Showing posts with label duka la vitabu. Show all posts
Showing posts with label duka la vitabu. Show all posts

Thursday, October 11, 2018

Mchakato wa Kwenda Kuongelea Kitabu

Leo nimepata ujumbe kutoka kwa Dan, ambaye hivi majuzi alikipigia debe kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, katika duka la Barnes and Noble, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Anaendelea na juhudi yake. Ameandika:

Happy to spread the word about your book. Let me know if you are ever interested in doing a talk at our store. I can connect you with our manager.

Tafsiri yangu:

Ninafurahi kukitangaza kitabu chako. Nijulishe iwapo utapenda kuja kukiongelea katika duka letu. Nitaweza kukuunganisha na meneja wetu.

Kuwaalika waandishi kuongelea vitabu vyao ni utamaduni wa kawaida hapa Marekani. Ni fursa ya mwandishi kukutana na watu wanaotaka kujua mambo kama  historia ya mwandishi, changamoto za uandishi, falsafa na mawaidha yake kuhusu uandishi, na kadhalika. Vinakuwepo vitabu vya mwandishi, kwa watu kuvinunua na yeye kuvisaini. Wa-Marekani wanapenda kusainiwa vitabu, kama nilivyowahi kusema katika blogu hii.

Saturday, July 1, 2017

Vitabu Nilivyonunua Leo

Ninaamini kuwa kila mtu ana kitu anachokipenda sana. Kuna watu wanaopenda sana soka. Ni mashabiki ambao daima wanafuatilia mechi. Wako tayari kukopa hela ili waende uwanjani kuangalia mechi. Wengine wanapenda bia. Katika baa za Tanzania, nimeona watu wanaokunywa na kuandikiwa deni walipe baadaye. Kama huku kupenda kitu namna hii ni ugonjwa, basi vitabu ndio ugonjwa wangu. Ndio maana katika blogu hii ninaandika mara kwa mara habari za vitabu.

Mtu anaweza kuuliza, inakuwaje katika ulimwengu huu wa vitabu pepe, tuko watu ambao tunaendelea kung'ang'ania vitabu vya jadi? Je, hatuoni udhia wa kubeba vitabu hivyo, na pia udhia wa kuvitafutia sehemu ya kuviweka, badala ya kutumia kifaa cha kuhifadhia vitabu pepe, ambacho kinaweza kubeba mamia ya vitabu au zaidi? Ukweli ni kwamba, mazoea yana taabu. Sio rahisi kuachana na mazoea.

Leo nilikwenda Minneapolis, na wakati wa kurudi, nilipita katika duka la vitabu la Half Price Books, mjini Apple Valley. Kama kawaida, niliangalia kwanza sehemu vinapowekwa vitabu vya Ernest Hemingway au vitabu juu ya Hemingway. Sikuona kipya, nikaelekea sehemu vinapouzwa vitabu vya bei rahisi kabisa. Hapo nilichagua vitabu vinne.

Kitabu kimoja ni Gilgamesh: A Verse Narrative, cha Herbert Mason. Wafuatiliaji wa fasihi simulizi za kale wanafahamu juu ya Gilgamesh, mtu maarufu katika masimulizi ya watu wa himaya ya Sumer, katika nchi ambayo leo inaitwa Iraq, na pia nchi zingine za Mashariki ya Kati. Masimulizi haya hatimaye yaliandikwa, katika lugha kadhaa za wakati ule, kwa hati iitwayo "cuneiform," ambayo ni tofauti kabisa na hizi hati tunazotumia leo, kama vile ya ki-Rumi, au ki-Arabu. Ugunduzi wa maandishi yale ulitokana na juhudi za wana akiolojia.

Lakini baada ya ugunduzi, hakuna aliyeweza kusoma hati ya "cuneiform." Baadaye sana siri ya hati hii iligunduliwa na usomaji wake ukawezekana. Tafsiri za masimulizi ya Gilgamesh zikaanza. Kwa upande wangu, kwa miaka mingi nimefundisha masimulizi ya Gilgamesh kwa kutumia tafsiri ya N. K. Sandars. Nilifahamu, hata hivyo, kwamba ziko tafsiri zingine pia. Kwa hivyo, leo niliona ninunue hii tafsiri ya kishairi ya Herbert Mason.

