Posts

Showing posts from March, 2011

Maskani Yangu Madison, 1980-86

Image
Wikiendi hii iliyopita, nilipokuwa Madison kwenye mkutano wa Peace Corps , nilitembelea sehemu kadhaa nilizozifahamu tangu wakati nasoma Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison , 1980-86. Nilivutiwa kwa namna ya pekee na wazo la kutembelea maskani yangu miaka ile. Niliingia Madison nikitokea Tanzania mwezi Agosti mwaka 1980. Sikumbuki tarehe. Lakini nilifikia mahali palipoitwa Union South, katika eneo la Chuo . Hapo nilikaa siku chache, nikingojea fedha kutoka Ofisi ya Fulbright , ambao ndio walinilipia gharama zote za masomo. Baada ya siku chache za kukaa Union South, nilihamia Saxony Apartments, sehemu inayoonekana hapa kushoto. Jengo nilimoishi liko nyuma ya hili linaloonekana. Saxony Apartments ilikuwa maarufu, kwa vile walikuwepo wa-Afrika wengi. Tulijisikia nyumbani. Nadhani nilikaa hapo Saxony Apartments kwa mwaka moja na zaidi, nikahamia Mtaa wa West Wilson, namba 420, jengo linaloonekana hapa kushoto. Ni karibu na Ziwa Monona. Wa-Tanzania tulikuwa na mshikamano sana, tukitembelea

Mkutano wa Peace Corps, Madison, Ulifana

Image
Machi 24-27 nilikuwa Madison, Wisconsin, kuhudhuria mkutano wa Peace Corps , uliojumuisha waMarekani walioenda kujitolea Afrika chini ya mpango wa shirika la Peace Corps. Mwaka huu ni mwaka wa maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Peace Corps, na maadhimisho hayo yanafanyika sehemu mbali mbali hapa Marekani. Mkutano huu wa Madison ulikuwa na mengi ya kuelimisha na kusisimua kuanzia historia ya kuanzishwa kwa Peace Corps hadi masimulizi na kumbukumbu za watu walioenda katika nchi mbali mbali za Afrika kujitolea katika nyanja mbali mbali. Kulikuwa na masumulizi kuhusu Rais Kennedy ambaye alichangia kuotesha mbegu ya Peace Corps kwa mtazamo wake wa kuwahamasisha raia wake wawe na moyo wa kujitolea, si kwa nchi yao tu, bali kwa ulimwengu. Rais Kennedy aliweka sahihi ya kuzindua Peace Corps tarehe 1 Machi, 1961. Kulikuwa na masimulizi kuhusu Sargent Shriver, ambaye ndiye alikuwa mwanzilishi wa Peace Corps, akiwa na moyo na ari isiyomithilika iliyowasha moto mioyoni mwa wana Peace

Dhana Duni ya Mfumo Kristo

Kila kukicha, unajitokeza ushahidi kwamba kiwango cha kufikiri miongoni mwa wa-Tanzania wengi ni duni. Siku hizi, kwa mfano, imeibuka hii dhana ya mfumo Kristo. Walioibuni dhana hii na ambao wanaieneza wana ajenda ya kujenga hoja kuwa mfumo wa utawala na uchumi Tanzania unaendeshwa kwa misingi ya kiKristu, na kwa lengo la kuwanufaisha wa-Kristu na kuwakandamiza na kuwanyima wa-Islam fursa na haki wanazostahili, katika nyanja mbali mbali, kama vile elimu na uongozi. Hii ndio dhana ya msingi ya hiki kinachoitwa mfumo Kristo. Wanaojenga hoja hii wanadai kuwa serikali ya Tanzania yenyewe inaendeshwa na maaskofu kama sehemu ya uendelezaji wa huu wanaouita mfumo Kristo. Kwanza napenda kusema, kama ninavyosema daima, kuwa kila mtu ana uhuru wa kutoa mawazo yake. Uhuru huu ni pamoja na uhuru wa kuyahoji au kuyapinga mawazo ya wengine, kufuatana na mchakato wa kujielimisha na kutafakari masuala. Ni pamoja na uhuru wa kuyapinga mawazo yako mwenyewe. Nashangaa kwa nini mfumo mbovu uhusishwe

