Showing posts with label uchapishaji mtandaoni. Show all posts
Showing posts with label uchapishaji mtandaoni. Show all posts

Monday, October 24, 2016

Ninarekebisha Kitabu Nilichochapisha Mtandaoni

Mara kwa mara, ninaongelea suala la kuchapisha vitabu mtandaoni, kutokana na uzoefu wangu. Ninatarajia kuwapa wengine uzoefu wangu wa kutumia tekinolojia za uchapishaji mtandaoni, ambazo zinatoa fursa tele kwa yeyote kujikomboa na taabu na vikwazo vya uchapishaji wa jadi.

Faida mojawapo ya uchapishaji wa aina ninayotumia kuchapishia vitabu vyangu ni fursa isiyo na mipaka ya kurekebisha kitabu chako wakati wowote uonapo dosari ndani yake au fursa ya kukiboresha. Hilo linawezekana kwa kuwa mswada wako unakuwa umehifadhiwa kama faili la kielektroniki mtandaoni, hata kama hukuuhifadhi katika kompyuta, disketi, au kifaa kingine.

Mimi ninatumia mtandao wa lulu.com. Hapo, ukishachapisha kitabu, nakala ya mswada inahifadhiwa hapo hapo mtandaoni. Unapotaka kurekebisha kitabu chako, unachofanya ni kuuingiza "(down-loading") mswada katika "flash drive" na kuufanyia marekebisho. Kisha unaurudisha ("up-loading") sehemu ya kuchapishia. Yeyote atakayekinunua baada ya hapo atakuwa ananunua kitabu kilichoboreshwa.

Hatua zote hizi zinafanyika bila mtu yeyote kutambua kinachotokea, bali wewe mhusika tu. Na wakati wote, unaporekebisha mswada, kitabu hakitoweki hapo mtandaoni. Kinakuwa kama kilivyokuwa mwanzo, na yeyote anaweza kukinunua, wakati wewe unaendelea na marekebisho. Unapomaliza marekebisho na kukiingiza tena mtandaoni ("up-loading"), ndipo kitabu kilichoboreshwa kinachukua nafasi ya kile cha awali.

Sasa hivi, niko katika kurekebisha kitabu changu, Notes on Okot p'Bitek's Song of Lawino. Hakuna anayetambua kuwa kinafanyiwa marekebisho, kwani kinaonekana hapo mtandaoni kama kawaida. Nitakapomaliza marekebisho na kukichapisha tena, itakuwa kama vile hakuna lililotokea.

Urahisi huu wa kurekebisha kitabu hauko katika uchapishaji wa jadi, ambapo inabidi kungoja hadi wakati wa kutoa toleo jipya la kitabu. Aghalabu, wachapishaji huwa hawana uwezo wa kifedha wa kutoa toleo jipya. Nakala zikiisha, huwa ndio mwisho wa kuchapishwa kitabu.

Lakini tatizo hili haliko katika uchapishaji wa mtandaoni kama huu ninaotumia. Kitabu hakiwezi kutoweka, yaani kuwa "out of print," labda mtu uamue kukiondoa wewe mwenyewe hapo mtandaoni. Ukibadili mawazo ukataka kukirudisha tena ulimwenguni, ni hiari yako kufanya hivyo, wakati wowote. 

Thursday, June 9, 2016

Kitabu Andika Kwa Ajili Yako

Mara kwa mara ninapata ujumbe kutoka kwa watu wanaohitaji ushauri kuhusu uandishi wa vitabu. Baadhi wanakuwa wameshaandika miswada na wanatafuta ushauri kuhusu kuchapisha vitabu.

Wengine, baada ya kupata ushauri wangu ambao kwa kawaida unahusu uchapishaji wa mtandaoni, wanaulizia utaratibu wa malipo. Yaani wanataka kujua watalipwaje kutokana na mauzo ya vitabu vyao.

Ninakaribisha maulizo kuhusu masuala haya ya uandishi, uchapishaji, na uuzaji wa vitabu, kama ninavyothibitisha katika blogu hii. Hapa ninapenda kusema neno la jumla kwa watu hao, hasa wanaowazia mauzo na malipo: kitabu andika kwa ajili yako.

Nimeona kuwa watu wana kiherehere cha kuchapisha vitabu na kuviuza, wajipatie fedha. Wanaamini kuwa wakishachapisha kitabu, kuna utitiri wa watu watakaonunua, na wao waandishi watajipatia fedha, na labda fedha nyingi.