Kitabu kingine nilichonunua leo ni A Play of Giants, ambayo ni tamthilia ya Wole Soyinka. Nimesoma na kufundisha maandishi ya Soyinka kwa miaka mingi, kuanzia tamthilia, riwaya, mashairi na insha. Ninavyo vitabu vyake kadhaa, lakini si A Play of Giants. Hata hivyo, nilifahamu tangu zamani kuwa tamthilia hii inawaumbua madikteta wa Afrika. Sasa nitaisoma.

Kitabu cha tatu nilichonunua ni Theban Plays of Sophocles. Ni tafsiri ya David R. Slavitt ya tamthilia tatu za Sophocles. Huyu ni mwanatamthilia maarufu wa u-Griki ya kale. Ninazo tatsiri tofauti za tamthilia hizo, lakini niliamua kununua hii pia. Ni jambo bora kusoma tafsiri mbali mbali za kazi ya fasihi, kwani kila tafsiri inaleta ladha tofauti na hata tofauti za ujumbe.

Kitabu cha nne nilichonunua ni Speaking of Books: The Best Things Ever Said About Books and Book Collecting, kilichohaririwa na Rob Kaplan na Harold Rabinowitz. Hicho sikuwahi hata kukisikia, lakini nilivyoangalia ndani, nilivutiwa. Ni mkusanyiko wa kauli za watu mbali mbali kuhusu vitabu, usomaji, uandishi, waandishi, wasomaji, na kadhalika. Nilikuwa ninafahamu baadhi ya mambo ambayo yamewahi kusemwa kuhusu vitabu, kama vile kauli ya Ernest Hemingway, "There is no friend as loyal as a book," yaani hakuna rafiki wa kweli kama kitabu. Kutokana na kupendezwa kwangu na mambo hayo, niliona ninunue kitabu hiki.

Saturday, March 4, 2017

Vitabu Nilivyonunua Leo

Leo nilikwenda Minneapolis, na wakati wa kurudi nilipitia Apple Valley nikaingia katika duka la Half Price Books. Kama kawaida, nilitaka kuona vitabu mbali mbali, lakini nilikuwa hasa na dukuduku ya kuona kama kuna vitabu juu ya Ernest Hemingway.

Kwa hivyo, nilivyoingia tu dukani, nilienda moja kwa moja kwenye sehemu vinapowekwa vitabu vya Hemingway, yaani vilivyoandikwa naye au juu yake. Tofauti na siku zingine, leo nilikuta vitabu vichache, na vyote ni vile alivyoandika Hemingway mwenyewe. Nilikiona kitabu ambacho sikumbuki kama nimewahi kukiona kabla, The Fifth Column and Four Stories of the Spanish Civil War, nikakiangalia.

Niliona kuwa "The Fifth Column" ni tamthilia, ambayo sina katika maktaba yangu. Papo hapo nilihisi kuwa hadithi zilizomo katika kitabu ziko katika kitabu cha The Complete Short Stories of Ernest Hemingway, ambacho ninacho. Nimethibitisha hivyo baada ya kuja nyumbani.

Nilipotoka sehemu vinapowekwa vitabu vya Hemingway, nilienda sehemu ambapo sikosi kuangalia, kwani hapo vinawekwa vitabu ambavyo vinauzwa kwa bei ndogo sana. Kama kawaida, niliviangalia vitabu vingi, nikaamua kuchukua kitabu cha Gulliver's Travels cha Jonathan Swift.

Hii nakala ya Gulliver's Travels niliyonunua ni toleo la andiko halisi la Swift, si toleo lililorahisishwa. Jambo hilo lilinivutia. Jambo jingine ni kuwa kuna utangulizi ulioandikwa na Jacques Barzun, mwandishi ambaye maandishi yake nimeyafahamu tangu miaka ya themanini na kitu nilipokuwa ninasoma katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Katika nakala hii, kuna pia michoro aliyochora Warren Chappell.

