Monday, March 7, 2011

Uandishi Bora wa ki-Ingereza

Suala la uandishi bora kwa ki-Ingereza limenifikirisha kwa miaka mingi na bado ninalifikiria. Nilipokuwa kijana, nilidhani kuwa uandishi bora wa ki-Ingereza ulihitaji matumizi ya maneno magumu na mbwembwe katika miundo ya sentensi. Kwa vile nilipata bahati ya kujifunza ki-Latini, nikiwa shule ya seminari, nilikuwa na uwezo wa kuyafahamu maneno mengi magumu ya ki-Ingereza, kwani asili yake ni ki-Latini.

Imani yangu hii ilikuja kugonga mwamba nilipokuwa nasomea shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Hapo nilikumbana na profesa Harold Scheub, ambaye alikuwa mkali kama mbogo katika suala la uandishi kwa maana kuwa alikuwa anataka uandishi unaotumia lugha nyepesi, kama ilivyoelezwa katika kitabu cha Elements of Style kilichotungwa na William Strunk na E.B. White. Huu ni uandishi usio na mbwembwe. Kila neno ni lazima lichunguzwe ili kuona kama ni lazima liwepo kwenye sentensi au la. Kama si lazima, sherti liondolewe.

Nilipata taabu sana kujifunza kuandika namna hiyo ya kutumia maneno yanayohitajika tu, tena yawe ya kawaida, bila mbwembwe. Sio mimi tu, bali kwetu wanafunzi wote ilikuwa ni kilio na kusaga meno.

Nilipopata jukumu la kufundisha uandishi bora wa ki-Ingereza hapa chuoni St. Olaf, nami nilianza tangu mwanzo kusisitiza hayo niliyojifunza kwa Profesa Scheub. Wakati huo huo, katika kuendelea kujibidisha katika kujifunza, nilitambua kuwa ni kweli huo ndio uandishi unaohesabiwa kuwa uandishi bora. Kwa mfano, ninajifunza mengi kutoka kwa mwandishi Ernest Hemingway, kama nilivyoelezea hapa.

Sasa basi, katika darasa langu la uandishi bora wa ki-Ingereza, huwa nawapa wanafunzi baadhi ya maandishi yangu ambayo yamechapishwa, ili wayachunguze na kuona ni vipi wanaweza kuyarekebisha ili yawe bora zaidi. Kwa mfano, nawapa insha yangu iitwayo "Do You Have an Accent?"

Insha hii imeandikwa vizuri. Hata walimu wengine wa ki-Ingereza wameipenda. Kwa mfano soma hapa. Lakini najua kuwa mtu makini akiichunguza zaidi, ataona vipengele ambavyo vingeweza kuboreshwa. Ndio maana nawapa wanafunzi wangu insha hii ili wajaribu kuvigundua vipengele hivi na kuvirekebisha. Ni zoezi ambalo linafaa kwa yeyote anayedhani anaifahamu lugha ya ki-Ingereza. Mimi mwenyewe nimegundua vitu yapata nane ambavyo vinahitaji kurekebishwa ili insha iwe bora zaidi. Hebu nawe iangalie insha hiyo kwa makini: "Do You Have an Accent?".

5 comments:

emuthree said...

Duh, profesa, mimi nawaza mbali sana na kufikiri jinsi hazina zetu zinavyopotelea nje, jinsi utaalamu wetu unavyowafaidisha wengine, na...
Watu kama nyie ni hazina ya taifa hili, na nani anayefadika na hazina hiyo, kama sio wenzetu.
Najiuliza mara nyingi, tunaomba misaada nje, hata ya walimu, wahasibu wataalamu mbalimbali, lakini wapo, wanaishi nje wanasomesha wanafanyakazi nje, sisi tunatumia mehala mengi kuagiza. Labda ndio hivyo, `kufa kufaana'...kila mtu na riziki yake!
Nashukuru kwa darasa lako hilo kuwa lugha sio `misamiati migumu' lugha ni kufikisha ujumbe kwa walengwa kwa lugha rahisi wanayoielewa. Watu wanafikiria kujua kiingereza ni kutoa `maneno' magumu...
Nashukuru sana mkuu, ooh , profesa, kila kitu umekiweka wazi.
Natafuta muda niwasiliane na wewe hasa kuhusu utungaji, na uchapaji wa vitabu...pindi nikiwa tayari nitawasiliana na wewe kama hutojali!

Mbele said...

Shukrani emu-three, kwa mawaidha yako. Kwa uzoefu wangu, ni kuwa hao wa-Marekani ninaowafundisha wanaheshimu ujuzi wangu kwa dhati.

