Showing posts with label u-Kristu. Show all posts
Showing posts with label u-Kristu. Show all posts

Sunday, June 4, 2017

Vitabu Vinavyopinga Dini

Ingawa mimi ni muumini wa dini, m-Katoliki, ninapenda kuzifahamu dini zingine. Sijiwekei mipaka. Sina tatizo na watu wa dini tofauti na yangu, wala watu wasio na dini. Ninajifunza kutoka kwao. Mtu unajifunza mengi kutoka kwa watu wenye mawazo tofauti na yako.

Ninasoma vitabu vya dini zingine, kama nilivyowahi kueleza katika blogu hii. Vile vile ninasoma vitabu vinavyohoji au kupinga dini. Fikra za wapinga dini zinafikirisha. Mfano ni kauli ya Karl Marx: "Religion is the sigh of the oppressed creature, the heart of a heartless world, and the soul of soulless conditions. It is the opium of the people."

Ninaipenda kauli hiyo ya Marx kwa kuwa inafikirisha na kusisimua akili. Kuna ubaya gani kwa mtu kuiponda dini namna hii? Kuna sababu gani ya mimi muumini kumchukia mtu wa aina hiyo? Kama vile mimi ninavyotetea haki na uhuru wa kuwa na mawazo yangu, naye ana haki na uhuru wa kuwa na mawazo tofauti na yangu. Ana uhuru wa kujieleza na kusambaza mawazo yake.

Ninavyo vitabu vinavyohoji u-Kristu. Mifano ni Jesus: Prophet of Islam, kilichotungwa na Muhammad Ata Ur-Rahim na Ahmad Thomson; The Gnostic Gospels, kilichotungwa na Elaine Pagels; na The Essential Gnostic Gospels, Including the Gospel of Thomas & The Gospel of Mary, kilichotungwa na Alan Jacobs. Nina vitabu vinavyouhoji u-Islam, vya waandishi kama Ayaan Hirsi Ali na Nawaal el Saadawi. Kuna vingine ambavyo bado sina, ila nitavinunua, kama vile vya Wafa Sultan na Ibn Warraq.

Kama mtu umejengeka katika dini yako na unatambua umuhimu na maana yake, kuna sababu gani ya kuvichukia vitabu vinavyoihoji dini? Jazba au masononeko ya nini, kama si ishara ya udhaifu na ubabaishaji wako mwenyewe? Binafsi, niko imara, na wahenga walisema, kelele za chura hazimzuii ng'ombe kunywa maji.

Fikra zinazohoji dini ninaziona kuwa zenye manufaa. Mimi kama muumini ninazichukulia hizo kama fursa ya kuimarisha imani, sawa na misukosuko inavyomkomaza mtu. Wakristu tunafundishwa uvumilivu, na hii ni njia ya kujipima tuna imani kiasi gani. Kama kawaida, nakaribisha maoni.

Thursday, May 5, 2016

Nimepata Qur'an Mpya

Nimekuwa na kawaida ya kuandika katika blogu hii taarifa za vitabu ninavyonunua, au vitabu ninavyosoma, ingawa siandiki juu ya vyote. Kwa siku nyingi sijafanya hivyo, lakini leo nimeamua kuandika kuhusu Qur'an mpya niliyoipata hivi karibuni, ambayo ni tafsiri ya ki-Ingereza ya Maulana Wahiduddin Khan na Farida Khanam ambaye ni binti yake.

Ninayo nakala nyingine ya Qur'an tangu mwaka 1982, ambayo ni tafsiri ya Abdullah Yusuf Ali. Hii ni kubwa kwa kuwa ina maelezo mengi. Hii mpya niliipata tarehe 28 Aprili, mwaka huu, kutoka kwa Dr. Nadia Mohamed, mzaliwa wa Misri.


Anaonekana amesimama kulia pichani. Nimefahamiana naye zaidi ya mwaka, tangu tuliposafiri kwenda kwenye semina chuoni Leech Lake, ambapo tulipiga hii picha, pamoja na profesa mwingine wa chuo kile.

Dr. Nadia Mohamed ni profesa mwenye shahada ya uzamili katika sheria za ki-Islam na shahada ya uzamifu katika elimu. Nilikuwa nimemwalika kuja kutoa mhadhara katika darasa langu la Muslim Women Writers, na baada ya kipindi ndipo alinipa Qur'an hiyo.

