Wednesday, March 2, 2011
Orijino Komedi Wamtangaza Yesu
Kibao hiki cha Orijino Komedi kiliniacha hoi kabisa tangu nilipokiona mara ya kwanza. Mimi ni m-Katoliki. Kila ninapokiangalia kibao hiki, naishiwa nguvu, kwa jinsi Orijino Komedi wanavyoimba na kukatika. Ni balaa babu kubwa. Papo hapo wanawasilisha ujumbe kwa namna isiyosahaulika. Najikuta nikisema Mungu asifiwe kwa vipaji alivyowajalia Orijino Komedi.
Nashukuru kwamba miaka zaidi ya kumi iliyopita niliamua kuanza kumtafakari Yesu mimi mwenyewe. Ninaamini kwa dhati kuwa, kwa jinsi alivyokuwa karibu na watu na pia mpenda michapo, Yesu angeafiki jinsi Orijino Komedi wanavyotangaza neno lake kwa huo mtindo wao wa kuyaruka majoka.
Nawashukuru sana Orijino Komedi kwa kuleta neno la Yesu kwa namna hii ya kuvutia na kugusa moyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
5 comments:
Kitu chochote tunachofanya watu wa Mungu ikiwa ni pamoja na kwaya, lazima kimtukuze Mungu, na pia hata wasioamini wasiwe na neno kwacho tunachokifanya. Maandiko yanasema, “Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni”, Mathayo 5:20.
Iwapo watu wasioamini, wanaweza kufanya mambo mazuri yanayohusiana na imani zao kwa kukwepa kukwaza wengine, si zaidi sana sisi tunaosema kuwa tunamjua Mungu? Iwapo hatutaweza kuwazidi hao, maandiko yanasema hatutaurithi kamwe ufalma wa Mungu. Kama watu wa Mungu tunapaswa kuliangalia hilo.
Watu wengi wenye nia ya kumtafuta Mungu, wanashindwa kuuamini wokovu, kwa sababu tu ya mambo yetu mengi tunayoyafanya katika ucha Mungu wetu ambayo hayana ushuhuda. Mambo hayo ni pamoja na hizo kwaya zinazoimbwa nyakati hizi n.k. Siku hizi nyimbo za INJILI tunazozitunga tunazitunga kwa kutazama tu jinsi sisi tutakavyopendezwa kwazo, hatutazami jinsi wasioamini watakavyoziona na kutuelewa!. Hatuangalii upande wa pili, na hiyo ndiyo sehemu ambayo shetani anapata goli kwetu.
Kuna namna nyingi tu na nzuri za kumwimbia Mungu, na kila mtu hata asiyeamini akaweza kusema kweli kuna Mungu eneo hilo. Namna hizo si lazima ziigizwe kwa mtindo wa tamaduni yoyote duniani. Tukiwa katika Roho katika kuimba, tunaweza kufanya namna zetu za kuimba zikawa moja duniani kote. Kinachotatiza sasa hivi ni kwa sababu, watu wanampenda Mungu na hapo hapo bado wanaipenda dunia, namna hiyo lazima tutachanganya tu, dunia na ya Mungu.
Nakumbuka kuanzia katikati ya miaka ya themanini na kuendelea, kulikuwa na kwaya moja ya Ulyankurlu Tabora, nyakati hizo nilikuwa mdogo bado, kuna ambao waliipenda sana ile kwaya, na waliinunua kanda yao ya kaseti.
Kununua kwa ile kanda hakukuwa kwa sababu ya kuburidika, bali kwa sababu ya ujumbe na umakini wa kiroho uliokuwemo katika kanda ile.
Japo kuna ambao walikuwa si watu wa Rohoni nyakati hizo, lakini kila walipokuwa wasikia walikuwa wanaguswa! Kutokana na jinsi nilivyokuwa mtu wa dini, ilikuwa si rahisi kuikubali kanda ile na nyimbo zake kama ingekuwa kama zilivyo kanda za nyimbo za nyakati hizi zenye vionjo vya miziki ya kidunia.
Kwaya ile kwa kweli kwa wale wanaoifahamu, watanielewa ninachokielezea, ilikuwa ni kwaya ambayo haikuwa na vionjo wala utamaduni wowote wa kidunia, lakini ilipendeza na iliweza kuliza watu, hasa kwa wimbo moja uliokuwa unajulikana kwa jina la, “Wakati ule wa Nuhu, watu walimwasi Bwana”.
Je, nyakati hizi ndiyo haiwezekani kuwa na kwaya kama zile? Je hatuoni kuwa tunazidi kuporomoka na kuingia anga jingine kiroho?
Ukiangalia hali halisi, inaonesha kuwa watu wasioamini wanaufahamu sana wa mambo ya Mungu kuliko sisi tunaosema tumeokolewa. Tunapingana na kila Neno jema la Mungu na kuweka ya kwetu wenyewe.