Saturday, May 14, 2016

Nimepita Tena Katika Duka la Half Price Books

Leo alasiri nilikwenda eneo la Minneapolis, mwendo wa maili 40, kwa shughuli binafsi. Ilikuwa siku nzuri, ya jua la wastani na hali ya hewa ya kupendeza. Wakati wa kurudi, nilipita mjini Apple Valley, nikaamua kupitia katika duka la Half Price Books. Nilitaka hasa kuangalia kama kuna chochote juu ya mwandishi Ernest Hemingway. Kufuatilia vitabu juu ya Hemingway imeshakuwa mazoea kwangu, wala siwezi kujizuia.

Ninajua kuwa sitakikuta kitabu kipya kilichoandikwa na Hemingway. Inafahamika kwamba miswada yote ya vitabu vya Ernest Hemingway imeshachapishwa. Kinachotokea ni kuwa yanachapishwa matoleo mapya ya vitabu vyake, kama vile matoleo yanayohaririwa na mjukuu wake, Sean Hemingway, ambavyo Mzee Patrick Hemingway, mtoto wa Ernest Hemingway, anaviandikia utangulizi.

Maandishi mapya kabisa ya Ernest Hemingway yanayochapishwa ni barua zake. Kuna mradi wa kukusanya barua zote za Ernest Hemingway tangu utotoni mwake. Wahariri wa mradi huu ni maprofesa Sandra Spanier na Robert W. Trogdon, ambao wamebobea katika utafiti juu ya Ernest Hemingway. Hadi sasa majuzuu matatu yamechapishwa, na kila juzuu ni mkusanyo wa barua za miaka michache. Inatarajiwa kuwa mradi huu ambao utachukua miaka mingi, utatoa majuzuu yatachapishwa 17.

Vitabu vingine vipya ambavyo vinaendelea kuchapishwa ni matokeo ya utafiti juu ya maisha na maandishi ya Ernest Hemingway. Tangu zamani, kumekuwa na watafiti wengi wanaojishughulisha na utafiti huu, na vitabu ambavyo wamechapisha na wanaendelea kuchapisha ni vingi. Si rahisi kwa mtu yeyote kufuatilia suala hili kikamilifu, lakini ninakuwa na duku duku ya kuona kuna vitabu gani vipya juu ya Hemingway katika duka la vitabu.

Nimefurahi leo kukikuta kitabu juu ya Hemingway ambacho sikuwa hata nimekisikia, The True Gen: An Intimate Portrait of Hemingway by Those Who Knew Him kilichoandikwa na Denis Brian. Katika kukipitia, niliona kuwa kitabu hiki ni taswira ya Hemingway inayotokana na kumbukumbu za watu waliomfahamu. Niliamua hapo hapo kukinunua. Baada ya kufika nyumbani, nimeanza kukisoma.  Kuna maelezo ya watu wengi, kuanzia wale waliokuwa watoto wakienda shule na mtoto Ernest Hemingway hadi waandishi, wake zake, na watu wengine.

Kama ilivyo kawaida, nilipokuwa hapo dukani Half Price Books niliwaona watu wengi humo wakizunguka zunguka kuangalia vitabu na kuvinunua. Wazazi wengi walikuwa na watoto wao. Kama kawaida, inavutia kuwaona watoto wa ki-Marekani wanavyolelewa katika utamaduni wa kupenda vitabu.

Sikukaa sana humo. Baada ya kununua kitabu changu, niliona niwahi nyumbani nikaanze kukisoma.


Saturday, December 5, 2015

Kuwalea Watoto Kupenda Vitabu

Kati ya mambo yanayonivutia sana hapa Marekani ni namna wazazi wanavyowalea watoto katika utamaduni wa kupenda kusoma vitabu. Katika matamasha ya vitabu, maduka ya vitabu, na maktaba, ninawaona wazazi wakiwa na watoto. Nimewahi kuandika kuhusu suala hilo katika blogu hii. Lakini kwa kuwa hii ni mada ninayoitilia maanani sana, nimeamua kuiongelea tena.

Picha ya juu hapa kushoto ilipigwa mwaka 2008, niliposhiriki sherehe za kumbukumbu ya uhuru wa Nigeria hapa Minnesota. Nilikuwa na meza ya vitabu vyangu. Nakumbuka vizuri jinsi huyu mama m-Nigeria anayeonekana pichani alivyokuja mezani pangu na binti yake. Tulisalimiana, wakaangalia na kuvifurahia vitabu vyangu, kama inavyoonekana pichani.

