Tuesday, September 7, 2010

Watoto wa Tanzania Wanapenda Vitabu

Wengi wetu tunalalamika kuhusu kufifia au kutoweka kwa utamaduni wa kununua na kusoma vitabu miongoni mwa wa-Tanzania. Inaonekana kuwa hata pale ambapo vitabu vipo, kama vile maktaba, wa-Tanzania hawaendi kusoma.

Ukweli ni kuwa tabia hii inajengeka na umri. Watoto wa Tanzania, wanapenda vitabu, sawa na watoto wengine popote. Nimeshuhudia hayo katika pita pita zangu Tanzania. Kwa mfano, ukienda kwenye maonesho ya vitabu Tanzania, utawaona watoto.

Mwanzoni mwa Septemba, 2004, kulikuwa na maonesho ya vitabu katika uwanja wa hifadhi ya kumbukumbu za Taifa, Dar es Salaam. Kama kawaida, waliohudhuria zaidi ni watoto.

Katika maonesho hayo, watoto wa shule walifanya michezo ya kuigiza, kuhusu umuhimu wa vitabu.
Waliimba pia nyimbo, wakiwahamasisha wazazi kuweka vitabu nyumbani na kuwa na utaratibu wa kusoma pamoja na watoto. Lakini, ujumbe wao uliishia hewani, kwani wazazi wenyewe hawakuwepo.

Wakati wa kuigiza mchezo, watoto hao walishika vitabu, kama vilelelezo. Nilimwona mtoto mmoja ameshika kijitabu changu kuhusu Things Fall Apart. Anaonekana hapa juu, wa pili kutoka kulia. Niliguswa na jambo hilo.

Mwaka huu, tarehe 24-25 Juni nilishiriki maonesho ya elimu na ajira, ambayo yaliandaliwa na Tripod Media. Yalifanyika Diamond Jubilee Hall, Dar es Salaam.
Nililipia banda, nikaweka vitabu vyangu na machapisho mengine, nikawa naongea na watu kwa siku zote mbili.

Walifika watoto wengi, na hapo nilijionea mwenyewe jinsi watoto walivyo na ari ya vitabu. Walikuwa wanaviangalia na waliniuliza masuali kem kem.
Nami nilitumia fursa hii kuwaelezea umuhimu wa kusoma na kutafuta elimu kwa dhati muda wote.Nilipata faraja kubwa katika kuwa na watoto hao na kuona moyo wao juu ya vitabu.Suali la msingi linabaki: Tufanyeje ili watoto waweze kukua na moyo huu walio nao bila kulegea au kufifia? Kuna njia gani ya kuwafanya watu wazima wahudhurie maonesho ya vitabu?

Katika jarida la Tanzania Schools Collection, toleo la kwanza, Moris Mwavizo anaripoti, ukurasa 12, kuwa katika maonesho fulani ya vitabu Dar es Salaam, mratibu mmoja alimwona mtoto akizunguka mwenyewe katika viwanja. Alipomwuliza kwa nini baba yake hakuja naye, mtoto alijibu kuwa baba yake angekuja kama kungekuwa na bia hapa kwenye maonesho. Je, hii si aibu?

7 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Hakika, wakati nasoma habari hii nimepatwa na hisia ambayo ni vigumu kuielezea. Binafsi nilipata bahati kuwa na vitabu ndani ya nyumba labda kwa vile babangu alikuwa mwl. Nasikitika sana wazazi wenzangu ambao wanasema hwataki kkwenda kwenye jambo kama hili mpaka ziwe bia. Na kama ulivyosema kwenda Maktaba na kutulia pale si gharama kkabisa na hata kama ni gharama si itakupa faida. Lakini utakuta wazazi wanasema we ndenda kuchunga mbu´zi au nenda kuokota kuni msituni. Watoto wana haki kama hii na ni sisi wazazi ndio wa kuwahamasisha. Katika hizo taswira hapo juu unaona kabisa jinsi watoto wanavtyoonyesha hamu ya vitabu. Pro. Mbele ni kazi nzuri sana unaifanya na inabidi tukuunge mkono kwa hali na mali.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

ni kweli hii

Mbele said...

