Showing posts with label Kiswahili. Show all posts
Showing posts with label Kiswahili. Show all posts

Saturday, April 2, 2011

Kitabu Kumhusu Hemingway

Leo nilipita tena katika duka la vitabu la Half Price Books la mjini Apple Valley. Kama kawaida, kutokana na ushabiki wangu wa maandishi ya Ernest Hemingway, nilianza kwa kwenda moja kwa moja kwenye sehemu vinapouzwa vitabu vyake: vile alivyoandika yeye mwenyewe au vilivyoandikwa juu yake.

Hadi sasa nina vitabu vingi vya Hemingway, lakini kila ninapoona kitabu kipya, au ambacho sina, napenda niwe nacho. Leo nimevikuta vitabu kadhaa vya aina hiyo, ila nilivutiwa zaidi ni Hemingway in Cuba, kilichoandikwa na Norberto Fuentes.

Sikuwa nimekiona kitabu hiki kabla. Nilikiangalia, nikaona kina utangulizi ulioandikwa na Gabriel Garcia Marquez. Hapo niliishiwa nguvu, kwani Marquez ni mmoja wa waandishi maarufu kabisa duniani.

Mawazo mengine yakafurika akilini mwangu. Ninajua kuwa Marquez ni rafiki mkubwa wa Fidel Castro, Castro ambaye watu wa kizazi changu tumemwenzi tangu tulipopata Uhuru. Najua pia kuwa Castro ni mshabiki wa maandishi ya Marquez. Cha zaidi ni kuwa najua kuwa Hemingway katika uhai wake alifahamiana na Castro, na pia kuwa Castro amekuwa shabiki wa Hemingway tangu miaka ile.

Pamoja na yote hayo, katika kusoma utangulizi wa Marquez, nimevutiwa kwa namna ya pekee na maelezo yake kuwa Hemingway ni mwandishi ambaye Castro anamsoma kuliko mwandishi mwingine yeyote. Hata anapozunguka nchini kwenye safari rasmi, Castro anakuwa na maandishi ya Hemingway. Marquez anatueleza kuwa Castro anaweza kuelezea maandishi ya Hemingway na kujibu masuali kwa uhodari wa kiwango cha juu.

Mimi kama shabiki mkubwa wa Hemingway najiandaa kukisoma kitabu hiki. Nimekipitia juu juu, nikaona kina mengi mapya kwangu, ingawa kilichapishwa mwaka 1984. Nina vitabu vingine vinavyoelezea maisha ya Hemingway Cuba, lakini hiki cha Fuentes kinazama zaidi katika maelezo yake.

Kwa wale ambao hawajui, Hemingway, ambaye ni m-Marekani aliyezaliwa mwaka 1899 karibu na Chicago, aliishi Cuba miaka 22. Hata alivyosafiri kuja Afrika Mashariki, mwaka 1933 na mwaka 1953, alitokea Cuba, na baada ya safari zake alirejea Cuba. Kuna vitu kadhaa alivyovipata Kenya na Tanganyika, kama vile vichwa vya wanyama aliowawinda, mikuki, na kinyago cha ki-Makonde. Vyote viko katika nyumba yake ya Finca Vigia, ambayo iko nje ya mji wa Havana, ambayo serikali ya Cuba inaihifadhi kwa heshima kubwa na vitu vyote vya Hemingway vilivyokuwamo humo, ingawa yeye alishaondoka na kurejea Marekani, ambako alijiua kwa bunduki mwaka 1961.

Cuba inamwenzi Hemingway kwa namna ambayo ingepaswa sisi wa-Tanzania tuwe tunawaenzi waandishi wetu kama vile Mgeni bin Faqihi wa Bagamoyo, aliyetunga Utendi wa Rasi l'Ghuli, au Shaaban Robert.

Thursday, September 16, 2010

Kwa Nini Ninablogu

Wiki kadhaa zilizopita, wanablogu watatu tulikutana Sinza, Dar es Salaam, tukaongea kuhuau masuala mbali mbali. Kati ya mambo mengi, tuliondoka na suali: kwa nini tunablogu? Bofya hapa. Baada ya kulitafakari suali hili kiasi, napenda kuelezea kidogo kwa nini ninablogu.

Kwanza, nakumbuka kuwa nilianza kublogu baada ya kuhamasishwa na ndugu Freddy Macha na Jeff Msangi, mmiliki wa Bongo Celebrity. Hao wawili walifahamu kuhusu maandishi yangu, wakanishawishi nianzishe blogu. Nami nilifuata ushauri wao.

Nilianzisha blogu mbili: ya ki-Swahili, na ya ki-Ingereza. Nilijifunza na naendelea kujifunza huku nikiblogu. Katika harakati hiyo, Dada Subi, mmiliki wa Wavuti amekuwa akinisaidia, kama anavyowasaidia wanablogu wengine.