Tafsiri ni mtihani mkubwa, nami nimesema hivyo tena na tena katika blogu hii. Kwa kuwa hii Qur'an niliyopata karibuni ni tafsiri tofauti na ile ya Abdullah Yusuf Ali, ninategemea kufananisha hizi tafsiri mbili kutanisaidia kupata mwanga zaidi kuhusu yasemwayo katika Qur'an.

Ninasoma Qur'an sawa na ninavyosoma misahafu ya dini zingine kwa lengo la kujielimisha. Ninaamini kuwa ni muhimu kwa wanadamu kufahamiana ili tuweze kujenga maelewano miongoni mwetu. Kuzifahamu dini za wengine, tamaduni zao, na lugha zao ni njia ya kulifikia lengo hilo.

Ninapenda kusisitiza hilo, kwani nimeshakumbana na watu wanaodhani au kutegemea kwamba kwa kuwa ninasoma Qur'an, hatimaye nitasilimu. Sioni mantiki ya dhana hiyo. Je, ninaposoma msahafu wa dini ya Hindu, inamaanisha nitaacha u-Kristu niwe m-Hindu? Ninaposoma maandishi ya watu wanaozikana dini, kama vile akina Karl Marx, inamaanisha kuwa hatimaye nitaikana dini? Nimesoma fikra za Karl Marx na wapinzani wengine wa dini kwa zaidi ya miaka 40, na bado mimi ni m-Katoliki.

Friday, April 8, 2011

Nasoma Vitabu vya Dini Mbali Mbali

Kati ya mambo ya manufaa kabisa maishani ni kujielimisha. Nami husoma vitabu kila siku kama njia mojawapo ya kujielimisha. Pamoja na vitabu vya taaluma mbali mbali, hadithi, mashairi, na kadhalika, hupenda kusoma vitabu vya dini.

Nina vitabu vya dini mbali mbali, hasa u-Hindu, u-Islam, na u-Kristu. Nina vitabu kama vile Bhagavad-Gita, Upanishads, Quran, na Biblia. Nina vitabu kuhusu watu muhimu wa dini hizo, kama vile Yesu Kristu, Muhammad na Swami Vivekananda. Vyote hivyo ninavipitia, angalau mara moja moja.

Mimi ni m-Katoliki; habari ndio hiyo. Kwa msingi wa dini yangu, nawajibika kuwajali na kuwapenda wanadamu wote. Yesu alifafanua amri kuu kuliko zote kuwa ni kumpenda Mungu kwa uwezo wetu wote, akili yetu yote, na nafsi yetu yote; kumpenda jirani yetu vile vile, na kuwapenda maadui zetu vile vile. Huu ndio mtihani aliotuachia Yesu.

Sasa kwa vile ukweli ndio huo, ninajiuliza ni njia ipi ya kufuata ili niweze kufaulu mtihani huo. Nimeamua kuwa ni wajibu kujielimisha: kuwafahamu wanadamu, maisha yao, fikra zao, na imani zao. Ni wajibu kuzifahamu dini zao. Naamini tungechangia kujenga mahusiano mema duniani iwapo tungekuwa na utamaduni huu wa kuviheshimu na kuvisoma vitabu vya dini zetu na vile vya dini za wenzetu. Ni muhimu vile vile kusoma vitabu vya wale wasioamini dini, na kuwaheshimu.

Wednesday, March 2, 2011

Orijino Komedi Wamtangaza Yesu



Kibao hiki cha Orijino Komedi kiliniacha hoi kabisa tangu nilipokiona mara ya kwanza. Mimi ni m-Katoliki. Kila ninapokiangalia kibao hiki, naishiwa nguvu, kwa jinsi Orijino Komedi wanavyoimba na kukatika. Ni balaa babu kubwa. Papo hapo wanawasilisha ujumbe kwa namna isiyosahaulika. Najikuta nikisema Mungu asifiwe kwa vipaji alivyowajalia Orijino Komedi.

Nashukuru kwamba miaka zaidi ya kumi iliyopita niliamua kuanza kumtafakari Yesu mimi mwenyewe. Ninaamini kwa dhati kuwa, kwa jinsi alivyokuwa karibu na watu na pia mpenda michapo, Yesu angeafiki jinsi Orijino Komedi wanavyotangaza neno lake kwa huo mtindo wao wa kuyaruka majoka.

Nawashukuru sana Orijino Komedi kwa kuleta neno la Yesu kwa namna hii ya kuvutia na kugusa moyo.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...