Kabla sijaja hapa Marekani, nilikuwa nafundisha Tanzania, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1976. Enzi zile, wa-Tanzania walikuwa wanathamini elimu kwa dhati, sio hizo njia za mkato, dezo na ufisadi wanazotafuta wengi.

Hatimaye nilikuja kusomea shahada za juu huku Marekani, 1980-86. Nilijiandaa kwa kila hali, ili wakati wa kurudi Tanzania, niweze kutoa utaalam wa hali ya juu kabisa.

Nilirejea nchini nikiwa na shahada hizo na shehena kubwa ya vitabu. Wa-Tanzania hawakujali hayo, bali waliniuliza kama nimeleta "pick up." Kwa vile sikuwa nimeleta pick up, bali vitabu, waliniona nimechemsha. Habari hii nimeieleza tena na tena.

Hii ndio hali ya Tanzania ya leo. Taaluma haithaminiwi kama zamani. Kwangu hii ni kero, na ninaridhika kuwafundisha wa-Marekani.

Hata hivi, sijawaweka kando wa-Tanzania. Vitabu ninavyoandika, ambavyo ndio hao wa-Marekani wanavisoma, nahakikisha kuwa ninavipeleka Tanzania pia. Vinapatikana kule.

Ninangojea nione kama kuna wenye moyo wa kutaka kujifunza kutoka kwangu. Wakisoma hivi vitabu wakawasiliana nami ili kutaka kujua zaidi, nitaamini kuwa wana mwamko wa kuthamini ninachojua. Nami nitakuwa nao bega kwa bega. Huu ndio mkakati niliouweka.

Vile vile, kwa miaka mitatu mfululizo, nimefunga safari kwenda Tanzania, kuendesha warsha. Matangazo niliweka sehemu mbali mbali, hadi kwa Michuzi.

Lakini mahudhurio ni hafifu. Mwaka jana, nilitangaza warsha kufanyika Tanga na Arusha, nami nilienda. Hakuna m-Tanzania hata moja aliyehudhuria.

Ni kinyume na hapa Marekani, kwani hapa watu wananialika wenyewe, na wanafanya matangazo wenyewe, nami nakwenda tu kutoa warsha au mihadhara.

Kwa maana hiyo, nina haki ya kuwa na hisia kuwa wa-Tanzania hawahitaji utaalam wangu. Kwa hivyo, ninajipanga kuendesha warsha zangu nchi zingine, kama vile Kenya.

emuthree said...

Profesa, maneno yako yamenitia uchungu sana, na uliyosema ni kweli kabisa, hii ndio Tanzania ambayo vijana wetu, wanaojiita taifa la leo, ambao kila kukicha wanaoimba na kutamani `bongo 'fleva'...simaanishi muziki, naamanisha `starehe'
Je ifanyike nini ili Watanzania tuamuke ili tujue kuwa `umasikini wetu' sehemu kubwa ni kutokana na adui ujinga(kutokupenda kusoma)...ni swali ambalo nimekuwa nikijiuliza sana, kwasababu kama kuna tatizo, kunatakiwa kuwe na njia ya kulitatua.
Nikagundua usemi wa jamaa yangu aliniambia kuwa watawala wetu waligundua kuwa `ni rahisi sana kuwaongoza raia `wajinga, kwani unaweza kuwafanya utakavyo. Usemi huu unaweza ukawa ndio moja ya sababu ya `kutokupenda kusoma' kwa Watanzania walio wengi. Je ina maana Watanzania wenyewe hawana akili ya kugundua hili. Jibu ni kuwa `maji hufuata mkondo'...familia zilizoerevuka zimegundua hili ndio maana wale wenye angalau kipato cha kuridhisha kidogo wamadiriki hata kuwapeleka watoto wao shule za nje, ili kesho na kesho kutwa kizazi chao kiwe bora!
Profesa, nitakuwa nafuatilia mada zako kwa ukaribu zaidi, kwaninimegundua kuwa `nina mwalimu muhimu ambaye sihitaji hata kwenda darasani.
Ngoja niishie hapa kwa leo, nikaandike chochote kwenye blog yangu. TUPO PAMOJA PROFESA

Mbele said...

emu-three, shukrani tena kwa ujumbe wako. Ni kweli, hali inasikitisha.

Tuendelee kuwasiliana na kubadilishana mawazo. Ninapangia kuja Tanzania katikati ya mwezi Julai na nitakuwepo huko kwa wiki kadhaa. Tutafutane, tuweze kuonana, Insh'Allah.

emuthree said...

Insha-Allah Profesor, nitafurahi sana, siku nikikutana nawe. Karibu sana nyumbani kwenu!

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...