Limited, 1996), na Funke Bugebuge (Dar es Salaam University Press, 1999). Semzaba ni rafiki yangu wa siku nyingi. Tulisoma darasa moja, kuanzia Mkwawa High School, Iringa, 1971-72, hadi Chuo Kikuu Dar es Salaam, 1973-76. Mwaka huu, aliposikia kuwa niko nchini, Semzaba alinipa nakala mpya ya Ngoswe , iliyochapishwa na Nyambari Nyangwine Publishers, 2008.

Upatikanaji wa Vitabu Vyangu

Kutokana na maulizo ya wadau, napenda kutangaza kuwa vitabu vyangu vinapatikana Tanzania, sehemu zifuatazo: Arusha (Kimahama Literature Center) 0786242222 Dar es Salaam (Sinza) 0754 888 647 0717 413 073 Bagamoyo 0754445956 Karatu (Bougainvillea Lodge) 0754576783 Longido (Cultural Tourism Program) 0787855185 Mto wa Mbu (Cultural Tourism Program) 0786373099 Walioko ughaibuni wanaweza kuvipata sehemu hizi: Duka la mtandaoni, Bofya hapa St. Olaf College Bookstore, Fax 507 786 3779, simu 1-888-232-6523 Africonexion (info@africonexion.com, simu 507 403 9756)

Watoto wa Tanzania Wanapenda Vitabu

Image
Wengi wetu tunalalamika kuhusu kufifia au kutoweka kwa utamaduni wa kununua na kusoma vitabu miongoni mwa wa-Tanzania. Inaonekana kuwa hata pale ambapo vitabu vipo, kama vile maktaba, wa-Tanzania hawaendi kusoma. Ukweli ni kuwa tabia hii inajengeka na umri. Watoto wa Tanzania, wanapenda vitabu, sawa na watoto wengine popote. Nimeshuhudia hayo katika pita pita zangu Tanzania. Kwa mfano, ukienda kwenye maonesho ya vitabu Tanzania, utawaona watoto. Mwanzoni mwa Septemba, 2004, kulikuwa na maonesho ya vitabu katika uwanja wa hifadhi ya kumbukumbu za Taifa, Dar es Salaam. Kama kawaida, waliohudhuria zaidi ni watoto. Katika maonesho hayo, watoto wa shule walifanya michezo ya kuigiza, kuhusu umuhimu wa vitabu. Waliimba pia nyimbo, wakiwahamasisha wazazi kuweka vitabu nyumbani na kuwa na utaratibu wa kusoma pamoja na watoto. Lakini, ujumbe wao uliishia hewani, kwani wazazi wenyewe hawakuwepo. Wakati wa kuigiza mchezo, watoto hao walishika vitabu, kama vilelelezo. Nilimwona mtoto mmoja am

Mh. Balozi Peter Kallaghe Afutarisha UK

Haya ndio mambo yanayotakiwa Tanzania. Nimevutiwa na kila kitu katika video hii, kuanzia ule wimbo mtamu wa kuienzi nchi yetu na utambulisho wetu kama wa-Tanzania, hadi mshikamano baina ya wa-Tanzania, na nasaha murua zilizotolewa na wasemaji. Mungu Ibariki Tanzania.

Aliyosema Marando Jangwani

Nimeiona video hii katika blogu ya Kulikoni Ughaibuni , nikaona niiweke hapa kwangu. Natanguliza shukrani kwa ndugu Chahali, kwa kuchangia suala la kupeana habari na kuelimishana. Ni haki ya msingi. Bofya hapa

Nimepiga Picha Nyingi Tanzania

Kila mwaka, ninapokuwa Tanzania, napiga picha nyingi niwezavyo na kuja nazo huku Marekani. Mwaka huu nimepiga picha nyingi sehemu nilizopata fursa ya kuzitembelea: Arusha, Dar es Salaam, Lushoto, Morogoro, Moshi, na Tanga. Watu ambao wameishi Tanzania tu wanaweza kuuliza kwa nini napiga picha hata sehemu ambazo si za pekee au muhimu. Siwezi kuwalaumu. Huku ughaibuni mambo ni tofauti, na napenda nitoe fununu kidogo. Mbali na kufundisha hapa katika chuo cha St. Olaf , ninashughulika na programu zinazopeleka wanafunzi Tanzania na sehemu zingine za Afrika. Kazi yangu ni kuwaandaa hao wanafunzi, kwa kuwaeleza mambo ya utamaduni, maisha, elimu, na kadhalika yahusuyo nchi hizo wanakokwenda. Picha zangu hizi ni hazina inayonisaidia katika shughuli hizi. Mbali ya kuwaelimisha, zinawahamasisha katika kupenda kuja Tanzania na Afrika kwa ujumla. Wiki iliiyopita, niliporejea hapa chuoni kutoka Tanzania, mkuu wa idara yangu ya ki-Ingereza aliomba nitundike picha za Tanzania kwenye ubao wetu wa m