Nimekutana na Mwandishi Edwin Semzaba

Katika mizunguko yangu Tanzania mwaka huu, nilitembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mara kadhaa, kwa shughuli rasmi na pia shughuli binafsi. Kwa vile nilisoma na kufundisha hapo, daima ninakutana na watu wengi tuliosoma au kufundisha pamoja au niliowafundisha ambao baadhi yao ni walimu pale. Kwa mfano, soma hapa na hapa.

Mmoja wa wale niliokutana nao mwaka huu ni Edwin Semzaba, mwandishi maarufu wa tamthilia na riwaya na ni mwigizaji hodari. Anaandika kwa ki-Swahili. Tamthilia zake, kama vile Ngoswe, zinafahamika Tanzania nzima na nje.

Baadhi ya riwaya zake, ambazo ninazo, ni Tausi Wa Alfajiri (Heko Publishers Limited, 1996), na Funke Bugebuge (Dar es Salaam University Press, 1999).

Semzaba ni rafiki yangu wa siku nyingi. Tulisoma darasa moja, kuanzia Mkwawa High School, Iringa, 1971-72, hadi Chuo Kikuu Dar es Salaam, 1973-76. Mwaka huu, aliposikia kuwa niko nchini, Semzaba alinipa nakala mpya ya Ngoswe, iliyochapishwa na Nyambari Nyangwine Publishers, 2008.
Nilikuwa na nakala ya Ngoswe tangu zamani, toleo lililochapishwa na Education Services Centre Ltd, 1988. Vile Vile, miaka kadhaa iliyopita, Semzaba alinipa nakala ya video ya tamthilia hii.
Mwaka huu alinipa pia nakala ya riwaya yake mpya, Marimba ya Majaliwa. Sikujua kuwa alikuwa ameandika riwaya hii. Alinieleza kwamba ni riwaya aliyoshinda kwenye shindano la hadithi za kusisimua, mwaka 2007. Shindano hili lilifadhiliwa na SIDA na kusimamiwa na Mradi wa Vitabu vya Watoto, Tanzania.Nilifurahi kusikia hivyo, kwani nafahamu alivyo makini na kazi yake, na jinsi alivyochangia fasihi na sanaa Tanzania na duniani kwa miaka mingi. Nafurahi kuwa mchango wake unatambuliwa kwa namna hiyo.

Kwa miaka kadhaa nimewazia kutafsiri baadhi ya maandishi ya Semzaba. Nilianza kutafsiri Mkokoteni, ila sikumaliza. Lakini katika kuongea na Semzaba mwaka huu, ilionekana kuwa tafsiri ya Tendehogo inahitajika mapema zaidi. Kazi hizi, na za waandishi wengine wa nchi yetu, inafaa zitafsiriwe, kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Comments

MARKUS MPANGALA said…
Nimebahatika kusoma kazi zake, na kwa kweli fasihi imenichonga sana kichwa changu, pamoja na falsafa za wastani.

Kwa kweli ni utamu kazi zake. Bahati mbaya pale nimesoma sayansi ya siasa.
Ila utamu tuu
Mbele said…
Tulipokuwa Mkwawa High School, tuliona jinsi Semzaba alivyo na kipaji cha uigizaji na utunzi wa tamthilia. Alifahamika sana mjini Iringa.

Nilizunguka naye mitaani siku moja, tukawaona akina mama wameketi mahali. Kule kumwona Semzaba tu, wakapiga kelele za msisimko, "Yule paleee!" Hata mwaka huu nilimkumbusha Semzaba tukio lile, tukawa tunacheka tu.
Simon Kitururu said…
Naheshimu sana kazi za huyu Mheshimiwa. Na asante kwa picha nimefurahi kumuona anavyoonekana siku hizi. Ukiniuliza bila kusita ntasema Mzee huyu ni hazina ya Taifa ambayo kuna baadhi ya Watanzania kutokana na tabia ya kutopenda kujisomea bado hawajaistukia.:-(
Ndiyo. Vitabu vya Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi vinatakiwa kutafsiriwa katika lugha kuu za kimataifa kwa faida ya walimwengu wote. Hii itasaidia sana katika kuieneza fasihi ya Kiswahili na utamaduni wa Mtanzania. Nafurahi kwamba umeamua kutafsiri vitabu vya E. Semzaba.
Mbele said…
Ndugu Kitururu, nafurahi kuwa umefurahi kuona Semzaba alivyo siku hizi. Kumbe kuweka picha namna hii kunaweza kuwagusa watu kwa namna mbali mbali. Nashukuru kwa hilo.

Mwalimu Matondo, ni kweli tunahitaji kutafsiri kazi za waandishi wetu maarufu. Ninapokumbuka tungo za mabingwa wa zamani kama vile Mgeni bin Faqihi, aliyetunga "Utendi wa Rasi 'lGhuli," au watunzi wa miaka iliyofuata, kama vile Shaaban Robert, Mathias Mnyampala na Amri Abedi, au Ebrahim Hussein, Haji Gora Haji, na Euphrase Kezilahabi, naafiki kabisa usemi wako.