Kwa ujumla, hii ni ndoto. Kwanza, ni waandishi wachache sana duniani wanaopata fedha kutokana na vitabu vyao za kutosha hata kumudu gharama za kawaida za maisha. Pili, tutafakari hali halisi ya mwamko wa jamii katika suala la kununua na kusoma vitabu. Je, tuna utamaduni wa kununua na kusoma vitabu? Wewe mwenyewe unanunua na kusoma vitabu? Kama sivyo, una sababu gani au una haki gani ya kudhani kuwa wengine watanunua kitabu chako?

Pamoja na yote hayo, ni kweli kuwa kama unaandika vitabu vinavyoitwa vya udaku, au vya mambo ya kusisimua hisia, kama vile mapenzi, kuna uwezekano kuwa vitanunuliwa. Lakini hivi ni vitabu vya msimu, au vitabu vya chap chap, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii. Havina thamani ya kuvifanya vidumu kama vinavyodumu vitabu vya akina William Shakespeare, Charles Dickens, Leo Tolstoy, au Shaaban Robert. Waandishi wa vitabu vya msimu wanaweza kujipatia fedha kiasi.

Kuna aina nyingine ya waandishi ambao nao wanaweza kujipatia fedha. Hao ni waandishi wanaofuata jadi mbaya ambayo imekuwepo Tanzania, ya watu kuandika vitabu na kuvisukumia mashuleni. Mashule yamekuwa kama majalala ya kupokea vitabu kiholela. Wahusika wanatafuta fedha na wanafunzi wanaathirika, kwa kuwa vitabu hivi havikidhi viwango vya hali ya juu kabisa vya taaluma na uandishi sahihi.

Tukiachilia mbali aina hizi za uandishi, tutafakari uandishi wa vitabu vya kuelimisha jamii, ambavyo havisukumwi na mahitaji ya shule. Tutafakari vitabu ambavyo mwandishi makini mwenye ujuzi fulani anaandika ili kuelezea yale anayoyajua kwa umahiri wote awezao. Ni aina ya uandishi unaotokana na msukumo wa ndani ya nafsi ya mwandishi, kiasi kwamba hawezi kutulia bila kuhitimisha kazi ya kujikomboa kutokana na msukumo huo.

Uandishi huo huwa ni kwa manufaa ya mwandishi mwenyewe. Ninaamini kuwa huo ndio uandishi wa dhati. Ndio uandishi wa kweli. Kitabu cha namna hiyo kikishachapishwa, haijalishi kama kinanunuliwa na kusomwa na yeyote. Mwandishi unakuwa umetua mzigo. Umejikomboa, na uko tayari kuanza shughuli nyingine, kama vile kuandika kitabu kingine.

Binafsi, nina ajenda yangu ya vitabu ninavyotaka kuandika. Siangalii kama vitasomwa au kama vitatumika mashuleni. Kuna vitabu vya fasihi ambavyo nimevisoma, ambavyo ninaviandikia tahakiki, kwa kupenda mimi mwenyewe, wala si kwa kusukumwa na mahitaji ya wengine.

Kwa mfano, kwa miaka mingi nilikuwa ninatafakari utungo wa Okot p'Bitek, uitwao Song of Lawino, na kuandika mawazo yangu, hadi hivi karibuni nikachapisha mwongozo, Notes on Okot p'Bitek's Song of Lawino. Vile vile, nilishawahi kuandika katika blogu hii kuwa ninataka kuandika mwongozo kuhusu kitabu cha Camara Laye kiitwacho The African Child. Ninaridhika kabisa na mtazamo wangu kwamba kitabu andika kwa ajili yako mwenyewe, na dhana hii nimeigusia kabla katika blogu hii.


Wednesday, December 23, 2015

Ninajivunia Binti Huyu: Bukola Oriola

Nimefurahi kupata taarifa kuwa Rais Obama amemteua Bukola Oriola, kuwa mjumbe katika tume ya kumshauri kuhusu masuala ya usafirishwaji wa ghilba na utumikishwaji wa binadamu, kama ilivyotangazwa katika taarifa hii. Bukola ni binti kutoka Nigeria anayeishi hapa Minnesota, Marekani. Nimemfahamu tangu mwaka 2009, kwa kusoma taarifa zake katika magazeti ya wa-Afrika hapa Minnesota.

