Saturday, March 5, 2011

Tafakari: Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

Makala hii, "Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM," niliichapisha kwanza mwaka jana. Soma hapa. Kwa kuzingatia umuhimu wa ujumbe, nimeona niichapishe tena.
----------------------------

Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa.

Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:

Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe. (Ukurasa 61)

Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii:

Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi! (Ukurasa 66)

Ni wa-Tanzania wangapi wenye utamaduni wa kusoma vitabu? Ni wangapi wanaosoma vitabu vya Mwalimu Nyerere? Ni wazi kuwa umbumbumbu miongoni mwa wa-Tanzania ni neema kwa CCM.

4 comments:

Fadhy Mtanga said...

Prof Mbele,
Awali ya mengine nigependa kuchukua fursa hii kukushukuru na kukupongeza kwa yale maandishi yako yenye kufikirisha.

tukija kwenye usomaji wa vitabu, nakumbuka kipindi kama hiki mwaka jana tulijadiliana sana (sipendi kusema tulibishana) na bwana Katu hapa hapa jamvini kwako.

kwa hakika, ningali nikisema kuwa Watanzania siyo wasomaji wazuri wa vitabu. tunapenda kusoma tu yale mambo mepesi mepesi. wiki iliyopita nilikuwa katika mazungumzo na rafiki yangu mwanafunzi wa shahada ya kwanza mwaka wa tatu. nilishangazwa sana pale aliponiambia hafahamu Dowans ni nini. hafahamu lolote juu ya mambo yanayoendelea nchini sasa. lakini nikaamua kubadili mada haraka na kuanzisha 'stori' za muziki wa bongo fleva, Marekani na filamu. rafiki yangu alikuwa mjuzi sana.

ninachotaka kusema ni nini? kwa kiasi kikubwa sana sisi ndiyo vijana wa kizazi hiki.

miaka minne iliyopita wakati nikianza kublog, nilipata kuyasoma masimulizi ya bwana mmoja aitwaje Born Again Pagan. kwa hakika nilivutiwa sana na masimulizi ya vijana wa kipinzi hicho wakiwa wanafunzi wa UDSM kina Sita, Museven, Shivji na wengineo. wale walipenda kusoma.

asubuhi ya leo nilikuwa nikisoma habari kumhusu William Mkufya. nikagundua kuwa yeye alikuwa akifanya kazi kiwanda cha kutengeneza balbu lakini akiutumia muda wake wa ziada kujisomea vitabu vya fasihi na falsafa. lakini naamini Prof umemsoma vema Mkufya kwenye 'Ziraili na Zirani' pengine utakubaliana nami kuwa Mkufya ni mmoja wa wanafalsafa wazuri wa Kitanzania.

hapa nataka kusema nini? nataka kuzungumza juu ya jamii yetu isiyojisomea kiasi kwamba hata mambo tunayoyajadili kwenye mitandao ya jamii ni yale mepesi mepesi. leo hii ukiandika 'status' ya kuchambua yale yanayoendelea Afrika Kaskazini, michango itakuwa michache sana, tena michango mizito utaipata kutoka kwa watu wa umri wenu. ila ukiandika status ya kipuuzi, labda mambo ya kingono ngono hukosi maoni mia moja. sisemi tusiandike haya, nami huyaandika sana. nasema yawe ni sehemu ndogo sana ya yale ya msingi tuyaandikayo.

lakini jamii itaandika nini cha msingi endapo haitaki kusoma mambo ya kufikirisha?

tukirudi kwenye kitabu cha Mwalimu Nyerere, ni moja ya vitabu nisivyochoka kuvisoma. ukikisoma kwa makini, na endapo wewe ni mzalendo wa kweli utaumia kuoona namna hata mwalimu alivyokuwa akisikitishwa na namna mambo yalivyokuwa yakiendelea. hata kuna wakati akatumwa 'kisanii' akaiwakilishe serikali kwenye maziko ya kiongozi mmoja huko Ulaya. aliporudi akakuta mambo ndivyo sivyo na hakupewa majibu yaliyomridhisha hadi anapokiandika kitabu.

kimsingi, Mwalimu alishachoshwa na mwenendo wa CCM. sikuona ajabu mwaka 1995 Mwalimu alipompigia kura mgombea ubunge wa NCCR kwenye jimbo lake.

Prof Mbele, nimeandika sana. pengine tu niseme, CCM si kile chama cha wakulima na wafanyakazi kilichozaliwa 1977.

malkiory said...

Nakumbuka Nyerere aliwahi kusema upinzani wa kweli utatoka ndani ya CCM,jambo ambalo ni dhahiri sasa. Dr. Slaa alifanyiwa mizingwe pale Karatu na CCM kwenye kura za maoni, kimsingi yeye alimshinda tena kwa kishindo Patrick Qorro, lakini chakushangaza ni kwamba CCM wakamtangaza Patrick Qorro kama mshindi. Hili jambo lilipingwa vikali na wananchi wa Karatu, wakamshauri Slaa kujiunga na CHADEMA, Slaa iliitikia wito wa wana Karatu na mwishowe kwenye uchaguzi alishinda tena kwa kishindo kupitia Chadema.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Kama hatua ya kwanza, mimi napendekeza CCM wapitishe Azimio kwamba kitabu cha Mwalimu Nyerere cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania ni LAZIMA kisomwe na kila mwanachama wa chama hicho kuanzia MAKADA hadi wakuu wa mashina na wanachama walio chini yao.

Wakikisoma kitawashtua na pengine kuwaonyesha ni wapi na lini chama chao kilipoanzia kwenda mrama; na muhimu zaidi nini cha kufanya!

Fadhy - maelezo na hoja nzuri !!!

John Mwaipopo said...

tofauti na idadi kubwa ya watanzania (hasa waliomo madarakani), mie humtazama nyerere katika sura zake mbili. sura ya kufaulu na sura ya kufeli kwake. inapokuja kufeli kwake huwa siwi na kigugumizi wala kwikwi. nasema yaliyomo kinagaubaga.

lakini leo tunamuongelea katika kufaulu. katika kulisema hili alifaulu. na ninadhani pia aliokuwa anawaambia walimuelea sana tu pengine kuliko sisi ambao hatukuwa tukiambiwa. kinachoendelea ni KIBURI tu na si vinginevyo.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...