Kwa Nini Ninablogu

Wiki kadhaa zilizopita, wanablogu watatu tulikutana Sinza, Dar es Salaam, tukaongea kuhuau masuala mbali mbali. Kati ya mambo mengi, tuliondoka na suali: kwa nini tunablogu? Bofya hapa. Baada ya kulitafakari suali hili kiasi, napenda kuelezea kidogo kwa nini ninablogu.

Kwanza, nakumbuka kuwa nilianza kublogu baada ya kuhamasishwa na ndugu Freddy Macha na Jeff Msangi, mmiliki wa Bongo Celebrity. Hao wawili walifahamu kuhusu maandishi yangu, wakanishawishi nianzishe blogu. Nami nilifuata ushauri wao.

Nilianzisha blogu mbili: ya ki-Swahili, na ya ki-Ingereza. Nilijifunza na naendelea kujifunza huku nikiblogu. Katika harakati hiyo, Dada Subi, mmiliki wa Wavuti amekuwa akinisaidia, kama anavyowasaidia wanablogu wengine.

Kwangu mimi blogu ni ukumbi wa kuelezea mawazo, hisia, fikra na mambo yangu mengine, na hivi kuyahifadhi na kuwashirikisha wengine. Siblogu kwa imani kuwa nina ujuzi au busara kuliko watu wengine. Blogu ni baraza inayonikutanisha na wengine kwa mazungumzo, mijadala na kubadilishana mawazo.

Vile vile, ninablogu kwa sababu nimeona umuhimu wa blogu kwa upande wa lugha. Ninavyoandika ki-Swahili najiongezea uzoefu wa kutumia lugha hiyo ipasavyo. Hiyo ndio jitihada yangu, na hili ndilo lengo langu.

Mazoezi ni mazoezi. Tunapofanya mazoezi ya viungo daima, tunajijengea afya bora, na tunaanza kuusikia mwili ukikaa sawa. Kwa namna hiyo hiyo, kuandika kwa ki-Swahili kumenifanya niisikie akili yangu ikizidi kukaa sawa, kwa upande huu wa matumizi ya lugha. Nazidi kujiamini katika utumiaji wa lugha hii.

Katika blogu yangu ya ki-Ingereza, naandika kwa lengo la kuonyesha uandishi bora wa ki-Ingereza. Ni lugha ambayo nimeipenda tangu nilipoanza kujifunza, darasa la tatu, na naifundisha hapa katika Chuo cha St. Olaf, Minnesota.

Kublogu kumeniunganisha na watu wengi ambao wanasoma blogu zangu, kutoka pande zote za dunia. Inaleta faraja, kwa mfano, ninapotambua kuwa kitu fulani nilichoandika katika blogu kimekuwa ni msaada kwa mtu fulani. Kwa mfano, miezi kadhaa iliyopita, nilipata ujumbe kutoka kwa mama mmoja aliyeko Ujerumani.

Aliulizia namna ya kufika Mbamba Bay na mahali pa kulala akishafika kule, kwani alikuwa anapangia kuja Tanzania. Alisema kuwa aliniuliza kwa vile alisoma habari za Mbamba Bay kwenye blogu yangu. Nilimpa maelezo aliyohitaji. Wakati huu wote yeye alikuwa Ujerumani na mimi nilikuwa Marekani. Alikuja Tanzania mwaka huu na familia yake, wakati nami niko nchini. Tulionana Ubungo, kwenye kituo cha mabasi, kama inavyoonekana katika picha hii, wakiwa wamefurahi kununua nakala ya Matengo Folktales.

Comments

Fadhy Mtanga said…
kublog kunaleta experience ya aina yake.
nami nilihamasika baada ya kusoma sana makala za Ndesanjo Macha kwenye gazeti la Mwananchi Jumapili.

leo najivunia kublog kwani kumeweza kunikutanisha na watu na kunifanya kujifunza vitu vingi sana.
Kwa kweli ni uzoefu mzuri na wa aina yake tuupatao kwa ajili ya kublog. Kwanza kama alivyosema mtani hapo juu kunakutanisha watu na mengi ambayo hukutegemea uyajifunza unajifunza humu kweny hizi blog.

Pili hizi blog za kiswahili zinakuza lugha ya kiswahili.
'''''''''Siblogu kwa imani kuwa nina ujuzi au busara kuliko watu wengine'''''''

hivi ikigundulika kuwa wewe una busara kuliko watu wengi na ikagundulika pia kuwa una busara kuliko bloggers wote na hilo likagundulika kupitia kwenye mitundiko yako ya kwenye blogu, si utajikuta ukiblogu kwa kuwa una busara kuliko wote?? na utajivunia hilo?
Mbele said…
Kamala umenichekesha sana kwa masuali yako ambayo pia ni mtihani wa kufikirisha.

