Ingawa mimi ni muumini wa dini, m-Katoliki, ninapenda kuzifahamu dini zingine. Sijiwekei mipaka. Sina tatizo na watu wa dini tofauti na yangu, wala watu wasio na dini. Ninajifunza kutoka kwao. Mtu unajifunza mengi kutoka kwa watu wenye mawazo tofauti na yako.
Ninasoma vitabu vya dini zingine, kama nilivyowahi kueleza katika blogu hii. Vile vile ninasoma vitabu vinavyohoji au kupinga dini. Fikra za wapinga dini zinafikirisha. Mfano ni kauli ya Karl Marx: "Religion is the sigh of the oppressed creature, the heart of a heartless world, and the soul of soulless conditions. It is the opium of the people."
Ninaipenda kauli hiyo ya Marx kwa kuwa inafikirisha na kusisimua akili. Kuna ubaya gani kwa mtu kuiponda dini namna hii? Kuna sababu gani ya mimi muumini kumchukia mtu wa aina hiyo? Kama vile mimi ninavyotetea haki na uhuru wa kuwa na mawazo yangu, naye ana haki na uhuru wa kuwa na mawazo tofauti na yangu. Ana uhuru wa kujieleza na kusambaza mawazo yake.
Ninavyo vitabu vinavyohoji u-Kristu. Mifano ni Jesus: Prophet of Islam, kilichotungwa na Muhammad Ata Ur-Rahim na Ahmad Thomson; The Gnostic Gospels, kilichotungwa na Elaine Pagels; na The Essential Gnostic Gospels, Including the Gospel of Thomas & The Gospel of Mary, kilichotungwa na Alan Jacobs. Nina vitabu vinavyouhoji u-Islam, vya waandishi kama Ayaan Hirsi Ali na Nawaal el Saadawi. Kuna vingine ambavyo bado sina, ila nitavinunua, kama vile vya Wafa Sultan na Ibn Warraq.
Kama mtu umejengeka katika dini yako na unatambua umuhimu na maana yake, kuna sababu gani ya kuvichukia vitabu vinavyoihoji dini? Jazba au masononeko ya nini, kama si ishara ya udhaifu na ubabaishaji wako mwenyewe? Binafsi, niko imara, na wahenga walisema, kelele za chura hazimzuii ng'ombe kunywa maji.
Fikra zinazohoji dini ninaziona kuwa zenye manufaa. Mimi kama muumini ninazichukulia hizo kama fursa ya kuimarisha imani, sawa na misukosuko inavyomkomaza mtu. Wakristu tunafundishwa uvumilivu, na hii ni njia ya kujipima tuna imani kiasi gani. Kama kawaida, nakaribisha maoni.
Showing posts with label u-Islamu. Show all posts
Showing posts with label u-Islamu. Show all posts
Sunday, June 4, 2017
Thursday, May 5, 2016
Nimepata Qur'an Mpya
Nimekuwa na kawaida ya kuandika katika blogu hii taarifa za vitabu ninavyonunua, au vitabu ninavyosoma, ingawa siandiki juu ya vyote. Kwa siku nyingi sijafanya hivyo, lakini leo nimeamua kuandika kuhusu Qur'an mpya niliyoipata hivi karibuni, ambayo ni tafsiri ya ki-Ingereza ya Maulana Wahiduddin Khan na Farida Khanam ambaye ni binti yake.Ninayo nakala nyingine ya Qur'an tangu mwaka 1982, ambayo ni tafsiri ya Abdullah Yusuf Ali. Hii ni kubwa kwa kuwa ina maelezo mengi. Hii mpya niliipata tarehe 28 Aprili, mwaka huu, kutoka kwa Dr. Nadia Mohamed, mzaliwa wa Misri.
Anaonekana amesimama kulia pichani. Nimefahamiana naye zaidi ya mwaka, tangu tuliposafiri kwenda kwenye semina chuoni Leech Lake, ambapo tulipiga hii picha, pamoja na profesa mwingine wa chuo kile.Dr. Nadia Mohamed ni profesa mwenye shahada ya uzamili katika sheria za ki-Islam na shahada ya uzamifu katika elimu. Nilikuwa nimemwalika kuja kutoa mhadhara katika darasa langu la Muslim Women Writers, na baada ya kipindi ndipo alinipa Qur'an hiyo.
Tafsiri ni mtihani mkubwa, nami nimesema hivyo tena na tena katika blogu hii. Kwa kuwa hii Qur'an niliyopata karibuni ni tafsiri tofauti na ile ya Abdullah Yusuf Ali, ninategemea kufananisha hizi tafsiri mbili kutanisaidia kupata mwanga zaidi kuhusu yasemwayo katika Qur'an.
Ninasoma Qur'an sawa na ninavyosoma misahafu ya dini zingine kwa lengo la kujielimisha. Ninaamini kuwa ni muhimu kwa wanadamu kufahamiana ili tuweze kujenga maelewano miongoni mwetu. Kuzifahamu dini za wengine, tamaduni zao, na lugha zao ni njia ya kulifikia lengo hilo.
Ninapenda kusisitiza hilo, kwani nimeshakumbana na watu wanaodhani au kutegemea kwamba kwa kuwa ninasoma Qur'an, hatimaye nitasilimu. Sioni mantiki ya dhana hiyo. Je, ninaposoma msahafu wa dini ya Hindu, inamaanisha nitaacha u-Kristu niwe m-Hindu? Ninaposoma maandishi ya watu wanaozikana dini, kama vile akina Karl Marx, inamaanisha kuwa hatimaye nitaikana dini? Nimesoma fikra za Karl Marx na wapinzani wengine wa dini kwa zaidi ya miaka 40, na bado mimi ni m-Katoliki.
