Sunday, April 12, 2015

Mazungumzo Kufuatia Mhadhara Lands Lutheran Church

Mhadhara wangu jana kwenye mkutano uliofanika katika kanisa la Lands Lutheran mijini Zumbrota, Minnesota, ulienda vizuri. Kulikuwa na mambo kadhaa katika ajenda, kama vile hotuba na ripoti mbali mbali, muziki na nyimbo. Halafu nilitambulishwa, nikatoa hotuba yangu fupi.

Mada yangu ilikuwa "The Dilemma of Cultural Differences: Challenges and Opportunites," ambayo inaendana na utafiti, uandishi, na mihadhara ambayo nimekuwa nikitoa sehemu mbali mbali. Niliongelea umuhimu wa kuzingatia athari za tofauti za tamaduni katika ulimwengu wa utandawazi wa leo. Kwa vile nilikuwa naongea katika mkutano wa waumini wa dini, nilisisitiza kuwa utandawazi huu unatuhitaji tutafakari namna ya kuthibitisha imani ya dini yetu, kwani kuwepo kwa tamaduni mbali mbali ni mtihani anaotushushia Mungu.

Kwa kuzingatia kuwa wote waliokuwa wananisikiliza ni wazungu, katika eneo la mashambani, na ambao wanajua propaganda zilizopo Marekani kuhusu wageni wanaoendelea kuingia nchini, niliwakumbusha kuwa Yesu tunayemwabudu alikuwa mchokozi na mkorofi alyewatibua watu kwa fikra na kauli zake. Angekuwepo leo hapa Zumbrota, hapa Marekani, bila shaka angebadilisha hadithi yake ya m-Samaria mwema, na badala yake angewatibua kwa kusimulia habari ya mu-Islamu mwema.

Basi, kwa hoja za aina hiyo, nilichochea fikra miongoni mwa wasikilizaji. Tulipomaliza mkutano, tulienda kula chakula cha mchana na watu wakaendelea kuongea nami. Kwa vile kulikuwa nakala za kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences mezani, kama ilivyotangazwa na mratibu wa mkutano wakati alipokuwa ananitamulisha, baada ya kula nilikwenda kwenye ile meza na kuwauzia na wengine kuwasainia.

Napenda kumalizia kwa kuleta mfano moja wa maongezi yaliyofanyika pale kwenye meza. Mama mmoja alipokiona kile kitabu, hakuchelewa kuniambia kuwa kitabu kile kiko katika maktaba ya kanisa lao la Zumbro. Nilifurahi nikamwambia kuwa nilifahamu jambo hilo. Aliponiuliza nilifahamuje, nilimweleza kuwa nilisoma katika kijarida cha kanisa la Zumbro uchambuzi wa kitabu changu, na mwandishi alikuwa amesema kuwa kitabu kiko katika maktaba ya kanisa lile. Aliniambia kuwa aliyeandika uchambuzi ule ni mchungaji mstaafu, akaongeza kuwa atamweleza kuwa tumeonana hapa mkutanoni Lands Lutheran Church.

Huo ni mfano mmoja tu wa mazungumzo ya jana na watu mbali mbali. Kweli dunia hii ni ndogo, na wanadamu hukutana kwa namna tusiyotegemea. Mambo ya aina hii ni mengi, na ndio yananipa hamasa ya kwenda popote kushiriki mambo ya aina hii ya manufaa kwa jamii.

(Picha ya kanisa la Lands Lutheran nilipiga wakati naondoka hapa mahali)

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...