Eti Wahadhiri Waeneza Siasa za Chuki Vyuoni

Niomeona taarifa hii hapa chini nikaona lazima niseme moja mawili, nikitumia wadhifa wangu kama mwanataaluma na mzoefu wa kufundisha au kutoa mihadhara vyuo vikuu sehemu mbali mbali za dunia. Sio kazi ya serikali kuingia darasani chuo kikuu ili kuchunguza mwalimu anafundisha nini au anafundishaje. Hii ni kazi ya wanataaluma na wahadhiri, kufuatana na taratibu zinazotambulika katika jumuia ya wanataaluma. Taratibu hizi ni za kulinda, kutathmini, kuratibu na kuboresha viwango vya utafiti, ufundishaji na taaluma kwa ujumla. Serikali inapaswa kutambua kuwa dhana ya chuo kikuu, duniani pote, inaendana na haitengeki na uhuru wa kitaaluma. Walimu wa vyuo vikuu sio tu wana wajibu, bali uhuru wa kufukuzia taaluma bila vipingamizi, kwa mujibu wa vigezo vya taaluma hizo vinavyotambulika miongoni mwa wanataaluma kimataifa. Kama kuna walakini katika utendaji kazi wa mwalimu wa chuo kikuu, kama vile kutofundisha somo inavyotegemewa, wanaowajibika kuchunguza ni wanataaluma wenzake, si serikali. Se

Kazi ya Kunywa

Image
Ukiondoa kazi ya kukaa vijiweni, kazi muhimu ya wa-Tanzania wengi ni kunywa. Huyu jamaa kwenye katuni ni m-Tanzania halisi. Yuko kazini, wala hafanyi mchezo. Ameshaamrisha kuwa kaunta ihamie hapa alipo, tena haraka sana. Wako wa-Tanzania ambao wanajifunza kunywa tangu utotoni. Wanapofikia ujana wanakuwa wameshahitimu. Kazi ya kunywa ni muhimu kwa wa-Tanzania wengi kiasi kuwa wamehamia baa, na wanaishi huko, kama nilivyoandika hapa . Shughuli nyingi za jamii Tanzania zinawezekana tu iwapo zinaendana na kunywa. Yaani ili watu waje kwenye hizi shughuli, ni muhimu ulabu uwepo. Hata kwenye uzinduzi wa kitu kama kitabu, ni muhimu pawe na ulabu, kama nilivyoelezea hapa . Nilisoma kwenye jarida la Tanzania Schools Collection , 1, (2009), kuwa mtoto mmoja wa miaka kumi alionekana kwenye maonesho ya vitabu Dar es Salaam akiwa mwenyewe. Mratibu mojawapo wa maonesho alipomwuliza kwa nini hakuja na baba yake, mtoto alijibu kuwa baba angefika kama kungekuwa na bia (uk. 12). Kwa mwendo huu, n

JK: Maprofesa Wananisikitisha

JK: Maprofesa wananisikitisha Chanzo: Uhuru NA JANE MIHANJI RAIS Jakaya Kikwete amewataka maprofesa na wasomi nchini kutunga vitabu ili kukabiliana na tatizo la kushuka kiwango cha elimu, kunakochangiwa na upungufu wa vitabu vya kiada na ziada. Amesema anasikitishwa na kitendo cha maprofesa na wasomi chini kulalamikia upungufu wa vitabu katika fani mbalimbali, huku wakikwepa kutoa mchango wa kutatua tatizo hilo. Rais Kikwete amewata kila mmoja kwa nafasi yake, kuhakikisha anafanya jitihada za kuboresha elimu ili kuwa na kizazi kilichowiva kitaaluma. Alisema hayo jana, mjini Dar es Salaam, alipotembelea Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Taarifa ya wizara iliyosomwa na waziri, Dk. Shukuru Kawambwa, ilieleza uhaba wa vitabu ni moja ya matatizo yanayokwamisha sekta ya elimu. Dk. Kawambwa alisema shule nyingi zinakabiliwa na upungufu wa vitabu na katika baadhi, wanafunzi hutumia vya tofauti, tatizo linaloweza kupatiwa ufumbuzi kwa wasomi kujikita katika uandishi wa vitabu. &quo