Picha ya pili hapa kushoto nilipiga katika tamasha la vitabu la Deep Valley, mjini Mankato, Minnesota. Nilivutiwa na namna hao watoto walivyokuwa wanafuatana na mama yao kutoka meza hadi meza wakiangalia vitabu.

Picha ya tatu hapa kushoto nilipiga mwezi Agosti mwaka huu mjini Brooklyn Park, Minnesota, katika tamasha la Afrifest. Huyu bwana, m-Marekani Mweusi, alikuja na watoto wake kwenye meza yangu, kuangalia vitabu. Watoto hao ni wadogo sana, na sijui kama walikuwa wanajua kusoma, lakini, nilivutiwa na kitendo cha baba yao kuwaleta kuangalia vitabu.

Kwa wa-Marekani, umri wa mtoto si tatizo. Wanawasomea vitabu hata watoto wadogo sana, hasa kabla ya kulala. Watoto wanapenda kusomewa vitabu. Hapa naikumbuka video ya kusisimua inayomwonyesha mtoto mdogo akisomewa vitabu, halafu anavyoangua kilio kila anapoambiwa kuwa hadithi imeisha. Hebu iangalie.


Tuesday, December 1, 2015

Nilitembelea Duka la Vitabu la Amkal

Tarehe 23 Mei, 2015, nilitembelea duka la vitabu la Amkal mjini Minneapolis, kama nilivyoripoti katika blogu hii. Ni duka la wa-Somali ambalo linauza zaidi vitabu vinavyohusu dini ya ki-Islam. Siku hiyo nilinunua kitabu kiitwacho Jesus: Prophet of Islam. Ninapenda kuongelea, kwa kifupi na wepesi kabisa, mawazo yanayonijia ninapokumbuka ziara yangu katika duka lile.

Jambo la msingi kwamba katika kuishi kwangu hapa Marekani, nimeona jinsi wa-Afrika wa nchi mbali mbali wanavyovithamini vitabu. Kwa mfano, nimewahi kuwaongelea wa-Kenya.

Wa-Somali ni mfano mwingine. Nimekutana na wa-Somali wanaoishi hapa Minnesota ambao wanaandika vitabu. Nimejionea wanavyojitokeza kuwasikiliza waandishi wa vitabu wa ki-Somali. Mfano ni Nuruddin Farah, ambaye huonekana hapa Minnesota mara kwa mara, ingawa makao yake kwa miaka hii ni Afrika Kusini. Wanamheshimu kwa jinsi anavyowakilisha taifa lao katika ulimwengu wa uandishi.

Kwa ujumla, hao wa-Somali ni wakimbizi au wahamiaji. Lakini pamoja na kadhia hiyo, pamoja machungu waliyoyapitia, wameshikilia umuhimu wa vitabu na elimu. Katika vyuo vya hapa Minnesota, kama vile Chuo Kikuu cha Minnesota, Metropolitan State University. Mankato State University, South Central College, na Minneapolis Community and Technical College, wanafunzi wa ki-Somali ni wengi. Wanawekeza katika elimu. Wanajijengea mtaji ambao wataweza kuutumia kwa maendeleo ya nchi yao.

Suala la elimu wanalishughulika kwa namna nyingine pia, kama vile magazeti na vituo vya televisheni. Hali hii nimeiona pia miongoni mwa wa-Afrika wengine, kama vile wa-Kenya na wa-Ethiopia. Kwa kutumia njia hizo, wanazitangaza nchi zao na shughuli zao, kama vile biashara. Ninawaona ni mfano wa kuigwa.

Tuesday, November 24, 2015

Kitabu Changu Bado Kiko Maoneshoni

Nimepita tena katika duka la vitabu la hapa chuoni St. Olaf, kama ilivyo kawaida yangu, kuangalia vitabu vipya, na pia kuangalia vitabu ambavyo maprofesa wa masomo mbali mbali wanapangia kufundisha.

