Posts

Showing posts from December, 2015

Nimekutana na Mdau wa Miaka Mingi

Image
Leo nimekutana na mdau wangu wa miaka mingi, Dr. Barbara Poole Galyen, ambaye anaishi California. Kwa siku chache hizi za Krismasi na Mwaka Mpya, yuko hapa Minnesota kwa ndugu zake. Kwa kupitia facebook tuliwasiliana na leo nilikwenda mjini Lakeville alikofikia. Dr. Galyen na mimi tulifahamiana mwaka 1995, wakati nilipokuwa natafiti masimulizi ya jadi na tamaduni mkoani Mwanza. Utafiti huo ambao nilifanya tangu mwaka 1993 hadi 1996 uligharamiwa na shirika la Earthwatch. Dr. Galyen alikuwa mmoja wa watu kutoka nchi mbali mbali waliokuwa wanakuja Tanzania kushiriki utafiti wangu. Yeye alikuja wakati wa utafiti kisiwani Ukerewe. Kwa kauli yake mwenyewe, huu ulikuwa mwanzo na msingi wa yeye kuipenda Afrika, hadi akaenda kufanya kazi Kenya katika United States International University, ambapo nilimtembelea mwaka 1997. Hatimaye alianzisha kampuni ya ushauri kuhusu masuala tamaduni ulimwenguni. Shughuli hizi, ambazo zinafanana na zangu, zimempa fursa ya kuzunguka sehemu mbali mbali za

Kitabu Juu ya Charles Dickens

Image
Siku chache zilizopita, niliingia katika gereji yangu ambayo imefurika vitabu. Katika kufukua fukua, nilikiona kitabu Dickens , kilichotungwa na Peter Ackroyd. Sikumbuki nilikinunua lini na wapi, ila niliamua kukichukua, kwa lengo la kukipitia angalau juu juu. Nina vitabu kadhaa vilivyotungwa na Dickens. Baadhi nimevisoma na baadhi sijavisoma. Dickens ni kati ya waandishi ambao watu wa rika langu tuliwasoma miaka ya ujana wetu Tanzania, tukawapenda sana. Kutokana na mvuto huu, nimeandika juu ya Dickens mara kadhaa katika blogu hii. Mifano ni hapa, na hapa. Kwa hivyo, nilivyokigundua kitabu cha Dickens katika gereji,  nilifurahi, nikakichukua hima. Nilikuwa nafahamu jina la mwandishi Peter Ackroyd, ingawa sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu chake chochote. Katika kupitia taarifa kwenye jalada la kitabu chake cha Dickens,  nimeona orodha ya vitabu alivyoandika na umaarufu wake. Kwa mfano, amejijengea heshima kubwa kwa kuandika vitabu vya historia na wasifu wa waandishi kama

Jólabókaflóð: Mafuriko ya Vitabu Nchini Iceland

Image
Nchi ya Iceland inaongoza ulimwenguni kwa usomaji wa vitabu, na pia kwa asilimia ya watu wanaochapisha vitabu. Hilo linatosha kuipambanua nchi ile. Lakini kuna pia jadi iitwayo Jólabókaflóð , yaani mafuriko ya vitabu, ambayo hutokea majira ya Krismasi. Kila mwaka, kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba, pilika pilika zinazohusiana na vitabu zinapamba moto. Wachapishaji wa vitabu wanaongeza juhudi ya kutangaza vitabu, na jamii nzima huwa katika heka heka ya kununua vitabu. Mazungumzo na malumbano kuhusu vitabu hushamiri kila mahali. Mwezi Novemba, katalogi kubwa ya vitabu iitwayo  bókatíðindi  inachapishwa na kugawiwa bure karibu kila nyumba. Katalogi hii huorodhesha vitabu karibu vyote vilivyochapishwa katika mwaka husika. Kadiri Krismasi inavyokaribia, shughuli ya kuzawadiana vitabu inapamba moto. Kilele huwa ni tarehe 24 Desemba, ambayo ni mkesha wa Krismasi. Watu hutumia mkesha wa Krismasi wakisoma vitabu. Taarifa hizo sikuwa ninazifahamu, hadi leo. Sikujua kuwa utamaduni wa Ic