Eti Wananchi Msiwasikilize Wapinzani

Kuna mambo mengi katika siasa Tanzania siku hizi. Katika hali ya ushindani wa kisiasa uliopo, mara kwa mara tunawasikia hao wanaoitwa viongozi wetu wakisema, pengine kwa jazba, kuwa wananchi msimsikilize fulani au msiwasikilize watu fulani. Wanaotajwa hasa ni wapinzani. Wananchi wanaambiwa wasiwasikilize wapinzani. Kiongozi wa kweli, mwenye busara na ufahamu, hawezi kutoa kauli za namna hiyo. Kila mtu ana haki ya kusikiliza mawazo mbali mbali, yawe vitabuni, magazetini, au kwenye mikutano ya hadhara. Haki hii inapaswa kutambuliwa, kutetewa na kuheshimiwa. Yeyote anayesemekana kuwa ni kiongozi anapaswa kufahamu hilo. Pamoja na kwamba ni haki ya kila mtu, vile vile ni sehemu ya uhuru alio nao binadamu. Kila mtu ana uhuru wa kutafuta maoni, mawazo na mitazamo ya wengine katika masuala mbali mbali. Ana uhuru wa kusoma vitabu na magazeti, au kusikiliza redio na televisheni, au kusikiliza hotuba kwenye mikutano ya hadhara. Zaidi ya suala la haki na uhuru, kuna suala la wajibu. Wananchi wa

Kichekesho: Eti Dr. Slaa Kama Savimbi!

KONA YA KARUGENDO Chanzo: Raia Mwema KICHEKESHO: ETI DR. SLAA KAMA SAVIMBI! Watwambie ni kwa lipi wanafanana? KAWAIDA ya mfa maji haishi kutapatapata, na katika hali hiyo ya kutapatapa anafanya mambo mengi na yasiyokuwa ya kawaida. Lengo zima likiwa ni kuyaokoa maisha yake. Mtu anayetapatapa anaweza kuropoka na wakati mwingine kuupotosha umma. CCM ni kama mfa maji; wanatapatapa, wameanza kuropoka na kupotosha. Eti Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa ni kama Savimbi wa Angola. Kwa lipi? Mbali na kwamba Savimbi alikuwa binadamu, na Dk.Slaa ni binadamu, Savimbi alikuwa Mwafrika na Dk. Slaa ni Mwafrika; hawana kingine cha kufanana! Savimbi alikuwa mwanajeshi, alipigana msituni zaidi ya miaka 20! Aliendesha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe; watu wengi walikufa. Wengine walipata ulemavu wa kudumu kutokana na vita alivyoviendesha Savimbi, na wengine waliikimbia nchi yao. Savimbi alipora raslimali za nchi yake ili kuendesha vita hiyo iliyokuwa ndefu kiasi chake. Hadi leo hii

Machafuko ya Arusha

Image

Mteja Nimefurahi

Image
Juzi niliandika makala fupi, "Mteja ni Mfalme" . Leo napenda kuendelea na mada hiyo, kutokana na jambo lililonitokea. Nilipeleka kigari changu kwenye kampuni ya CarTime , kubadilisha "oil." Kama kawaida, wakati fundi anaendelea na shughuli, nilikuwa kwenye sehemu ya mapumziko ambako wateja hungojea magari yao. Baada ya muda, niliitwa na kuambiwa kuwa gari yangu tayari, nikalipia na kuchukua ufunguo. Kama kawaida, mhudumu wa hapo mapokezi alinishukuru. Nilienda nje fundi alikopaki gari nikafungua mlango. Kwenye kiti cha mbele alikuwa ameweka karatasi ambayo picha yake nimeiweka hapa juu. Fundi makenika alikuwa ameiweka hapo. Ujumbe wake ni huu: Asante kwa kuchagua CarTime. Tumefurahi kuhudumia gari lako . Kama vile hii haitoshi, fundi ameshukuru tena na kuandika jina lake, Eric. Katika makala yangu ya juzi niliongelea umuhimu wa kumridhisha mteja. Sasa leo hapa nimeweka mfano hai. Mimi kama mteja nimefurahi kwa huduma niliyopata. Lakini kwa hapa Marekani, hili

Mteja ni Mfalme

Image
Kwamba mteja ni mfalme ni dhana inayojulikana, hata kama wengi wenye biashara hawaifuati. Mantiki ya usemi kuwa mteja ni mfalme iko wazi, kwamba mteja akiridhika anakuwa ndio mpiga debe wako, bila wewe kumlipa chochote. Kwa hivi, kama wewe ni mfanyabiashara, ukiwa na tabia ya kumridhisha kila mteja, utafanikiwa. Kwa kawaida nadharia ni rahisi, ila utekelezaji unaweza kuwa mtihani mgumu. Hayo ninayaona wakati huu ninapoandika makala hii. Kuna mtu ameanza mawasiliano nami, kunialika nikazungumze kwenye kampuni anapofanyia kazi, kuhusu masuala ninayoongelea katika kitabu changu cha Africans and Americans . Ingawa nimethibitisha kuwa shughuli hii itafanyika, nimeona kuwa huyu mhusika hana uzoefu mzuri katika kupanga mipango ya aina hii. Nimeanza kupata usumbufu fulni, kwani wakati fulani anasema kitu nami nikadhani nimemwelewa, kumbe baadaye inaonekana hatukuelewana. Hata tarehe aliyopangia tufanya hiyo shughuli ameniambia kuwa imebidi waibadili. Ninajua kabisa kuwa hatimaye nitaenda ku