Katika kuzunguka humo dukani, nilipita tena sehemu ambapo vinawekwa vitabu vilivyoandikwa na maprofesa wa chuo hiki. Kabla sijafika kwenye sehemu hiyo, macho yangu yalivutiwa na kitabu change cha Matengo Folktales, ambacho kilikuwa bado kiko sehemu maalum vinakowekwa vitabu ambavyo uongozi wa duka huamua kuvipa fursa ya kuonekana vizuri zaidi kwa kipindi fulani, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii.

Kuna mambo yanayonigusa kila niingiapo katika duka hili la vitabu na maduka mengine ya vitabu popote hapa Marekani. Kubwa zaidi ni jinsi wahudumu wanavyokuwa ni watu makini katika masuala ya vitabu. Wanajua habari za vitabu, na wanaweza kukuelimisha kwa namna mbali mbali. Hawako katika kazi hii kwa kubahatisha au kwa kubabaisha. Wanajua wanachokifanya. Unaweza kuingia katika duka la vitabu hapa Marekani bila mpango wa kununua kitabu, lakini ukianza kuongea na wahudumu, unaweza kujikuta umeelimishwa kuhusu vitabu fulani ukaishia kununua.

Katika haya maduka ya vyuo, nimeona wana huu utaratibu wa kuwa na sehemu ya kuweka vitabu vilivyoandikwa na maprofesa wa vyuo hivyo, na pengine pia vitabu vya watu waliohitimu zamani, ambao huitwa "alumni" (wanaume) au "alumnae" (wanawake). Ni namna mojawapo ambayo taasisi hizo huwatambua na kuwaenzi waalimu na wahitimu. Nami najisikia vizuri kama profesa wa chuo hiki cha St. Olaf kuwa kazi zangu zinatambuliwa, vikiwemo vitabu.

Kwa upande wa biashara, naona kuwa haya maduka ya vitabu ya vyuo vya Marekani yanaonyesha ubunifu wa kibiashara kwa kuweka vitabu vyetu namna hiyo. Mbali  ya wanafunzi, tuna wageni wengi wanaopita hapa chuoni kila siku, wakiwemo wazazi wa wanafunzi, wahitimu wa zamani, na wale wanaokuja kuangalia ubora wa chuo ili wawalete vijana wao kusoma hapa. Duka la vitabu ni sehemu moja muhimu wanamoingia. Humo wanakuwa na fursa ya kununua vitabu vyetu hasa inapokuwa kwamba wamesikia habari zetu. Kwa mfano, duka la St. Olaf limeshauza nakala mia kadhaa za vitabu vyangu.

Hayo ni baadhi ya mambo niliyojifunza katika suala hili ambayo nimeona niyaweke katika blogu yangu, kwa lugha rahisi kabisa. Labda yanaweza kuwa na manufaa kwa vyuo nchini mwangu.

Tuesday, August 25, 2015

Nimekikuta Kitabu Changu Kinameremeta Dukani

Mchana huu nimemaliza kusahihisha mtihani wa kumalizia muhula wa somo langu la "African Literature." Nimekwenda chuoni kuwarudishia wanafunzi daftari zao, nikiwa na furaha ya kuwa na wiki mbili tatu za "uhuru," kabla ya kuanza muhula mwingine.

Baada ya kurudisha daftari, niliingia katika duka la vitabu. Nilizunguka kidogo tu humo ndani nikaona kitabu changu cha Matengo Folktales kimewekwa mahali pa wazi, pamoja na vitabu vingine vichache. Kinaonekana pichani chenye rangi ya manjano na ramani ya Afrika.

Huu ni utaratibu wa duka letu la vitabu. Kila wakati wanachagua vitabu vichache na kuviweka sehemu hizo za wazi ili viweze kuonekana kirahisi kwa wateja. Kufuatana na utaratibu uliopo, kitabu kitakuwa hapo kwa siku kadhaa, na hata wiki kadhaa, kabla ya kurudishwa sehemu yake.

Katika duka hili la chuoni St. Olaf vinapatkana vitabu vyangu vyote. Mbali ya wanafunzi, waalimu, na wafanyakazi wengine wa chuo, wageni wanaokitembelea chuo hupenda kuingia katika hili duka la vitabu, ambalo huuza pia bidhaa mbali mbali, kama ilivyo kawaida katika maduka ya vitabu ya vyuo vya Marekani.