Kwangu mimi blogu ni ukumbi wa kuelezea mawazo, hisia, fikra na mambo yangu mengine, na hivi kuyahifadhi na kuwashirikisha wengine. Siblogu kwa imani kuwa nina ujuzi au busara kuliko watu wengine. Blogu ni baraza inayonikutanisha na wengine kwa mazungumzo, mijadala na kubadilishana mawazo.

Vile vile, ninablogu kwa sababu nimeona umuhimu wa blogu kwa upande wa lugha. Ninavyoandika ki-Swahili najiongezea uzoefu wa kutumia lugha hiyo ipasavyo. Hiyo ndio jitihada yangu, na hili ndilo lengo langu.

Mazoezi ni mazoezi. Tunapofanya mazoezi ya viungo daima, tunajijengea afya bora, na tunaanza kuusikia mwili ukikaa sawa. Kwa namna hiyo hiyo, kuandika kwa ki-Swahili kumenifanya niisikie akili yangu ikizidi kukaa sawa, kwa upande huu wa matumizi ya lugha. Nazidi kujiamini katika utumiaji wa lugha hii.

Katika blogu yangu ya ki-Ingereza, naandika kwa lengo la kuonyesha uandishi bora wa ki-Ingereza. Ni lugha ambayo nimeipenda tangu nilipoanza kujifunza, darasa la tatu, na naifundisha hapa katika Chuo cha St. Olaf, Minnesota.

Kublogu kumeniunganisha na watu wengi ambao wanasoma blogu zangu, kutoka pande zote za dunia. Inaleta faraja, kwa mfano, ninapotambua kuwa kitu fulani nilichoandika katika blogu kimekuwa ni msaada kwa mtu fulani. Kwa mfano, miezi kadhaa iliyopita, nilipata ujumbe kutoka kwa mama mmoja aliyeko Ujerumani.

Aliulizia namna ya kufika Mbamba Bay na mahali pa kulala akishafika kule, kwani alikuwa anapangia kuja Tanzania. Alisema kuwa aliniuliza kwa vile alisoma habari za Mbamba Bay kwenye blogu yangu. Nilimpa maelezo aliyohitaji. Wakati huu wote yeye alikuwa Ujerumani na mimi nilikuwa Marekani. Alikuja Tanzania mwaka huu na familia yake, wakati nami niko nchini. Tulionana Ubungo, kwenye kituo cha mabasi, kama inavyoonekana katika picha hii, wakiwa wamefurahi kununua nakala ya Matengo Folktales.

Sunday, September 12, 2010

Nimekutana na Mwandishi Edwin Semzaba

Katika mizunguko yangu Tanzania mwaka huu, nilitembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mara kadhaa, kwa shughuli rasmi na pia shughuli binafsi. Kwa vile nilisoma na kufundisha hapo, daima ninakutana na watu wengi tuliosoma au kufundisha pamoja au niliowafundisha ambao baadhi yao ni walimu pale. Kwa mfano, soma hapa na hapa.

Mmoja wa wale niliokutana nao mwaka huu ni Edwin Semzaba, mwandishi maarufu wa tamthilia na riwaya na ni mwigizaji hodari. Anaandika kwa ki-Swahili. Tamthilia zake, kama vile Ngoswe, zinafahamika Tanzania nzima na nje.













Baadhi ya riwaya zake, ambazo ninazo, ni Tausi Wa Alfajiri (Heko Publishers Limited, 1996), na Funke Bugebuge (Dar es Salaam University Press, 1999).

Semzaba ni rafiki yangu wa siku nyingi. Tulisoma darasa moja, kuanzia Mkwawa High School, Iringa, 1971-72, hadi Chuo Kikuu Dar es Salaam, 1973-76. Mwaka huu, aliposikia kuwa niko nchini, Semzaba alinipa nakala mpya ya Ngoswe, iliyochapishwa na Nyambari Nyangwine Publishers, 2008.




Nilikuwa na nakala ya Ngoswe tangu zamani, toleo lililochapishwa na Education Services Centre Ltd, 1988. Vile Vile, miaka kadhaa iliyopita, Semzaba alinipa nakala ya video ya tamthilia hii.








Mwaka huu alinipa pia nakala ya riwaya yake mpya, Marimba ya Majaliwa. Sikujua kuwa alikuwa ameandika riwaya hii. Alinieleza kwamba ni riwaya aliyoshinda kwenye shindano la hadithi za kusisimua, mwaka 2007. Shindano hili lilifadhiliwa na SIDA na kusimamiwa na Mradi wa Vitabu vya Watoto, Tanzania.



Nilifurahi kusikia hivyo, kwani nafahamu alivyo makini na kazi yake, na jinsi alivyochangia fasihi na sanaa Tanzania na duniani kwa miaka mingi. Nafurahi kuwa mchango wake unatambuliwa kwa namna hiyo.