Ninajivunia Binti Huyu: Bukola Oriola

Image
Nimefurahi kupata taarifa kuwa Rais Obama amemteua Bukola Oriola, kuwa mjumbe katika tume ya kumshauri kuhusu masuala ya usafirishwaji wa ghilba na utumikishwaji wa binadamu, kama ilivyotangazwa katika taarifa hii. Bukola ni binti kutoka Nigeria anayeishi hapa Minnesota, Marekani. Nimemfahamu tangu mwaka 2009, kwa kusoma taarifa zake katika magazeti ya wa-Afrika hapa Minnesota. Niliguswa kwa namna ya pekee niliposoma kauli yake kuwa alikuwa ameandika mswada wa kitabu bali hakujua auchapishe vipi. Kwa kuwa nilikuwa na uzoefu wa kujichapishia vitabu, dhamiri yangu ilinisukuma niwasiliane naye ili nimsaidie. Nilielezea kisa hicho katika blogu hii. Baada ya kitabu chake, Imprisoned: The Travails of a Trafficked Victim kuchapishwa, niliendelea kumhamasisha. Kwa mfano, nilimwalika kwenye tamasha la vitabu mjini Minneapolis tarehe 10 Oktoba, 2009, ambalo nilikuwa nashiriki. Nilitaka yeye kama mwandishi chipukizi aone na kujifunza kazi inayomngoja mwandishi baada ya kuchapisha kitabu

Kuchapisha Vitabu Mtandaoni

Image
Kutokana na taarifa ninazoandika katika blogu hii,  na sehemu zingine, watu wengi wanafahamu kuwa nimechapisha vitabu vyangu mtandaoni.  Nimeshawasaidia waandishi kadhaa wa mataifa mbali mbali kuchapisha vitabu vyao kwa mtindo huo. Kwa upande wa Tanzania, niliwahi kuongea na wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu suala hilo, na nilinukuliwa katika gazeti la Mwananchi . Mara kwa mara, watu huniulizia kuhusu kuchapisha vitabu vyao. Napenda kuongelea tena suala hili, hasa matokeo ya kuchapisha vitabu mtandaoni. Kwanza, ni muhimu kufahamu kwamba kuna njia nyingi za kuchapisha vitabu mtandaoni. Ni juu ya mwandishi kuchagua. Binafsi, ninatumia njia ambayo ni rahisi kabisa, isiyo na gharama, au yenye gharama ndogo kiasi kwamba haiwi kizuizi kwangu. Kuchapisha kwa namna hii ni rahisi sana. Mbali ya kutokuwa na gharama, haichukui muda, ili mradi mswada umeshaandaliwa kama faili la kielektroniki. Kinachobaki ni kuuingiza mswada kwenye tovuti ya kuchapishia, na haichukui dakika

Mdau Kanishukuru kwa Kutafsiri "Kimbunga"

Image
Ninavyoandika katika blogu hii na blogu ya ki-Ingereza huwa sina namna ya kujua ni nani atasoma nilichoandika. Siwezi hata kujua kama niandikacho kitasomwa na yeyote. Ni kubahatisha. Kwa kutambua hilo, nimediriki kusema kwamba ninapoandika katika blogu, ninajiandikia mwenyewe. Hata hivi, ukweli unajitokeza kuwa kuna watu wanaosoma niandikayo. Katika blogu kuna sehemu ambapo ninafuatilia na kuona takwimu za utembeleaji wa blogu na orodha ya makala zinazosomwa au kupitiwa siku hadi siku. Nimefurahi kusoma leo ujumbe wa mdau akinishukuru kwa tafsiri yangu ya "Kimbunga," shairi la Haji Gora Haji. Ameandika: Thank you so much for translating this poem. I'd been searching to read poems originally written in Swahili. Immense gratitude Joseph. Nimefurahi kuwa nimempa mdau huyu angalau tone la kutuliza kiu yake kuhusu mashairi ya ki-Swahili. Amenipa motisha ya kuendelea kutafsiri tungo za ki-Swahili, ili afaidike zaidi kwa kutambua utajiri wa jadi ya tungo za ki-Swahili