Uandishi Bora wa ki-Ingereza

Suala la uandishi bora kwa ki-Ingereza limenifikirisha kwa miaka mingi na bado ninalifikiria. Nilipokuwa kijana, nilidhani kuwa uandishi bora wa ki-Ingereza ulihitaji matumizi ya maneno magumu na mbwembwe katika miundo ya sentensi. Kwa vile nilipata bahati ya kujifunza ki-Latini, nikiwa shule ya seminari, nilikuwa na uwezo wa kuyafahamu maneno mengi magumu ya ki-Ingereza, kwani asili yake ni ki-Latini. Imani yangu hii ilikuja kugonga mwamba nilipokuwa nasomea shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison . Hapo nilikumbana na profesa Harold Scheub, ambaye alikuwa mkali kama mbogo katika suala la uandishi kwa maana kuwa alikuwa anataka uandishi unaotumia lugha nyepesi, kama ilivyoelezwa katika kitabu cha Elements of Style kilichotungwa na William Strunk na E.B. White. Huu ni uandishi usio na mbwembwe. Kila neno ni lazima lichunguzwe ili kuona kama ni lazima liwepo kwenye sentensi au la. Kama si lazima, sherti liondolewe. Nilipata taabu sana kujifunza kuandika namna hiyo

Tafakari: Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

Makala hii, "Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM," niliichapisha kwanza mwaka jana. Soma hapa . Kwa kuzingatia umuhimu wa ujumbe, nimeona niichapishe tena. ---------------------------- Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa. Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake: Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Cham

Makala Yangu Imepita

Blogu yangu ni sehemu ninapoweka chochote nipendacho, hata mambo binafsi, kama kumbukumbu au hata kujifurahisha. Niliwahi kusema hivyo . Leo nina taarifa ambayo imeniletea furaha moyoni. Niliandika siku chache zilizopita kwamba mhariri wa jarida la Monday Development alikuwa ameiomba makala yangu , "What is Development?" Baada ya kuikarabati kidogo, niliipeleka. Ni siku chache tu zimepita, nami nimefurahi kupata ujumbe kutoka kwa msahihisha makala (copy editor) wa jarida hilo. Hakuona kitu cha kusahihisha. Badala yake ameandika: "Thank you for the thoughtful, honest and well-written article." Kwa huku Marekani, uamuzi wa msahihisha makala ni wa mwisho kabla ya makala kuchapishwa. Taarifa kama hii inaniongezea ari ya kuendelea na jitihada ya kuandika vizuri. Ninajua kuwa ninaweza kuandika vizuri kwa ki-Ingereza. Kama andiko langu likawa si zuri, sababu itakuwa ni uvivu au kukosa muda, sio kutojua ki-Ingereza bora kinakuwaje. Wakati moja, mwandishi Jim Heynen

Orijino Komedi Wamtangaza Yesu

Image
Kibao hiki cha Orijino Komedi kiliniacha hoi kabisa tangu nilipokiona mara ya kwanza. Mimi ni m-Katoliki. Kila ninapokiangalia kibao hiki, naishiwa nguvu, kwa jinsi Orijino Komedi wanavyoimba na kukatika. Ni balaa babu kubwa. Papo hapo wanawasilisha ujumbe kwa namna isiyosahaulika. Najikuta nikisema Mungu asifiwe kwa vipaji alivyowajalia Orijino Komedi. Nashukuru kwamba miaka zaidi ya kumi iliyopita niliamua kuanza kumtafakari Yesu mimi mwenyewe. Ninaamini kwa dhati kuwa, kwa jinsi alivyokuwa karibu na watu na pia mpenda michapo, Yesu angeafiki jinsi Orijino Komedi wanavyotangaza neno lake kwa huo mtindo wao wa kuyaruka majoka. Nawashukuru sana Orijino Komedi kwa kuleta neno la Yesu kwa namna hii ya kuvutia na kugusa moyo.