Kwa miaka kadhaa nimewazia kutafsiri baadhi ya maandishi ya Semzaba. Nilianza kutafsiri Mkokoteni, ila sikumaliza. Lakini katika kuongea na Semzaba mwaka huu, ilionekana kuwa tafsiri ya Tendehogo inahitajika mapema zaidi. Kazi hizi, na za waandishi wengine wa nchi yetu, inafaa zitafsiriwe, kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Friday, May 21, 2010

Mteja wa Pili wa CHANGAMOTO

Kitabu cha Changamoto kimepata mteja wa pili leo, hapo mtandaoni kinapochapishwa. Amenunua nakala tano.

Kwanza ninamshukuru mteja huyu kwa imani yake juu ya kitabu hiki, kama nilivyomshukuru mteja wa kwanza. Jambo la pili ni kuwa nafurahi kuona kuwa habari za kitabu hiki zinaenea. Hii ni ndoto na mategemeo ya kila mwandishi. Kwa upande wangu, nangojea kwa hamu mijadala itakayotokana na changamoto niliyotoa katika masuala mbali mbali ya jamii ya Tanzania na dunia ya leo.

Nikizingatia imani ya wateja, namalizia kwa kuahidi kuwa nitaendelea kujibidisha katika kuifahamu zaidi lugha hii ya ki-Swahili, ili niweze kuitumia kwa ufasaha zaidi na kuandika maandishi bora zaidi. Hii ndio shukrani yangu kwao.

Wednesday, March 3, 2010

Mfinyanzi Aingia Kasri: Siti Binti Saad

Mwaka jana, nilipokuwa Dar es Salaam, niliingia katika duka la vitabu, Dar es Salaam Bookshop, nikanunua vitabu kadhaa vya ki-Swahili. Vitatu vilikuwa vya Shaaban Robert, na kingine ambacho sikuwa nimewahi kusikia habari zake, kilikuwa juu ya Siti Binti Saad.
Kitabu hiki Mfinyanzi Aingia Kasri: Siti Binti Saad Malkia wa Taarab, kimeandikwa na Nasra Mohamed Hilal wa Malindi, Zanzibar, ambaye alikuwa mtangazaji wa Radio Tanzania Zanzibar kwa miaka 27. Kimechapishwa na Mkuki na Nyota Publishers, 2007.

Kwa mujibu wa taarifa iliyo ukurasa wa nyuma ya kitabu, Bibi Nasra "(a)mefanya utafiti wa historia ya wanawake wa makabila mbali mbali walioishi mjini Zanzibar na kuacha nyayo zao juu ya mila, utamaduni na sanaa. Hivi sasa anakamilisha vitabu vingine viwili. Zaidi ya uandishi Bibi Nasra ni mtengenezaji wa filamu wa kujitegemea na amekwishatoa filamu tano fupi, zote katika Kiswahili."

Natoa pongezi na shukrani kwa juhudi za mama huyu. Kitabu chake hiki kinathibitisha juhudi yake katika utafiti, kwani amekusanya habari na kumbukumbu nyingi kutoka kwa watu mbali mbali waliomfahamu Siti Binti Saad, wakiwemo ndugu zake.

Amekusanya nyimbo mbali mbali za Siti Binti Saad, nyingine zikiwa mpya kwetu ambao ufahamu wetu wa Siti Binti Saad unatokana na maandishi. Tuna bahati ya kuzipata taarifa na nyimbo nyingi namna hii katika kitabu kimoja.

Kuna mengi ya kujifunza kutokana na maisha na tungo za Siti Binti Saad, ambaye alipambana na matatizo mengi katika maisha yake, lakini akawa shujaa mwenye kujiamini muda wote. Alituachia mafundisho mengi murua. Kwa mfano, katika wimbo wake moja alisema

Ukicha kutajwa
Hutotenda jambo....

Alimaanisha kuwa kama unaogopa maneno ya watu, hutafanya kitu cha maana maishani.

Kama tunavyofahamu, msingi wa utafiti juu ya Siti Binti Saad uliwekwa na Shaaban Robert, katika kitabu chake cha Wasifu wa Siti Binti Saad. Katika kufuatilia habari za Shaaban Robert, nimeshangazwa na vipaji vyake. Kwa mfano, ingawa hakuwa na elimu kubwa ya shuleni, ikiwemo elimu ya utafiti wa masuala ya aina hii, Shaaban Robert alifanya kazi nzuri, akizingatia maadili ambayo leo tunafundisha vyuoni. Bibi Nasra ameutaja vizuri mchango wa Shaaban Robert na amemtolea sifa na shukrani ipasavyo.

Nategemea kupata wasaa wa kukichambua kitabu hiki cha Mfinyanzi Aingia Kasri siku zijazo na kuelezea maoni yangu vizuri. Kwa leo nimeona nikitaje tu, ili walimwengu wapate kufahamu uwepo wake.


















Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...