Monday, January 4, 2016
Nawazia Dini na Uandishi wa Wanawake wa ki-Islam
Muhula ujao, kuanzia mwezi Februari hadi Mei, nitafundisha kozi mpya hapa chuoni St. Olaf ambayo nimeiita "Muslim Women Writers." Ni kozi ya fasihi kwa ki-Ingereza, ambamo tutasoma maandishi ya wanawake wa-Islam kutoka Bangladesh, India, Iran, Misri, Sudan, Senegal, na Marekani. Taarifa fupi ya kozi hiyo nimeandika hapa.
Wakati huu ninapongojea kufundisha kozi hii katika mazingira ya leo ambamo maelewano miongoni mwa waumini wa dini na madhehebu mbali mbali yanatatanisha, ninajikuta nikiwazia mara kwa mara masuala ya dini. Katika siku zijazo, labda kwa miezi kadhaa, ninategemea kuandika tena na tena katika blogu hii kuhusu dini na kozi yangu.
Nimeshaandika mara kadhaa kuhusu dini. Nimeandika kuhusu umuhimu wa mijadala ya dini, umuhimu wa kuziheshimu dini zote, na nilivyozuru nyumba za ibada za dini nyingine. Sioni mantiki kwa dini yoyote kuwafundisha waumini wake kwamba Muumba anawapenda wao zaidi kuliko watu wa dini nyingine. Msimamo wangu ni kwamba Mungu (Allah) hana ubaguzi.
Ninafurahi na kujivunia kwamba kanisa langu Katoliki linasimama katika msingi huo, kama ilivyodhihirishwa katika ziara na ujumbe wa Papa John Paul wa Pili nchini Nigeria, ziara ya Papa Francis katika msikiti Uturuki, na katika sala ya Papa Francis ya kuuombea ulimwengu. Na zaidi ni kuwa Kanisa Katoliki lina baraza la kujenga maelewano miongoni mwa dini mbali mbali liitwalo Pontifical Council for Inter-religious Dialogue.
Katika kujiandaa kwa kozi yangu, nimekuwa nikiwazia kuwa ingekuwa vizuri kama ningesoma Quran yote. Ninayo Quran takriban tangu mwaka 1982. Nimekuwa nikisoma visehemu hapa na pale, lakini si yote kikamilifu. Ingawa ninafahamu misingi ya u-Islam kiasi cha kuridhisha, wazo la kuisoma Quran linanivutia.
Kuna mambo mengine ambayo nimekuwa nikifanya, kama vile utafiti ili kufahamu misimamo na mitazamo ya wanawake wa-Islam kuhusu u-Islam na nafasi yao katika dini hiyo. Nimeanza pia kuwatafuta wanawake wasomi wa ki-Islam na kujitambulisha kwao, ili waweze kuniongezea elimu kwa manufaa yangu na ya wanafunzi wangu. Ninafurahi kwa mafanikio ya kutia moyo ambayo nimeanza kuyaona.
Nimeandika ujumbe huu kwa kuzingatia kuwa wengi wanaosoma blogu yangu ni waumini wa dini. Wana wajibu wa kuchangia mawazo, hasa wakiona nimepotosha jambo lolote. Kwa muumini yeyote, hili si suala la hiari, bali ni wajibu.

Saturday, June 13, 2015
Nimepata Kitabu "Infidel" cha Ayaan Hirsi Ali
Leo nimepata kitabu Infidel cha Ayaan Hirsi Ali ambacho nilikinunua mtandaoni tarehe 3 Juni. Ayaan alizaliwa Somalia, akakulia Somalia, Saudi Arabia, Ethiopia na Kenya. Kisha alihamia u-Holanzi, ambako aliwahi hata kuwa mbunge.Katika kukua kwake alianza kuhoji malezi ya ki-Islam aliyoyapata, na hatimaye alijitoa katika dini hii na kuwa mtu asiye na dini. Hayo amekuwa akisimulia katika vitabu na mihadhara yake. Kitabu chake cha kwanza, ambacho sina, ni The Caged Virgin: An Emancipation Proclamation for Women and Islam, ambacho Salman Rushdie amekielezea hivi:
This is an immensely important book--passionate, challenging, and necessary. It should be read as widely as possible, because it tells the truth--the unvarnished, uncomfortable truth.
Mtazamo wa Ayaan Hirsi Ali umemletea matatizo makubwa tangu mwanzo. Anatafutwa kuuawa. Alikuwa chini ya ulinzi u-Holanzi na hatimaye alihamia Marekani. Bado anaandika, anatoa mihadhara na anafanya mahojiano.
Baada ya kusikia habari zake kwa miaka kadhaa, niliamua kutafuta ukweli mimi mwenyewe. Nilinunua kitabu chake kiitwacho Nomad, nikakisoma, kama nilivyoandika katika blogu hii. Nilifahamu kuwa kitabu chake kingine kinachofahamika sana ni Infidel. Sikuwa na haraka nacho, kwani ninanunua na kusoma vitabu vingine muda wote. Lakini, hatimaye, nimeamua kukinunua nikisome. Sijui anasema nini katika kitabu hiki, na duku duku inanisukuma nisome.
Subscribe to:
Posts (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Ukizunguka mitaani Dar es Salaam, utakuta matangazo mengi ya waganga wa kienyeji. Waganga hao wanatoka sehemu mbali mbali, kama vile Sumbaw...
-
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...