Naamini hili ni suala muhimu lakini lenye utata pia. Watoto wengine wanasoma katika shule zenye vitabu na vifaa na walimu wa kutosha na wanatoka kwenye familia zenye mazingira muafaka, yaani wazazi wenye mwamko na uwezo, na kadhalika.

Lakini watoto wengine wanakabiliwa na tatizo hili la kuwa na wazazi wasio na mwamko au uwezo. Moyo wa watoto hao wa kupenda kusoma haupati changamoto.

Watoto wengine wanaishi mazingira magumu, katika nyumba ya kupanga ambamo watu wengi wamesongamana, kila mtu na tabia yake, na kusoma inakuwa shida, au pembeni ya nyumba kuna baa ambamo walevi wanapiga kelele usiku na mchana, na inakuwa vigumu watoto kulala usingizi itakiwavyo.

emuthree said...

Unajua kila kitu huanzia kwa wazazi, hebu jaribu kudadisi watoto wengi kwamba kwanini yeye anapenda kuwa dakitari au kufanya jambo fulani, ni lazima atakuambia kwasababu baba au mama niliwaona wakifnaya hivyo.
Kama sis wazazi tutajenga tabia ya kupenda vitabu na watoto wetu watapenda pia. Hebu tujiulize tunapojenga nyumba zetu kwanini hatufirii kuweka chumba maalumu cha library, humo utaweka vitabu vya kila aina na hapo ndipo unapoweza hata kujua kipaji cha mtoto wako, anapendelea vitabu vya aiana gani nk

Unknown said...

Profesa Je uliwauliza hao watoto wantoka katika familia za namna kwenye suala la kipato?. Nategemea maonyesho ya vitabu yalipofanyika siyo eneo la kisimaguru-Madenko, Mvomero ambao hawana barabara, umeme, huduma ya maji wala zahanati. Lugha inayotumika kwa mawasiliano ya kienyeji na siyo kiswahili. Kuna Mwalimu mmmoja tuu wa shule ya msingi tena yeye huwa anafika hapo mara kwa mwezi na pengine asifike kabisa...Matukio haya ndiyo ya kawaida kabisa.

Mbele said...

Ndugu Ildiko, sikuwauliza hili suali lako, kwamba wanatoka familia zenye kipato gani.

Kuhusu vijiji vya Kisimaguru-Madenko na Mvomero ambako hakuna barabara au umeme, naweza kubahatisha tu na kusema kuwa ukipeleka vitabu kule, watoto watavichangamkia. Naamini hivyo.

Lakini cha muhimu ni vitendo. Mimi nilikulia kule milimani Umatengo (Ruvuma) bila umeme. Tulikuwa tunasomea koroboi.

Miaka hii ya karibuni nimeazimia kuanzisha kijimaktaba pale kijijini pangu, hata kama ni kabati moja tu. Nina imani kuwa watoto wataingia humo kusoma.

Lakini kama nilivyogusia hapa juu, hili suala la vijijini si suala la kinadharia. Bora nikaweke hiyo maktaba, halafu nitaweza kuleta taarifa.

Na wewe ningekushauri kuwazia hivyo hivyo. Badala ya kuongelea ukosefu wa umeme, barabara, na zahanati kule Kisimaguru-Madenko na Mvomero, jaribu kufanya mkakati wa kuanzisha kijimaktaba. Halafu tutaangalia matokeo.

Pro Dr Ing Rev Academia Temuu said...

Maktaba ni Muhimu Kuliko kitu chochote

Msomaji na Mpiga Debe Wangu Aikwaa Tuzo

Jana niliandika taarifa za msomaji na mpiga debe wangu Joy Zenz, mKenya aishiye uJerumani. Napenda niseme kuwa juhudi zake za kuwaunganisha ...