Nimeitafsiri Sala ya Papa Francis

Image
Nilielezea katika blogu hii nia yangu ya kuitafsiri sala ya Papa Francis ambayo ni sehemu ya waraka wake wa kitume, "Laudato Si." Papo hapo, ninafahamu vizuri kuwa kutafsiri ni suala tata.  Katika ujumbe wangu, niliandika kuwa "napenda kusema kwamba sala hii ilivyo katika ki-Ingereza ikiwa imesheheni uchaji, busara, na maudhui, imeundwa kwa lugha iliyotukuka. Ninajiuliza iwapo tunaweza kuitafsiri kwa ki-Swahili, tukahifadhi utukufu wake kwa msingi wa uhalisia wa ki-Swahili. Ninajiuliza hivyo pamoja na kufahamu jinsi suala la tafsiri lilivyo gumu na tata. Ninatarajia kujaribu kuitafsiri sala hii siku zijazo." Hata hivi, nimejaribu kutafsiri sala ya Papa Francis, ili kuwapa angalau fununu wale ambao hawajui ki-Ingereza. Ni bora kufanya hivyo, kuliko kuacha kabisa. Ye yote anayekijua ki-Ingereza vizuri, na pia anakijua ki-Swahili vizuri, ataona kuwa nimejipa mtihani mgumu. Ninamhimiza naye ajaribu kutafsiri. A prayer for our earth All-powerful God, you are

Mtunzi Haji Gora Haji

Image
Leo nimeamua kuongelea kifupi utunzi wa Haji Gora Haji wa Zanzibar, mmoja wa waandishi maarufu wa ki-Swahili wa zama zetu hizi. Nafurahi kuwa niliwahi kuonana naye mjini Zanzibar na kuzungumza naye. Panapo majaliwa, nitaandika taarifa ya mazungumzo yetu, ambayo yalihusu maisha yake katika sanaa. Ni muhimu kuutangazia ulimwengu kazi murua inayofanywa na watu wetu wenye vipaji kama Haji Gora Haji. Nina vitabu vyake vinne: Kimbunga (Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press, 1994), Utenzi wa Visa vya Nabii Suleiman Bi Daudi (A.S.) (Zanzibar: Al-Khayria Press Ltd, 1999), Kamusi ya Kitumbatu (Zanzibar: Express Printing Services, 2006), na Siri ya Ging'ingi (Dar es Salaam: Taasisi ya Taaluma za Kiswahili Chuo Kikuu Dar es Salaam, 2009). Kadiri siku zinavyopita, wasomaji na wahakiki wanajitokeza na kuongelea uandishi wa Haji Gora Haji. Mifano ya kutambuliwa huko ni taarifa ya Amanda Leigh Lichtenstein,  ya Ridder Samson, na  ya Pascal Bacuez . Nami nimetafsiri mashairi yak

Nimesaini Vitabu Kwa Ajili ya Filamu ya "Papa's Shadow"

Image
Wakati wa kampeni ya Ramble Pictures ya kuchangisha fedha kulipia gharama za filamu ya Papa's Shadow, nilichangia fedha kiasi na pia nakala za kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences .  Walikuwa wameweka viwango mbali mbali vya michango ambavyo viliendana na vizawadi na vivutio kwa wachangiaji. Waliochangia dola 200 au zaidi waliahidiwa nakala ya kitabu changu kama zawadi. Leo, Jimmy Gildea, mwanzilishi wa Ramble Pictures na mtengenezaji wa Papa's Shadow, ambaye alikuwa mwanafunzi katika kozi yangu ya Hemingway, alinifuata hapa  chuoni St. Olaf, nikasaini nakala tano za kitabu changu, na kumkabidhi. Tulipata fursa ya kuongelea habari za Ernest Hemingway, ziara yetu ya Montana, msisimko na mafanikio ya kampeni ya kuchangisha fedha, na kadhalika. Vile vile, Jimmy alinirekodi nikiwa nasoma kitabu cha Green Hills of Africa na pia nikiwa natembea katika sehemu iliyoonyesha vizuri mandhari ya chuo. Jimmy aliniuliza iwapo nina picha za uja

