Posts

Showing posts from November, 2015

Utendi wa Mikidadi na Mayasa

Image
Wiki hii, bila kutegemea, nimevutiwa na wazo la kusoma Utendi wa Mikidadi na Mayasa . Ninazo tendi kadhaa, kuanzia za zamani kama vile Mwana Kupona , Fumo Liongo , na Ras il Ghuli , hadi za enzi zetu hizi. Ninapenda kuzisoma na kuzitafakari, sambamba na tungo za aina hiyo za mataifa mengine, kama vile Gilgamesh , Iliad na Odyssey , Sundiata , na Kalevala . Nimeusikia Utendi wa Mikidadi na Mayasa tangu zamani. Sijui lini nilinunua nakala yangu ya utendi huu, lakini sikupata wasaa wa kuusoma. Kwa kuupitia haraka haraka, nimeona kuwa una mambo yanayofanana na yale yaliyomo katika tendi zingine maarufu za ki-Swahili kama Ras il Ghuli . Kwa mfano, dhamira ya mapigano kama njia ya kuthibitisha ushujaa imejengeka katika Utendi wa Mikidadi na Mayasa , kama ilivyo katika Utendi wa Ras il Ghuli . Mayasa ni shujaa mwanamke anayenikumbusha shujaa mwanamke aitwaye Dalgha katika Utendi wa Ras il Ghuli . Wote wawili ni wapiganaji hodari na hatari sana, ambao yeyote anayetaka kuwaoa sherti kw

Kitabu Changu Bado Kiko Maoneshoni

Image
Nimepita tena katika duka la vitabu la hapa chuoni St. Olaf, kama ilivyo kawaida yangu, kuangalia vitabu vipya, na pia kuangalia vitabu ambavyo maprofesa wa masomo mbali mbali wanapangia kufundisha. Katika kuzunguka humo dukani, nilipita tena sehemu ambapo vinawekwa vitabu vilivyoandikwa na maprofesa wa chuo hiki. Kabla sijafika kwenye sehemu hiyo, macho yangu yalivutiwa na kitabu change cha Matengo Folktales , ambacho kilikuwa bado kiko sehemu maalum vinakowekwa vitabu ambavyo uongozi wa duka huamua kuvipa fursa ya kuonekana vizuri zaidi kwa kipindi fulani, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii. Kuna mambo yanayonigusa kila niingiapo katika duka hili la vitabu na maduka mengine ya vitabu popote hapa Marekani. Kubwa zaidi ni jinsi wahudumu wanavyokuwa ni watu makini katika masuala ya vitabu. Wanajua habari za vitabu, na wanaweza kukuelimisha kwa namna mbali mbali. Hawako katika kazi hii kwa kubahatisha au kwa kubabaisha. Wanajua wanachokifanya. Unaweza kuingia katika duka

Kutafsiri Fasihi

Image
Dhana ya tafsiri si rahisi kama inavyoaminika na jamii. Wataalam wanaijadili, kwa misimamo tofauti. Kuna vitabu na makala nyingi juu ya nadharia za tafsiri na shughuli ya kutafsiri. Kati ya vitabu vyangu, kuna ninachopenda kukipitia, kiitwacho Theories of Translation , ambacho ni mkusanyo wa insha za watu kama Johann Wolfgang von Goethe, Friedrich Nietzsche, Walter Benjamin, Roman Jakobson, Michael Riffaterre na Jacques Derrida. Insha hizi zinafikirisha. Jose Ortega y Gasset, kwa mfano, anasema kuwa kutafsiri ni jambo lisilowezekana. Ni kama ndoto. Ni kujidanganya. Walter Benjamin anauliza masuali mengi magumu. Derrida, katika insha yake juu ya Mnara wa Babel, iliyotafsiriwa na Joseph F. Graham, anaandika:           The "tower of Babel" does not merely figure the irreducible multiplicity of tongues; it exhibits an incompletion, the impossibility of finishing, of totalizing, of saturating, of completing something on the order of edification, architectural construction, s