Ninavyofahamu mimi kuimba, ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu, na wala si kwa ajili ya kuwafurahisha wanadamu wanaokuwa wanasikiliza au kuona kimwili. Kama ni kuwafurahisha hao wanadamu, basi ni kuwafurahisha kwa kuwafanya kufikia toba kwa nyimbo tunazoziimba. Nyimbo zinapaswa kuheshimiwa na kuogopwa na watu wasioamini kama wanavyoyaheshimu na kuyaogopa mahubiri ya watumishi wa Mungu. Iwapo watapata neema ya kusikiliza basi wafikie toba kama vile wamesikia mahubiri.
Mahubiri mengine ya watumishi wa Mungu, yanaheshimiwa na kuogopwa kusikilizwa hata na watu wanaodhaniwa kuwa ni waumini wazuri wa imani hiyo waliopo. Wanayaogopa wasije wakayasikia na kuelewa, na wakabadili misimamo yao ya mafundisho yao ya awali. Iwapo katika mahubiri ya Neno la Mungu kuna nguvu kiasi hicho, kwa nini nyimbo zetu za injili nazo zisiwe na nguvu ya Mungu kama ilivyo katika mahubiri hayo?. Bila shaka kwaya zetu na waimbaji wote wa nyimbo za injili wangekuwa hivyo, shetani asingekuwa na nafasi kabisa ya kulichezea Kanisa la Mungu.
JE ULISHAWAHI SIKIA WIMBO WA KAYA IITWAYO MUUNGANO UNAOITWA NATEMBEA NIKIWA NI MAREHEMU?
Nitaitafuta halafu nitakutumia CD yao kama hauna.
Mwalimu Mbele;
Japo mimi si Mhafidhina wa mambo ya kidini, nilikuwa pia na wasiwasi kuhusu uchezaji wa aina hii, na Mcharia pengine kaelezea vizuri na kwa ufasaha zaidi. Kama unavyojua, ninaendesha pia blogu ya nyimbozadini.blogspot.com ambayo imetokea kupendwa sana (ina watembeleaji zaidi ya milioni moja sasa!). Wakati naanza, na kabla sijajua vizuri kipi ni kipi, nilikuwa nikiweka kila aina ya video huko. Nakumbuka kuna wakati niliweka video ya mwimbaji mmoja wa kike aliyekuwa anakata mauno kama vile wacheza shoo wa Kongo. Basi nilishambuliwa sana mpaka nikaamua kuitoa video ile. Hoja kubwa ilikuwa ni ile ile iliyozushwa na Mcharia hapa. Watu walioko nje ya Ukristo wanaona na kujifunza nini wakiangalia miziki na uchezaji wa aina hii? Kweli hii ndiyo njia sahihi ya kueneza neno la Mungu? Walokole wao wanaweza kwenda mbali zaidi na kudai moja kwa moja kwamba hii ni kazi ya shetani !!!
Hawa Orojino Komedi pia wana video yao moja ambayo wamecheza huku wakisindikizwa na wimbo mmoja mzuri wa kwaya ya Mabibo External kama sikosei. Katika wimbo huo wanaume hawa wanaonekana wamejifunga vitenge na wengine wanaonekana wameweka matiti ya bandia.
http://www.youtube.com/watch?v=hJzo7v8RUGg&feature=related
Nimeangalia baadhi ya maoni machache katika video hii na baadhi ya watu wanafikiri kwamba lengo la Orijino Komedi katika video hii ni kueneza na kutukuza ushoga. Ngoja tuone maoni ya wadau wengine wanasemaje kuhusu suala hili. Lakini pia lilishawahi kujadiliwa kwa kina kule Strictly Gospel.
@Mcharia: Nyimbo za Kwaya ya Barabara ya 13 Ulyankulu Tabora zinapatika katika blogu yangu ya nyimbozadini.blogspot.com juu kabisa. Hizi nyimbo ziliimbwa wakati uimbaji wa nyimbo za injili haujageuzwa na kuwa biashara na tofauti unaweza kuiona. Ni nyimbo ambazo ukizisikia hata sasa ni lazima uache ulichokuwa unakifanya na kutega sikio. Ukiipata hiyo CD uliyoahidi kumtumia Profesa Mbele, naomba nami unitumie nyimbo hizo kupitia prfesamatondo@gmail.com ili niziweke katika blogu ya nyimbozadini.blogspot.com. Nitashukuru sana !!!
Mungu Aendelee kutubariki !!!
Ndugu Mcharia, asante kwa changamoto yako. Naona umegusia mambo mengi ya kufikirisha, nami nitaendelea kuyatafakari. Na papo hapo nitashukuru kusikia maoni ya wengine, kama haya aliyotoa Profesa Matondo au mengine.
Video hii ya Orijino Komedi nimeipenda tangu nilipoanza tu kuiona, nadhani mwaka jana. Tangu mwanzo niliwazia kuiweka hapa kwenye blogu yangu. Inanigusa kwa namna nzuri niliyoelezea, ya kunikumbusha neno la Yesu kwa mtindo unaonivutia na usiosahaulika.