Sasa nitakuwa makini kufuatilia wanayosema wasomaji. Bila ufuatiliaji huwezi ukajua, bwana. Huenda wanaona mimi ni mzee wa busara kweli :-)
Mbele said…
Dada Yasinta, kwa kuongezea hapa kwenye suala la kuitangaza lugha ya ki-Swahili, sisi wanablogu tuna fursa nzuri ya kuitangaza nchi yetu. Tuko wanablogu wengi na tunawafikia watu wengi sana.

Angalia, kwa mfano kazi kubwa anayofanya shangazi yetu mumyhery ya kuitangaza Tanzania na utamaduni wake, wakati blogu ni yake binafsi, wala si kitengo cha serikali au wizara husika kule nyumbani.
Subi Nukta said…
Nimevutiwa kusoma na kufahamu sababu yako ya kublogu na kuendelea kufanya hivyo. Tafadhali usiache, mimi nadhani na wengine hapa, tunajifunza mengi toka kwako Mwalimu.

Nadhani pia una-blogu kwa kuwa unacho cha kuandika na kuifunza jamii kutokana na maisha yako ya kila siku na yale unayokumbana nayo, aidha kwa kukupendeza ama kutokukupendeza, mathalan, nadhani unapendezwa sana uonapo watu wananunua vitabu na kuvisoma lakini hupendezwi uonapo watu wananunua bia na kufanya starehe za gharama ambazo haziisaidii jamii zaidi tu ya kuingiza pato la fedha ambayo wengine huiita 'malipo haramu'.

Nakuunga mkono kwa kazi zako Prof. Mbele!
SN said…
Blogging ni darasa la aina yake na nakubaliana na Prof kuwa utagundua ujuzi wako wa uandishi ukikua kila baada ya muda fulani.

Mimi dukuduku langu ni kwa wasomaji ambao hupenda kusoma tu kitu fulani na kuondoka. Sio lazima kila mtu akiona kila post aache maoni. La hasha. Ila ni jukwaa la "kubadilishana" mawazo. Kwa mfano, mwandishi anazungumzia mambo kadhaa kwa kifupi kwenye makala fulani, basi kwanini watu husita kuongezea au kuacha ujuzi wao kwenye sehemu ambazo (labda) wana ujuzi zaidi; au ile kunyambua tu mambo...

Mimi - binafsi - hapo ndipo naona labda Watanzania hatutumii hii tasnia ipasavyo au kikamilifu?
Nimekuwa na MFULULIZO wa matundiko kuhusu BLOGU KUWA SHULE ambapo tunafunza tukifunzwa. Na nakumbuka wazo hili lilinijia kutokana na mawazo yako (YAREJEE HAPA)
Hakuna utani wala masihara juu ya NGUVU ZA KU-BLOGU
Kuna mengi mema tunayojifunza na naamini nitakapoenda nyumbani nitafurahia zaidi hili kwani nitakutana na WAPENDWA wengi wambao WANANOA AKILI YANGU kwa mawazo, maoni na hata maswali katika maandishi yangu
Sio tu NAWAHESHIMU NA KUWAPENDA, lakini pia NAJIVUNIA KWA UALIMU WAO.
Nawe umekuwa mwangalifu wa kile unachoandika ambavyo mara nyingi ni kile kiifaacho jamii hata kama hakina mkumbo.
Na huu ni ujasiri mkuu.
Ndio namna ambavyo TUTASALIA NA BLOGU MAKINI na kuachana na zile zilizo na maradhi ya mkumbo. Kama nilivyowahi kusema hapa kuwa Blogu zetu na Maradhi ya Bongo flava

BARAKA KWAKO PROFESA
Mbele said…
Mzee wa Changamoto, umefanya jambo jema sana kuturejesha kwenye makala za zamani. Nimefuatilia ulivyoelekeza nikaona kumbe wanablogu tulibadilishana mawazo murua sana na ya kufikirisha, wakati wa kujadili mada husika.

Tukaze buti, kama wanavyosema mitaani. Labda kidogo kidogo tutafanikiwa kuziengua hizi blogu za upupu na udaku ;-)
Musagasa said…
Blog yako ya kiingereza inaitwaje nadhani itakuwa kwangu darasa bora la lugha hi ya kigeni.
Mbele said…
Ndugu Musagasa, asante kwa ulizo lako. Blogu inaitwa Mbele

Makala ninazoandika kule kuhusu "literature" zinasomwa sana na watu sehemu mbali mbali duniani.
Nina imani utaifurahia, na kufaidika nayo.

Popular posts from this blog

Tenzi Tatu za Kale

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Filamu ya "Papa's Shadow:" Fursa ya Kuitangaza Tanzania