Kila ninapoviona vitabu vyangu katika duka hili, mawazo hunijia, hasa kuhusu namna vitabu hivi vinavyowafaidia wa-Marekani. Vinawafaidia kielimu, kwa kuwa vinatumika katika masomo. Vinawafaidia kibiashara, kwa kuviuza, na vinachangia ajira hata kama ni kiasi kidogo sana, kwa wachapishaji, wasafirishaji, na wahudumu wa duka kama hili la Chuo cha St. Olaf. Nawazia mambo ya aina hii.

Monday, March 2, 2015

Nimeulizwa Inakuwaje Siuzi Vitabu Vyangu Tanzania

Leo katika mtandao wa Facebook kuna mdau kaniuliza inakuwaje siuzi vitabu vyangu Tanzania. Nimemshukuru kwa ulizo lake, nikajaribu kulijibu. Napenda kuandika machache kuhusu suali hili.

Napenda kuanza kwa kusema kuwa vitabu hivyo vinapatikana mtandaoni, kama vile kwenye tovuti ya lulu na tovuti ya Amazon. Yeyote mwenye kadi ya "credit" kama vile VISA au MasterCard, anaweza kuvinunua. Haijalishi kama yuko Chake Chake, Dar es Salaam au Tukuyu. Ataletewa. Kama ana kifaa kama "kindle," ananunua bila tatizo.

Ninafahamu kuwa ni wa-Tanzania wachache walioko Tanzania wanaoweza kununua vitu mtandaoni. Lakini kuna maelfu ya wa-Tanzania katika nchi kama Marekani wenye hizo kadi. Kama kuna nia ya dhati ya kununua kitabu, haikosekani njia.

Mimi mwenyewe nimekuwa tayari kufanya mipango na wa-Tanzania wenye nia ya kuuza vitabu vyangu, kwa kuwapelekea. Nimewahi kufanya hivyo na Cultural Tourism Program (Longido), Bougainvillea Lodge (Karatu), na Cultural Tourism Program (Mto wa Mbu).

Kila inapowezekana, nafanya mpango wa kuvifikisha vitabu vyangu kwenye matamasha nchini Tanzania, kama ilivyoelezwa hapa.

Kwa kuwa mimi si mfanyabiashara, ningependa kuona wafanyabiashara wanajipatia faida kutokana vitabu vyangu. Duka la vitabu chuoni St. Olaf linauza vitabu vyangu kwa bei kubwa kuliko mtandaoni. Vile vile, nilipotembelea chuo cha South Central, katika duka la vitabu walikuwa wanauza kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kwa dola 17.95.

Hata hivi, huwa najiuliza ni wa-Tanzania wepi wanaotaka kusoma vitabu vyangu. Sijaona kama kuna utamaduni wa kununua na kusoma vitabu. Wa-Marekani ndio wasomaji wangu wakuu, kama ninavyobainisha mara kwa mara katika blogu hii. Kwa vyovyote, kuepusha lawama, na kuwatendea haki wa-Tanzania wanaoamini nina jambo la kuwaambia, najitahidi kuhakikisha vitabu vyangu vinapatikana Tanzania.

Wednesday, February 25, 2015

Yatokanayo na Mihadhara ya Jana Chuoni South Central

Tangu nilipomaliza ziara yangu chuoni South Central jana, nimekuwa na furaha kutokana na mafanikio ya ziara ile. Kuanzia jana ile ile, taarifa zimeenea za kuisifia ziara ile. Mfano ni namna mwenyeji wangu, Mwalimu Becky Fjelland Davis, alivyoandika katika blogu yake. Ninafurahi kuwa sikumwangusha, kwani katika kuandaa ujio wangu, alikuwa ameutangazia umma kama ifuatavyo:

Come one, come all, to hear what he has to say. You'll be touched by his wisdom and wit, as well as his gentle demeanor.

Mwalimu Fjelland Davis aliandika hivyo kwa kujiamini, kwani alishanialika mwaka 2013 kuongea na wanafunzi wake, kama alivyoripoti katika blogu yake.