Profesa Clement Ndulute aliyatafsiri baadhi ya mashairi ya Shaaban Robert kwa ki-Ingereza, na kitabu chake, "The Poetry of Shaaban Robert," kilichapishwa na Dar es Salaam University Press, 1994. Lakini hii ni sehemu ndogo sana ya tungo za Shaaban Robert.

Kwa hivi, tunakubaliana kuwa tuna kazi kubwa mbele yetu. Lakini tuna matatizo makubwa. Tatizo moja ni hili alilolitaja Kitururu, la watu kutopenda kusoma. Kwa maana hiyo, watu hata hawayajui haya maandishi ambayo tungepaswa kuyatafsiri.

Tatizo jingine ni lugha. Wa-Tanzania ni wavivu sana katika suala la lugha. Hakuna lugha wanayoimudu vizuri, iwe ni ki-Swahili, ki-Ingereza, au lugha nyingine. Ni shida tupu na ubabaishaji.
John Mwaipopo said…
edwin ni mwalimu mzuri pia. alinifundisha topic ya tamthilia kule fine and performing arts. hufundisha mtu aelewe kuliko afaulu tu. pia siku moja jioni aliigiza 'mkokoteni'.

pia alituambia kisa cha yeye kutunga 'ngoswe'. ni kisa kinachofanana na kisa cha ukweli kilichotokea huko kigoma alikokwenda kusimamia sensa. anakumbuka kushawishiwa na mzee mmoja kuwa ni vema mambo waliyokuwa wakiyaona wayaweke katika kumbukumbu za maandishi. ndipo kikazaliwa 'ngoswe'
Mbele said…
Ndugu Mwaipopo, shukrani kwa nyongeza yako. Wanavyosema kuwa blogu ni shule ni kweli. Hapo tayari tunaona jinsi hazina ya kumbukumbu inavyoongezeka.
Edina George said…
Asante kwa blog yako,nimefurahi kupata habari ya mwandishi wetu mkongwe,pia wazo lako la kutasfiri baadhi ya kazi mimi nilalibariki sababu utasaidia hata mataifa mwengine kuweza kutambua kazi za waandishi wetu,lulu yetu kutambulika zaidi mbali na mipaka yetu,pia nina tafiti nafanya ya chuo kikuu,tafadhali nahitaji mawasiliano yake au namna ya kumpata nguli huyu.
Mbele said…
Dada Edina George, shukrani kwa ujumbe wako. Jana nilimwandikia ujumbe rafiki yangu Edwin Semzaba, kule Facebook, kumwomba aniletee anwani yake. Lakini sijui anaangalia mtandao huu mara ngapi.

Hata hivi, najua anafanya kazi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na pamoja na mengine, anafundisha katika idara ya "Fine and Performing Arts."
Mbele said…
Jana tulipata habari kuwa Edwin Semzaba amefariki hiyo jana. Mungu amweke mahala pema Peponi na awafariji ndugu na jamaa. Kwa upande wangu, ninawazia kufuatilia suala la kutafsiri nililoongelea hapa juu. Vitabu ninavyo. Vingine nilisainiwa na kupewa na Semzaba mwenyewe, na picha za vitabu nilizoambatanisha na hiyo makala yangu nilipiga mwenyewe. Miaka ya nyuma zaidi Semzaba alinipa pia kaseti ya video ya "Ngoswe." Alinipa mamlaka kamili ya kufanya chochote nitakachoona kinafaa kuitangaza. Mungu akipenda, nitaelekeza akili yangu kwenye masuala hayo.
Ushairi said…
Ni kweli, Semzaba ametutoka na bado unaomboleza. Jumatatu 15 Februari 2016 TATAKI inafanya Kumbukizi ya Semzaba, Chiduo, Kihore na Katikiro - wote walimu waliotutoka siku za karibuni. Mimi nitaongea kuhusu Semzaba, maana nilimfahamu fika na tulikuwa wote Mkwawa na Chuo Kikuu Dsm, pamoja na UWAVITA na jumuiya nyinginezo. Mnakaribishwa. Shughuli itafanyika ukumbi wa nkrumah kuanzia saa 3 asubuhi hadi 7 mchana.

M.M. Mulokozi
Mbele said…
Profesa Mulokozi,

Asante kwa taarifa. Makala yangu hii juu ya Semzaba inatembelewa sana hapa kwenye blogu yangu. Kwa hivi, ninafahamu kuwa ujumbe wako utawafikia wengi. Mnafanya jambo jema kuwakumbuka hao wenzetu, nasi tulioko mbali tutakuwa nanyi mioyoni na mawazoni.

Popular posts from this blog

Tenzi Tatu za Kale

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Filamu ya "Papa's Shadow:" Fursa ya Kuitangaza Tanzania