Wametoa muhtasari wa mambo na matukio fulani yaliyomo katika Biblia. Kwa upande wangu, wanaigusa akili yangu na kunifanya nikumbuke maandishi husika, na pia niwe na motisha ya kwenda kuyasoma tena.
Na kila nitakapokuwa nasoma maandishi hayo katika Biblia, nitakuwa nakumbuka haya majoka ya Orijino Komedi. Wamenifungulia mlango wa kuyapenda maandishi ya Biblia kwa namna iliyo tofauti na zamani.
Orijino Komedi, kwa mtazamo wangu, wamefanya kazi nzuri ya ufundishaji. Somo linaingia vizuri.
Kama nilivyogusia hapa mwanzo, masuali na mawaidha yenu ni mengi na yanahitaji tafakari pana na mchango wa watu wengine. Ninashukuru kwa changamoto yenu, nami nitaendelea kutafakari.
Napenda tu niongeze kuwa katika juhudi yangu ya kujifunza habari za Yesu, nimetambua kuwa jadi tunayotumia ya kuwafanya watoto wamwogope Mungu au wamwogope Yesu si jadi sahihi. Yesu mwenyewe alipozungukwa na vitoto halafu mitume wakataka kuvifukuza vitoto hivyo, kwa kudhani kuwa vilikuwa vinaleta bughudha na kero kwa Yesu, Yesu aliwaambia waviache vitoto viendelee kujimwaga.
Lakini sisi tunaendekeza hofu. Neno la Mungu tumeliingiza kwenye mkondo wa kuwatia watu hofu. Nawasikia wahubiri wengi wanavyokoroma na kunguruma, na kuendeleza hofu. Sitaki kuwahukumu, maana labda nao hii ni njia yao ya kuwa karibu na Mungu.
Mimi nami nimeanza kujitafutia njia yangu. Na njia yangu hii ni ile ya kuondoa hofu na kuanza kujisikia raha mbele ya Yesu. Ni hii raha ndio inanifanya niafiki jinsi Orijino Komedi wanavyohubiri.
Kuna jambo jingine ambalo nalo ni muhimu. Kuna ukweli usiopingika kuwa kila mwanadamu anaposikia au kusoma taarifa, anaposoma hadithi, shairi au utungo mwingine wowote, au anapoangalia filamu, au video kama hii ya Orijino Komedi, anaitafsiri kwa namna tofauti na mtu mwingine. Inamgusa kwa namna tofauti na inavyomgusa mtu mwingine.
Mtu mmoja anapoangalia hii video ya Orijino Komedi anaweza kuguswa zaidi na maneno, au zaidi na mtindo wa kuruka majoka, au tukio hili au lile. Kila mtu anafanya mchanganyiko tofauti wa hayo mambo katika kuiangalia na kuichukulia video hiyo. Mwingine atazingatia zaidi kitu fulani, akafurahi, na mwingine zaidi kitu tofauti akaudhika, na kadhalika.
Kusoma au kusikiliza habari ni kitendawili kikubwa kwa jinsi kinavyozaa matunda mbali mbali akilini na mioyoni mwa wasomaji. Tafsiri zinakuwa nyingi na tofauti, na hili halikwepeki. Kwa hivi, tuna kazi kubwa ya kuendelea kubadilishana mawazo, ili mradi tuzingatie tu kila mtu kuwa mkweli.
http://strictlygospel.wordpress.com/2009/02/26/aina-gani-ya-muziki-wa-injili-unafaa-makanisani/
Shukrani Profesa Matondo, kwa kutuletea kiunganishi hiki hapa. Naona mjadala kule ulikuwa mzito.
Nikirudi tena kidogo kwenye ujumbe wa Ndugu Mcharia, napenda kusema kuwa naamini hao Orijino Komedi wamefanya kazi ya Mungu kwenye hii video yao, sio tu kwa kutangaza neno la Yesu, bali pia kwa burudani.
Wamepewa vipaji na Mwenyezi Mungu vya kutuchekesha. Ni wajibu wao watumie vipaji hivi, kwa manufaa ya wanadamu, kama vile sote tunavyopaswa kutumia vipaji vyetu kwa manufaa ya wenzetu.
Video hii ya Orijino Komedi inaweza kuleta faraja kubwa moyoni mwa mtu mwenye masononeko, kicheko kwa aliyenuna, na ahueni kwa wagonjwa. Utafiti unaonyesha kuwa michapo na vicheko vinachangia katika kuboresha afya na hata uponyaji wa wagonjwa.
Naichukukulia dhana ya kazi ya Mungu kwa mapana sana. Pamoja na masuala ya kueneza imani na kuwafanya watu waamini hiki tunachoita uokovu, naamini pia kuwa kazi ya Orijino Komedi wakiifanya kwa umakini kama wanavyofanya, nayo ni kazi ya Mungu.
Post a Comment