Niliguswa kwa namna ya pekee niliposoma kauli yake kuwa alikuwa ameandika mswada wa kitabu bali hakujua auchapishe vipi. Kwa kuwa nilikuwa na uzoefu wa kujichapishia vitabu, dhamiri yangu ilinisukuma niwasiliane naye ili nimsaidie. Nilielezea kisa hicho katika blogu hii.

Baada ya kitabu chake, Imprisoned: The Travails of a Trafficked Victim kuchapishwa, niliendelea kumhamasisha. Kwa mfano, nilimwalika kwenye tamasha la vitabu mjini Minneapolis tarehe 10 Oktoba, 2009, ambalo nilikuwa nashiriki. Nilitaka yeye kama mwandishi chipukizi aone na kujifunza kazi inayomngoja mwandishi baada ya kuchapisha kitabu. Alikuja, tukapiga picha inayoonekana hapa kushoto tukiwa kwenye meza yangu.

Kitabu kilimfungulia milango. Alikuwa anazunguka sehemu mbali mbali kutoa mihadhara kuhusu utumwa na mateso wanayopata wanawake wanaorubuniwa, kutoroshwa, kutekwa, na kisha kutumikishwa na kunyanyaswa. Alianzisha kipindi cha televisheni na pia taasisi aliyoiita The Enitan Story. Yote hayo ni kwa ajili ya kuwasaidia waathirika na kuielimisha jamii kuhusu tatizo hili ambalo limeota mizizi duniani.

Ninafurahi kwa mafanikio ya binti huyu. Naye, kwa kukumbuka nilivyomsaidia, aliandika ifuatavyo katika utangulizi wa kitabu chake:

     I would also like to thank those who worked with me to get this book published. My profound gratitude goes to Prof. Joseph Mbele of St. Olaf College, Northfield, Minnesota, who showed me how to get my book published, otherwise it would have been another Word Document on my computer. It would have not been able to give the message of hope to the hopeless. God bless you sir.

Kitendo cha Rais Obama kumteua Bukola kwenye tume hiyo ni heshima kubwa kwake. Hapa Minnesota na Marekani kwa ujumla watu wamezipokea taarifa hizi kwa furaha. Nchini kwake Nigeria taarifa hii imekuwa kishindo katika vyombo vya habari. Kwa upande wangu, naona fahari kuwa niliitikia wito wa dhamiri yangu nikamwelekeza namna ya kuchapisha kitabu ambacho kilichangia na bado kinachangia mafanikio yake. Mungu ni mkubwa.

Bukola mwenyewe anatambua kuwa kuna mkono wa Mungu katika mambo anayopitia na kuyashuhudia maishani. Anaamini kuwa ana wajibu mbele ya Mungu wa kuwasaidia wanyonge, na kuwa mtetezi wa wanaonyanyaswa na kudhulumiwa. Msikilize anavyojieleza:

Saturday, December 19, 2015

Kuchapisha Vitabu Mtandaoni

Kutokana na taarifa ninazoandika katika blogu hii, na sehemu zingine, watu wengi wanafahamu kuwa nimechapisha vitabu vyangu mtandaoni. Nimeshawasaidia waandishi kadhaa wa mataifa mbali mbali kuchapisha vitabu vyao kwa mtindo huo. Kwa upande wa Tanzania, niliwahi kuongea na wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu suala hilo, na nilinukuliwa katika gazeti la Mwananchi.

Mara kwa mara, watu huniulizia kuhusu kuchapisha vitabu vyao. Napenda kuongelea tena suala hili, hasa matokeo ya kuchapisha vitabu mtandaoni. Kwanza, ni muhimu kufahamu kwamba kuna njia nyingi za kuchapisha vitabu mtandaoni. Ni juu ya mwandishi kuchagua. Binafsi, ninatumia njia ambayo ni rahisi kabisa, isiyo na gharama, au yenye gharama ndogo kiasi kwamba haiwi kizuizi kwangu.

Kuchapisha kwa namna hii ni rahisi sana. Mbali ya kutokuwa na gharama, haichukui muda, ili mradi mswada umeshaandaliwa kama faili la kielektroniki. Kinachobaki ni kuuingiza mswada kwenye tovuti ya kuchapishia, na haichukui dakika kumi kumaliza shughuli hii na kitabu kikawa tayari kununuliwa na watu popote ulimwenguni.