Kwa kuwa nilialikwa ili nikaongelee masuala yaliyomo katika kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, nimefurahi kuona jinsi ziara yangu ilivyotekeleza mategemeo ya waandaaji na wote waliohudhuria  mihadhara yangu.

Ninafurahi kuwa ziara ya jana imefanyika mwezi huu, ambapo ninasherehekea kutimia kwa miaka kumi tangu nilipochapisha kitabu hiki. Pia ni faraja kwangu, baada ya miezi mingi ya kuwa katika matatizo ya afya. Nakumbuka kauli ya wahenga kuwa baada ya dhiki, faraja.

Makala hii fupi haiwezi kumaliza tathmini ya ziara ya jana. Kumbukumbu itaendelea mawazoni mwangu na katika jamii. Ila kuna jambo moja ambalo napenda kulitaja. Duka la vitabu la chuoni South Central lilikuwa linauza kitabu changu kwa dola 17.95. Ukifananisha na bei yake ya dola 13 niliyoweka mtandaoni, ni wazi kuwa mwuzaji anajipatia faida. Hakuna kizuizi kwa muuzaji yeyote kujipangia bei yake.

Friday, December 26, 2014

Kitabu Changu Katika Jalada Gumu

Leo nimepata nakala ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kikiwa katika jalada gumu ("hard cover"). Wiki iliyopita, kwa kutumia tekinolojia ya uchapishaji vitabu mtandaoni, niliuchapisha upya mswada wa kitabu changu, ili kitabu kipatikane pia katika jalada gumu. Nilipomaliza tu kuchapisha, niliagiza nakala, ambayo nimepata leo. Ni nakala ya kwanza kabisa, nami nimeridhika nayo.

Ni jambo la kawaida, huku ughaibuni, kwa kitabu kupatikana katika jalada jepesi ("paperback") na pia katika jalada gumu. Kuna vitabu vingine ambavyo hupatikana katika jalada jepesi tu, au katika jalada gumu tu.

Ninaamini, tangu zamani, ingawa sijafanya utafiti, kwamba maktaba ndizo zinazohitaji sana vitabu hivi vyenye jalada gumu, kwani vinaweza kuhimili vizuri zaidi misukosuko ya kuazimwa azimwa na wasomaji. Lakini kuna pia watu binafsi wanaopenda vitabu vya aina hiyo, hata kama nakala zenye jalada jepesi ziko pia.

Mimi mwenyewe nina vitabu vingi vyenye jalada gumu. Kila mtu ana sababu zake za kuvinunua vitabu vya aina hiyo. Kwa upande wangu, kisaikolojia, ninaviona vina hadhi ya pekee, mbali na kwamba vina nafasi ya kudumu zaidi katika hali nzuri.

Nimefurahi kuipata nakala hii ya kitabu changu wakati hali ya Krismasi bado iko hewani. Naona kama nimejipatia zawadi nyingine ya sikukuu. Kuanzia sasa, nitakuwa nachukua nakala hii popote nitakapokwenda kutoa mihadhara inayohusu au inayotokana na yale niliyoandika humo. Ni uamuzi wangu, hata kama hauna mantiki maalum. Ni binadamu gani anatafakari kwa makini kila kitu ambacho moyo wake unapenda?

Yeyote atakayehitaji nakala ya kitabu hiki anaweza kukipata kwenye stoo yangu ya mtandaoni. Nakala ya "kindle" inapatikana Amazon.com. Anayesita au asiyeweza kununua vitu mtandaoni awasiliane nami kwa barua pepe, africonexion@gmail.com au kwa simu, namba (507) 403-9756.

Saturday, October 6, 2012

Nimejipatia iPad

Pamoja na kuwa mimi ni mmoja wa wale watu wa zamani tuliozaliwa na kukulia kijijini na ambao tunababaishwa na hizi tekinolojia zinazofumuka kwa kasi, nimejipatia kifaa kiitwacho iPad siku chache zilizopita. Nimenunua iPad Wi-Fi+3G. Nilishinikizwa na binti yangu Zawadi. Ndiye anayenisukuma niende na wakati.