Jana Nilikwenda Kusimulia Hadithi

Image
Jana jioni nilikwenda Maple Grove, Minnesota, kwenye sherehe ya watu wa Liberia ya kumbukumbu ya kuzaliwa mtoto. Nilikuwa nimealikwa kusimulia hadithi, kama nilivyoandika katika blogu hii. Nilifika saa moja jioni, kama nilivyotegemewa, nikakuta sherehe zimeshamiri. Watoto walikuwa katika michezo, na watu wazima walikuwa katika mazungumzo.  Baada ya kukaribishwa kuongea, nilijitambulisha kifupi, nikashukuru kwa mwaliko. Nilifurahi kumwona binti mdogo ambaye alikuwa amehudhuria niliposimulia hadithi katika tamsha la Afrifest. Yeye na mama yake, ambaye alikuwa mwenyeji wangu hiyo jana, ndio watu pekee nilowafahamu. Nilijiandaa kusimulia hadithi kutoka Afrika Magharibi. Nilisimulia hadithi moja kuhusu urafiki baina ya Chura na Buibui ("Frog and Spider") na ya pili juu ya mhusika aitwaye Pesa ("Money"). Baada ya kusimulia hadithi ya Chura na Buibui, nilitumia muda kuwauliza watoto mawazo yao kuhusu hadithi hiyo. Hawakusita kujieleza. Sikushangaa, kwani katika uzoe

Waumini Waikumbuka Hotuba Niliyotoa Lands Lutheran Church

Niliwahi kuandika katika blogu hii kuhusu hotuba niliyotoa tarehe 11 Aprili, 2015, katika mkutano wa waumini wa Sinodi ya Minnesota ya Kusini Mashariki ya Kanisa la ki-Luteri la Marekani.  Nimeona ripoti fupi ya hotuba katika jarida la kanisa la First Lutheran la mjini Red Wing, Minnesota, The Spire (July/August 2015) uk. 4. Ninaiweka hapa kwa kumbukumbu yangu. ------------------------------------------------------------------------------------- CANNON RIVER CONFERENCE REPORT In April some representatives from First Lutheran, United Lutheran, and St. Paul’s Lutheran attended the women’s Cannon River Conference in Zumbrota. There was a very thorough explanation of the history of the beginnings of the Lutheran church in this area of the country, so there was less time for the main speaker, Joseph Mbele, a St. Olaf professor. Besides teaching, Professor Mbele works with groups in the area to mediate cultural conflicts. He asked us to look at the positive and the potential in all

Shairi la "The Layers" la Stanley Kunitz na Tafsiri Yangu

Image
Tarehe 9 Machi, 2005, nilipata ujumbe kutoka kwa Dr. Arthur Dobrin, mwandishi na profesa katika Chuo Kikuu cha Hofstra, New York, akiniulizia iwapo ningekubali kulitafsiri kwa ki-Swahili shairi la Stanley Kunitz liitwalo "The Layers." Aliniambia kuwa inaandaliwa sherehe ya kumbukumbu ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Stanley Kunitz na kwamba tafsiri za shairi hili katika lugha mbali mbali zitawasilishwa kama sehemu ya kumbukumbu. Aliambatanisha shairi hilo katika ujumbe wake. Sikuwa ninalifahamu shairi hilo. Jina la Stanley Kunitz huenda nilikuwa nalifahamu kwa mbali, lakini sidhani kama nilikuwa nimesoma mashairi yake. Katika mazingira hayo yaliyokuwa mithili ya giza akilini mwangu, nililisoma shairi la "The Layers" nikakubali kulitafsiri, ingawa niliona ingekuwa kazi ngumu. Kazi ya kutafsiri haikuwa rahisi, kutokana na jinsi fikra na taswira zilivyosukwa katika shairi hili. Ingawaje kwa ujumla ni shairi linaloelezea mawazo ya mzee anayeangalia maisha aliyopitia

