Wednesday, March 16, 2011

Eti Wananchi Msiwasikilize Wapinzani

Kuna mambo mengi katika siasa Tanzania siku hizi. Katika hali ya ushindani wa kisiasa uliopo, mara kwa mara tunawasikia hao wanaoitwa viongozi wetu wakisema, pengine kwa jazba, kuwa wananchi msimsikilize fulani au msiwasikilize watu fulani. Wanaotajwa hasa ni wapinzani. Wananchi wanaambiwa wasiwasikilize wapinzani.

Kiongozi wa kweli, mwenye busara na ufahamu, hawezi kutoa kauli za namna hiyo. Kila mtu ana haki ya kusikiliza mawazo mbali mbali, yawe vitabuni, magazetini, au kwenye mikutano ya hadhara. Haki hii inapaswa kutambuliwa, kutetewa na kuheshimiwa. Yeyote anayesemekana kuwa ni kiongozi anapaswa kufahamu hilo.

Pamoja na kwamba ni haki ya kila mtu, vile vile ni sehemu ya uhuru alio nao binadamu. Kila mtu ana uhuru wa kutafuta maoni, mawazo na mitazamo ya wengine katika masuala mbali mbali. Ana uhuru wa kusoma vitabu na magazeti, au kusikiliza redio na televisheni, au kusikiliza hotuba kwenye mikutano ya hadhara.

Zaidi ya suala la haki na uhuru, kuna suala la wajibu. Wananchi wana wajibu wa kufahamu yanayoendelea nchini mwao. Ni lazima wajibidishe kutafuta taarifa, mitazamo na uchambuzi mbali mbali kuhusu masuala ya nchi yao na dunia kwa ujumla. Bila hivyo, wananchi hao watakuwa ni wajinga na maamuzi yao yatakuwa ni ya kijinga na pengine ya hatari kwa nchi yao. Kuweka vizuizi au mipaka, kwamba tuwasikilize watu fulani tu au mitazamo ya aina fulani tu ni kukiuka wajibu. Kutafuta elimu ni wajibu wa kila binadamu mwenye akili timamu.

Kwa kuzingatia hayo, kila ninapowasikia hao wanaoitwa viongozi wakiwaasa wananchi eti wasiwasikilize watu fulani, najiuliza kama tuna viongozi au la. Na kama kuna wananchi wanaoafiki maelekezo hayo yasiyo na mantiki wala tija, ni wazi kuwa bado tuna njia ndefu, na labda niseme tunaelekea kubaya, kwa kuendekeza ujinga.

Kilipopigwa marufuku kitabu cha Hamza Njozi kuhusu mauaji ya Mwembechai, nilifanya juhudi kutetea haki ya mwandishi na nilipinga kitendo cha kupiga marufuku kitabu kile. Hamza Njozi mwenyewe, kwenye utangulize wa kitabu chake kilichofuata alinishukuru kwa msimamo wangu.

Msingi huu huu wa kutetea uhuru na haki ndio nautumia katika kuwashutumu hao wanaoitwa viongozi, ambao wanawaasa watu wasiwasikilize watu fulani. Kitu muhimu ni kila mtu mwenye fikra au wazo apewe fursa kamili ya kujieleza, na wenye kupinga nao wapewe fursa kamili ya kutoa hoja zao. Kuhusu kitabu cha Njozi, msimamo wangu ulikuwa kwamba wasiokubaliana naye, waandike vitabu vyao. Kwa njia hiyo tutaelimika sana.

4 comments:

emuthree said...

Unajua umenikumbusha hekima za babu yangu siku moja alisikia hayo maneno ya kukataza watu wasitoe maoni yao eti yataleta uchochezi, babu yangu akaniambia;
'Hawo ni wale wenye shati lililochafuka kwa matope, hawataki kumabiwa shati ni chafu, wanataka waambiwe shati lina madoa-doa, na ukitaka akupende zaidi umwambie shati lako limependeza na hayo madoadoa...!
Profesa, uongozi umekuwa ni `ajira' sio wito...na wengi wanaogopa sana kuwa kiti alichokikalia , akiinuka tu kitaanguka, ...hata kama ataambiwa kuwa kiti hicho kinatengenezeka, hebu inuka kidogo kitengenezwe, atasema kwanini, mbona nimekalia, hakina matatizo...tatizo kubwa ni ubinafsi!
Lakini ubinfasi huo wa nini wakati kiongozi kaajiriwa na mwananchi ambaye ni mpiga kura, leo hii mwajiri wako unampangia masharti kuwa usimsikilize yule, usifanye hivi...bosi wako leo hana maana!
Labda tuhitimishe kwa kusema `mengine tunajitakia wenyewe, kama mtu tumemuajiri wenyewe, kwanini atunyanyase...!'

Mbele said...

Kweli usemavyo, kwamba uongozi, badala ya kuwa ni uongozi, umekuwa ni ajira.

Kwa wale wanaofuatilia elimu, inaeleweka kuwa uongozi unaendana na kitu kinachoitwa "emotional intelligence." Sijaona tafsiri yake kwa ki-Swahili, ila naweza kutafsiri kama akili hisia.

Ni akili inayomfanya kiongozi kuwa na ushawishi mbele ya umma, anayeleta mshikamano katika jamii, msuluhishi, na anayeweza kuwahamasisha watu kwa namna ya kuwavutia kwa mawazo yake, na kwa jinsi yeye mwenyewe anavyokuwa ni mfano wa kuigwa.

Sasa fananisha na hao tunaowaita viongozi leo.

Christian Sikapundwa said...

Profesa nadhani kuna semi nyingi zinasemwa na watu waoga,kauli ya kuwaambia watu wasiwasikilize wapinzani,ni kauli ya uoga,ni kama vile kuna kitu hupendi watu wakisikie lakini kuna mtoto anasema kwa sauti,wengine wanamziba mdomo kwa mkono.

Mfano huo ni sawa na hao wanaotumia muda wao wa kuwaambia watu wasiwasikilize wapinzani.

Kelele hizo zina wasaidia wapinzani kukaza buti baada ya kugundua udhaifu katika uongozi labda.Hasa kama hawata zibiti mfumuko wa bei za bidhaa muhimu,Rais awe mkali kidogo kwa wabadhirifu na wnaokiuka maadili ya uongozi,vijana watafutiwe ufumbuzi wa kulegeza ugumu wa maisha kwa kuwapa mikopo yenye masharti nafuu.

Unafikiri waliosema Mbanga na Mungu walikosea,ni kweli kabisa wapinzani wanawachanganya sana viongozi ambao wameyasahau waliyo wa ahidi wakati wa kuomba kura.

Mbona hii ni moja mambo yatakolea katika kikao kijacho cha bunge.Profesa Ijumaa njema.

Simon Kitururu said...

Hii nayo kali! Ukizingatia waowenyewe inasemekana PINDA na Magufuli wanapingana kwa hiyo nin wapinzania! ndani ya CCM hiyohiyo!

Kwa hiyo maana yake asikilizwe PINDA tu kwa kuwa ndiye WAZIRI MKUU?

Nimewaza tu kwa sauti!:-(

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...