Tangu ninunue kifaa hiki, yapata wiki mbili zilizopita, nimekuwa katika kujifunza namna ya kukitumia, maana kina mambo mengi sana. Angalau naweza kutembelea mitandao, kutuma na kupokea barua pepe, na kupiga picha na kisha kuziangalia. Hata video najua namna ya kupiga.

Kitu ninachotaka kukifanya hima ni kuingiza vitabu pepe kwenye hii iPad, nikianzia na kitabu changu kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho wadau wanakipata mtandaoni, pamoja na vitabu vyangu vingine, kwa njia hiyo.





Kidogo najisikia vibaya kwamba nilikiweka kitabu hiki katika muundo wa kitabu pepe na wadau wanakinunua, wakati mimi mwenyewe sikuwa na kifaa cha kuingizia vitabu pepe wala sikuwahi hata kuona kinakuwaje katika umbo la kitabu pepe. Nimejisikia kama mpishi ambaye anawapikia wengine lakini yeye mwenyewe hata kuonja haonji. Sasa, na hii iPad yangu, ngoja nikae mkao wa kula, kwa vitabu vyangu na vya wengine.

Wednesday, October 6, 2010

Vitabu Vyangu Kwa Bei Nafuu

Lulu.com, ambako nachapisha vitabu vyangu, kumetokea tangazo linalotoa fursa kwa mwandishi kupunguza bei ya vitabu vyake akipenda.

Kwa heshima ya wasomaji wangu, nimeamua kutumia fursa hiyo. Nimepunguza bei ya vitabu vyangu vyote kwa mwezi huu Oktoba.

Vitabu hivi vimetajwa hapo kulia na pia hapa. Bofya sehemu ya kununulia, ili kuona punguzo hilo.

Wale ambao hawanunui vitu mtandaoni na wanavihitaji vitabu hivi wanaweza kuwasiliana nami kwa barua pepe: info@africonexion.com.

Siku ya mwisho ya punguzo hili ni Oktoba 31.

Sunday, September 26, 2010

Ujumbe Kuhusu Vitabu

Leo nilienda mji wa Duluth kwa matembezi ya masaa machache nikiwa na mwalimu mwenzangu katika idara yetu. Baada ya kuzunguka na gari sehemu kadhaa za mji huo, niliegesha gari kwenye mtaa uitwao Superior Street, unaoonekana katika picha hizi mbili, tukaanza kutembea katika mtaa huu, kuangalia mazingira.

Hatukwenda mbali, tukaona duka la vitabu na moja kwa moja tukaingia humo.

Humo ndani kulikuwa na vitabu vingi sana na vitu vingine vidogo vidogo vya nyumbani, kama vile sahani, glasi, mishumaa, na maua ya mapambo.

Nilipoingia tu, kwenye meza moja karibu na mlango niliona ujumbe uliowekwa kwenye fremu, kuhusu vitabu. Nilivutiwa sana na ujumbe ulioandikwa na Clarence Day, Jr.

Nilimwuliza mama mhudumu humo dukani kama naweza kupiga picha. Alisema kwa uchangamfu kuwa ni sawa kabisa.

Jioni hii, wakati naandika habari hii kwenye blogu, nimetafuta taarifa nikagundua kuwa Clarence Day, Jr. aliandika ujumbe wake mwaka 1920. Kwa jinsi nilivyoupenda, nimeona niuweke hapa na nijaribu kuutafsiri kwa ki-Swahili. :


VITABU

Ulimwengu wa vitabu ni kitu kilichotukuka kwa namna ya pekee kilicholetwa na binadamu. Hakuna anachounda binadamu ambacho kinadumu hivyo: majengo ya kumbukumbu huanguka, mataifa hutokomea, himaya za ustaarabu hupitwa na wakati na kutoweka duniani; kufuatia zama za giza, mataifa mapya hujenga himaya zingine. Lakini ulimwengu wa vitabu una majuzuu yanayodumu daima, yakiwa na upya na ubichi kama siku yalipoandikwa, na yanaendelea kuelezea mioyoni mwa wanadamu kuhusu yaliyojiri hata mioyoni mwa wanadamu waliokwishafariki karne za zamani.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...