Kuwalea Watoto Kupenda Vitabu

Image
Kati ya mambo yanayonivutia sana hapa Marekani ni namna wazazi wanavyowalea watoto katika utamaduni wa kupenda kusoma vitabu. Katika matamasha ya vitabu, maduka ya vitabu, na maktaba, ninawaona wazazi wakiwa na watoto. Nimewahi kuandika kuhusu suala hilo katika blogu hii. Lakini kwa kuwa hii ni mada ninayoitilia maanani sana, nimeamua kuiongelea tena. Picha ya juu hapa kushoto ilipigwa mwaka 2008, niliposhiriki sherehe za kumbukumbu ya uhuru wa Nigeria hapa Minnesota. Nilikuwa na meza ya vitabu vyangu. Nakumbuka vizuri jinsi huyu mama m-Nigeria anayeonekana pichani alivyokuja mezani pangu na binti yake. Tulisalimiana, wakaangalia na kuvifurahia vitabu vyangu, kama inavyoonekana pichani. Picha ya pili hapa kushoto nilipiga katika tamasha la vitabu la Deep Valley, mjini Mankato, Minnesota. Nilivutiwa na namna hao watoto walivyokuwa wanafuatana na mama yao kutoka meza hadi meza wakiangalia vitabu. Picha ya tatu hapa kushoto nilipiga mwezi Agosti mwaka huu mjini Brooklyn Park, Minn

Kuhusu Kublogu

Nimekuwa mwanablogu tangu mwaka 2008. Ninaendesha blogu hii ya Hapa Kwetu na nyingine ya ki-Ingereza. Kublogu kuna mambo mengi. Kublogu kunanipa fursa ya kujieleza kwa uhuru. Hili ni jambo la msingi, kama alivyoelezea  mwanablogu Christian Bwaya. Lakini kublogu kuna matokeo yenye manufaa. Kumeniwezesha kuwafikia watu mbali mbali ambao wanatembelea blogu zangu. Siwezi kujua wanapata ujumbe gani katika maandishi yangu. Kama taaluma inayotufundisha, hili ni suala tata. Ujumbe wa andiko ni zao la kazi anayofanya msomaji juu ya andiko. Na kwa kuwa wasomaji wana akili zinazotofautiana, na wana nidhamu na uzoefu tofauti wa kusoma, kila mmoja anaibuka na ujumbe tofauti, kwa kiwango kidogo au kikubwa. Niliwahi kuelezea kwa nini ninablogu, lakini sidhani kama nilikuwa na majibu ya uhakika. Baadaye, katika kutafakari suala hili, nilifikia hatua ya kutamka kwamba ninablogu kwa ajili yangu mwenyewe.  Labda huu ndio ukweli wa mambo. Imani iliyojengeka katika jamii ni kuwa mwandishi anawa

Nilitembelea Duka la Vitabu la Amkal

Image
Tarehe 23 Mei, 2015, nilitembelea duka la vitabu la Amkal mjini Minneapolis, kama nilivyoripoti katika blogu hii. Ni duka la wa-Somali ambalo linauza zaidi vitabu vinavyohusu dini ya ki-Islam. Siku hiyo nilinunua kitabu kiitwacho Jesus: Prophet of Islam . Ninapenda kuongelea, kwa kifupi na wepesi kabisa, mawazo yanayonijia ninapokumbuka ziara yangu katika duka lile. Jambo la msingi kwamba katika kuishi kwangu hapa Marekani, nimeona jinsi wa-Afrika wa nchi mbali mbali wanavyovithamini vitabu. Kwa mfano, nimewahi kuwaongelea wa-Kenya. Wa-Somali ni mfano mwingine. Nimekutana na wa-Somali wanaoishi hapa Minnesota ambao wanaandika vitabu. Nimejionea wanavyojitokeza kuwasikiliza waandishi wa vitabu wa ki-Somali. Mfano ni Nuruddin Farah, ambaye huonekana hapa Minnesota mara kwa mara, ingawa makao yake kwa miaka hii ni Afrika Kusini. Wanamheshimu kwa jinsi anavyowakilisha taifa lao katika ulimwengu wa uandishi. Kwa ujumla, hao wa-Somali ni wakimbizi au wahamiaji. Lakini pamoja na ka