Nimealikwa Kusimulia Hadithi

Image
Leo nimepata ujumbe kutoka kwa mama mmoja m-Liberia aishiye hapa Minnesota. Amejitambulisha kwamba tulikutana katika tamasha la Afrifest, akauliza iwapo nitaweza kwenda kusimulia hadithi mjini Maple Grove tarehe 14 mwezi huu, katika sherehe ya kumbukumbu ya kuzaliwa mtoto. Nilielezea katika blogu yangu ya ki-Ingereza nilivyosimulia hadithi katika tamasha la Afrifest, hapa na hapa. Nilisimulia hadithi mbili kutoka katika kitabu cha Matengo Folktales . Mama aliyeniletea mwaliko wa tarehe 14 amenikumbusha kwamba mtoto wake na wengine walioshuhudia hadithi zangu katika Afrifest walivutiwa na wanataka nikasimulie tena. Hii itakuwa mara yangu ya kwanza kusimulia hadithi katika mkusanyiko wa wanafamilia na marafiki zao, katika sherehe ya kifamilia. Nimezoea kusimulia katika vyuo. Nitatumia sehemu ya muda nitakaokuwa nao kuelezea dhima ya hadithi katika jadi za wa-Afrika na wanadamu kwa ujumla, halafu nitasimulia hadithi, na kisha nitawahimiza wasikilizaji kusaidia kuichambua hadit

Tafsiri ya "Nyang'au," Shairi la Haji Gora Haji

Image
Kwa siku kadhaa sasa, nimekuwa nikisoma Kimbunga , kitabu cha mashairi ya Haji Gora Haji wa Zanzibar. Sambamba na kusoma, nimevutiwa na wazo la kujaribu kuyatafsiri baadhi. Nimeshatafsiri shairi la "Kimbunga."  Leo nimeona nitafsiri "Nyang'au." Ni shairi linalohusiana na fasihi simulizi, kama yalivyo mashairi na maandishi mengine kadhaa ya Haji Gora Haji. Kwa kuwawezesha wasomaji wa ki-Ingereza kuonja utunzi wa Haji Gora Haji, ninategemea kuchangia kumtangaza ulimwenguni mshairi huyu mahiri. Anastahili kuenziwa kwa kila namna. Yeyote anayekijua ki-Swahili vizuri, na pia ki-Ingereza, atajionea ugumu wa mtihani niliojipa wa kutafsiri shairi hili. Ingawa nimejitahidi sana, siwezi kusema ninaridhika na tafsiri yangu. Jaribu nawe kulitafsiri shairi hili, upate maumivu ya kichwa, na pia raha ukifanikiwa.                                                               Nyang'au 1.        Fisi alikichakani, mtu kapita haraka           Kwa vile yuko mbiyoni, mk

"Equal Rights:" Wimbo wa Peter Tosh

Image
Mimi ni shabiki mkubwa wa miziki ya aina mbali mbali, ikiwemo "reggae." Kati ya wana "reggae ninaowapenda sana ni Peter Tosh wa Jamaica, ambaye ni marehemu sasa. Wimbo wake mojawapo niupendao sana ni "Equal Rights." Nilianza kuusikia wimbo huu miaka zaidi ya 30 iliyopita. Ujumbe wake ni chemsha bongo ya aina fulani. Anasema "I don't want no peace; I need equal rights and justice," yaani "Sitaki amani; nahitaji usawa kwa wote na haki."

Hifadhi ya Majengo ya Kihistoria

Image
Miezi kadhaa iliyopita, niliposikia kuwa jengo la CCM mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam, limebomolewa ili kujengwa jengo la kisasa, nilifadhaika. Niliwazia utamaduni ninaouona hapa Marekani wa kuhifadhi majengo ya kihistoria. Nimeona katika miji wanahifadhi maeneo wanayoyaita "historic districts." Mfano ni picha zinazoonekana hapa, ambazo nilipiga mjini Faribault. Ninaona maeneo haya katika miji mingine pia. Maeneo ya kihistoria, yenye majengo ya zamani, ni kumbukumbu ya historia ambayo inastahili kuhifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo. Vile vile, ni kivutio kwa watalii. Kwa mtazamo huo, nililiwazia jengo la awali la CCM Lumumba. Lilikuwa na umuhimu wa pekee katika historia za harakati za kupigania Uhuru. Ni jengo ambamo TANU ilizaliwa. Ni urithi wetu sote wa-Tanzania. Sijui ni nani walioamua kulibomoa na kwa nini. Sijui kwa nini hawakutafuta sehemu nyingine ya kujenga hilo jengo la kisasa. Ninafahamu kuwa majengo yanaweza kuzeeka mno yakawa si salama kwa watu kuingia. Pap