Jambo moja linalovutia sana katika kuchapisha vitabu mtandaoni kwa namna nifanyavyo ni kwamba vitabu hupatikana bila kikomo. Vinahifadhiwa kama mafaili ya kielektroniki, na huchapishwa kama kitabu halisi pale tu mdau anapoagiza nakala. Akiagiza nakala moja, inachapishwa hiyo hiyo. Akiagiza mia au elfu ni hivyo hivyo. Hakuna udhia wa kutunza shehena ya vitabu ghalani na kungojea wateja, huku vikiwa katika hatari ya kuharibiwa na unyevu, mende, au panya.

Hata hivi, nimeona kuna matatizo. Kwanza kwa upande wa mnunuzi. Ni lazima awe na namna ya kununua mtandaoni. Kwa kawaida hii inamaanisha awe na "credit card" kama vile VISA na Mastercard. Jambo la pili ni bei. Nikiangalia vitabu vyangu, naona wazi kuwa kama vingechapishwa mahali kama Tanzania kwa mtindo wa jadi, vingekuwa na bei nafuu kuliko ilivyo sasa.

Lakini, kwa upande mwingine, kama kitabu kinachapishwa kama kitabu pepe, yaani "e-book," kinaweza kuuzwa kwa bei ndogo sana, kuliko bei ya kuchapisha kwa mtindo wa jadi. Mdau anatakiwa awe na kifaa cha kuhifadhia na kusomea kitabu pepe, yaani "e-reader" au "e-book reader," kama vile Kindle au Nook.

Pamoja na kuwepo kwa vitabu pepe na vifaa vya kuhifadhia na kusomea vitabu hivyo, imethibitika tena na tena kwamba wadau wengi bado wanavitaka vitabu vya jadi, yaani vya karatasi na majalada. Mazoea haya na mapenzi ya vitabu vya jadi yamejengeka na hayaonekani kutoweka mioyoni mwa wengi.

Tekinolojia ya kuchapisha vitabu mtandaoni inawaathiri wachapishaji wa jadi kwa namna mbali mbali. Kadiri siku zinavyopita, wengi wao wanaona faida ya kuchapisha vitabu mtandaoni. Tekinolojia hii mpya inawasukuma kwenda na wakati ili wasipoteze biashara katika mazingira ya ushindani na mabadiliko yasiyoisha.

Friday, December 26, 2014

Kitabu Changu Katika Jalada Gumu

Leo nimepata nakala ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kikiwa katika jalada gumu ("hard cover"). Wiki iliyopita, kwa kutumia tekinolojia ya uchapishaji vitabu mtandaoni, niliuchapisha upya mswada wa kitabu changu, ili kitabu kipatikane pia katika jalada gumu. Nilipomaliza tu kuchapisha, niliagiza nakala, ambayo nimepata leo. Ni nakala ya kwanza kabisa, nami nimeridhika nayo.

Ni jambo la kawaida, huku ughaibuni, kwa kitabu kupatikana katika jalada jepesi ("paperback") na pia katika jalada gumu. Kuna vitabu vingine ambavyo hupatikana katika jalada jepesi tu, au katika jalada gumu tu.

Ninaamini, tangu zamani, ingawa sijafanya utafiti, kwamba maktaba ndizo zinazohitaji sana vitabu hivi vyenye jalada gumu, kwani vinaweza kuhimili vizuri zaidi misukosuko ya kuazimwa azimwa na wasomaji. Lakini kuna pia watu binafsi wanaopenda vitabu vya aina hiyo, hata kama nakala zenye jalada jepesi ziko pia.

Mimi mwenyewe nina vitabu vingi vyenye jalada gumu. Kila mtu ana sababu zake za kuvinunua vitabu vya aina hiyo. Kwa upande wangu, kisaikolojia, ninaviona vina hadhi ya pekee, mbali na kwamba vina nafasi ya kudumu zaidi katika hali nzuri.

Nimefurahi kuipata nakala hii ya kitabu changu wakati hali ya Krismasi bado iko hewani. Naona kama nimejipatia zawadi nyingine ya sikukuu. Kuanzia sasa, nitakuwa nachukua nakala hii popote nitakapokwenda kutoa mihadhara inayohusu au inayotokana na yale niliyoandika humo. Ni uamuzi wangu, hata kama hauna mantiki maalum. Ni binadamu gani anatafakari kwa makini kila kitu ambacho moyo wake unapenda?

Yeyote atakayehitaji nakala ya kitabu hiki anaweza kukipata kwenye stoo yangu ya mtandaoni. Nakala ya "kindle" inapatikana Amazon.com. Anayesita au asiyeweza kununua vitu mtandaoni awasiliane nami kwa barua pepe, africonexion@gmail.com au kwa simu, namba (507) 403-9756.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...